Tuesday, 27 May 2025

TAKUKURU YADHIBITI UBADHIRIFU WA MILIONI 92 ZA WAKULIMA WA TUMBAKU USHETU, SHINYANGA

 

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kudhibiti ubadhirifu wa kiasi cha shilingi milioni 92.16 zilizotengwa kwa ajili ya kuwafidia wakulima wa tumbaku wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Ibambala, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 27, 2025 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kessy, fedha hizo zilitolewa kwa wakulima waliopata hasara kutokana na mafuriko yaliyoathiri uzalishaji wa tumbaku katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024, lakini hazikufika kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.

“TAKUKURU ilibaini kuwa shilingi milioni 11.62 zilichukuliwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa matumizi yao binafsi, akiwemo Katibu Meneja Bw. Charles Alex Shiyengo na Mwenyekiti Bi. Faida Paulo Deda,” amesema Kessy.

Aidha, TAKUKURU imebaini kuwa kiasi kikubwa cha fedha—shilingi milioni 151.53—kiligawiwa kwa watu wasiostahili, wakiwemo ndugu wa viongozi hao. Miongoni mwa waliopokea fedha hizo ni Bi. Lucy Masanja Dglibata, mke wa Katibu Meneja, ambaye alipokea shilingi milioni 34.58, pamoja na Bw. Charles Charles Masanja aliyelipwa shilingi milioni 5.58.

Hatua za awali za kurejesha fedha hizo zimeanza kuchukuliwa huku wahusika wakikabiliwa na hatua za kisheria.

Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, TAKUKURU Shinyanga pia imepokea jumla ya taarifa 57 za tuhuma za rushwa, ambapo 52 zilifanyiwa uchunguzi na 13 kati yake zimefikishwa mahakamani.

Kwa upande wa elimu kwa umma, taasisi hiyo imeendesha mikutano ya hadhara 61, semina 30, na vipindi vya redio na runinga 13 kupitia programu yao ya Takukuru Rafiki, lengo likiwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.

Kessy amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa njia ya simu ya bure 113 au kupitia tovuti yao ya www.pccb.go.tz.


Share:

Monday, 26 May 2025

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE MEI 27,2025





Share:

SERIKALI ,WANAZUONI KUJADILI PPP, UCHUMI NA DIRA 2050

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPPC), David Kafulila, na Mwenyekiti wa REDET, Prof. Rwekaza Mukandala.

Mei 26, 2025

Na Mwandishi Wetu _ Dar es Salaam

Serikali inatarajiwa kukabiliana na hoja za wanazuoni na sekta binafsi kesho kuhusu dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), mwenendo wa uchumi chini ya Awamu ya 6 na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia (PPPC) David Kafulila, mjadala huo wa wazi utafanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kituo cha PPPC kitafanya kongamano kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET)  ambayo iko chini ya UDSM.

Mada kuu ya kongamano ni: Dola, Masoko na Uhamasishaji wa Mitaji: Nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi Kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Kafulila atafanya wasilisho kuhusu Dhana ya PPP na Nafasi yake Kuelekea Dira ya Taifa 2050 na Mwenyekiti wa REDET, Prof. Rwekaza Mukandala, ataongoza kongamano kama moderator.

Kongamano litafanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jumanne tarehe 27 Mei 2025 kuanzia saa 3:00 asubuhi mpaka saa 6:00 mchana.

Maafisa waandamizi wa serikali, wakuu wa makampuni ya sekta binafsi, wanazuoni na wawakilishi wa kada nyingine mbalimbali wanatarajiwa kushiriki kwenye mjadala wa wazi utakaorushwa mubashara na vituo kadhaa vya televisheni.

"Wananchi wote wanakaribishwa kuhudhuria kongamano hili la wazi ili waweze kushiriki kwenye mjadala kuhusu dhana ya PPP na nafasi yake kwenye kutekeleza Dira ya Taifa 2050," Kafulila amesema.

"Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) una nafasi kubwa kwenye mwelekeo mpya wa uchumi na maendeleo ya Tanzania."

Kituo cha PPPC kinasimamia jumla ya miradi 84 ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Miradi hiyo ipo kwenye sekta za usafirishaji, nishati, miundombinu na maeneo mengine.

Baadhi ya miradi hiyo ni Barabara ya waendao haraka (Express way) ya Kibaha–Chalinze -Morogoro (205km), na ile ya Isongole-Tunduma (210km) ambazo zikijengwa njia nne za barabara (epxress way), zinaweza kugharimu karibu dola za Marekani Bilioni 1.6.

