Monday 27 February 2023

POLISI SHINYANGA WAKAMATA WAGANGA WA RAMLI ZA MAUAJI.. RPC MAGOMI AONYA ASKARI WANAOSHIRIKI KUFANYA UHALIFU


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha vifaa vya uganga vilivyokamatwa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 27,2023 - Picha na Kadama Malunde

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata waganga wa jadi watatu wakiwa na vifaa vinavyotumika katika kupiga ramli chonganishi ambayo husababisha mauaji ya kikatili yakiwemo ya kuua kwa mapanga huku likikemea vikali tabia ya baadhi ya askari polisi wasio waadilifu ambao wanavujisha siri na wanaoshirikiana na wahalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 27,2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema vifaa hivyo na watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia misako na doria za jeshi la polisi kwa kipindi cha Februari 5 hadi 27,2023.

“Tumekamata waganga wa jadi wakiwa na vifaa vya kufanyia ramli chonganishi zinazopelekea mauaji ya kikatili yakiwemo mauaji ya mapanga. Pia tumefanikiwa kukamata watuhumiwa watatu wakiwa na vifaa tiba vya hospitali ambavyo haviruhusiwi kumilikiwa na mtu pasipo na idhini ya serikali”,ameeleza Kamanda Magomi.


“Pia tumekamata jumla ya lita 780 za mafuta ya diesel katika maeneo tofauti ya mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na pikipiki tatu zilizokuwa zinatumika katika uhalifu ikiwemo kubeba mafuta ya wizi katika mradi wa SGR. Hali kadhalika tumeokota pikipiki 2”,amesema.

Amevitaja vitu vingine vilivyokamatwa kuwa ni pamoja na milango 9 ya chuma,mabomba matatu ya chuma,bomba moja la alama za barabarani, milango mitano ya mbao, mzani wa kupimia uzito, mashine ya kutobolea miamba, godoro moja,viti vinne vya plastiki, bangi kete 31, ngoma moja ya shule na magitaa mawili,mashine mbili za kuchezea kamali, subwoofer 2,feni 1,mtungi mmoja wa gesi.

“Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linakemea vikali tabia ya baadhi ya askari polisi wasio waadilifu ambao wanavujisha siri na ambao wanashirikiana na wahalifu na kusababisha kudhoofika kwa upatikanaji wa taarifa za kihalifu kutoka kwa wananchi. Hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao”, ameongeza Kamanda Magomi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 27,2023. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 27,2023
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 27,2023.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha vifaa vya uganga vilivyokamatwa na Jeshi la polisi kufuatia misako na doria zilizofanyika
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha vifaa vya uganga vilivyokamatwa na Jeshi la polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha vitu  mbalimbali vilivyokamatwa na Jeshi la polisi Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha vitu  mbalimbali vilivyokamatwa na Jeshi la polisi Shinyanga

Vitu  mbalimbali vilivyokamatwa na Jeshi la polisi Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog



Share:

WAFANYAKAZI WA BARRICK NORTH MARA WASHIRIKI MBIO ZA KILI MARATHON 2023


Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick wakishiriki kukimbia mbio za masafa marefu
***

Wafanyakazi wa Mgodi wa Barrick North Mara, uliopo wilayani Tarime Mkoa wa Mara, wameshiriki katika mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika Mkoani Kilimanjaro ambapo baadhi yao wamemudu kukimbia mbio za masafa marefu.

Kampuni ya Barrick imekuwa na program za mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa na nguvu na afya bora.

Kila mwaka kampuni imekuwa ikiwezesha wafanyakazi wake kushiriki mashindano mbalimbali ya michezo ikiwemo mashindano ya mbio za kilomita 42 ya Bulyanhulu Healthy Lifestyle Marathon yanayofanyika kila mwaka.
Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick North wakifurahia kumaliza kukimbia mbio za Kili Marathon zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick North wakifurahia kumaliza kukimbia mbio za Kili Marathon zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick North wakifurahia kumaliza kukimbia mbio za Kili Marathon zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick North wakifurahia kumaliza kukimbia mbio za Kili Marathon zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wafanyakazi wa Barrick North wakifurahia kumaliza kukimbia mbio za Kili Marathon zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.
Share:

GGML YANG’ARA TUZO ZA ATE, MAJALIWA AAHIDI MAKUBWA


Meneja Mwandamizi (Rasilimaliwatu) kutoka GGML, Charles Masubi akipokea tuzo kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia). GGML iliibuka mshindi wa pili katika tuzo zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa lengo la kutambua mchango wa uzalishaji wa rasilimaliwatu wenye ubora kwa soko la ajira.

 Na Mwandishi wetu 
JITIHADA za Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu kwa kuwapatia mafunzo kazini zimeendelea kuonekana baada ya kampuni hiyo kuibuka mshindi wa pili katika tuzo zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).


GGML ilibeba tuzo katika kundi la waajiri wakubwa kutokana na mchango wake wa uzalishaji wa rasilimaliwatu wenye ubora kwa soko la ajira.


Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya kampuni hiyo kupokea wahitimu 50 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini ambao wameanza kupatiwa mafunzo kazini mwaka huu. Kati yao 30 ni wanawake na 20 wanaume. Mwaka jana jumla ya vijana 26 walihitimu mafunzi hayo ndani ya GGML.


Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Meneja Mwandamizi (Rasilimaliwatu) kutoka GGML, Charles Masubi aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika uzalishaji wa vijana bora wanaokubalika katika soko la ajira.


Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alisema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.


Pia aliwapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo, uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.


Alitoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.


“Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu,” alisema.


Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda. “Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana.”


Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania”, Waziri Mkuu alisema kauli hiyo ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.


Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau na vyuo au taasisi za elimu.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran alisema ili Tanzania iweze kushiriki kikamilifu katika soko shindani la Afrika Mashariki na dunia ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe katika kukuza ujuzi hususani kwa vijana.


Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATATU FEBRUARI 27,2023






















Share:

Sunday 26 February 2023

VIJANA WA ULINZI SHIRIKISHI WAONYWA KUJIHUSISHA NA VITENDO VYA KIHALIFU





Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala liwewaonya baadhi ya vijana wa ulinzi shirikishi kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya kihalifu wakati wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi katika mitaa yao.



Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala Dr. Debora Magiligimba ACP katika bwalo la Polisi Buguruni alipokutana na vijana wa ulinzi shirikishi katika Wilaya ya Kipolisi Buguruni kwa lengo la kuwapa maelekezo na mwongozo wa utakaosaidia kuboresha utendaji wa kazi za ulinzi shirikishi katika maeneo yao.


 "Baadhi ya vijana wa ulinzi shirikishi mmekuwa mkishirikiana na wahalifu kwani mnatoa taarifa ya doria zenu kwa wahalifu mkiwajulisha sehemu mlipo jambo ambalo linawasaidia wahalifu hao kujipanga na kubadili sehemu ya kwenda kufanya matukio ya uhalifu",amesema.


Pia Kamanda Dr. Debora Magiligimba ametaka kila kikundi cha ulinzi shirikishi kuhakikisha kunakuwa na sare kwa ajili ya kuvaa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya ulinzi katika mitaa yao.


" Sare zinasaidia kuwatofautisha na vibaka pindi uhalifu unapotokea jambo ambalo litawasaidia wananchi kuwatofautisha na wahalifu", ameongeza.


Aidha Kamanda Dr. Debora Magiligimba amewataka vijana hao wa ulinzi shirikishi kuepuka vitendo vya ukatili katika familia zao na kutoa rai kwao kama kuna kijana wa ulinzi shirikishi ametendewa matendo ya ukatili wawezekufika katika madawati ya kijinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya Polisi kutoa malalamiko yao.




Kikao hicho cha ulinzi shirikishi kiliudhuriwa Wakaguzi Kata 08 na vijana wa ulinzi shirikishi wapatao 139 kutoka katika Kata 08 zinazopatikana katika Wilaya ya Kipolisi Buguruni.
Share:

ASIYEJULIKANA AVAMIA KANISA KATOLIKI GEITA, AHARIBU VITU VITAKATIFU


Sehemu ya uharibifu uliofanywa

NA ROSE MWEKO, GEITA
MTU asiyefahamika amevamia na kuingia ndani ya kanisa Katoliki jimbo la Geita na kufanya uharibifu katika altare na sakrestia na kuvunja tabernakulo huku akimwaga ekaristi takatifu na kuchana kitabu kitakatifu Biblia huku akiharibu mfumo wa camera za ulinzi.

Taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo katoliki la Geita kwa njia ya simu Flavian Matindi Kasalla amesema mtu huyo alivunja kioo cha mlangoni na kuharibu madhabahu takatifu huku akiharibu sehemu mbalimbali za ibada na kuharibu vitabu vitakatifu.
“mpaka sasa hatujajua alikotokea na wala hatujui aliingia saa ngapi japo ilikua ni usiku wa kuamkia siku ya jumapili, kanisa letu linalindwa na kampuni ya ulinzi ila mpaka sasa ni kitendawili kuwa mlinzi alikuwa wapi, mtu aliyefanya tukio hilo amekamatwa na ameshafikishwa katika vyombo vya usalama pamoja na mlinzi aliyekuwa zamu siku hiyo” alisema Askofu Kasalla.
Watu wawili wanashilikiwa na jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi akithibithisha kukamatwa kwa watu hao Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ACP Berthaneema Mlay alisema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini nani kamtuma na sababu za kufanya uharibifu huo.
“mtu huyo anaonekana alikuwa mlinzi na ni mtu ambaye amekuwa akihudumu katika kanisani haswa huko alikotoka Bukoba hivyo jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi na itakapobainika tutatoa taarifa zaidi kwani mpaka sasa kuna mambo tunayafuatilia tatutayazungumza ili kutovuruga upelelezi.

Chanzo - The Profiletv blog

Share:

BABA AKAMATWA TUHUMA ZA KULAWITI WATOTO WAKE WA MIAKA 8 na 11 SHINYANGA MJINI


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linachunguza tukio linalomhusisha mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 35 kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wake wawili wenye umri wa miaka 8 na 11 wanafunzi wa shule ya msingi Mapinduzi B, iliyopo kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amethibitisha mwanaume huyo kukamatwa kwa ajili ya uchunguzi.

Kamanda Magomi amesema upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Kambi Butete amesema Februari 22 Mwaka huu majira ya saa tano asubuhi watoto hao walifikishwa katika Hospitali hiyo na kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari ambapo majibu ya vipimo vyao yamekabidhiwa kwa vyombo vya usalama kwa ajili ya hatua za kisheria.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mapinduzi B, Hassan Hemed ambaye ameeleza namna alivyopokea taarifa za tukio hilo, na kusema kuwa kushamiri kwa matukio hayo inachangiwa na wazazi na walezi kutowajibikia jukumu la malezi bora na makuzi kwa watoto.

‘Hizi taarifa za hawa watoto wawili nilizipokea kwa kuletewa na watu ambao wao wanasema ni wanaharakati ndiyo waliniletea hawa watoto saa sita usiku asubuhi nikaenda kwa hawa watoto mpaka wanapoishi mpaka ndani kwao ni kweli wanalala chumba kimoja na baba yao mzazi", amesema Mwalimu Hemed.

Taarifa za kulawitiwa kwa watoto hao ziliripotiwa kwa Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mapinduzi B, usiku wa Februari 22, Mwaka huu 2023.

Via Misalaba blog

Share:

CHRISTINA MNDEME ATEULIWA KUWA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA, FRANCIS MICHAEL SONGWE, KINDAMBA TANGA


 Mhe. Christina Mndeme

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na uhamisho wa wakuu wa mikoa mitatu ya Shinyanga, Tanga na Songwe.


Wakuu wa mikoa wapya walioteuliwa ni Christina Mndeme ambaye anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga huku aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Francis Michael ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

Christina Mndeme anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, ambae alichaguliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.

Aidha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba amehamishiwa Mkoa wa Tanga, huku aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Omary Mgumba uteuzi wake ukitenguliwa.

Share:

VIONGOZI NA WATUMISHI WA CHUO CHA MWEKA WAASWA KUWA WAADILIFU


Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini – Arusha Bw. Baraka Mgimba akitoa mada kuhusu Uadilifu katika mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori –Mweka. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 24 February, 2023 chuoni hapo mkoani Kilimanjaro

Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini – Arusha Bw. Musiba Magoma akitoa mada kuhusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu katika mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori –Mweka. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 24 February, 2023 chuoni hapo mkoani Kilimanjaro.



Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini- Arusha imetoa mafunzo kuhusu Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa Umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori -Mweka mkoani Kilimanjaro na kuwaasa kuwa waadilifu katika Utumishi wa Umma.Mafunzo hayo yalifanyika chuoni hapo tarehe 24 February, 2023.

Akitoa mada kuhusu Uadilifu, Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili kanda ya Kaskazini- Arusha Bw. Baraka Mgimba alieleza kuwa Viongozi na watumishi wote wa Umma wanapaswa kutenda kazi kwa uadilifu wa hali ya juu ikiwa ni moja ya misingi ya maadili katika utumishi wa Umma.

Bw. Mgimba alieleza kuwa uadilifu ni hali ya kufanya jambo sahihi katika wakati sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayekuona “uadilifu huanza nafsini mwa mtu mwenyewe ndipo unaanza kuonekana kwa wengine.”alisema.

Bw, Mgimba alielezea sifa za mtu muadilifu kuwa ni pamoja na; kujali wengine, kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji, kuwa msikivu, kujizuia na tamaa, kuwa mnyenyekevu, kuwa mwaminifu katika hali zote pamoja sifa nyingine nyingi ambazo binadamu yeyote anapaswa kuwa nazo.

Aidha Bw. Mgimba aliendelea kusema kuwa kiongozi ama mtumishi wa Umma anapaswa kutenda kazi kwa kufuata kanuni misingi na miongozo mbalimbali iliyowekwa ili kuleta tija katika utendaji kazi wao ‘‘ Misingi hii pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa nchini ikifuatwa vizuri itakuza hali ya uadilifu kwa viongozi na watumishi wote nchini ”

Kwa mujibu wa Bw. Mgimba alieleza kuwa Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili imedhamiria kukuza hali ya uadilifu nchini kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa viongozi na watumishi wa umma nchini lengo likiwa ni kuwakumbusha jinsi wanavyotakiwa kuenenda katika utendaji kazi wao.

Pamoja na hayo Bw. Mgimba aliongeza kuwa kiongozi na mtumishi yeyote ni kioo cha jamii inayomzunguka hivyo anapaswa kuishi maisha yatakayoipa jamii imani juu serikali yao kwani kiongozi na mtumishi wa Umma anafanya kazi kwa niaba ya serikali ‘‘ Kiongozi na mtumishi wa umma anapokua muadilifu na kutenda kazi katika hali ya uadilifu anajenga imani ya wananchi kwa serikali yao’’

Aidha akitoa mada nyingine iliyohusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa umma Bw. Musiba Magoma ambaye ni Afisa maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya kaskazini –Arusha alieleza kuwa kila kiongozi na mtumishi yeyote wa umma mara tuu anapoteuliwa ama kuajiriwa anapaswa kukiri Ahadi ya Uadilifu ambayo itampa dira ama mwongozo wa ni yapi anapaswa kufanya ama kutokufanya katika nafasi ama wadhifa wake .

Bw. Magoma alifafanua kuwa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa umma ina lengo la kuwahamasisha na kuwafanya kuwa na mwenendo unaofaa, inatoa nafasi kwa kiongozi na mtumishi wa Umma kujitathmini mwenyewe kutokana na kile alichoahidi na pia kuhamasisha viongozi na watumishi wa umma kuzingatia misingi ya maadili katika utendaji kazi wao.

Pamoja na hayo Bw. Magoma alieleza kuwa ipo misingi ya Ahadi ya Uadilifu inayomuongoza kiongozi kama vile Uwazi, uwajibikaji, uzingatiaji wa sheria kanuni na taratibu, kutoa huduma bora bila upendeleo, kuwa na matumizi sahihi ya taarifa pamoja na nyingine nyingi.

Katika hatua nyingine Bw. Magoma alifafanua kuwa zipo athari mbalimbali zinazotokana na kukiukwa kwa Ahadi ya Uadilifu kama vile wananchi kupoteza imani kwa serikali yao, kiongozi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni sheria na taratibu,kiongozi ama mtumishi kusimamishwa kazi na nyingine nyingi ambazo zitaathiri hali ya kiongozi ama mtumishi wa umma, familia jamii na hata serikali kwa ujumla.

Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi hao, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Wahab Kimaro alisema kuwa mafunzo kama hayo ni muhimu kwa viongozi na watumishi wa Umma na ni vyema yakatolewa mara kwa mara kwani yanaongeza ufanishi katika utendaji kazi wao wa kila siku.

“Tumepata watumishi wapya, wapo waliohamia pia kwa hiyo ni vyema wakapata mafunzo haya ya uadilifu ili sote tuzungumze lugha moja katika kutekeleza majukumu yetu” alisema.

Pamoja na hayo Pro. Kimaro alifafanua kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi na watumishi wa Umma ni moja ya silaha muhimu ya kuwafanya kuwa waadilifu kwani binadamu yeyote huwa muadilifu ikiwa kuna mahala atapaswa kujieleza ama kuchukuliwa hatua na pia kinamfanya awe na hamasa ya kutekeleza kile alichoapa.

Prof. Kimaro aliongeza kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kinasaidia sana kukuza nidhamu kwa viongozi na watumishi wa umma “ Kiapo hiki ni muhimu sana kwani mtumishi wa umma anapokwenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa anachukuliwa hatua kwa kile alichosema kwamba atatekeleza katika kiapo chake” alisema.

Mafunzo hayo ya Siku moja yaliandaliwa na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori –Mweka mkoani Kilimanjaro.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger