Wednesday, 14 December 2022
RAIS SAMIA ATEUA MAKATIBU WAKUU WA WIZARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Desemba 14, 2022 amefanya uteuzi wa makatibu wakuu wawili wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara (Uwekezaji) na Mambo ya Ndani.
Dkt. Samia amemteua Dk Hashil Twaibu Abdallah kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji ambaye awali alikuwa Naibu Katibu mkuu wizara hiyo kwenye upande wa Viwanda na Biashara nafasi ambayo iliyokuwa wazi.
Rais Samia amemteua Kaspar Mmuya kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ambaye awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu akishughulikia Sera, Bunge na Utaratibu.
Kabla ya Mmuya kuchukua nafasi hiyo, awali Katibu Mkuu wa wizara hiyo alikuwa Christopher Kadio
MWANDISHI WA HABARI NA MPIGA PICHA WA TBC JOACHIM KAPEMBE AFARIKI AKISHUKA MLIMA KILIMANJARO
Mwandishi wa habari na mpiga picha wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mkoani Manyara Joachim Kapembe amefariki dunia alipokuwa akishuka kutoka katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Kapembe pamoja na watendaji wengine wa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari walipanda kwenye mlima Kilimanjaro tarehe 9 mwezi huu kwa ajili uzinduzi wa intaneti ya mwendokasi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Alizaliwa tarehe 26 Februari mwaka 1977 wilayani Muheza mkoani Tanga.
Aliajiriwa na TBC Oktoba Mosi mwaka 2011 kwa cheo cha mpiga picha daraja la II.
Hadi anafariki dunia tarehe 13 mwezi huu alikuwa na cheo cha mpiga picha mkuu daraja la I.
Joachim Kapembe ameacha mke na watoto wawili.
Chanzo - TBC
Tuesday, 13 December 2022
WAGONJWA 25 WA HIMOFILIA KUFANYIWA TOHARA SALAMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,Prof.Mohamed Janab akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 13,2022 Jijini Dar es Salaam. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa wa Damu Muhimbili Dkt.Stella Rwezaula akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 13,2022 Jijini Dar es Salaam.Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Dkt.Victor Mgotta akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 13,2022 Jijini Dar es Salaam.
******************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Kwa mara ya Kwanza,Kambi rasmi maalum ya Tohara Salama kwa wanaume imeanza Disemba 12 mwaka huu hadi Disemba 16, inayotolewa na Hospital ya Taifa Muhimili kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Kenya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 13,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,Prof.Mohamed Janab amesema kuwa kambi hiyo itawahusisha wagonjwa 25 wenye changamoto ya uvujaji wa damu na kwenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wataalamu nane kutoka Hospitali mbalimbali za Tanzania zenye kliniki ya Himofilia.
"Aina ya upasuaji utafanyika kwa njia tofauti na ilivyozoeleka kwani wagonjwa hawa wanahitaji uangalizi wa karibu ili kuepuka athari ya kupoteza damu,pia mgonjwa atahitajika kulazwa kwa muda wa siku tano hadi saba". Amesema Prof.Janab.
Amesema tangu kuanzishwa kwa miradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji huduma kwa wagonjwa wa damu, umefanikiwa kwa kuzindua kliniki ya Himofilia nchini katika hospitali mbalimbali, mafunzo kwa watoa huduma za afya wapatao 548, mafunzo ya nje ya nchi kwa wataalamu saba pamoja na manunuzi ya vifaa vya maabara.
Amemaliza kwa kusema kubwa Hospitali ya Taifa Muhimbili itaendeleza kampeni za aina hiyo ili kuendelea kuboresha huduma na kuzidi kuwajengea uwezo wataalamu.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa wa Damu Muhimbili Dkt.Stella Rwezaula amesema kuwa kuwa zaidi ya watanzania 5800 wana tatizo la haemophinia bila kujua kuwa wanatatizo hilo.
Aidha Dkt.Stella amewashauri watu kuacha imani za kishirikina, wasiende kwa waganga wa kienyeji pale wanapomuona mgonjwa anayetokwa damu puani, au anayetokwa na damu isivyokawaida aking'olewa jino au baada ya kufanyiwa tohara n.k, bali waende kwa wataalamu wa afya ili wapewe matibabu sahihi.
Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Dkt.Victor Mgotta ametoa wito kwa wanaotokwa na damu bila udhibiti wajitokeze kwenye vituo vya afya vya kanda ili waweze kupatiwa matibabu.
Hoemophibia ni ugonjwa wa kutokwa damu bila ukomo, ambapo imeelezwa kuwa asilimia 70 ya wagonjwa hurithi kutoka kizazi hadi kizazi, na asilimia 30 hupata kutokana na mabadiliko ya vinasaba.
WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI YATOA MAFUNZO YA ANWANI ZA MAKAZI KWA WAFANYABIASHARA DODOMA
Na Dotto Kwilasa,DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari imekutana na wafanyabiasha wa Jiji la Dodoma kuwapa mafunzo kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi utakaosaidia kuinua uchumi kidigitali
Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na mtaalamu wa Tehama, Wizara ya ardhi,Nyumba na maendeleo ya makazi Anord Mkude kwenye kikao kazi kati ya Wizara ya habari , mawasiliano na Teknolojia ya habari na wafanyabiasha wa Jiji la Dodoma kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi.
Amesema umuhimu wa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini,Mkude alisema unawezesha mipango na tafiti kufanyika kwa tija, kuongeza vyanzo vya fedha , kuimarisha usalama ,kuwezesha utoaji , upatikanaji na upelekaji wa huduma za bidhaa hadi mahali husika.
Ametaja manufaa mengine kuwa ni kusaidia wawekezaji kufanya maamuzi kabla ya kuamua kufanya uwekezaji na kuwezesha biashara mtandao kufanikiwa hali itakayo inua fursa ya uchumi wa kidigitali.
Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kueleza muundo wa anwani za makazi kwa upande wa vijijini kuwa unahusisha namba ya nyumba au jengo,jengo la kitongoji au shehia na namba maalumu ya postikodi na kwa upande wa Miji,muundo wa anwani za makazi unahusisha namba ya nyumba ,jina la mtaa au barabara,namba ya kata au postikodi.
"Jamii inapaswa kutambua kuwa postikodi ni utaratibu wa kitaalam unaotumika kutenga maeneo ya makazi wakati amwani za makazi ni miundombinu ambayo Kwa Pamoja inatambulisha mahali halisi mtu ama kitu kilipo,aina hii ya utambulisho inaundwa na vitu vikuu vitatu ambavyo ni namba ya anwani,jina la barabara na postikodi,"amefafanua
Mkude amesema,ili kupata tija iliyokusudiwa Katika uanzishwaji wa anwani za makazi na postikodi kila mdau wa maendeleo ana jukumu la kutekeleza kujiwekea miundombinu ya mfumo wa anwani za makazi ikiwa ni pamoja na kutambulisha barabara Kwa kutumia anwani za makazi.
Amesema wananchi pia wanapaswa kuwajibika kutoa na kupokea huduma Kwa kutumia mfumo wa anwani za makazi na kuhakiki taarifa za mfumo huo mara kwa mara .
Kwa upande wake Kaimu Katibu tawala Mkoa wa Dodoma Aloyce Mhogofi amesema kikao kazi hicho ni muhimu kwa kuwa kinalenga kujenga uelewa wa pamoja katika kuhamasisha matumizi ya anwani za makazi na kueleza kuwa wananchi hususani wafanyabiasha wanapaswa kutumia mfumo wa anwani za makazi kuwezesha mafanikio ya kijamii na kiuchumi kufanisi maendeleo Kwa wakati.
Amesema ikiwa wafanyabiasha watatumia mfumo huo utawawezesha kukutana na wateja wengi na kuwanufaisha kiuchumi.
"Kundi hili ni muhimu linapaswa kupewa maelezo,ujuzi,taarifa muhimu Kwa ajili ya kufanikiwa kibiashara ,lazima tuelewe kuwa maendeleo ya biashara yanayegemea zaidi mfanyabiashara anayejitambua na kukubali kwenda na wakati,"amesema.
LIKIZO KWA WATUMISHI WA UMMA NYAKATI ZA SIKUKUU ZISIWE KIKWAZO CHA KUWAHUDUMIA WANANCHI-Mhe. Ndejembi
Na. Veronica E. Mwafisi-Kinondoni
Tarehe 13 Disemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema likizo za mwaka kwa watumishi wa umma katika kipindi cha sikukuu zisiwe kikwazo cha kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Mhe. Ndejembi amesema, likizo ya mwaka ni haki ya mtumishi lakini inatakiwa kuchukuliwa kwa tahadhari hasa katika kipindi cha sikukuu ili isiathiri utoaji wa huduma kwa wananchi wanaofuata huduma katika taasisi za Serikali.
Mhe. Ndejembi amesema watumishi wanapochukua likizo kipindi cha sikukuu, ni vema baadhi wakabaki ofisini ili kuendelea kutoa huduma kama kawaida kwani wananchi wanahitaji huduma nyakati zote za sikukuu na za kawaida.
“Tuhakikishe huduma zinatolewa kama kawaida katika vituo vyetu vya kazi katika kipindi hiki cha Sikukuu kama zinavyotolewa katika siku za kawaida kwani serikali hailali, hufanya kazi wakati wote,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kujitathmini kiutendaji kwa kujiwekea malengo kupitia watumishi binafsi, Idara na Taasisi kwa ujumla katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ili kuunga mkono kwa vitendo Kaulimbiu ya Kazi Iendelee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika wilaya yake.
Bi. Msofe, ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri aliyoyatoa kwa watumishi kwa kushirikiana na wasaidizi wake kuanzia ngazi ya Kata, Mtaa na Halmashauri kwa ujumla.
Naye, Mtumishi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Happyfania Mabala amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa Halmashauri hiyo kwa muda mrefu.
Kadhalika, Bi. Mabala ameushukuru uongozi wa Wilaya yake kwa kuwakaribisha viongozi mbalimbali na kuzungumza nao masuala ya kiutumishi, jambo ambalo linawaongezea ari kubwa katika utendaji kazi wao kupitia utumishi wa umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza ziara ya kikazi jijini Dar es salaam yenye lengo kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam (hawapo pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika Wilaya hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Umma wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Wilaya hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Mhandisi Mitambo wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Hamed Hamdun akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na mtumishi wa Manispaa ya Kinondoni, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Wilaya hiyo. Kulia kwake ni Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe na kushoto kwake ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Hanifa Suleiman akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Manispaa ya Kinondoni kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya ya Kinondoni.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge akitoa salamu za Manispaa ya Kinondoni kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya ya Kinondoni.
BABA ALIYEKWEPA TOHARA KWA MIAKA 44 ATAHIRIWA KWA NGUVU MBELE YA WATOTO MKE AKISIMAMIA SHOO
Mwanamue mwenye umri wa miaka 44, katika kaunti ya Bungoma nchini Kenya, alilazimishwa kukabiliana na kisu cha ngariba mbele ya mkewe na watoto wake watatu baada ya kukwepa kisu hicho kwa miaka kadhaa.
Peter Onyango, mkazi wa Lukhome katika kaunti ndogo ya Kiminini alipelekwa mtoni Jumamosi, Disemba 10,2022 asubuhi, na umati wenye ghadhabu, ambapo alipakwa matope kabla ya kuanikwa mbele ya watu kupashwa tohara.
Mkewe, Janet Musenya, alisema kwa muda wa miaka minane tangu walipooana, mumewe alikuwa akikwepa kisu cha ngariba na hivyo kumlazimu kupanga njama ya kutahirishwa kwake.
“Niligundua kuwa anaogopa maumivu lakini sikuweza kustahimili kuishi naye. Nina furaha kuwa sasa ni mwanaume kamili,” alisema.
Aliahidi kutekeleza majukumu yote ya kumuuguza mumewe hadi atakapopona kidonda cha kupashwa tohara.
Kulingana na jirani wa wanandoa hao, Amos Sikuku alisema kuwa wanandoa hao walikuwa wanagombana na kwa hasira, mkewe Onyango aliropokwa na kuanika siri yao ya muda mrefu. Lakini Onyango alionekana kuwa na ahueni baada ya kukatwa, akisema alikuwa amekejeliwa kwa miaka mingi kwa sababu ya hali yake.
“Ninawaomba wasamaria wema kusaidia familia yangu kwa chakula katika wakati huuu ambao bado nitakuwa nikiuguza jeraha hili kwani siwezi kufanya kazi yoyote ya maana,” akasema baba huyo wa watoto watatu.
Jamaa mwenye wake wawili akamatwa na kulazimishwa kutahiri
Katika tukio sawia na hilo, wenyeji wa mji wa Chwele katika kaunti ya Bungoma wamejionea kioja cha bure, wakati jamaa mmoja mwenye wake wawili alipokamatwa na umati kisha kulazimishwa kukabiliana na kisu cha ngariba.
Inasemekana kuwa ugomvi wa kinyumbani kati ya jamaa huyo na mkewe wa kwanza ndio chanzo cha mwanamke huyo kumripoti mumewe kwa wazee wa jamii ya wabukusu kuwa hajatairiwa, akiifanya njia mojawapo ya kumtia adabu.
MAWAKALA NA WAMILIKI WA MABASI WAONYWA KUPANDISHA NAULI MWISHO WA MWAKA
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomon Mwangamilo
***
Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha kupitia kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, limewaonya baadhi ya mawakala wanaopandisha nauli kiholela kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kuwa halitowafumbia macho wao pamoja na wamiliki wa magari hayo.
Akizungumza hii leo Desemba 13, 2022, katika kituo kikuu cha mabasi yaendeayo mikoani, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomon Mwangamilo, amesema kuwa kwa sasa tiketi zinakatwa kwa mfumo wa kielektroniki ambapo amebainisha kuwa hatopenda kusikia wamiliki na wakala wa mabasi hayo hawafuati utaratibu na maelekezo ya serikali.
Mwangamilo ameleza kuwa endapo atasikia mwananchi analalamika juu ya kupandishiwa nauli hatua kali zitachukuliwa kwa wakala atakayebainika kukiuka maagizo ya serikali pamoja na mliki kushindwa kusimamia watendaji wake.
Nae Yahaya Mbwana ambaye ni dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Singida na Arusha amewataka madereva wenzake kufuata sheria za usalama Barabarani ili kuepusha ajali ambazo chanzo chake ni ukikwaji wa sheria za usalama barabarani.
Nao baadhi ya mawakala wa mabasi yaendayo mikoani wamesema changamoto kubwa kutoka kwa abiria wao ni uelewa mdogo juu ya mfumo mpya na bei elekezi ya serikali ambapo wamesema imekuwa chanzo cha malalamiko kwa abiria.
Chanzo - EATV
JENGENI UADILIFU KWA WANATAALUMA SEKTA YA ARDHI KUEPUKA DHURUMA NA RUSHWA KWA KIZAZI KIJACHO-DKT MABULA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula katikati na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kushoto pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Ardhi Tabora Dkt. Lucy Shule wakiwa katika ya pamoja na Wajumbe wapya wa Bodi ya Chuo cha Ardhi Tabora. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akisoma ujumbe wa jiwe la Msingi mara baada ya kufungua jengo la miadhara kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo cha Ardhi Tabora uku Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi akifuatilia kwa makini. Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi akitoa maneno ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Wiziri Angeline Mabura kuzindua Bodi ya Chuo cha Ardhi Tabora. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Ardhi Tabora Dkt. Lucy Shule jana Mkoani Tabora. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi vitendea kazi Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Ardhi Tabora Bw. Seushi Mburi jana Mkoani Tabora.
********************
Na Anthony Ishengoma
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka Bodi ya Chuo Cha Ardhi Tabora inayosimamia maendeleo ya taaluma Chuoni hapo kuhakikisha mitaala ya Chuo hicho inalenga kutoa elimu sahihi itakayowaandaa wahitimu wake kuwa watumishi waadilifu watakaopiga vita uonevu, migogoro, udanganyifu, dhuruma na rushwa katika Sekta ya ardhi Nchini.
Waziri Mabula amesema hayo jana alipofika Chuo cha Ardhi Tabora kwa lengo la kuzindua Bodi mpya ya Chuo hicho na kuongeza kuwa uadilifu kwa wanafunzi unatakiwa kujengwa kwa wanachuo wanaosomea taaluma ya masuala ya ardhi ili hapo baadae waweze kuwa watumishi waadilifu kwa wananchi ukizingatia ardhi ni sehemu ambayo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini.
Dkt. Mabula ameihakikishia bodi hiyo mpya kuwa kadri itakavyowezekana, Wizara yake itawapa kila aina ya ushirikiano kwa kutoa miongozo na mahitaji yote muhimu kwa wakati kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kukisimamia na kukiendeleza Chuo ili kiweze kuendelea kuleta manufaa nchini.
‘’Kuhusu changamoto zinazokikabili Chuo, Serikali kupitia Wizara yangu inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali kwa kujenga miundombinu mipya na kukarabati iliyokuwepo kulingana na upatikanaji wa fedha’’. Aliongeza Dkt. Angeline Mabula, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Waziri Mabula aliongeza kuwa Ujenzi wa maktaba kubwa ya kisasa inayokaribia kukamilika, ni moja ya utekelezaji wa mipango hiyo na nia thabiti ya Wizara katika kuzikabili changamoto ni kuongeza ufanisi kitaaluma.
Waziri Mabula aliongeza kuwa Wizara itaendelea kuongeza idadi ya watumishi hasa wakufunzi na kuhakikisha pia Chuo kinapatiwa vifaa na mitambo ya kufundishia na kujifunzia ili kiweze kutoa mafunzo yanayokidhi viwango.
‘’Ni ukweli usiopingika kuwa mafunzo yakitolewa kwa viwango vinavyohitajika, tutapata wahitimu wenye ubora katika fani zao utakaowawezesha kufanya kazi kwa kujiamini na kwa ufanisi mkubwa’’. Aliongeza Waziri Mabula.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi aliwaambia wajumbe wapya ya bodi hiyo kuwa moja ya kazi yao ni kuhakikisha wanakiendesha chuo kwa kuzingatia maendeleo ya yaliyopo hususani madiliko ya kidigitali yanayotumika kwasasa duniani.
Dkt. Allan Kijazi aliongeza kuwa kwasasa dunia inaendesha uchumi wake kwa maendeleo ya sayansi na teknlojia hivyo mitaala ya chuo hicho inatakiwa kuangalia upya ili kuendana na maendeleo ya kiteknolojia yaliyopo.
‘’Hatuwezi kuendelea na mipango ileile ya miaka kumi na tano iliyopita hivyo ni lazima tubadilike ili kuendana na mabadiliko yaliyopo kwani muhimu kukivusha chou ili kiendane na uchumi wa kidigitali kwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya utawala wa ardhi yanayoendeshwa kidijitali.’’ Aliongeza Dkt. Allan Kijazi.
Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Ardhi Tabora Dkt. Lucy Shule alihaidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyopo lakini pia kuendeleza mazuri ya Bodi iliyopita ili kuleta mafanikio ambayo yeye na Bodi yake watayapuitia na kuyafanyia kazi.
Chuo cha Ardhi Tabora kinapokea Bodi mpya ya chuo hicho inayundwa na Wajumbe tisa ambayo imeteuliwa hivi karibuni na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabura na imeanza kazi jana baada ya kuzinduliwa na Waziri huyo.
TBS YATOA ELIMU NAMNA YA KUTUMIA ALAMA YA UBORA KWA WAJASIRIAMALI SINGIDA
Meneja Uhusiano na Masoko ( TBS), Bi. Gladness Kaseka akitoa maelezo kuhusu utaratibu wa kupata leseni ya kutumia alama ya ubora ya TBS bila gharama yoyote kwa baadhi ya Wajasiriamali wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
TBS ilitoa elimu hiyo wakati wa kampeni ya elimu kwa Umma kuhusu viwango mkoani Singida.
Mkaguzi (TBS) , Bw. Magesa Mwizarubi akitoa elimu kuhusu utaratibu wa kusajili majengo ya chakula na vipodozi pamoja na umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo katika bidhaa hususani muda wa mwisho wa matumizi kwa wafanyabiashara katika Stendi mpya, Stendi ya zamani na Soko Kuu mkoani Singida. TBS iliwakumbusha wafanyabiashara wa chakula na vipodozi mkoani Singida kufanya usajili wa majengo ili kuepuka usumbufu.