Mradi wa barabara kwa ajili ya kupunguza foleni katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Outer ring roads) nao ni miongoni mwa miradi ya kutekelezwa kwa ubia wa PPP.

Share:

MWENGE WA UHURU WAZINDUA VISIMA TANDAHIMBA, WANANCHI WAPATA MAJI YA BOMBA KWA MARA YA KWANZA TANGU UHURU

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akikagua miundombinu ya mradi wa Kisima cha maji katika Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara kabla ya kuzindua mradi huo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akizindua mradi wa Kisima cha Maji katika Kijiji cha Mivanga Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara,kulia Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damasi

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara Falaura Kikusa,akimuonyesha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi ,mchoro wa mradi wa Kisima cha maji uliotekelezwa katika Kijiji cha Mivanga.

Na Regina Ndumbaro-Tandahimba 

Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 umeweka historia katika Kijiji cha Mivanga, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara baada ya kuzindua mradi wa uchimbaji wa visima vya maji, hatua iliyowapatia wakazi wa kijiji hicho huduma ya maji ya bomba kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate Uhuru. 

Uzinduzi huo umefanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ambaye alikagua na kuzindua rasmi kisima hicho akiwa ameongozana na viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba, Falaura Kikusa, amesema jumla ya Shilingi 452,500,000 zimetengwa kwa ajili ya kuchimba visima vitano katika vijiji vya Mivanga, Lyenje, Dinduma, Mchangani na Michenjele. 

Mradi huo ni sehemu ya programu ya uchimbaji wa visima 900 kote nchini, unaotekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani (force account), kwa kipindi cha miezi sita tangu Mei 2024, na unatarajiwa kukamilika Juni 2025 baada ya kuchelewa kutokana na changamoto mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kikusa, hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya maji na usimikaji wa matanki ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 10,000 umekamilika katika vijiji viwili, huku usimikaji wa pampu na mfumo wa nishati ya jua ukifanyika katika vijiji vinne. 

Kisima cha Mivanga pekee kinazalisha lita 372,000 za maji kwa siku. 

Fedha za utekelezaji zinatokana na program ya Lipa kwa Matokeo, Mfuko wa Taifa wa Maji pamoja na michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Katani Ahmed, ameishukuru serikali kwa kutatua tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, akisema kuwa mradi huo umepunguza changamoto kubwa iliyokuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo vijijini. 

Kwa upande wake, Ismail Ali Ussi amewataka wananchi kushirikiana na serikali kulinda miundombinu ya miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa jamii.

Asha Seleman, mkazi wa Kijiji cha Mivanga, amesema kabla ya mradi huo walilazimika kununua ndoo moja ya maji kwa Shilingi 1,000, jambo ambalo liliongeza gharama za maisha. 

Amesema sasa wameondokana na adha hiyo, na wana matumaini makubwa kuwa huduma hiyo itaboresha maisha yao kiuchumi na kiafya.

Share:

MAPEPELE AWANOA MAAFISA HABARI WA TAMISEMI, AWATAKA WAWE WAZALENDO


Na Mwandishi Wetu, OR- TAMISEMI

Mkuu wa Kitengo Cha Mawasilino Serikali na Msemaji Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI, John Mapepele ametoa wito kwa Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kutanguliza uzalendo na weledi wakati wa utoaji wa taarifa ili habari hizo ziwe na tija kwa taifa.

Mapepele ametoa wito huo mwisho wa juma wakati akiwasilisha maada kuhusu Mawasilino ya Kimkakati ya Kutangaza Nafanikio ya Sekta za Afya, Elimu na Miundombinu chini ya TAMISEMI kwa Maafisa Habari zaidi ya 200 wa Mikoa na Halmashauri zote nchini jijini Dodoma kwenye kikao kazi cha siku mbili kwa MaafisaHabari hao kilichoratibiwa na Wizara hiyo.
Kikao kazi hicho kilichofunguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe.Mohamed Omary Mchengerwa na kufungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa kimejadili pamoja na mambo mengine, mikakati mbalimbali ya kutangaza mafanikio ya Serikali, pia kuwajengea uwezo Maafisa Habari hao kwa mada mbalimbali za kitaaluma hususan matumuzi ya mifumo ya kidigitali kwenye utoaji wa taarifa na kuja na maazimio kadhaa ya kuboresha utendaji kazi.

