Mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba akizungumza wakati wa Mdahalo wa jamii kuhusu kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanaume wenye umri kati ya miaka 18 hadi 60 kata ya Shilela Halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga kwa lengo la kujenga uelewa wa jamii kuhusu mila na desturi zinazochangia ukatili wa kijinsia
Jamii imeitaka serikali kwa kushirikiana na Mashirika ya kiraia kuweka nguvu katika kutoa elimu ya Jinsia kwa wanaume wote ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo mila na desturi kandamizi.
Hayo yamesemwa jana Machi 25,2021 wakati wa mdahalo kwa wanaume wa kata ya Lunguya na Shilela katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mkoani Shinyanga, uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Umoja la Idadi ya watu (UNFPA) kwa lengo la kuwafanya wanaume kupata nafasi ya kujadili, kutafakari na kupendekeza njia za kuondoa Ukatili wa kijinsia ikiwepo wao wenyewe kubadilisha mitazamo hasi juu ya wanawake.
Akizungumza, Mwezeshaji wa Mdahalo huo kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kama wanaume watatumia vizuri nafasi yao vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hasa unyanyasaji wa wanawake ikiwemo ndoa na mimba za utotoni vitapungua kabisa.
“Tukibadilisha mtazamo hasi juu ya wanawake, tukaona kuwa mtoto wa kike hawezi kuwa bidhaa ya kuuzwa ili tupate mahari, tukaondoka kwenye kutegemea uchumi wa ng’ombe kama njia ya kupata mali na kugeukia vyanzo vingine vya mapato tunaondoa kabisa tatizo la ndoa za utotoni”, alisema.
Washiriki walisema kwamba, suala la mahari linawaathiri vijana wengi kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira pia.
Katika mdahalo huo uliowashirikisha vijana na wanaume kuanzia miaka 18 hadi 60 zaidi ya watu 300 kwa kata hizo mbili, suala la ulinzi wa kwa wasichana lilijadiliwa na kuazimia kutumia zaidi sheria ndogo ndogo za vijiji na jeshi la sungunsugu kulinda vijana wanaowarubuni wasichana wa shule.
0 comments:
Post a Comment