Friday, 3 December 2021

SAID MNDEME ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA MRADI WA NYUMBA ZA NZUGUNI NA KISASA ZINAZOJENGWA NA TBA


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme,akimsikiliza Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 Nzuguni Jijini Dodoma,Fedrick Jackson akitoa ya mchoro wa ramani ya nyumba zote zitakapokamilika mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba hizo leo Desemba 3,2021 jijini Dodoma.


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme,akikagua ujenzi wa nyumba 3500 zilizopo Nzuguni Jijini Dodoma.


Mafundi wakiendelea na ujenzi wa nyumba 3500 zilizopo Nzuguni Jijini Dodoma u


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme,akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 zilizopo Nzuguni Jijini Dodoma mara baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi huo leo Desemba 3,2021 jijini Dodoma.


Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 Nzuguni ,Fedrick Jackson,akielezea jinsi walivyojipanga kukamilisha kwa wakati wa ujenzi wa nyumba hizo .


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme,akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Uzalishaji Kiwanda cha Kuzalishaji zege na tofali Mhandisi Athu Chulla mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba 3500 Nzuguni leo Desemba 3,2021 jijini Dodoma.


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme,akitoa maelekezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa nyumba 20 za viongozi Mhandisi Imabaraka Shedafa mara baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi huo leo Desemba 3,2021 jijini Dodoma.


Muonekano wa nyumba 20 za viongozi zilizofanyiwa maboresho ya TBA zilizopo Kisasa jijini Dodoma.


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme,akizungumza na wanadishi wa habari mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba 3500 Nzuguni na nyumba 20 za viongozi Kisasa leo Desemba 3,2021 jijini Dodoma.


Msimamizi wa Mradi wa Ukarabati Q.S Juliana Zegera,akizungumzia jinsi wanavyotekeleza miradi katika mikoa mbalimbali nchini.

.............................................................................

Na.Alex Sonna,Dodoma

KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Said Mndeme ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa nyumba 3500 na nyumba 20 za viongozi zinazojengwa Jijini Dodoma na Wakala huo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Desemba 3,2021 Jijini Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba hizo,Kaimu Mkurugenzi huyo ameridhishwa na jinsi Wakala huo ulivyojipanga kutekeleza miradi hiyo kwa kuwa na vifaa vya kutosha na vya uhakika.

“Tumeridhika kwa jinsi ambavyo wamejipanga tuna Cementi ya kutosha nondo za kutosha haya ni maono ya wakala,hatuna sababu ya kuwa na vikwazo vyovyote binafsi nimeridhika na nimefurahi katika kuhakikisha tunapunguza gharama na ubora unakuwa mzuri mashine ya kisasa ya kuchakata zege.

“Tumeona Kiwanda kingine cha uzalishaji wa tofali hii itatisaidia tofali zenye ubora tumeambiwa kiwanda kinauwezo wa kuzalisha tofali 6000,”amesema.

Amesema mradi wa Nzuguni unaenda kwa kasi ambapo zitajengwa nyumba 3500 ambapo amedai awamu ya kwanza zinajengwa nyumba 150 na kwamba nyumba 86 zimeanza kujengwa.

“Nyumba hizi 3500 zitakuwa ni za kisasa kutakuwa na ujenzi maghorofa 100 na nyumba kubwa 200 na nyumba za saizi ya kati 1400, maghorofa yatakuwa nyumba tofauti tofauti 800 na za size za chini nyumba 1000.

Aidha,amesema katika eneo hilo kutakuwa na huduma za kijamii ambapo kutajengwa shule za awali tano,nyumba za ibada misikiti na makanisa,Soko na kituo cha biashara.

Kuhusiana na nyumba 20 za viongozi katika eneo la Kisasa Jijini Dodoma,Bw.Mndeme amesema zimeboreshwa na kuongezewa ubunifu ikiwa ni pamoja na vyumba vyote vitakuwa na vyoo vya ndani .

“Lakini tumeona jitihada kubwa ambazo zimefanyika nyumba hizi zinajengwa katika nyumba 300 katika eneo la Kisasa lakini nyumba hizi sasa hivi zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa Kwanza nyumba hizi muonekano ni tofauti na zile nyumba 300 ambazo zilijengwa za sasa hivi kila chumba kina choo,”amesema.

Kwa upande wake,Kaimu Meneja Maendeleo ya Miliki TBA,Suzan Ulula amesema wanaamini watafikia malengo ambayo wamejiwekea ikiwa ni pamoja na kukamilisha kwa wakati ujenzi wa nyumba hizo.

“Baada ya kutembelea Nzuguni na Kisasa tunaamini tutafikia malengo wakala ambayo imeyaweka kwa watumishi wa Serikali.Kwa mkoa wa Dodoma tunamaeneo mengine Iyumbu na katika Mikoa mbalimbali Arusha na Dar tunategemea tutaendelea na sehemu zingine,”amesema.

Naye,Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 Nzuguni Jijini Dodoma,Fedrick Jackson amesema ujenzi huo ulianza Oktoba 25,2021 ambapo amedai matarajio ni kwa nyumba zote 150 ziwe zimekamilika Septemba 30 mwakani.

“Kwa matarajio ya miezi mitatu mitatu kwa nyumba 50 lakini tunajaribu kukimbizana ili tuzikamilishe nyingi kwa wakati mmoja hizi nyumba 86 ambazo tumeanza nazo mwezi wa tatu mwishoni kuelekea wanne mwanzoni tunatakiwa tuwe tumeishazimaliza.