Aidha, Mapepele amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa katika mikoa na Halmashauri zote nchini ambayo haijatangazwa ipasavyo na Maafisa Habari katika maeneo hayo na kuwataka kuwa wabunifu wa kutoa taarifa hizo

"Ndugu zangu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu ambapo tumeshuhudia mabarabara, madaraja, vituo vya mabasi na masoko yakitengenezwa kila uchao, ukiachia mbali madarasa, zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba kwenye kila kona hivyo ni wajibu wetu sisi Maafisa Habari wa Halmashauri na Mikoa kuwa wazalendo na kuisemea Serikali yetu ili wananchi waweze kujua na kutumia huduma hizi kikamilifu". Amefafanua Mapepele

Akifungua kikao kazi hicho Mhe. Mchengerwa amewataka Maafisa Habari wote wa TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi kwa wakati za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ya kazi. 

"Mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi hivyo msiache watanzania walishwe habari potofu". Amesisitiza Mhe. waziri Mchengerwa

Akifunga kikao kazi hicho, Katibu Mkuu Msigwa ameipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kuratibu kikao kazi hiki ambapo ameshauri kiwe kinafanyika kila mwaka ili kufanya tathmini wa utendaji wa kazi na kujadiliana masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi wa kundi hili kubwa la Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri nchini katika kutoa taarifa za miradi ya maendeleo.



Share:

Sunday, 25 May 2025

TAASISI YA UDOPRESA YAZINDULIWA UDOM




Kamati ya Uzinduzi wa UDOPRESA ikikabidhi zawadi ya Picha kwa Mgeni Rasmi Bi. Rose Joseph katika Hafla ya Uzinduzi wa Taasisi hiyo.

.......

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu cha Dodoma, Bi. Rose Joseph katika Ukumbi wa LT2 (CHSS) UDOM amefanya Uzinduzi wa Taasisi ya Wanafunzi wanaosomea Uandishi wa Habari na Uhusiano wa Umma Chuo Kikuu cha Dodoma - The University of Dodoma Public Relations Students Association (UDOPRESA) yenye jumla ya wanachama 250.

Taasisi hiyo imeanzishwa kwa dhamira kuu ya kuwaunganisha wanafunzi wanaosoma Taaluma ya Uhusiano na Umma na Uandishi wa Habari wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Kuimarisha Taaluma, Kushirikiana katika Tafiti na Mafunzo na kuwa chachu ya Maendeleo ya Taaluma hiyo Nchini.

Akizungumza wakati wa Hafla ya Uzinduzi; Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu cha Dodoma Bi. Rose Joseph ameahidi kuwapa ushirikiano wowote watakaohitaji huku akiwaasa kutumia Taasisi hiyo katika kulinda taswira ya Chuo na kuwataka watangulize uzalendo kwa Taifa mbele, kulinda na kuheshimu fani hiyo; pamoja na kuzingatia Sheria, Taratibu na Miongozo yote ya maafisa Uhusiano na Habari.

"Hili ni Jukwaa muhimu sana ambalo si tu kwamba linawaleta pamoja wanafunzi wanaosomea Uhusiano wa Umma UDOM, lakini naamini ni jukwaa zuri la kuwanoa, kuwaweka tayari kwa ajili ya kwenda kulitumikia Taifa, kutetea Tasnia na kwenda kuwa waandishi bora na maafisa bora wa umma" Aliongeza Bi. Rose.

Kwa Upande wake; Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari, Dkt. Deograsia Ndunguru amewapongeza Wanachama wote wa UDOPRESA huku akisisitiza kuwa Taasisi hiyo itawasaidia kuongeza ujuzi, Maarifa hasa katika kuwajenga kuwa maafisa Uhusiano Bora wa baadae.

Naye; Mlezi wa Taasisi hiyo Dkt. Mary Kafyome, amesema ulikuwa ni mchakato mkubwa kufanikisha jambo hilo huku akitoa pongezi kwa wote walihusika kufanikisha tukio hilo na ametoa wito kwa wanafunzi wanaobaki kuendeleza taasisi hiyo.

"UHUSIANO BORA, JAMII BORA!"
Mgeni Rasmi kwenye Hafla ya uzinduzi wa chama cha UDOPRESA, Bi. Rose Joseph akihutubia wakati wa uzinduzi.
Mlezi wa Taasisi ya UDOPRESA Dkt. Mary Kafyome akitoa neno la Shukurani wakati wa Uzinduzi wa Hafla ya UDOPRESA
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko Chuo kikuu cha Dodoma Bi. Rose Joseph akikata keki kama ishara ya Uzinduzi wa Taasisi ya UDOPRESA kutoka kulia kwake ni Mkuu wa Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari Dkt. Deograsia Ndunguru, akifuatiwa na Mlezi wa UDOPRESA Dkt. Mary Kafyome na Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa UDOPRESA Bw. Swerd Mwakage akifuatiwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi UDOM Bw. Gabriel Elia.
Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Deograsia Ndunguru akitoa neno wakati kwa Washiriki wakati wa Uzinduzi wa Taasisi hiyo.
Wanachama wa UDOPRESA wakiwa katika hali ya furaha wakati wa Uzinduzi wa Taasisi hiyo.
Mgeni Rasmi Bi. Rose Joseph akikabidhi Cheti cha Uongozi Bora kwa Mwenyekiti wa UDOPRESA Bw.Swerd Mwakage wakati wa Uzinduzi wa Taasisi hiyo.
Kamati ya Uzinduzi wa UDOPRESA ikikabidhi zawadi ya Picha kwa Mgeni Rasmi Bi. Rose Joseph katika Hafla ya Uzinduzi wa Taasisi hiyo.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI MEI 25,2025

Magazeti




Share:

Saturday, 24 May 2025

MWENYEKITI ACT-WAZALENDO TAIFA MHE. OTHMAN AELEZA MKAKATI MZITO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025, "TUNALINDA DEMOKRASIA NA KUTHAMINI UKOMBOZI"


Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akihutubia wananchi mkoani Shinyanga.

Na Mwandishi Wetu, Malunde 1 Blog Shinyanga

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa chama chake kiko tayari kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa dhamira thabiti ya kuendeleza harakati za mabadiliko ya kweli, haki kwa wananchi, na ukombozi wa Taifa.

Akihutubia wananchi katika viwanja vya shule ya Msingi Town iliyopo Manispaa ya Shinyanga Mei 24, 2025, Mheshimiwa Othman ameweka wazi kuwa dhamira ya kuasisi Taifa hili ilikuwa ni kuwapatia wananchi uhuru, sauti, na heshima katika kufanya maamuzi ya taifa lao – dhamira ambayo inazidi kudhoofishwa na mfumo wa sasa wa uongozi.

"Ndugu wananchi, lile ambalo tulilipambania sasa halipo tena, na wenzetu ndio ambao wamelipoteza," amesema kwa msisitizo, akirejea misingi ya uhuru na usawa wa wananchi.

Mheshimiwa Othman ameongeza kuwa kunyima wananchi haki ya kupaza sauti na kuchagua viongozi wanaowataka ni sawa na kuwafanya kuwa watumwa katika nchi yao wenyewe.

"Pale ambapo wananchi hawana sauti wala haki ya kuchagua wanaowaamini, Taifa hubaki dhaifu na tegemezi – hali ambayo siyo stahiki ya Watanzania," amesema Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman pia ameeleza kuwa licha ya Mkoa wa Shinyanga, na maeneo ya jirani, kubarikiwa na rasilimali nyingi kama dhahabu na almasi bado, rasilimali hizo zimekuwa zikitumiwa vibaya, huku wananchi wa maeneo hayo wakibaki maskini.

"Shinyanga kama ingekuwa nchi inayojitegemea, ingeweza hata kuikopesha Tanzania nzima," aamesema Othuman.

Ameongeza kuwa wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakihadaiwa na kushawishiwa kila msimu wa uchaguzi, lakini hali halisi haibadiliki kwao.

Ziara ya Mheshimiwa Othman ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya ACT-Wazalendo inayoitwa Operesheni Linda Demokrasia, inayolenga kufufua matumaini ya wananchi na kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika kupitia sanduku la kura.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ndugu Ado Shaibu, amempongeza Mhe.Othman kwa kuwa kiongozi asiye na chembe ya kuyumba katika misingi ya haki huku akiwapokea wanachama 26 walio jiunga na chama hicho kutoka katika vyama vingine vya upinzani .

Mkutano huo wa kisiasa umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kanda ya ziwa, akiwemo Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Shinyanga, Ndugu Hassan Ibrahim, pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama.Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akihutubia wananchi wa mkoa wa Shinyanga.Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.
Katibu mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Taifa , Ndugu Ado Shaibu, aa cha ACT-Wazalendo Taifa Shangwe Ayo akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakati wa mkutano nakupokea wanachama wapya 26 waliohama vyama vyao na kujiunga na ACT Wazalendo.Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.Katibu Mwenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Shangwe Ayo akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakati wa mkutano.Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.
Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.
Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT-Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman wakati wa mkutano.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger