Sunday, 20 February 2022
Saturday, 19 February 2022
AGONGELEWA KWENYE MTI KWA MISUMARI KAMA YESU AKISULUBIWA MADAI YA KUIBA REDIO
Polisi wameanzisha msako mkali ili kumkamata mshukiwa aliyempigilia misumari katika mikono ya mwanaume mmoja mwa madai ya kuiba redio katika Kaunti ya Vihiga nchini Kenya.
Collins Sambaya mwenye umri wa miaka 19 alipatikana mikono yake miwili ikiwa imepigiliwa kwenye mti kwa misumari ya kuezeka paa mfano wa Yesu akisulubiwa.
Sambaya alinusuriwa kwa mashine ya kukata miti huku mshukiwa akikimbilia mafichoni alipowaona polisi wakifika eneo la tukio.
Collins Sambaya aliyedaiwa kuiba redio alipatikana mikono yake yote ikiwa na misumari ya kuezeka paa katika kijiji cha Chemasili, Sabatia, Kaunti ya Vihiga
“Katika kisa ambacho kiliduwaza kijiji cha Izava eneo la Sabatia, Collins Sambaya mwenye umri wa miaka 19 alipatikana mikono yake ikiwa imepigiliwa kwa mti kutumia misumari ya kuezeka,” Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema.
Wakaazi walimuarifu Chifu wa kata ya Izava Kaskaini Evans Endesha ambaye aliwaapa taarifa maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kilingili.
Ripoti zinaarifu kuwa mshukiwa alikimbilia mafichoni baada ya kuwaona maafisa wa polisi wakiwasili eneo la tukio.
“Msako umeanzisha kuwakamata washukiwa waliotekeleza unyama huo. Vikosi vya usalama eneo hilo inatumia kila mbinu kuhakikisha kuwa washukiwa wananaswa,” taarifa hiyo ya DCI iliongeza.
Kwa mujibu wa picha za video, wakaazi chini ya uangalizi wa maafisa wa polisi, walijaribu kumwondoa Sambaya kutoka kwa mti huo kwa kutumia mashine ya kukata miti.
Juhudi zao zilifua dafu, Sambaya akiokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbale kwa matibabu ambako amelazwa akiwa kwa hali nzuri.
“Wanakijiji walipigwa na butwaa kwa kile kilichokuwa kimempata mwenzao walitazama kwa mbali maafisa wa polisi wakimwokoa na kumkimbiza hospitalini,” DCI iliongeza.
Chanzo - Tuko Swahili
MKULIMA ALIYEOKOTA FURUSHI LENYE MAMILIONI YA FEDHA AKITOKA SHAMBANI ARUDISHA KWA MWENYEWE
Nchini Benin, mkulima mtaalamu amepokea tuzo ya heshima kutoka kwa mamlaka ya nchi yake.
Alimrudishia mmiliki wake kiasi cha mamilioni ya fedha zilizokuwa kwenye begi la kusafiria alilolichukua alipokuwa njiani Ijumaa iliyopita alipokuwa akirejea kutoka shambani kwake.
Baraka Amidou ana umri wa miaka 37. Ameoa na baba wa watoto 5. Alipowasiliana na BBC Afrique, alitufanya tuwasiliane na mpwa wake Soule Mohamed Taïrou ili awe mkalimani kwa sababu hazungumzi Kifaransa.
Kuhusu uamuzi wake wa kurejesha fedha hizo, anasema ulichochewa na imani na malezi ya kidini na anasema wala hajutii alichokifanya.
Alitunukiwa cheti cha kutambuliwa na bahasha ya fedha. Kwa mujibu wa mamlaka, ni suala la kumtia moyo na kutambua kitendo chake cha uadilifu.
"Siku hizi tunazidi kushuhudia upotevu wa maadili. Haijapata kutokea kijana ambaye bado ana kila kitu cha kufanya ili kujijenga akafanya kitendo kama hicho. Haya yalitangazwa na Djibril Mama Cissé, Gavana wa Borgou kaskazini mwa Benin.
Aliokota begi alipokuwa akirudi kutoka shambani kwake. Baada ya kusikia kupitia tangazo la mjini kwamba mwenye nyumba alikuwa akitafuta mfuko huo, alienda kuukabidhi kwa chifu wa kijiji chake.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, begi hilo ni la mfanyabiashara aliyefika kununua nafaka mkoani humo.
Amidou Baraka alikataa CFA 100,000 ambayo mmiliki alitaka kumpa ili kumshukuru. Baada ya kusisitiza, hatimaye alikubali kupokea 50,000 FCFA.
Hadithi inayokumbusha ile ya Mliberia Emmanuel Tolué, dereva wa pikipiki ambaye aliokota na kurejesha dola za Marekani 50,000, au zaidi ya faranga za CFA milioni 28.
Rais wa Liberia George Weah alikutana naye katika sherehe katika mji mkuu Monrovia na kumpa pesa na kumsomesha.
Chanzo - BBC Swahili
MWILI WA Dkt. MWELE MALECELA WAAGWA KARIMJEE
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson wameongoza waombolezaji viwanja vya Karimjee kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele katika Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Mwele Malecela aliyefariki nchini Uswizi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwili wa Dk. Mwele umewasili usiku wa kuamkia leo Februari 19, 2022 kutokea Geneva ambako umauti ulimkuta.
Akizungumza wakati wa kutoa salam za pole, Rais Mwinyi amesema; “Kwa muda wote ambao nimemfahamu Dkt. Mwele, kikazi alikuwa ni mtu wa kujituma sana ‘committed and very professional.
“Dkt. Mwele ameitumikia Nchi yake, sisi sote tunapaswa tujiulize endapo tutaweza kufikia yale ambayo ameyafikia na ukiacha upande wa kazi kama mtu alikuwa na utu mkubwa, alikuwa karibu sana na watu alikuwa anapenda kusaidia, amesema Mwinyi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa amesema; “Nimekuja kutoa salamu za Rais
Samia Suluhu ambaye angependa kujumuika hapa kutoa pole amenituma nilete salamu za pole kwa familia kufuatia kifo cha mpendwa wetu Dkt. Mwele, amesema atakaporudi atakuja kukusalimia mzee Malecelam, amesema Majaliwa.
Baada ya kuagwa Karimjee, Mwili wa Dk. Mwele utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Dodoma kwa ajili ya maziko.
WAWILI WAJERUHIWA KWA RADI 'WAKI - CHAT KWA SIMU' MVUA KUBWA IKINYESHA ARUSHA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo
Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishina Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema tukio hilo limetokea Februari 17,2022 saa 9 alasiri na kuwataja waliojeruhiwa na radi hiyo ni Sasines Onarok Babu (25)mkazi wa Ololosokwani na mwingine ni Kishuyan Terya Kiyomi (28) na walikimbizwa katika zahanati ya kijiji cha Ololosokwani na kupatiwa matibabu.
"Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni matumiziya simu wakati mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha na kuambatana na radi ambayo ilipelekea vijana hao kujeruhiwa sehemu mbalimbali ya miili yao na radi hiyo",amesema Kamanda Masejo.
Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na kuchukua tahadhari hasa kipindi cha mvua kubwa ambazo huambatana na radi kali huku akiwataka kuacha mara moja matumizi ya vifaa vya umeme ikiwemo simu wakati wa mvua kwani kwa kufanya hivyo kutawaepusha na madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Friday, 18 February 2022
RC SOPHIA MJEMA AZINDUA RASMI MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI MKOA WA SHINYANGA..AWEKA VIBAO MTAA WA SOKONI NA UHURU ROAD
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (katikati) akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga kwa kuweka Vibao vya Maelekezo ya Mtaa wa Sokoni "Market Street" na Barabara ya Uhuru "Uhuru Road" katika Manispaa ya Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amezindua Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga kwa kuweka Vibao vya Maelekezo ya Mtaa wa Barabara ya Uhuru (Uhuru Road) na Sokoni (Market Street) pamoja na Namba za Majengo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Manispaa ya Shinyanga huku akisisitiza kuwa zoezi hilo linatakiwa likamilike ifikapo mwezi Aprili 2022 katika mitaa yote mkoani Shinyanga.
Uzinduzi wa Mfumo wa Anwani za Makazi unaohusisha uwekaji mabango (vibao) ya maelezo ya mtaa, uwekaji namba kwenye nyumba na taarifa za ndani ya nyumba umefanyika leo Ijumaa Februari 18,2022 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya Mkoa na Halmashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga likishuhudiwa na wananchi Mjini Shinyanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Mjema amesema uzinduzi wa Mtaa wa Sokoni katika Manispaa ya Shinyanga unawakilisha mitaa yote katika mkoa wa Shinyanga akibainisha kuwa mfumo wa Anuani za Makazi utasaidia kuwatambua wananchi hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali katika jamii.
“Zoezi hili la kutambua makazi linatakiwa likamilike hadi ifikapo mwezi Aprili mwaka huu. Anuani za Makazi utasaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Mwaka huu zoezi la Sensa litafanyika kikamilifu kwani itakuwa ni Sensa ya Watu na Makazi. Hii itakuwa tofauti na miaka ya nyuma kidogo ambapo tumekuwa na Sensa ya watu pekee bila makazi yao. Anuani za Makazi zitarahisisha zoezi hili kwani Sensa itahusisha kujua idadi ya wakazi, nyumba zao na kutambua mitaa yao”,amesema Mjema.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko amewataka wananchi kutunza alama hizo za utambuzi wa makazi kwani zitasaidia kurahisisha kutambua mitaa na nyumba za wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (katikati) akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga kwa kuweka Vibao vya Maelekezo ya Mtaa wa Sokoni "Market Street" na Barabara ya Uhuru "Uhuru Road" katika Manispaa ya Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (katikati aliyevaa kiremba) baada ya kuzindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga kwa kuweka Vibao vya Maelekezo ya Mtaa wa Sokoni "Market Street" na Barabara ya Uhuru "Uhuru Road" katika Manispaa ya Shinyanga.
Muonekano wa Maandishi ya upande wa pili wa Vibao vya Maelekezo ya Mtaa wa Sokoni "Market Street" na Barabara ya Uhuru "Uhuru Road" katika Manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema akizungumza wakati akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema akizungumza wakati akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema akizungumza wakati akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema akizungumza wakati akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Kaimu Meneja TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Ibrahim Kiyungu akizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema kuzindua Namba 28 ya Jengo la TANESCO wakati akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Namba 28 ya Jengo la TANESCO
Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Pendolake Msangi akizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema kuzindua Namba 32 ya Jengo la TANESCO wakati akizindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko akizungumza baada ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema kuzindua rasmi Mfumo wa Anwani za Makazi mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Februari 18,2022.
Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
MAJAMBAZI WAVAMIA MABASI YA SHULE,WAJERUHI WANAFUNZI NA WALIMU KWA RISASI, WAUA DEREVA
Basi la shule
Dereva wa basi la shule ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya majambazi kuvamia msafara wa mabasi matatu huko Marakwet katika eneo la Kerio Valley nchini Kenya.
Kulingana na komanda wa polisi kaunti ya Elgeyo Marakwet, baadhi ya wanafunzi na walimu walipelekwa katika hospitali za karibu kupata matibabu huku ikihofiwa kwamba huenda kuna walio katika hali mahututi.
Inasemekana kwamba walimu na wanafunzi walikuwa wanarejea shuleni baada ya kuhudhuria tukio la kitaaluma.
Kulingana na waliofika kuwaokoa, wavamizi hao walimiminia risasi dereva aliyeaga dunia papo hapo kabla ya kuanza kurusha risasi dhidi ya walimu na wanafunzi.
Hata hivyo Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen ameonekana kuwashutumu Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai
Waziri wa Mambo ya ndani Fred Matiangi anasema dereva na mwalimu mkuu wamekamatwaImage caption: Waziri wa Mambo ya ndani Fred Matiangi (pichani) anasema dereva na mwalimu mkuu wamekamatwa
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i, ameagiza kukamatwa kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo mara moja.
Akizungumza katika tulio kuhusu elimu na washika dau wengine, Matiang'i amelaumu utawala wa shule kwa kukiuka sheria zilizowekwa na serikali kuhusu utumiaji wa mabasi ya shule.
Matiang'i ameeleza kuwa serikali iliweka sheria ya kukataza mabasi ya shule kutumika baada ya saa kumi na mbili unusu jioni.
Bunge lashauri Daraja la Tanzanite liwe la kulipia
Bunge la Tanzania limeishauri Serikali kuangalia uwezekano wa Daraja la Tanzanite, kuwa la kulipia (Toll Bridge) ili isaidie kurejesha fedha za mkopo zilizotumiwa kujenga daraja hilo, kama ambavyo inafanyika kwa Daraja la Kigamboni.
Daraja la Tanzanite jijini Dar es Salaam lenye urefu 1.03km na barabara unganishi 5.2km limejengwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 107.4 (Shilingi bilioni 243.8).
Fedha za ujenzi wa daraja hilo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Serikali ya Tanzania.
Daraja hilo ambalo pamoja na kurahisisha usafiri na usafirishaji na kutumika kama kivutio cha utalii linatarajiwa kudumu kwa muda wa miaka 100.
Hata hivyo, wakati Bunge likipitisha ushauri huo, Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile amesema wananchi wamemtuma kuwasilisha serikalini kilio chao wakiomba kuondolewa tozo kwenye Daraja la Kigamboni.
NEMC YAAGIZA HALMASHAURI YA MJI WA KIBAHA KUFANYA TATHMINI ATHARI ZA KIMAZINGIRA BONDE LA RUVU
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) limeiagiza Halmashauri ya Mji wa Kibaha kufanya tathimini ya athari za kimazingira katika bonde la Ruvu kwa lengo la kuepusha athari zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu katika eneo hilo zikiwemo za ujenzi.
Aidha NEMC imeendelea kuwasisitiza wakuu wa mikoa yote nchini, kuendelea kusimamia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango waliotoa agizo la kulindwa mazingira katika maeneo yao yakiwemo ya vyanzo vya maji kwa ajili ya kuepusha athari zinazoweza kusababishwa kutokana na kukauka kwake.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo Dk. Samuel Gwamaka aliyasema hayo mara baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ya bonde kwa lengo la kujionea hali halisi ya uhifadhi sambamba na kufanya tathimini ya baadhi ya maeneo ambayo halmashauri ya Mji wa Kibaha ilikusudia kufanya ujenzi wa shule.
"Nimekagua maeneo mbalimbali ya bonde hili na kubaini kuwa kuna athari nyingi za uharibifu wa kimazingira, sote tunatambua kuwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani mategemeo yao wote ya maji ni kutoka katika bonde hivyo tunapaswa kulitunza kwa nguvu zote", alisema Dk. Gwamaka.
Alisema changamoto inayojitokeza kwa Halmashauri ya Kibaha ni kuyachagua maeneo ni oevu ambayo pia ni vyanzo kwa ajili ya kujenga shule hizo, jambo ambalo kimsingi Mkurugenzi huyo alisema haliwezekani na Halmashauri hiyo inafapaswa kufanya tathimin upya.
"Wote tunajua kuwa maji yanatoka katika milima hasa kipindi cha mvua, sehemu ambayo ni hifadhi yake hata kama kuna mafuriko ni maeneo kama haya ambayo kama yasipotunzwa athari zake ni kubwa kubwa changamoto inayojitokeza ni msukumo wa maendeleo kama ilivyo kwa Kibaha ambayo inataka kujenga shule ndani hayo jambo ambalo ni hatari kwa mazingira haya" alisisitiza Dk. Gwamaka
Alisema hata jengo la Halmashauri ya Mji huo limejengwa katika eneo Oevu hali iliyolifanya likabiliwa na changamoto katika mifumo yake ya maji taka huku akisisitiza kwa wadau wote wakiwemo wawekezaji kusubiri ripoti ya athari za kimazingira katika eneo hilo kabla ya kufanya ujenzi wowote.
Mbali na hilo Mkurugenzi huyo alisema pia ujenzi wa kituo cha kuuzia mafuta katika eneo jirani na kambi ya JKT Ruvu unapaswa kusitishwa kwa kuwa utaathiri vyanzo vya maji kutokana na matangi yatakayowekwa ardhini ambayo yanaweza kusababisha mafuta kuvuja na hivyo kuathiri vyanzo vya maji.
Aliwataka wadau wote wa kimaendeleo kusubiri ripoti ya tathimini ya kimkakati inayofanyiwa kazi na Ofisi ya Rais ambayo itatoa majibu kuwa kama eneo hilo linafaa kwa ujenzi wa makazi au viwanda katika bonde hilo la Ruvu.
Awali Afisa Mazingira wa Halmashauri wa Mji wa Kibaha Maximilian Mtobu alisema wao kama taasisi ya Serikali wameupokea maagizo ya NEMC kwa umakini mkubwa kwa kuwa ndiyo taasisi inayotambua athari za kimazingira nchini yakiwemo maeneo ambayo walikusudia kufanya ujenzi huo
Alisema baada ya tathimini iliyofanywa na Baraza hilo ambayo imepinga ujenzi wa shule katika maeneo waliyokuwa wamekuusudia, watakaa na kujadili ili kuangalia ni wapi watafanya ujenzi huo ili pamoja na mambo mengine kuufanya ujenzi huo kuwa wa kudumu na wenye manufaa kwa Taifa.
WAJANE WA FAMILIA MOJA WAKABIDHIWA NYUMBA, SHILOLE, GLADY WAFUNGUKA “INAUMIZA”
Taasisi ya Glady Welfare imekabidhi Nyumba kwa Wajane watatu waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya makazi, Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Katika hafla hiyo, ambayo geni rasmi ni Mwanamuziki na Mfanyabiashara, Shilole maarufu kama Shishi Baby/ Shishi Food amezindua na kuwakabidhi nyumba Wajane hao ambao awali walikuwa wakiishi katika Kibanda cha Udongo akiwemo mmoja ambaye ni Mlemavu wa Macho.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Bi.Gladness Lyamuya amesema nyumba hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Original East na michango ya Watu mbalimbali kupitia mitandao baada ya kuona ugumu wa maisha unaowakabili wajane hao, ambao wote ni ndugu.
Amesema kuwa mbali ya kukabidhi nyumba hiyo, pia wametoa kiasi cha Shilingi Milioni 1 kama mtaji wa kibiashara.
“Huu ni muendelezo wa kusaidia, kama Taasisi hatuwezi kuwaacha hivi hivi lazima tuwape na mtaji, msaada huu tumeutoa kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali kupitia Instagram na Shirika la Original East ,” amesema Mkurugenzi Glady.