“Lakini wakati huo zile nyumba 64 ambazo zitatutimizia nyumba 150 zinatakiwa ziwe mpaka mwezi wa sita ziwe zimekamilika.Hapa kila kitu kimepimwa maabara na namna ujenzi unavyokuwa tunasimamia na kupitia mara kwa mara kwa maana kile cha maabara tunakipeleka kupimwa,”amesema.
Share:

NHC YATAKIWA KUTIMIZA AHADI RORYA


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dakt. Angelina Mabula akioneshwa ramani ya eneo la Saro plot na 400 wilayani Rorya mkoa wa Mara wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo jana. Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Musoma Eliasa Keenja akimweleza jambo Naibu Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na ujumbe wake katika eneo la Saro plot no 400 wilayani Rorya alipokuwa katika ziara ya siku moja mkoa wa Mara.

*************************

Na Mwandishi Maalum, RORYA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dakta. Angelina Mabula (Mbunge), amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha katika mwaka ujao wa fedha linaanza kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa nyumba za makazi ishirini (20) katika eneo la Saro plot no 400 Wilayani Rorya Mkoani Tarime.

Dk. Mabula ameyasema jana katika kikao chake na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na Ofisi ya Kamishina wa Ardhi mkoa wa Mara.

Alisema kuwa, NHC ilitoa ahadi ya kujenga nyumba za makazi 20 katika eneo la Saro kwa ajili ya kupangishwa kwa watumishi wa Halmashauri na wananchi wengine, eneo liko tayari kwa ajili ya ujenzi huo na mahitaji ya nyumba ni makubwa sana.

“Nawaagiza NHC kuhakikisha katika kipindi kijacho cha mwaka wa fedha 2022/2023 mnaanza kutimiza ahadi yenu ya ujenzi wa nyumba hizo katika eneo hilo, kwani kiwanja tayari kipo na mahitaji ya nyumba ni makubwa kwani watumishi wa Halmshauri wanatoka maeneo ya mbali sana” Amesema Dk. Mabula

Aliongeza kwa kusema kuwa, kama NHC inashindwa kutimiza ahadi yake hiyo, basi fursa itolewe kwa taasisi zingine au makampuni ya ujenzi ambayo yatakuwa tayari kujenga nyumba hizo ambazo zitasaidia kupunguza adha ya makazi wanayoipata watendaji wa Halamashauri hiyo na kwa wananchi wengine ambao watahitaji kupanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Mahusiano NHC Muungano Saguya alisema kuwa, Shirika bado lina dhamira ya dhati kujenga nyumba 20 za makazi katika eneo la Saro kwa ajili ya kupunguza uhitaji wa makazi kwa watendaji wa Halmashauri, hivyo ahadi hiyo itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.

“Ni kweli NHC ilitoa ahadi ya ujenzi wa nyumba hizo na bado ahadi hiyo ipo, nikuahidi Mkuu wa Wilaya na watendaji wa Halmshauri muwe na subira, kwani Shirika haliwezi kuacha kuchangamkia fursa hiyo adhimu yenye lengo la kuisaidia Serikali kuhakikisha watendaji wake wanapata makazi bora” Amesema Saguya.

Kwa mujibu wa Saguya, NHC katika Mkoa wa Mara imejenga jengo kubwa na zuri la biashara la Mukendo Plaza katikati ya mji wa Musoma kwa ajili kupangisha lakini pia zimejengwa nyumba za makazi 50 eneo la Buhare ambazo zimepangishwa hivyo bado Shirika linaendelea na uwekezaji katika Mkoa wa Mara na mipango iliyopo ni kujenga jengo kubwa na biashara katika mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la Kirongwe.
Share:

SHUGHULI ZA KIBINADAMU ZIENDANE NA UHIFADHI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA - DKT.GWAMAKA

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC akiongea na vyombo vya habari kwenye mapango ya Amboni Jijini Tanga kufuatia mgogoro baina ya wachimbaji wa madini wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini karibu na mapango hayo na mamlaka ya uhifadhi ya Ngorongoro inayohifadhi mapango hayo.

Sehemu ya mapango ya Amboni ambayo yanahifadhiwa na mamlaka ya Ngorongoro.

Sehemu ya Maafisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, waandishi wa habari pamoja na Maafisa kutoka mamlaka ya Ngorongoro wakiwa kwenye mapango ya Amboni.

******

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC amesema shughuli za kibinadamu ni muhimu kufanyika kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji wa mazingira ili kuepuka madhara ya uharibifu wa mazingira yasijitokeze katika Taifa letu.

Dkt. Gwamaka ameyasema hayo alipofanya ziara katika hifadhi ya mapango ya Amboni Jijini Tanga alipokwenda kukagua uhifadhi wa mazingira katika mapango hayo.

"Kuna shughuli za uchimbaji wa madini kwa kutumia baruti karibu na mapango haya zinazopelekea mitetemo ambayo inasababisha kuleta nyufa zinazoruhusu maji kujaa kwenye mapango haya.

Dkt. Gwamaka ameongeza kuwa shughuli za uchimbaji wa madini karibu na mapango ya Amboni zinapingana na uhifadhi wa mazingira, lakini pamoja na hayo Waakazi wa eneo hilo wameshiriki kuyahifadhi mapango hayo kwakuwa wapo hapo toka mwaka 1934 hivyo NEMC itashirikiana na mamlaka husika yaani watu wa madini, mamlaka ya Ngorongoro na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga ili kupata suluhu ya tatizo hili mapema kabla mapango hayo hayajapotea lakini wakati huo huo na Wananchi wapate haki yao ya kuyahifadhi kwa muda wote huo.

Naye Bw. Thobias Mwesiga Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka NEMC amesema milipuko inayosababishwa na uchimbaji wa madini karibu na mapango ya Pangani ina athari kubwa kwasababu inaweza kusababisha nyufa kwenye mapango hatimaye yanaweza kupoteza uhalisia wake.

Bw. Mwesiga amesema ni muhimu kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kwani itasaidia kuepuka uharibifu wa mazingira.

Naye Bi. Luhuvilo Mwamila Mhandisi Muandamizi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Kanda ya Mashariki Kaskazini NEMC amesema ingawa mapango yamekuta kijiji lakini kuna umuhimu wa kuangalia athari za kimazingira zinazoweza kusababishwa na shughuli za wachimbaji wadogo wa madini wanaotumia milipuko karibu na mapango.

B. Luhuvilo ameongeza kwa kushauri kuwa mamlaka za madini (waliotoa leseni za uchimbaji), NEMC na Hifadhi ya Ngorongoro zikae pamoja pamoja kutatua changamoto hii.
Share:

RAIS SAMIA ASHUSHA NEEMA SEKTA YA ELIMU NCHINI, MWELI AWEKA WAZI MAMBO YALIVYO


**************************

NA NTEGHENJWA HOSSEAH-OR TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (anayeshughulikia Elimu), Gerald Mweli amesema, zaidi ya shilingi Bilioni 500 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili kuboresha Elimumsingi nchini.

Mheshimiwa Mweli ameyasema hayo leo Desemba 3,2021 katika ziara yake wilayani Kongwa mkaoni Dodoma.

"Fedha shilingi bilioni 304 kupitia mpango wa mapambano na ustawi wa jamii dhidi ya Uviko-19 zimepokewa ambapo Shilingi Bilioni 240 zinajenga vyumba vya madarasa 12,000

"Shilingi Bilioni 60 zinajenga vyumba vya madarasa 3,000 kwenye vituo shikizi 907 na Shilingi Bilioni 4 zinajenga mabweni 50 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum,"amesema Naibu Katibu Mkuu huyo anayeshughulikia Elimu.

Pia amesema, kupitia Programu ya GPE – LANES II na EP4R - Shilingi Bilioni 113 zimetolewa kujenga miundombinu ya shule za msingi na sekondari nchini.

"Kupitia programu hizo, ujenzi wa shule mpya za msingi 19 na sekondari 15 unafanyika kwa gharama ya shilingi Bilioni 21.25

"Fedha za tozo ya mawasiliano Shilingi bilioni 7 zimepelekwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya madarasa 560 ya shule za sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ili kuunga mkono jitihada hizo.

"Vile vile fedha shilingi Bilioni 8.5 zimepokelewa kwa ajili kuzuia maambukizi na athari za UVIKO-19 zinajenga miundombinu ya kunawia mikono,"amebainisha Mheshimiwa Mweli.

Pia ameongeza kuwa, kupitia Mradi wa Kuinua Ubora wa Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP) fedha shilingi Bilioni 130.5 zimetolewa kwa ajili ya kujenga shule 214 za sekondari za kata na shule 10 za wasichana za mikoa (shule moja kila mkoa) na hii ni katika mwaka huu wa fedha wa 2021/22.
Share:

VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA WATAKIWA KUTAFUTA MASOKO

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma

Mrajis Msaidizi Robert Nsuza akieleza baadhi ya masuala muhimu ya kuzingatia katika utafutaji wa fursa za masoko wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Victoria Michael akichangia mada wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Bw. Bakari Hussein Kassia Kaimu Meneja Mkuu wa Mradi wa Pamoja wa Vyama vya Vikuu vya Tumbaku (T.C.J.E) akiongea kwa niaba ya Viongozi wa Ushirika waliokuwa wakipata mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege (hayupo pichani) wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma

....................................................................

Na.Alex Sonna,Dodoma

Viongozi wa Vyama vya Ushirika wametakiwa kutafuta masoko ya mazao mbalimbali yanayozalishwa kwenye maeneo yao kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata uhakika wa masoko yenye tija kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akizungumza wakati wa mafunzo ya Masoko na Biashara kwa viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Novemba 3 Desemba 2021, Jijini Dodoma amewataka Viongozi hao kutafuta fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Dkt. Ndiege amesema Viongozi wa Vyama vya Ushirika wana wajibu wa kuwasaidia wakulima katika kutafuta fursa za masoko ya mazao yao ambapo amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia Wakulima kuendelea kupata bei zenye ushindani. Ameongeza kuwa hivi sasa ni wakati kwa viongozi kushirikiana na wadau kuongeza thamani ya mazao kupitia uchakataji na uwekezaji wa viwanda ili kupanua wigo wa masoko.

“Ni wakati sasa kwa viongozi kuhakikisha mnatumia fursa mbalimbali za kujitangaza, kushirikiana na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili Wakulima wetu wapate masoko ya bidhaa zao na tusiishie kuuza bidhaa ghafi bali tujielekeze kwenye bidhaa zilizoongezwa thamani,” alisema Mrajis

Akiongea katika mafunzo hayo Mrajis amesema mafunzo hayo ya biashara na masoko yanalenga kuwaongezea uwezo viongozi na Maafisa masoko wa Vyama vya Ushirika kupanua wigo wa utafutaji wa masoko ili Wakulima waendelee kunufaika na Ushirika. Hivyo, amesema Tume itaendelea kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu.

Akichangia mada katika mafunzo hayo mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Victoria Michael amesema Vyama vya Ushirika vina fursa kubwa ya kuongeza pato la Vyama kwa kufufua viwanda vingi zaidi vitakavyosaidia kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao akitolea mfano mazao ya Korosho na Kahawa yanayosafirishwa nje ya nchi. Akiongeza kuwa uongezaji wa thamani Pamoja na ufungashaji mzuri wa bidhaa za mazao unaongeza na kuitangaza nchi Kimataifa.

Kwa upande wake Bw. Bakari Kassia Kaimu Meneja Mkuu wa Mradi wa Pamoja wa Vyama vya Vikuu vya Tumbaku (T.C.J.E) kwa niaba ya washiriki amesema mafunzo hayo yatawawezesha kupanua fursa za masoko kupitia mada ziliangazia mifumo ya masoko ya Ushirika, masoko ya Kimkakati, Kilimo cha Mkataba, mikataba ya mauzo, aina ya minada ya uuzaji wa mazao, namna bora ya kufikia masoko ya nje ya nchi kwa kushirikisha Serikali na Balozi zilizopo katika mataifa mbalimbali.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Wenyeviti, Mameneja na Maafisa masoko 145 kutoka mikoa mbalimbali, ambao ni watendaji muhimu katika uuzaji wa mazao ya wakulima katika Vyama vya Ushirika.



Share:

BILIONI MOJA KUTUMIKA KUPANGA MAENEO RORYA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wakazi wa Mji wa Kirongwe wilayani Rorya mkoa wa Mara wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka (katikati) wakitoka ofisi za Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato kwa upande wa Kenya eneo la mpaka wa nchi hizo mbili alipofanya ziara katika kijiji cha Kirongwe wilayani Rorya mkoa wa Mara jana.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kirongwe wilayani Rorya mkoani Mara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya idara ya Uhamiaji iliyopo mpaka wa Tanzania na Kenya katika kijiji cha Kirongwe wilaya ya Rorya mkoani Mara
…………………………………………………………………

Na Munir Shemweta, WANMM RORYA

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoa wa Mara Shilingi Bilioni moja kwa ajili mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika wilaya hiyo na kiaumbele kikubwa ni eneo la mkakati la mji wa Kirongwe uliopo mpaka wa Tanzania na Kenya.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kirongwe kilichopo kata ya Bukura wilayani Rorya mkoa wa Mara akiwa katika zira ya siku moja mkoani humo.

Hata hivyo, Dkt Mabula alisisitiza kuwa, wakati wa kuupanga upya mji huo wa Kirongwe kupitia mradi wa KKK hakuna eneo la mwananchi litakalochukuliwa bila ya kulipwa fidia.

‘’Serikali ya Rais Samia imetoa shilingi Bilioni moja kama mkopo kwa ajili ya upangaji maeneo mbalimbali wilayani Rorya ikiwemo kuupanga vizuri mji wa Kirongwe uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya na lazima fidia ilipwe kabla ya kuchukua maeneo ya wananchi ‘’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kupitia mradi huo mji wa Kirongwe utapangwa vizuri na kuainishwa maeneo ya makazi, uwekezaji, viwanda pamoja na huduma za jamii na kusisitiza kuwa upangaji huo ni vyema ukazingatia pia makundi maalum kama vile wamachinga na mamalishe.

Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Fredy Kyalawa alieleza kuwa, fedha walizopatiwa halmashauri ambazo ni za mkopo zitatumika kupanga maeneo katika wilaya ya Rorya na kipaumbele ni eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya katika mji wa Kirongwe.

‘’fedha tuliyopewa tutaitumia kupanga na kupima maeneo mbalimbali katika wilaya yetu ya Rorya na kipaumbele ni eneo la mkakati la mji wa Kirongwe ambapo huko tutalipa fidia na kufanya urasimishaji makazi holela kwa takriban viwanja 5000 na baada ya hapo tutaenda maeneo mengine kama Shirati, Utegi, Mika na Kinesi’’ alisema Kyalawa.

Kwa upande wao, wananchi wa Kirongwe kupitia mkutano na Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula walieleza kuwa pamoja na mpango wa upangaji upya mji huo kuna hatari wakazi hao kuwa watazamaji kwa fursa zitakazokuja kutokana na changamoto kadhaa wanazopata ikiwemo ile wanayopata wakati wa kufanya shughuli zao za uvuvi.

‘’Tunashukuru kwa serikali kuamua kuendeleza mji wetu wa Kirongwe ila kuna hatari ya sisi kuwa watazamaji maana hivi sasa hatuna amani katka eneo la ziwa, wakenya wanasema wamenunua ziwa tunaomba kilio chetu ukipeleke kwa Rais Samia’’ alisema Samson Sabanya mkazi wa kijiji cha Kirongwe.

Naibu Waziri Dkt Mabula aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa ataziwasilisha changamoto zao kwa mawaziri wa Uvuvi na Mifugo pamoja na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ili ziweze kushughulikiwa haraka na wao wafaidike na fursa zitakazopatikana wakati wa kuuendeleza mji huo wa Kirongwe.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alitembelea mpaka wa Tanzania na Kenya ambapo katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa na taswira nzuri kwa upande wa Tanzania, alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuharakisha mchakato wake wa kujenga jengo kubwa la ofisi na biashara litakalojumishga taasisi zinazotoa huduma eneo la mpakani kama vile idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Niseme tu ukweli hali ya ofisi zetu hizi hairidhishi ukilinganisha na wenzetu kwa upande wa Kenya eneo la Migori ambapo wana majengo mazuri. Ila nafarijika kusikia NHC inatarajia kujenga jengo kubwa hapa ambalo nina uhakika litakwenda kubadilisha mandhari ya eneo hili niwaombe Shirika la Nyumba kuchangamkia fursa hii itakayotoa fursa kwa wawekezaji wengi kuwekeza hapa” Alisema Dk. Mabula

Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka alisema kuwa, kufuatia Serikali kutoa Bilioni moja kwa ajili ya upangaji na upimaji sasa wilaya nzima ya Rorya inaenda kufunguka kimaendeleo na kuongeza kuwa miji ya Shirati, Utegi na Kinesi nayo inaenda kufunguka kimaendeleo.

‘’Ndugu zangu muda siyo rafiki ili wote kuwa na lugha moja tutakaa kikao cha pamoja na wadau kuona namna tutakavyoweza kwenda fursa hii tuliyoipata , unapowekeza katika ardhi lazima upate mafanikio maana ardhi ndiyo kila kitu’’ alisema Chikota akizungumza katika kikao cha wadau na Naibu Waziri wa Ardhi.
Share:

MZAZI AMFUNGULIA KESI KIJANA WAKE .."ANA FEDHA NYINGI HANIPI MSAADA..ANAKULA TU STAREHE MJINI..NATAKA ANILIPE MSHAHARA'


Mzee Gideon Kisira Cherowo
Mzee Gideon Kisira Cherowo (73) Mkazi wa Bungoma nchini Kenya amemfungulia kesi katika mahakama Kuu ya Kitale Mtoto wake aitwaye Washington Chepkombe akitaka akatwe asilimia 20 ya mshahara wake ili apewe Mzee huyo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya Familia kwa kuwa Mtoto wake huyo hampi msaada licha ya kuwa na kazi nzuri na fedha nyingi.

Mzee huyo anasema Sasa ni miaka 17 tangu kijana wake aonekane nyumbani na mzee ameamua kufika mahakamani ili kijana ashurutishwe kuwa awe anatuma 20% ya mshahara wake.

Mzee huyo anasema alilazimika kuuza hadi ardhi yake na mali zake nyingine ili kulipia ada za masomo ya Mtoto wake huyo hadi Chuo Kikuu na akafanikiwa kupata kazi kwenye Mamlaka ya Viwanja vya Ndege lakini baada ya kupata kazi hampi msaada.

Mzee huyo amesema ana Watoto wanne lakini mwenye kazi ni Washington pekee na kusema kwa sasa yeye na Familia yake wanaishi katika nyumba ya udongo kijijini kwao huku Mtoto wao mwenye uwezo akila starehe Mjini.


“Nimepambana sana kumtafutia maisha Mtoto ili atusaidie lakini hatupi msaada kwa kuwa mshahara wake ni mzuri nimefungua kesi ili 20% ya mshahara wake nilipwe mimi..”,amesema


Gideon Kisira Cherowo mwenye umri wa miaka 73 alisema mwanae ni mwajiri wa Halmashauri ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege nchini KAA ambapo hupokea mshahara kila mwezi.

 Hata hivyo, alisema mwanawe hajaweka kiwango chochote kuwafikia wazazi wake ambao sasa wamekosa namna kutokana na uzee.

Kisira aliambia mahakama kuwa alifanya kila awezalo ili mwanawe kusoma akijua atakuwa tegemeo kwake siku za uzeeni.

 "Nilitumia mali yangu yote ili kuhakikisha kuwa atakuwa katika nafasi ya kutusaidia. Kwa sasa, mimi na mke wangu tuko katika hali mbaya licha ya kuwa tuna mtoto ambaye yuko kazini. Naomba mahakama iamuru atupe asilimia 20 ya mshahara wake nikiwa kama babake," alisema mzee huyo


Inaarifiwa mwanawe ana miaka 48 na mzee Kisira anasema aliuza hadi shamba lake ili weze kumpa masomo.

"Niliuza shamba langu eneo la Cheptais, Bungoma, na kumsomesha kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu. Nilimpa pia robo ekari. Mimi pia nilimlipia mke wake mahari ambapo ilinigharimu ng'ombe wanne na fedha," Kisira alisema kwenye kesi katika mahakama Kuu ya Kitale. 

Alisema mwanawe alipata kazi na KAA 2008 lakini hajawahi kuwasaidia wazazi wake kwa chochote.

 Aidha aliongeza kuwa kwa miaka 17 sasa hajawahi kufika nyumbani wala kutuma hata sumni nyumbani. 

Sasa anataka mahakama iagize kijana huyo kuwa akituma nyumbani asilimia 20 ya mshahara wake ili wazazi wake wapate riziki. Hata hivyo, kesi hiyo ni ya namna yake kwani hakuan sheria iliyopo kuhusu jinsi watoto wanafaa kusaidia wazazi wao.
Share:

MTOTO MCHANGA ALIYETUPWA CHOONI AOKOLEWA



Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limemuokoa mtoto mchanga wa kiume anayekadiliwa kuwa na umri wa siku mbili hadi tatu aliyekuwa ametupwa katika shimo la choo linalokadiliwa kuwa na urefu wa mita zaidi ya 20 la Shule ya Msingi Rukajange iliyopo kata ya Bugene Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.


