Monday, 26 February 2024
Sunday, 25 February 2024
SAGINI AFIKA ENEO LA AJALI ILIYOUA WATU 25 ARUSHA...ATOA MAELEKEZO JESHI LA POLISI
Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimimiwa Jumanne Sagini amefika Jijini Arusha na kukagua eneo la ajali lilotokea Februali 24, 2024 katika barabara ya Arusha - Namanga, Eneo la Ngaramtoni kibaoni Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Mhe Jumanne Sajini Pamoja nakutoa pole kwa wahanga wa ajali hiyo, amelitaka Jeshi la Polisi kuweka mikakati madhubuti ya ukaguzi wa magari yanayotoka nje ya nchi pamoja na yale yaliyopo ndani ya nchi pasipo kusubiria wiki ya nenda kwa usalama ili kuepuka ajali zinazoweza kujitokeza kutokana na uzembe wa madereva ama ubovu wa magari.
Aidha Mheshimiwa Sagini ametoa Pongezi kwa Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Wa Arusha Mount
Meru, Madaktari, wauguzi pamoja na Jeshi la Polisi na kwa namna walivyotoa huduma bora kwa majeruhi waliopata ajali siku ya jana.
Amefafanua kuwa ajali hiyo imehusisha raia wa kigeni kutoka nchi za Marekani, Afrika kusini, Nigeria, Togo, Bukinafaso, Madagasca na Kenya.
Pia ametoa salamu za Pole toka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa watanzania hususani wananchi wa Mkoa wa Arusha kufuatia ajali hiyo.
Kwa upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP. Awadh Juma Haji amesema amepokea maelekezo yalitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi na kuahidi kuwa watayafanyia kazi ili kuhakikisha watumiaji wa barabara wanafuata sheria za usalama Barabarani ikiwemo watembea wa Miguu ili kuhakikisha wanafuata sheria zilizowekwa.
CP Awadhi amesema kuwa katika kuhakikisha wanatokomeza ajali tayari Jeshi hilo limeingia makubali ya shirika viwango Tanzania (TBS) ili kutumia vifaa vya kisasa katika ukaguzi wa vyombo vya moto.
WADAU WASISITIZA UMUHIMU WA MATUMIZI SALAMA YA MTANDAO KUELEKEA CHAGUZI
Na Rose Ngunangwa, Dar
Wadau wa teknolojia ya kimtandao mwishoni mwa wiki waliadhimisha Siku ya Usalama Mtandaoni kwa kufanya majadiliano yenye lengo la kukabiliana na upotoshaji na taarifa za uzushi hususani nyakati za uchaguzi.
Akifungua maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam, Bi. Rachel Magege ambaye ni Afisa Programu kutoka Shirika la POLLICY alisema lengo la maadhimisho hayo ni kujadili changamoto za data na teknolojia hususani tunapoelekea kwenye uchaguzi na kusisitiza kuwa suala la uadilifu na data ni mambo muhimu.
Kwa upande wake, mwasilishaji kutoka Kenya bwana Muthuri Kathure alisema mara nyingi taarifa za upotoshaji na uzushi zimekuwa zikijitokeza sana wakati wa uchaguzi au mabadiliko ya tabia nchi huku matangazo ya baadhi ya bidhaa zisizofaa kwa walaji zikiendelea kurushwa mtandaoni.
Alisema kuwa haki za kimtandao ni mtambuka kwani zinaathiri sekta za umma na sekta binafsi.
“ Changamoto kubwa ambayo Afrika tunakutana nayo ni teknolojia kuandaliwa kwingine bila kuzingatia muktadha wa nchi zetu ambapo jamii zetu huwa hazina uwezo wa kufanya maamuzi katika utengenezaji wa teknolojia hiyo na kuishia kuipokea, alisema.
Akichangia mjadala huo, Wakili Philomena Stanslaus alikiri kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa sana kwenye matumizi ya teknolojia ya kidijiti na kutoa mfano wa malipo katika idara nyingi ambapo hufanywa mtandaoni tofauti na miaka iliyopita.
Alisisisiza umuhimu wa wadau kutumia vyombo vya habari ili kuelimisha jamii juu ya matumizi salama ya mitandao na kukwepa taarifa za upotoshaji.
Kwa mjibu wa takwimu za TCRA za mwaka 2021, Tanzania ilikadiriwa kuwa na watumiaji wa intaneti (mtandao) wapatao milioni 29, karibu nusu ya idadi ya watu.