Friday, 4 June 2021

NEC yatangaza ratiba ya uchaguzi mdogo jimbo la Konde


Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na Kata 6 za Tanzania Bara.

Tayari Tume imekwisha kupokea Barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuwa kiti hicho kiko wazi.

Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari Jijini Dodoma  3 Juni, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk. Willson Mahera imesema uchaguzi huo umeapangwa kufanyika tarehe 18 Julai, 2021.

“Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ameitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha Ubunge katika Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,” alisema Dkt Mahera.

Kiti cha Mbunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kiko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Khatib Said Haji na hivyo kukoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha, Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara.


Share:

Mwanafunzi Mbaroni Kwa Kumuua Mpenzi Wake


Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, linamshikilia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Prudence Patrick (22) kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga shingo mpenzi wake Petronila Mwanisawa (21), mkazi wa Semtema, Kata ya Kihesa, Iringa.

Imedaiwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo ni mwenyeji wa Sumbawanga na ni mwanafunzi wa kozi ya uandishi wa habari na marehemu pia alikuwa mwanafunzi mwenzake na alikuwa mwenyeji wa Mkoa wa Kagera.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea majira ya 12 alfajiri katika eneo la Semtema, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa kwenye chumba alichokuwa akiishi mtuhumiwa huyo.

Alisema kuwa mwanafunzi anayedaiwa kunyongwa, alifika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo usiku wa kuamkia Juni Mosi mwaka huu akiwa na rafiki yake aliyefahamika kwa jina la Belnada Njafula kwa lengo la kuchukua pesa yake kiasi cha Sh. 5,000 ambayo alikuwa anamdai mpenzi wake huyo.

"Baada ya kufika nyumbani kwa mtuhumiwa rafiki yake aliondoka na kuwaacha wawili hao kwa muda ili walipane deni walilokuwa wakidaiana.

"Hata hivyo, marehemu hakurudi nyumbani kwao hadi pale mwili wake ulipokutwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa ukiwa umefungiwa ndani na umelazwa kitandani ukitokwa na povu mdomoni na damu puani," alisema Kamanda Bwire.

Alidai kuwa taarifa za awali za kiuchunguzi zinaonyesha mtuhumiwa baada ya kufanya unyama huo, alitumia simu ya marehemu kutumiana ujumbe na rafiki yake kumjulisha kama ana mimba ya Jay ambaye ni rafiki yake.

"Mtuhumiwa alitumia simu ya marehemu kuchati na rafiki wa marehemu kumjulisha kuwa ana mimba ya Jay na baadaye kuwajulisha wazazi wa marehemu kuwa 'binti yenu amefariki dunia'," alisema.

Kamanda Bwire alisema taarifa za awali kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo zilitolewa na wazazi wake kutokana na taarifa walizotumiwa na kijana huyo mtuhumiwa.

Alisema kuwa baada ya kufanya unyama huo, mtuhumiwa alikamatwa na Jeshi la Polisi akijaribu kutoroka kuelekea mkoani Dodoma na alikamatwa maeneo ya Mgongo kilomita chache kutoka maeneo ya Semtema anakodaiwa kufanya mauaji hayo.

Kamanda Bwire alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo unaendelea na pindi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani.


Share:

NSSF YASHIRIKI MAONYESHO YA WIKI YA MAZIWA KUTEKELEZA AGIZO LA KUWAFIKIA SEKTA ISIYORASMI NA WAFANYABIASHARA WADOGO WADOGO

 

Afisa Mwandamizi Mkuu Idara ya Matekelezo Mkoa wa NSSF Tanga Abubakari Mshangama akizungumza na waandishi wa habari wakati maonyesho ya wiki ya maziwa inayoendelea kwenye viwanja vya Tangamano Jijini Tanga
Meneja Kiongozi Mahusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao kwenye maonyesho ya wiki ya maziwa
Meneja Kiongozi Mahusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele kushoto akieleza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima wakati alipotembelea  Banda lao
Afisa Mwandamizi Mkuu Idara ya Matekelezo Mkoa wa NSSF Tanga Abubakari Mshangama kulia akimkabidhi vipeperushi mbalimbali Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji mara baada ya kutembela banda lao kushoto anayeshuhudia ni Meneja Kiongozi Mahusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele

NA OSCAR  ASSENGA,TANGA

SHIRIKA la Hifadhi za Jamii (NSSF) wameamua kushiriki maonyesho ya wiki ya maziwa inayoendelea kwenye viwanja vya Tangamano Jijini Tanga ili kutekeleza agizo la kuwafikia sekra isiyorasmi na wafanyabiashara wadogo wadogo.

Hayo yalisemwa na Afisa Mwandamizi Mkuu Idara ya Matekelezo Mkoa wa NSSF Tanga Abubakari Mshangama wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema mpango huo wamepewa na serikali kuanzia mwaka 2018 kufikisha lengo la kuwafikia wananchi MIlioni 18.

Alisema katika kutekeleza agizo hilo na kupunguza umaskini kwa wananchi na kuongeza wigo wa uandikishaji Shirika hilo wameona washiriki kwenye maonyesho hayo lengo kuwahudumia  wafanyakazi ambao wapo kwenye sekta iliyorasmi na wananchi ambao hawapo kwenye sekta isiyorasmi ili kuwaonyesha mafao walionayo na utaratibu wa kujiunga na NSSF.

Alisema pia na taratibu za wanachama kupata mafao kwa sababu wamekuwa na mafao tofauti tofauti kama watu wengi ambao wapo kwenye sekta isiyorasmi na iliyorasmi wana fao la kukosa ajira lakini zamani ilikuwa fao la kujitoa.

“Fao la kukosa ajira zamani lilizoelewa fao la kujitoa lakini hivi sasa serikali imekuja na fao la kukosa ajira ambalo kwa watu ambao wana taaluma na elimu kidogo nzuri na wamechangia zaidi ya miezi 18 watalipwa asilimia 33.3 ya wastani wa mshahara wake wa mwisho lakini kama hatakuwa hajafikisha ile michango 18 watalipwa asilimia 50 ya michango yake”Alisema

Alisema lakini serikali haikuwatupa wale ambao hawana elimu au ujuzi zaidi hao watapewa asilimia 100 ya mafao yake ambapo mpango huo wa kuwa na sekta rasmi na isiyorasmi kupewa NSSF ni kuzidisha wigona kupunguza umaskini wa wananchi ikiwemo kutoa fursa zilizopo za hifadhi ya jamii kwa kujijengea maisha yao ya sasa na baadae.

Aidha pia alisema kuwa NSFF wanatoa mafao ya muda mfupi na muda mrefu ambapo muda mfupi ni mafao ya matibabu,uzazi,mazishi na ukosefu wa ajira huku akielezea mafao ya muda mrefu  ni pensheni ya urithi,pensheni ya uzee na pia kwa ajili ya mwanachama ambaye lakini alitakiwa kupata pensheni lakini akafariki basi familia yake itaendelea kunufaika.

Hata hivyo alisema kwa mkoa wa Tanga katika sekta isiyorasmi hivi sasa wameinuka kutokana na hamasa waliyoifanya ikiwemo kupitia maonyesho mbalimbali na semina wamepata mwamko watu wameanza kujiandikisha na kuanza kujua thamani ya hifadhi za jamii ni nini.

“Lakini hivi sasa tuna mpango wa kupitia kwenye vyuo vya Tanga na Taasisi zenye wajasiriamali wadogo na wakubwa ikiwemo kuwa na mabalozi wadogo wa NSSF ambao tukifundisha wakiwa wadogo basi baadae watasaidia kujua maana nzuri ya Hifadhi ya Jamii”Alisema

Share:

HAYA HAPA MAGAZTI YA LEO IJUMAA JUNI 4,2021

















Share:

Thursday, 3 June 2021

HALMASHAURI YA SHINYANGA YAZINDUA ZOEZI LA UTOAJI WA KINGATIBA YA KICHOCHO NA MINYOO YA TUMBO KWA WANAFUNZI

 

Wanafunzi wa shule ya Msingi Iselamagazi wakipata chakula kwa ajili ya kujiweka sawa ili wapewe kingatiba ya kichocho na  minyoo ya tumbo

 Na Shinyanga Press Club Blog
HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga, imezindua zoezi la utoaji wa kingatiba ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ya Kichocho na Minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Iselamagazi katika halmashauri hiyo.

Uzinduzi huo uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba, ambaye amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wanaowazuia watoto wao kwenda shule ili kukwepa wasipate kingatiba za minyoo ya tumbo na kichocho, huku akiwaondolea wananchi hofu kwani dawa hizo hazina madhara kwa watoto bali zinalenga kuwakinga na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Aidha Mahiba ameagiza viongozi wa kata na vijiji kufanya ufuatiliaji na kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya watu wanaoeneza uvumi kwamba dawa hizo ni dawa za Virusi vya Corona, ambapo ameeleza kuwa Serikali ipo makini na kamwe haiwezi kuangamiza watu wake.

“Ndugu zangu dawa hizi ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa watoto wetu wanajikinga na magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele wakati mwingine wanaweza kukondeana nakupatwa na magonjwa mbalimbali kutokana na magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho ,hali mabayo inaweza kupelekea mtoto kudumaa au kudumaza akili wataalamu wanasema inaweza hata kukusababishia kifo,” alisema Mahiba.

Shule ya msingi Iselamagazi yenye jumla ya wanafunzi 1,323 ambapo wanafunzi wote wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi 14 watapewa dawakinga hiyo.

DED Mahiba aliwaeleza wananchi wa halmashauri hiyo kuwa ili kudhibiti magonjwa hayo, wanapaswa kuzingatia watoto kuvaa viatu kwa kuwa kutovaa viatu ni njia hatarishi ya maambukizi hayo na kuwasisitiza walimu nao kuzingatia suala la usafi katika vyoo vinavyotiririsha hovyo maji machafu.

Kwa upande wake, Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kutoka hospitali ya wilaya - Iselamagazi, Dk. Charles Zacharia alisema kuwa wamelenga kutoa kingatiba hizo kwa wanafunzi 91,882 katika halmashauri hiyo, na wanatarajia kuendelea kutoa kingatiba kwa wanafunzi wote wenye sifa ili kuwakinga na magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo.

“Kwa ushirikiano wa walimu na wahudumu wa afaya waliopo zoezi litakwenda vizuri kama lilivyo agizo la serikali, niwaombe wazazi tuendelee kuruhusu watoto wetu waje kupata kinga na tiba hii muhimu sana,” alisema Dkt. Charles.

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iselamagazi, Elias Lutubija ameeleza kuwa kabla ya zoezi la kuwapa kinga tiba, wanafunzi wote wamepewa chakula cha kutosha ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mwanafunzi kumeza dawa kabla ya kula chakula.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba (kulia) akimpatia dawa za kichocho na Minyoo ya tumbo mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Iselamagazi
Wanafunzi wa shule ya Iselamagazi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakinywa dawa za kichocho na minyoo ya tumbo baada ya zoezi za ugawaji wa dawa hizo kuzinduliwa na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba (kulia). Wa pili kushoto ni Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hapewi Kipaumbe halmashauri hiyo, Dk. Charles Zakaria
Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hapewi Kipaumbe halmashauri hiyo, Dk. Charles Zakaria akizungumza wakati wa kuzindua zoezi hilo
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iselamagazi, Elias Lutubija akizungumza wakati wa kuzindua chanjo hiyo katika shule yake
Wanafunzi wa Shule ya msingi Iselamagazi wakiwa katika maandalizi ya kupata kinga tiba ya kichocho na minyoo ya tumbo

Picha na Shinyanga Press Club Blog
Share:

MWANAFUNZI CHUO KIKUU CHA IRINGA AUAWA KWA KUNYONGWA NA MPENZI WAKE


Mwanafunzi Petronila Mwanisawa aliyeuawa
***
Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Prudence Patrick (21) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Iringa mkazi wa Semtema Iringa ,mwenyeji wa mkoa wa Kagera kwa tuhuma za kumnyonga mpenzi wake Petronila Mwanisawa (22) ambaye pia ni mwanafunzi katika chuo hicho, mkazi wa Semtema Iringa chanzo kikielezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, amesema tukio hilo limetokea Juni 2, mwaka huu maeneo ya Kihesa mkoani Iringa ambapo taarifa za awali za upelelezi zinaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi baina ya marehemu na mtuhumiwa na kwamba wote walikuwa wanafunzi katika Chuo Kikuu Iringa.

"Juni 2, 2021 majira ya saa 12 jioni, maeneo ya Semtema Kata ya Kihesa Manispaa na Mkoa wa Iringa, Petronila Pascal Mwanisawa miaka 22 ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa zamani Tumaini na mkazi wa Semtema alifariki dunia, baada ya kunyongwa shingo na mpenzi wake mwanafunzi mwenzake wa chuo hicho aitwaye Prudence Patrick miaka 21 mkazi wa Semtema Kihesa.

"Kabla ya tukio hilo Juni 1, 2021 saa 12 jioni marehemu alifika nyumbani kwa mtuhumiwa pamoja na rafiki yake aitwaye Belnada Njafula kwa lengo la kuchukua pesa yake shilingi 5000 ambayo alikuwa anamdai mpenzi wake huyo ambapo marehemu alibaki peke yake nyumbani kwa mtuhumiwa kwa muda ili alipwe deni hilo, baada ya rafiki aliyeongozana naye kuondoka kwa ajili ya majukumu mengine.

"Hata hivyo, marehemu hakurudi nyumbani kwao mpaka pale mwili wake ulipokutwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa umefungiwa ndani na umelazwa kitandani ukitokwa na povu mdomoni na damu puani.

"Taarifa za awali za upelelezi zinaonesha kuwa, chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa mapenzi baina ya marehemu na mtuhumiwa ambaye amekamatwa na upelelezi wa tukio bado unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kujibu mashtaka yanayomkabili,"amesema Kamanda Bwire.

Kamanda Bwire amesema, siku ya tukio marehemu hakurudi nyumbani kwao jambo ambalo si kawaida yake, hivyo wazazi wake waliingiwa na hofu na kuanza kumtafuta.

"Marehemu alikuwa anaishi na wazazi wake, na huyu mtuhumiwa yeye alikuwa amepanga. Kwa hiyo siku ya tukio alitoka kwenda chuo, lakini mpaka usiku akawa hajarudi, ndipo wazazi walianza kupata wasiwasi, wakampigia simu rafiki yake lakini hawakufanikiwa,"ameeleza.

"Kwa hiyo jana ndiyo tukampata, na hiyo ni baada ya mtuhumiwa mwenyewe kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa mzazi wa marehemu akisema alikuwa na Petronela na kwamba amefariki dunia. Baada ya hapo hakupatikana tena,"amesema.

Pia amesema, baada ya wazazi kupata taarifa hizo waliripoti kituo cha polisi, ndipo askari walikwenda katika nyumba ya mtuhumiwa na kuukuta mwili wa marehemu.

"Mtuhumiwa tulimkamata njia ya kuelekea Dodoma alipokuwa akijaribu kutoroka na upelelezi wa tukio hilo unaendelea,"ameongeza.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Bwire, wanafunzi hao walikuwa wanasomea fani ya uandishi wa habari chuoni hapo.



Share:

Zuchu Na Professor Jay Ndani Ya Jukwaa Moja Uzinduzi Wa Infinix Note 10 Pro.....Fanya Yote Kwa Wepesi Na Infinix Note 10 Pro G95 Processor.


Hayawi hayawi sasa yamekuwa Kampuni ya simu Infinix kuzindua Infinix simu ya kwanza yenye sifa kuu ya G95 processor NOTE 10 pro. Infinix NOTE 10 pro kuzinduliwa kesho 4/6/2021 majira ya saa 12 jioni Mlimani City. Uzinduzi wa Infinix NOTE pro kupewa heshima ya namna yake kwa kuhudhuriwa na Mh. Joseph Haule na wageni wengine kutoka makupuni ya mawasiliano Tigo na Vodacom Plc.  
 

Infinix NOTE 10 pro ni simu ambayo imekuwa ikizungumziwa kwa muda mrefu sana mitandaoni na shahuku la wengi ni kutaka kuexperience ubora wa kamera 4 za nyuma zinavyochukua picha kwa pamoja zikiongwozwa na kamera kuu ya MP64. 


Uzinduzi wa Infinix NOTE 10 pro kushereheshwa na msanii wa kike maarufu kutoka lebo ya WCB almaarufu Zuchu na wakali wa dance kutoka Jsquare. Vilevile uzinduzi huu kuhudhuriwa na wasanii maarafu kutoka kwenye industry ya music Hemed Suleiman, Billnas, Meena Ally, Mimi Mars, Fridah Amani, Moses Iyobo na Alliaah wa WCB.
 


Uzinduzi utaanza kwa kutoa historia fupi ya kampuni tangu kuanzishwa kwake nchini inchini Hong Kong na hadi ilivyoingia rasmi Tanzania mwaka 2018 na nini malengo ya Infinix kwa wananchi wa Tanzania kwa miaka ijayo. 


Infinix imeonyesha kuwajali wateja wake na mashabiki zake kwa kutoa mialiko kwa washiriki wa Infinix Star Alliance #10ya10search, wateja waliotanguliza kiasi cha Tsh.50,000 ya kupre-order NOTE 10 na NOTE 10 pro kwa punguzo la 10% https://ift.tt/3g4luc1 . 


Kushuhudia uzinduzi huu wa kihistoria ungana @infinixmobiletz.
Tembelea https://www.infinixmobility.com/ au piga nambari ya simu 0744606222.
 

 



Share:

Waziri Mkuu: Hakuna Makinikia Yanayouzwa Bila Kulipiwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema makinikia yote yanayosafirishwa yamefuata taratibu na hakuna makinikia yanayouzwa bila kulipiwa kwanza.

“Makontena yote yanayosafirishwa hivi sasa, tayari yameshauzwa na kulipiwa na fedha iko kwenye akaunti zetu. Hapo yako chini ya mnunuzi na yeye yuko huru kuyapeleka anakotaka. Kwa hiyo, Watanzania hatupati hasira. Nataka niwaondolee hofu ya awali… makontena hayo yameshauzwa tayari na hakuna kontena linatoka bila kulipiwa,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa ufafanuzi huo leo (Alhamisi, Juni 3, 2020) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Msalala, Mheshimiwa Iddi Kassim Idd kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani juu ya makontena yaliyoshuhudiwa yakisafirishwa kupitia barabara ya Bulyanhulu-Kahama na bandari ya Dar licha ya kuwa ilishazuia makinikia kusafirishwa nje ya nchi.

Waziri Mkuu alikiri kwamba Serikali ilishazuia usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2017-2018 na kwamba zaidi ya makontena 300 yalizuiwa bandarini kwa sababu wahusika hawakufuata utaratibu na kulikuwa na udanganyifu.

“Makontena hayo yalizuiwa hadi tulipoweka utaratibu mpya, na utaratibu uliowekwa na Serikali ulikuwa kwanza ni kuwatambua nani asafirishe makinikia kwenda nje na nani ametoa vibali hivyo vya kwenda nje.”

“Mheshimiwa Rais wa Serikali ya awamu ya tano aliunda timu ya kufanya uhakiki wa sekta yote ya madini yakiwemo hili la usafirishaji mchanga na makinikia na ikabanikia kwamba ufumbuzi wa suala hilo ni kuunda kampuni ya Kitanzania ambayo ingeshirikiana na makampuni ya nje yaliyopo hapa nchini. Na leo tunayo kampiuni ya Twiga Minerals ambayo imeingia ubia na makampuni ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara yaliyo chini ya Barrick.”

Amesema kuundwa kwa kampuni hiyo kumesaidia Serikali ibaini kuwa kuna aina tano za madini kwenye mchanga unaouzwa. “Baada ya kuchimba, tunapitia kujua aina zote za madini zilizomo. Mwanzo tuliambiwa kuna aina moja tu (dhahabu) lakini sasa tunauza aina zote tano. Tukishapata ule mchanga na kubaini aina zote za madini, kupitia kampuni yetu ya Serikali tunauuza hapa hapa nchini na siyo nje ya nchi.”

Amesema hata bandarini kuna timu ya wataalamu wa kuhakiki nyaraka zote za mauzo tangu yalipofanyika hukohuko kwenye mgodi.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,



Share:

Hatutaruhusu Mtendaji Abaki Na Fedha Akisubiri Muda Wa Nyongeza – Waziri Mkuu

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitaruhusu mtendaji wake abaki na fedha kwa uzembe halafu ategemee kupewa muda wa nyongeza baada ya mwaka wa fedha kuisha.

“Tunatarajia kufanya maboresho ya kanuni ambayo yataruhusu matumizi ya fedha miezi kadhaa baada ya mwaka fedha kuisha ili ziweze kukamilisha miradi ambayo haijakamilika. Hatutahitaji kuona mzembe akibaki na fedha bila kuzitumia, huku akitarajia kuwa atapewa muda wa nyongeza… wananchi wanahitaji kuona miradi ikikamilika.”

“Pamoja na maboresho hayo hatutamvumilia yeyote atakayekaa na fedha bila kuzitumia akitegemea kuongezewa muda. Tutaweka kipengele ambacho kitambana mtendaji wetu kuhakikisha kila fedha inayoingia inatumika kwa kipindi kinachotakiwa,” amesisitiza.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni 3, 2020) Bungeni jijini Dodoma kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Magharibi, Mheshimiwa Elibariki Kingu ambaye aliitaka Serikali ione umuhimu wa kubadilisha utaratibu wa kurejesha fedha zilizobakia kwenye Halmashauri kila inapofika Juni ambayo mwisho wa mwaka wa fedha.

“Serikali inapopeleka fedha kwenye Halmashauri kati ya Machi na Juni zisipotumika zote, fedha zinazobaki huwa zinarudishwa Hazina. Lakini fedha hizi huwa zimepangiwa miradi ya ujenzi wa mabweni au vituo vya afya na zikirudi zinachelewesha kukamilika kwa miradi husika. Je serikali haioni umuhimu wa kubadilisha utaratibu huu ili fedha hizo zitumike kukamilisha miradi iliyokusudiwa?, lihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita imepeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri kwa ajili ya maendeleo. “Ni kweli Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepeleka fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo na upelekaji huu ni wakati wote tangu mwanzo wa mwaka ili kuwafanya wananchi wapate maendeleo kupitia miradi inayolengwa.”

Amesema Serikali iliweka sheria ambayo inataka ifikapo tarehe 15 Juni ya mwaka wa fedha husika, kama Halmashauri haijamudu kumaliza fedha ilizopangiwa ni lazima fedha hizo zirudi.

“Utaratibu huo unazitaka Halmashauri zitoe taarifa kuwa wana kiasi cha fedha ambacho hakijatumika ni lazima waandike barua kuonesha kwamba hadi tarehe hiyo bado wana fedha kiasi gani, na zinasubiri utaratibu upi, waeleze majengo yamefikia linta au wanasubiri taratibu za manunuzi,” amesema.

Waziri Mkuu amesema sheria hiyo imewekwa kwa kuzingatia kuwa fedha hizo zinatoka kwa awamu kulingana na hatua za utekelezaji wa miradi.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Dkt. Ndugulile Ataka Wasiolipa Kodi Waondolewe


Na Loema Joseph, DSM
 
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amelitaka Shirika la Posta Tanzania kukusanya madeni kutoka kwa watu wote wanaotumia milki za Shirika (wapangaji) ikiwemo wa majengo na viwanja kulipa kodi zao ndani ya miezi mitatu na kinyume cha hapo hatua za kuondoa watu hao zichukuliwe.
 
 “Watu wote wanaokaa kwenye milki za Shirika wanapaswa kulipa kodi na watu ambao hawajalipa waondolewe,nakupa miezi mitatu, kuhakikisha wenye madeni wawe wamelipa kikamilifu kwa sababu hatuwezi kuona watu wanatumia rasilimali za Shirika na hawalipi” Alisema Dkt. Ndugulile.
 
Ameyasema hayo jana wakati akifanya kikao kazi na Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania mara baada ya kufanya ziara yake ya kikazi kutembelea ofisi, milki na rasilimali zinazomilikiwa na Shirika hilo, Dar es salaam pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa Menejimenti hiyo alipolitembelea Shirika mwezi Januari, 2021.
 
Amelitaka Shirika kubadilika ili kuendana na kasi ya sasa ya dunia ili kuendana na matakwa na mahitaji ya wananchi kwa kujikita zaidi kwenye mabadiliko ya utendaji, mikakati, mitazamo ndani ya taasisi pamoja na bidhaa na huduma zinazotolewa na Shirika kwa wananchi.
 
Sambamba na hilo amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo kutimiza majukumu yao kwa wakati na hasa kuhakikisha ufanisi katika maeneo wanayosimamia kwa lengo la kuleta matokeo chanya kwa taasisi na taifa kwa ujumla na amesisitiza ushirikiano katika maeneo ya kazi kwa kuwa wafanyakazi wote wanawajibika kwa umma na sio mtu binafsi hivyo italeta  ufanisi.
 
“Sipendi kutuma mtu kazi nataka kila mtu ajitume kwenye majukumu yake katika eneo analolisimamia ahakikishe anawajibika katika kuleta matokeo chanya ndani ya taasisi yetu jengeni ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja katika kuyatimiza haya”. Alisisitiza Dkt. Ndugulile.
 
Kwa upande wake Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Macrice Mbodo amemshukuru Dkt. Ndugulile kwa kutenga muda wake na kuja kuwatembelea  na ameyapokea maagizo yaliyotolewa na kwa kushirikiana na Menejimenti ya Shirika ameahidi kuyafanyia kazi usiku na mchana katika kuhakikisha malengo ya Shirika na Serikali yanafikiwa.
 
“Mhe. Waziri kwanza nikushukuru kwa kututembelea na kwa maelekezo uliyoyatoa, tumeyapokea na tunakuahidi kwamba tunaenda kuyafanyia kazi kama ulivyoelekeza.” Alisema Mbodo
 
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serilalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari




Share:

TUME YA UCHAGUZI YATANGAZA RATIBA YA UCHAGUZI JIMBO LA KONDE, KATA SITA


 Na Mwandishi Maalum, Dodoma

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na Kata 6 za Tanzania bara.

Tayari Tume imekwisha kupokea Barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuwa kiti hicho kiko wazi.

Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari Jijini Dodoma leo, 3 Juni, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Willson Mahera imesema uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 18 Julai,2021.

 “Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ameitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha Ubunge katika Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,” alisema Dkt Mahera.

Kiti cha Mbunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kiko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Khatib Said Haji na hivyo kukoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha, Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara.

“Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume imeandaa chaguzi ndogo ili kujaza nafasi ya Mbunge iliyo wazi katika Jimbo la Konde na nafasi za udiwani kwenye Kata sita (06) za Tanzania Bara,” alisema taarifa hiyo ya Dkt. Mahera.

Kata zitakazohusika katika uchaguzi huo ni Kata ya Mbagala Kuu Jimbo la Mbagala Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kata ya Diringish iliyopo jimbo la Kiteto, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Kata ya Mitesa, Jimbo la Lulindi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Kata nyingine ni Kata ya Gare, jimbo la Lushoto Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kata ya Mchemo,Jimbo la Newala Vijijini, Wilaya ya Newala mkoani Mtwara na Kata ya Chona, Jimbo la Ushetu, Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga. 

 Maandalizi kwaajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa wagombea inaanza Juni 21 hadi 27,2021huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo ukifanyika  Juni 27 mwaka huu.

Aidha Dkt Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika jimbo la Konde na Kata utaanza Juni 28, 2021 na zitafikia ukomo wake Julai 17 mwaka huu na uchaguzi kufanyika 18 Julai,2021.

 Mahera alisema yayari Tume imekwisha vitaarifu Vyama vya Siasa kwa njia ya barua juu ya kuwepo kwa uchaguzi huo mdogo na inavikumbusha kuzingatia sheria, kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Miongozo na Maelekezo ya Tume wakati wote wa kipindi cha Uchaguzi.

Share:

NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI AWAJULIA HALI MAJERUHI BASI LA CLASSIC, AONYA MADEREVA KUENDESHA KWA MWENDOKASI


 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Khamis Hamza Chilo akizungumza na waandishi wa Habari ,alipotembelea kuona majeruhi wa ajali ya basi katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga

****

Na Marco Maduhu, Shinyanga

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Khamis Hamza Chilo, amesikitishwa na ajali ya basi la Classic iliyotokea jana mkoani Shinyanga, na kuonya madereva wa vyombo vya moto kuacha kuendesha mwendo kasi ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

Amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, alipotembelea majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga.


Amesema madereva wa vyombo vya moto wanapaswa muda wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa pale wanapokuwa na abiria, ili kutosababisha ajali ambazo hugharimu maisha ya watu.

“Katika ajali hii ya basi hapa mkoani Shinyanga, nimeambiwa chanzo chake ni mwendokasi hivyo nawaomba madereva wazitii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kugharimu maisha ya watu,”amesema Chilo


Naye Kaimu Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Dkt. Agostine Maufi, amesema katika majeruhi 26 waliowapokea jana, Sita wamepewa Rufaa ya kwenda kutibiwa Bugando Jijini Mwanza, na 20 waliobaki wanaendelea na matibabu na hali zao ni nzuri.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Debora Magiligimba, amesema Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Dereva wa basi hilo Maxison Mkuru, ambaye alikimbia mara baada ya kutokea ajali, ambapo wanamhoji na atachukuliwa hatua kali za kisheria.


Aidha katika ajali hiyo ya basi ambayo ilitokea jana katika jijiji cha Buyubi kona ya Didia wilayani Shinyanga, na basi la Kampuni ya Classic likitokea Kampala nchini Uganda kwenda Jijini Dar es salaam lilisababisha vifo vya watu wanne na kujeruhi watu zaidi ya 20.

Share:

Tanzania Na Uturuki Zanuia Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi

 


Na Mwandishi wetu, Dodoma
Serikali ya Uturuki imeahidi kushirikiana na Tanzania kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili Jamii hapa nchini ikiwemo mapambano dhidi ya ukatili kwa Wanawake na watoto.

Hayo yamebainishwa na Balozi wa Uturuki hapa nchini Dkt. Mehmet Gulluoglu alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Dkt.Gulluoglu ambaye pamoja na mambo mengine, amesema nchi yake kupitia wafadhili mbalimbali nchini Uturuki iko tayari kushiriki katika Maendeleo ya Tanzania hususan katika masuala ya Elimu, Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi na kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

 Awali, akizungumzia Shughuli zinazoratibiwa na Wizara yake, Katibu Mkuu Dkt. Jingu alisema Serikali imeanza kuwekeza katika Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi lengo likiwa kuboresha uchumi wa Kaya na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

" Serikali kupitia Wizara yetu, tumeanza ajenda ya kuwawezesha Wanawake kiuchumi kupitia afua mbalimbali ili kuhakikisha uchumi unapanda kuanzia ngazi ya kaya," alisema Dkt. Jingu.

Amesema katika kuhakikisha mipango hiyo inafakikiwa Serikali kupitia Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali imeanza kuwekeza katika Kilimo cha Parachichi kwenye mikoa ya Iringa,Njombe na Mbeya na Kilimo cha Alizeti kwa mikoa ya Singida na Dodoma huku Mkoa wa Kigoma ukitumika kwa Kilimo cha michikichi.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma kwa Wazee nchini, Dkt. Jingu amesema suala hilo ni moja ya Vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita ambapo amesema Serikali inahudumia makazi ya Wazee wasiojiweza 13 katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu Maendeleo ya Mtoto, amesema Jukumu la Serikali kupita Wizara ni kuhakikisha huduma na haki zao zinapatikana ikiwemo haki kwa watoto waliokinzana na Sheria.

Kuhusu  Mashirika Yasiyo ya Kiserikali,  Dkt. Jingu amesema Wizara inatoa miongozo na kuratibu uendeshaji wake ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa misingi ya Uwazi na Uwajibikaji.

Moja ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa ni Turkish Maarif Foundation  linalijishughulisha na masuala ya elimu ambalo kwa sasa linaendesha Shule katika Mikoa ya Dar Es Salaam, Arusha na Zanzibar.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo, Oguz Hamza amesema lengo lao ni kutoa elimu bora kwa Wanafunzi wa Tanzania kwa gharama nafuu.

Amesema Uturuki kuna Mashirika mengi yanayojihusisha na masuala mbalimbali ya Maendeleo ambayo yanaweza kuratibiwa ili kuongeza huduma zake nchini Tanzania.

Akifafanua kuhusu ushirikiano miongoni mwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Msajili wa Mashirika hayo hapa Nchini, Vickness Mayao amesema suala hilo linahitaji uratibu wa pamoja kulingana na maeneo husika huku vigezo na Masharti yakizingatiwa.

Mayao amesema pia kuwa kuna uwezekano wa Serikali kuingia Makubaliano kuhusu namna ya kushirikiana katika maeneo yanayokusudiwa.

MWISHO


Share:

Rais Samia Suluhu Hassan apokea Ujumbe Maalumu kutoka kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame,



Share:

Vyama vya Upinzani Israel vyakubaliana kuunda serikali ya muungano


Vyama vya upinzani nchini Israel, vimekubaliana kuunda serikali mpya, na hii inamaanisha kuwa uongozi wa muda mrefu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa miaka 12 unafika mwisho.


Kiongozi wa chama cha Yesh Atid cha mrengo wa kati Yair Lapid, ametangaza hatua hiyço baada ya vyama nane vya upinzani kukubali kuja pamoja na kuunda serikali hiyo mpya.

Wanasiasa hao wa upinzani wamekubaliana kuwa nafasi ya Waziri Mkuu miongoni mwao itakuwa kwa mzunguko, na kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha Yamina, Naftali Bennet, ndiye ataanza kushika madaraka hayo kabla ya kumkabidhi Bwana Yair Lapid.

Baada ya makubaliano hayo, Bwana Lapid amesema kuwa amemwarifu rais Reuven Rivlin kuwa amefanikiwa kuunda serikali ambayo ameeleza kuwa itawatumikia Waisraeli wote.

Kabla ya kuanza kazi, serikali hii mpya, itapigiwa kura na wabunge ili kuidhinishwa.

Iwapo serikali hiyo itashindwa kupata uungwaji mkono wa wabunge 120, basi itawazalimu Waisraeli wapige tena kura, utakuwa ni uchaguzi wa tano ndani ya miaka miwili ili kupata serikali.

Netanyahu amesema, makubaliano ya kuundwa kwa serikali hii mpya, kunahatarisha usalama wa Israel, baada ya chama chake cha Likud kushindwa kuunda serikali.



Share:

Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Mulamula Awasilisha Makadirio Ya Mapato Na Matumizi Bungeni Jijini Dodoma


Mheshimiwa Balozi Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo amewasilisha bungeni makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika Mkutano wa Bajeti unaoendelea jijini Dodoma. 

Akiwasilisha bungeni hotuba hiyo Balozi Mulamula ameeleza kuwa ili Wizara iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, analiomba Bunge Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 192,265,438,000. Kati ya fedha hizo shilingi 178,765,438,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 13,500,000,000 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

Aidha Balozi Mulamula ameyataja majukumu ambayo Wizara imeyapa kipaumbele kuyatekeleza katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, kama ifuatavyo;

  • Kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuwezesha balozi zetu kuwa kiungo muhimu cha kukuza uwekezaji, upatikanaji wa masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na kuvutia watalii; 
  • Kuendelea kuboresha na kuimarisha uhusiano na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa;
  • Kuendelea kuweka mazingira wezeshi, kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ili kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya nchi;
  • Kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Taifa letu ndani na nje ya nchi;
  • Kuendelea kushawishi na kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa nchi moja moja, jumuiya za kikanda na kimataifa;
  • Kuendelea kushiriki katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani duniani na maendeleo kupitia Umoja wa Mataifa;
  • Kuendelea kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya balozi zetu ili kupunguza gharama na kuleta mapato kwa Serikali;
  • Kuendelea kufungua ofisi za Balozi na Konseli Kuu mpya katika nchi za kimkakati;
  • Kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC);
  • Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara, masuala ya uhusiano wa kimataifa na utangamano wa kikanda; 
  • Kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara; na
  • Kuendelea kusimamia rasilimali watu na fedha Makao Makuu ya Wizara na Balozini.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha bajeti ya Wizara, jumla ya shilingi 192,265,438,000 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger