Thursday, 17 February 2022
KIWANDA CHA MARMO CHA MKOANI MBEYA CHATOA WITO KWA TAASISI ZA UJENZI KUNUNUA BIDHAA ZAKE
Tuesday, 15 February 2022
GWAJIMA AZITAKA KAMATI ZA ULINZI WA WANAWAKE NA WATOTO NGAZI YA MKOA KUANDAA MIKAKATI MADHUBUTI KUTOKOMEZA UKATILI NCHINI
WATATU WAKAMATWA WAKIUZA PEMBEJEO ZA SERIKALI
Viuatilifu vya zao la pamba
Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
WAFANYABIASHARA watatu wilayani Maswa mkoani Simiyu wamekamatwa kwa kosa la kujihusisha na uuzaji wa viuatilifu vya zao la pamba vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya wakulima wa pamba.
Akizungumza jana na waandishi wa Habari, Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa halmashauri ya wilayani humo, Robert Urasa alisema kukamatwa kwa wafanyabiashara hao kunatokana na msako kwa wanaouza pembejeo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo mnadani.
Aliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni Samson Sikambundwa, Paschal Siwingwa na Mashaka Daudi wakazi wa Maswa na wamekamatwa na Maafisa wa kilimo wakiuza dawa za kuulia wadudu kwenye zao la pamba zilizotolewa na serikali kupitia bodi ya pamba nchini kinyume cha sheria na taratibu.
Alisema wamekuwa wakipokea malalamiko mengi ya kuwepo kwa viuawadudu vilivyotolewa na serikali ikiwa ni mkopo kwa wakulima wa pamba, lakini vimekuwa vikiuzwa kwenye maeneo ya minada kutoka kwa wakulima na viongozi wasio waaminifu.
‘’Tumeamua kufanya msako kwa watu wote kwenye maduka yanayouza pembejeo pamoja na minadani…kuna baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walipatiwa viuadudu ili vitumike kunyunyuzia mashamba katika musimu wa kilimo 2021/22, lakini wanaviuza tutawakamata wote’’, alionya Urasa.
Alisema kuwa kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao ni Uhujumu Uchumi na watahakikisha mtandao mzima walioshirikiana kuhujumu viuadudu hivyo wanakatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Urasa alisema baada ya kupata taarifa kuwepo kwa viuadudu hivyo katika mnada wa Maswa Mjini walifanya upekuzi kwenye maeneo ya wafanyabiashara hao na kukamata Hekapaki 230 zenye thamani ya shilingi 917,800/= zilizokuwa na nembo ya Bodi ya Pamba Tanzania(TCB) zikiuzwa kinyume na utaratibu.
Alitaja thamani ya viuadudu vilivyokamatwa kwa kila mfanyabiashara kwenye mabano, Samson Sikambundwa (Sh 132,000), Paschal Siwingwa (Sh 49,000) na Mashaka Daud (Sh 736,800).
Alisema wafanyabiashara hao wamefikishwa kituo cha Polisi wilaya ya Maswa na wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili mara baada taratibu za jeshi la polisi kukamilika.
Aliongeza kuwa zoezi hilo ni endelevu na hawatovumilia kuona upotevu wa fedha za serikali pia waliwataka wafanyabiashara wote kuacha tabia hiyo vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika na biashara hiyo Haramu.
Naye Mkaguzi wa Bodi ya Pamba, Ally Mabrouck alisema amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wakulima waliopewa viuadudu hivyo na viongozi waliopewa jukumu la kugawa viuadudu kuviuza kwa wafanyabiashara wakati vimetolewa na serikali kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kwa kiasi hicho cha viuadudu kilichokamatwa kitasababisha hekta 230 za zao la pamba kutonyunyiziwa dawa na hivyo kusababisha wilaya hiyo kutofikia malengo yake ya kuzalisha pamba tani 130,000 kama ilivyotarajia.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge baada ya kupokea taarifa hiyo alisema ameona pembejeo zilizokamatwa ambazo ni ruzuku ya serikali zinazotakiwa kwenda kwa wakulima moja kwa moja.
"Kuna kodi ya wananchi ilipelekwa wilayani humo ili kuinua sekta ya kilimo ya zao la pamba, lakini baadhi ya watu wasio na uzalendo wameamua kuzifanyia biashara pembejeo hizo hivyo ni lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watu wote watakaobainika kuhujumu viuadudu hivyo’’ ,alisema Kaminyoge.
BoT YAELEZEA BAADHI YA MAJUKUMU YA KURUGENZI YA MASOKO YA FEDHA
Fidelis Mkatte Mchambuzi wa Masuala ya Fedha Katika Benki Kuu ya Tanzania BoT wakati akitoa mada kwa waandishi waandamizi na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini katika semina inayofanyika kwa siku 5 kwenye Tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
Bi. Vick Msina Kaimu Meneja wa Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akifafanua jambo kabla ya kuanza majadiliano mara baada ya wasilisho la mada kwa waandishi waandamizi na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini katika semina inayofanyika kwa siku 5 kwenye Tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
.......................................
Majukumu ya Kurugenzi ya Masoko ya Fedha katika Benki Kuu ya Tanzania BoT ni Kusimamia na kuendesha soko la dhamana za serikali ambapo Kurugenzi huendesha minada ya Dhamana za Serikali ili Kudhibiti ujazi wa fedha unaosababisha mfumuko wa bei na kuainisha mwelekeo wa riba katika soko la fedha.
Hayo yameelezwa leo na Fidelis Mkatte Mchambuzi wa Masuala ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati akitoa mada kwa waandishi waandamizi na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini katika semina inayofanyika kwa siku 5 kwenye Tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
Amesema majukumu mengine ya kurugenzi hiyo ni kuiwezesha serikali kukopa kwa ajili ya shughuli mbali mbali za maendeleo ili kuziba nakisi ya bajeti ya matumizi ya kawaida ya serikali katika utendaji wa majukumu yake ya utekelezaji wa maendeleo na shughuli za kawaida za serikali.
Sambamba na hilo, Kurugenzi hiyo ni msimamizi wa Soko la Ndani la Fedha - Inter-bank Cash Market (IBCM). Pamoja na usimamizi wa minada, Kurugenzi husimamia pia soko la jumla la fedha za kigeni (Interbank Foreign Exchange Market (IFEM)..
"Jambo lingine kubwa ni kutekeleza sera ya uangalizi wa thamani ya shilingi na Kuleta utulivu katika soko (Orderly Market) ambapo pia Benki Kuu hushiriki katika soko hilo sambamba na benki za biashara ili kuimarisha na kuilinda thamani ya shilingi yetu na Usimamizi wa Akiba ya Fedha za Kigeni," Amesema Fidelis Mkatte.
Aidha amebainisha kuwa Kurugenzi pia inawajibika kusimamia akiba ya fedha za kigeni kwa mujibu wa sera ya fedha za kigeni na sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kuhakikisha kuwa kuna kiasi cha kutosha ikiwa ni pamoja na kuiwezesha serikali kulipia kwa wakati mahitaji mbali mbali kama vile Deni la taifa
Ameongeza kuwa kazi nyingine ya Kurugenzi hiyoni kuwekeza katika taasisi salama na kwenye amana zilizo salama ili kulinda thamani na usalama wa akiba yenyewe (“Capital preservation”), Usimamizi wa Akiba ya Fedha za Kigeni na utunzaji na Uwekezaji wa Fedha za Kigeni Nchi za Nje
Ameongeza kuwa Benki Kuu ndiyo yenye dhamana ya kutunza hazina ya fedha za kigeni za nchi kwa niaba ya Serikali kwa kuziwekeza katika mabenki na taasisi mbalimbali za fedha nje kwa faida. ambapo Benki Kuu ina Sera na Mwongozo (“Reserve Management Policy and Guidelines”) zinatoa mwongozo wa utunzaji wa fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na Usimamizi wa Akiba ya Fedha za Kigeni, Utunzaji na Uwekezaji wa Fedha za Kigeni Nchi za Nje.
Amefafanua kuwa jukumu lingine ni uamuzi wa wapi pa kuwekeza au taasisi gani ya kuwekeza ambapo Benki Kuu huzingatia zaidi usalama wa fedha hizo za kigeni sambamba na jukumu hilo, Benki Kuu hutumia hazina hiyo ya fedha kufanya malipo mbalimbali ya nje kutokana na majukumu mbalimbali yanayoikabili Serikali.
Bi. Vick Msina Kaimu Meneja wa Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania BoT akifafanua jambo kabla ya kuanza majadiliano mara baada ya wasilisho la mada kwa waandishi waandamizi na wahariri wa vyombo mbalimbali nchini katika semina inayofanyika kwa siku 5 kwenye Tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mada kuhusu Majukumu ya Kurugenzi ya Masoko ya Fedha katika semina ya waandishi wa habari inayofanyika katika tawi la (BoT) jijini Mbeya.