Mtoto huyo alibainika Desemba Mosi, 2021 wakati mwalimu wa shule hiyo, George Ishoko alipokuwa akipita kilipo choo kusikia sauti ya mtoto ikitokea ndani ya shimo na kutoa taarifa ofisi za Zimamoto waliofika eneo hilo na kumtoa.


Kaimu mkuu wa jeshi hilo Wilaya ya Karagwe, Karata Ramadhan Karata amesema mtoto huyo alikuwa amefungwa kwenye mfuko na kitambaa cheusi.


Amesema mtoto huyo amelazwa hospitali teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga kwa ajili ya matibabu na uangalizi wa madaktari.


Mganga mkuu katika hospitali hiyo, Dkt. Furaha Kahindo amesema hali ya kichanga hicho inaendelea vizuri na leo anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali na atakabidhiwa kwa mama ambaye ameomba kumnyonyesha baada ya kukubaliwa na mamlaka aishi naye.


Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo mwalimu katika shule ya msingi Rukajange, George Ishoko amesema kuwa, wakati akiwa anapita karibu na choo hiyo alisikia sauti ya kichanga hicho.
Share:

MWANAFUNZI WA DARASA LA SITA ABAKWA KISHA KUTUPWA KWENYE MAPANGO YA MIAMBA YA MTO



Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Maendeleo Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara, Zinati Alifa mkazi wa mtaa wa Mchema mwenye umri wa miaka 13 amebakwa na kisha kuuawa na mwili wake kutupwa kwenye mapango ya miamba ya Mto Kabomola.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo Shaibu Chande alisema mwili huo uliokotwa ukiwa umetobolewa macho, kabla ya kutokea kwa tukio hilo Septemba 26 mwaka huu majira ya saa 11:30 jioni mwanafunzi huyo aliwaaga wazazi wake kuwa anakwenda kuokota korosho na maembe kwenye mashamba yaliyopo maeneo ya Mchemba.

“Mwanafunzi huyo hakurejea hadi usiku ndugu walihofia usalama wake na kuanza kumtafuta bila mafanikio kwa kuwa haikuwa tabia yake, walikwenda hadi kwenye shamba ambalo aliaga anakwenda na hawakumpata”, alisema Chande.

Baada ya juhudi za Ndugu na majirani kumtafuta kwa muda wa siku mbili kutozaa matunda, waliamua kutoa taarifa serikali za mitaa pamoja na Kituo cha Polisi Wilaya ya Masasi.

 Mpaka kufikia Desemba 1 wasamaria wema walitoa taarifa za kuuona mwili huo majira ya saa 9:00 alasiri na kutokana na mwili kuharibika ulizikwa siku hiyo hiyo saa 10:00 jioni.
Share:

MIFUGO MKOMBOZI WA WANUFAIKA WA TASAF


SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Hai Kilimanjaro akimhudumia ng'ombe wake aliyemnunua kwa ruzuku ya TASAF mara baada ya kuingizwa kwenye mpango wa kaya masikini.
ELINE MASAWE mnufaika kutoka Gezaulole akiwa na mumewe Benjamin Fanuel Masawe wakiwa nyumbani kwao kijiji cha Gezaulole mara baada ya kutembelewa na waandishi wa habari kuona miradi yao.
Benjamin Fanuel Masawe akiwalisha mbuzi wao waliowanunua mara baada ya kuingizwa na TASAF kwenye mpango wa Kaya Masikini majani.
SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Hai Kilimanjaro akizungumza na maofisa wa TASAF kuelezea namna alivyofaidika kwa ruzuku ya TASAF mara baada ya kuingizwa kwenye mpango wa kaya masikini.
Afisa Malalamiko wa TASAF Bw. Dismas Yusuf Makwinja akimsikiliza Michael Zakaria Mumburi Mratibu TASAF Wilaya ya Hai wakati waandishi wa habari walipowatembelea wanufaika wa TASAF kijiji cha Foo Machame Kaskazini wilaya ya Hai.
Afisa Malalamiko wa TASAF Bw. Dismas Yusuf Makwinja akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu wanufaika wa TASAF katika kijiji cha Foo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Foo Machame wilaya ya Hai Kilimanjaro Judica Munisi akiongozana na Mwandishi wa Clouds Jerome Risasi kuelekea kwa Bi SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Kaskazini Hai Kilimanjaro
Afisa Malalamiko wa TASAF Bw. Dismas Yusuf Makwinja akifanya utambulisho kwa Bi. SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Hai mara baada ya timu ya waandishi wa habari kuwasili nyumbani kwake.
Bi. SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Hai akionesha ndama wake ambaye ametokana na ng'ombe aliowanunua kwa ruzuku ya TASAF.
Baadhi ya ng'ombe wa Bi. SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Hai aliowanunua kwa ruzuku ya TASAF baada ya kuingizwa kwenye mpango wa Kaya Masikini.

................................................

Halmashauri ya Wilaya ya Hai ina kaya 3,523 zilizo katika Vijiji 43 zinazonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF ili kuwaondolea hali ya umaskini iliyokuwa ikiwakabili.

Kwa mwaka 2021/22 Halmashauri hiyo imetenga Shilingi Milioni 140 zitakazotumika kuziwezesha kaya hizo kuanzisha miradi ya kimaendeleo ikiwemo ujasiriamali na ufugaji ili zenyewe ziweze kujikimu kimaisha.

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa shughuli za ugugaji hasa wa Ng’ombe na mbuzi ndizo zinazoleta tija kimaendeleo hivyo Tasaf inatakiwa kuwekeza katika kutoa elimu ili ufugaji huo uwe na tija.

ELINE MASAWE mnufaika kutoka Gezaulole, MARGRETH NKYA na SAYANDE SHUNA wa Kijiji cha Foo Machame Hai Kilimanjaro wamesema ili shughuli hiyo iwe na tija wanahitaji zaidi elimu ya ufugaji bora.

“Nina ng’ombe wangu mmoja niliyemnunua kwa fedha za Tasaf, namfuga kwa kumkatia majani, na hata sasa ameshawahi kuzaa mara tatu hivyo huuza ndama kwa kiasi cha shilingi 250,000 na fedha ninayoipata najiendeleza kimaisha ikiwemo kujenga nyumba yangu,” alisema Margareth Nkya.

Sayande Shuna yeye mbali ya ufugaji pia ni mkulima wa mbogamboa ambapo amekuwa akitumia mbolea kutokana na mifugo kurutubisha mazao yake kama ndizi na miparachichi ili kutoa mavuno bora.

“ Licha ya kuuza maziwa ya ng’ombe na mbuzi, mbolea kutoka kwa ng’ombe wangu watatu na mbuzi imekuwa ikinisaidia kurutubisha mazao yangu hapa shambani,” alisema Syande.

Akizungumzia juu ya hali ya uwezeshwaji kwa kaya maskini Katibu wa Mtaa wa Gezaulole Tumaini Mkojela amesema, shughuli za ufugaji zimewawezesha wanufaika wengi kusomesha watoto wao ikilinganishwa na zamani.

Mbali na hilo Mwenyekiti wa Kijiji cha Gezaulole FADHILI NG’ANZI amesema kaya zinazowezeshwa na Tasaf zimekuwa msaada kwa wakazi jirani baada ya kujifunza stadi mbalimbali zilizowaendeleza wanufaika kimaisha.
Share:

GGML YATOA MILIONI 84 MAPAMBANO DHIDI YA VVU NA UKIMWI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akimkabidhi cheti na ngao Makamu wa Rais wa Kampuni ya GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo (kushoto) kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu) Jenista Mhagama (katikati) na Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko. GGML imekabidhiwa cheti hicho jana jijini Mbeya katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imechangia zaidi ya Sh milioni 84 kusaidia mipango ya serikali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya. 


GGML na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), kupitia Kampeni ya Kilimanjaro Challenge, wanashirikiana kwa namna mbalimbali ikiwamo kuongeza uelewa kuhusu janga la VVU na UKIMWI ili siku moja Tanzania itangazwe kuwa imetokomeza kabisa janga hilo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.


Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani juzi jijini Mbeya, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo alisema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza magonjwa ya mlipuko,” ni muhimu kwa jamii ya Geita na Tanzania kwa ujumla.


Alisema mpango wa GGML Kili Challenge ni mradi mahsusi kutoka katika sekta binafsi ambao umeisaidia serikali kwa zaidi ya miaka 20 katika mapambano dhidi ya VVU.


“Kupitia mpango huu, wachangiaji wenzetu wameendelea kuwa mstari wa mbele kudhibiti janga la VVU kwa kuhakikisha utoaji huduma za kimatibabu unazingatia utu na haki za wale wote wanaoweka imani yao kwetu hususani wale walio hatarini zaidi.


“Tunaziomba sekta binafsi nchini kuungana na GGML na kusaidia mfuko wa Ukimwi ili kuwezesha mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kuwa endelevu. Bila kuwa na mipango imara ya kuhakikisha usawa katika utoaji wa huduma hizi za kimatibabu ni dhahiri duniani itashindwa kufikia lengo lake la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030”, alisema.

Kama raia anayewajibika, GGML pia iliandaa kampeni ya upimaji wa VVU kwa hiari kwa wiki mbili ikilenga kufikia asilimia 80 ya wafanyakazi wake 5000. Hao ni wafanyakazi walioajiriwa moja kwa moja na wakandarasi.

Shayo aliongeza kuwa maendeleo chanya ya kijamii na kiuchumi ya mkoa na nchi yetu ni matokeo ya jamii yenye afya.


"GGML ni kampuni inayothamini mali na watu wake. GGML inaamini kuwa uwekezaji unaofaa katika afya ya wafanyakazi utaleta nguvu kazi yenye afya na kuongeza tija katika utendaji na ukuajiji wa kibiashara,” alisema Shayo.


Alisema kuanzia tarehe 1 – 14 Desemba 2021, GGML imealika jumla ya washauri nasaha 15 waliopata mafunzo ya UKIMWI kutoka serikalini na hospitali binafsi kufanya Upimaji wa VVU kwa hiari katika eneo lote la Mgodi.


“Ikiwa na wafanyakazi walioajiriwa na wakandarasi zaidi ya 5,000, GGML inawakilisha sehemu kubwa ya jamii ya Mji wa Geita ambao kama wakiwa wameelimishwa vya kutosha kuhusu VVU na UKIMWI, watakuwa na ushawishi chanya miongoni mwa jamii nzima ya Geita.

GGML Kilimanjaro Challenge dhidi ya VVU & UKIMWI ilizinduliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kwa lengo la kuongeza uelewa wa janga hili na kutoa msaada wa kifedha kwa mipango ya VVU na UKIMWI.

Tangu kampeni ya GGML Kilimanjaro Challenge ilizinduliwe miaka 20 iliyopita, zaidi ya watu 800 kutoka sehemu mbalimbali dunia wameshiriki kwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa njia ya kawaida na kuuzunguka mlima kwa kutumia baiskeli.

Kilimanjaro Challenge imebadilika na kushirikisha makampuni ya ndani na nje ya nchi na watu binafsi kutoka duniani kote hali iliyosaidia kuchangisha zaidi ya Sh bilioni 1.3 tangu 2018 kwa ajili ya miradi ya kinga, matunzo na matibabu ya VVU nchini kote.



Share:

MTOTO ACHOMWA KWA MKASI WA MOTO AKITUHUMIWA KUIBA 'FLASH' YA MOVIE SHINYANGA MJINI


Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo  kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash’ ya mama na bibi yake.
Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo.
Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo.
Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo  kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash’ ya mama na bibi yake.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la tatu shule ya Msingi Bugoyi A Mjini Shinyanga amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash’ ya mama na bibi yake.


Mashuhuda wa tukio wameiambia Malunde 1 blog kuwa mtoto huyo alifanyiwa ukatili huo Desemba 1,2021 majira ya saa 2 usiku katika mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Wameeleza kuwa siku ya tukio jioni alipewa Flash na bibi yake aitwaye Adelida Leonard (50) na mama yake mzazi Beatrice Mwombeki (28) ili aende eneo jirani akaweke Movie (Filamu) kwenye ‘Flash’ lakini akiwa njiani alidondosha Flash hiyo na kurudi nyumbani kutoa taarifa juu ya kupotea kwa Flash hiyo.

“Baada ya mtoto huyo kurejea nyumbani na kuwaelezea bibi na mama yake kuwa Flash imepotea,walimwambia aende akaitafute lakini hakufanikiwa kuipata na akaogopa kurudi nyumbani na ilipofika usiku alirejea nyumbani ndipo akafanyiwa ukatili kwa kuchomwa na kipande cha mkasi wa kukatia maua/ fensi kilichochemshwa kwenye jiko la mkaa sehemu mbalimbali za mwili wake hasa mgongoni na mapajani na kumsababishia majeraha”, wamesema mashuhuda wakizungumza na Malunde 1 blog.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo cha tukio ni kumtuhumu mtoto huyo kuwa ameiba Flash na kwamba mbinu iliyotumika ni kuchemsha kipande cha mkasi wa kukatia fensi kwenye jiko la mkaa kisha kumuunguza sehemu mbalimbali za mwili wake.

Amesema watuhumiwa ambao ni Adelida Leonard (bibi) na Beatrice Mwombeki (mama mzazi) wamekamatwa na madhura amelazwa katika hospital ya rufaa mkoa wa Shinyanga.

Share:

BENKI YA CRDB YAAHIDI MITAJI NA MIKOPO KWA WAFANYABIASHARA, WAWEKEZAJI KUTOKA ITALIA


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake kwa wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Sekta ya Hoteli Zanzibar, Paulo Rosso walipokutana katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Benki ya CRDB imewahakikishia wafanyabiashara na wewekezaji wa Tanzania na Italia utayari wake wa kutoa mikopo na mitaji ya kutosha watakapo kuwa tayari kuwekeza nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati wa jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Itali liloandaliwa na ubalozi wa Tanzania lililofanyika Jijini Roma, nchini Italia.

Nsekela amesema Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na wawekezaji katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazoendana na huduma za kibenki zinatatuliwa.

“Nawahakikishia kuwa Benki ya CRDB itawawezesha mikopo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hivyo msiwe na wasiwasi kuhusu mitaji ya kuwekeza ipo karibuni sana tuijenge Tanzania,” amesema Nsekela.

Nsekela ameongezea kuwa Benki ya CRDB inafarijika kuona wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza zaidi Tanzania, huku akimpongeza Balozi wa Tanzania nchini Itali, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo kwa kuandaa Jukwaa hilo ambalo limetoa fursa ya kueleza sekta mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.

“Benki ya CRDB pamoja na mambo mengine tutahakikisha kuwa sisi kama benki tunawawezesha wawekezaji wanaowekeza nchini na kuwapa mitaji ya biashara pamoja na biashara za kimataifa kati ya nchi moja na nyingine…,” alisisitiza.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo ameipongeza Benki ya CRDB kwa utayari wake wa kusaidiana Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kupitia utoaji wa mikopo na mitaji, pamoja na huduma nyengine za kifedha zinazoongeza ufanisi katika uendeshaji wa biashira.

“Benki ya CRDB imeonyesha uzalendo mkubwa kwa kushirikiana na Serikali kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini, binafsi sina shaka na uwezo wao kimtaji. Nimefurahi pia wamekwenda mbele zaidi kwa kutoa huduma za ushauri katika uwekezaji, hii inaonyesha ni jinsi gani wamejipanga vizuri,” amesema Balozi Kombo.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.

“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza….nawahakikishia mimi nimewekeza Tanzania na ninaona ni sehemu salama ya kuwekeza karibuni sana kuwekeza kwa maendeleo ya Tanzania na Italia,” amesema Bw. Rosso

Jukwa hilo la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limehudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji takribani 250 kutoka nchi zote mbili. Wafanyabiashara na wawekezaji hao ni wa sekta za utalii, kilimo, madini, na ujenzi.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
--
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger