INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
WAFANYAKAZI
wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), wametakiwa kuanza
kujisafisha huku wakiambiwa kwamba taasisi hiyo haitaepuka kutumbuliwa
majipu.
Aidha,
wameagizwa kuwasilisha upya taarifa za mali zao kwa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, zifanyiwe uhakiki wa mali; moja baada ya
nyingine kubaini waliofanya udanganyifu wa umiliki wa mali zao.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki
alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa
viongozi wa taasisi hiyo.
Alisisitiza
kuwa tayari anazo taarifa zinazohitaji baadhi ya viongozi wa taasisi
hiyo kutumbuliwa majipu muda muafaka utakapowadia.
Kairuki
aliagiza taasisi hiyo kufanyia tathmini kesi zake zote, ilizowahi
kushindwa na kuja na majibu ya sababu za kushindwa na endapo itabainika
hazikushinda kutokana na mchezo mchafu wa wachunguzi, wahusika
wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo.
“Niliposikia
mnataja majina yenu wakati wa kujitambulisha, nilikuwa nafurahi sana
kwani wengi wenu nawajua na nina taarifa zenu. Haiwezekani wewe mtu
mmoja watu wengi wawe wanakuongelea vibaya. Msifikiri majipu humu
(Takukuru) hakuna, yapo na nawahakikishia tutayatumbua tu,” alisisitiza Waziri huyo.
Alisema
iwapo yupo mtumishi hasa viongozi wa taasisi hiyo, anayejitambua kuwa
ni ‘jipu’, ajisalimishe kwani akiendelea kusubiri na kutumbuliwa, mwisho
wake utakuwa mbaya.
“Tukiwatumbua
hali itakuwa mbaya kwani nyie mko chini ya Ofisi ya Rais, hata Rais (Dk
John Magufuli) hatasita kuwachukulia hatua si tu za kinidhamu bali hata
za kisheria,” alibainisha.
Alisema
katika taasisi hiyo, yapo maeneo mengi yanayohitaji kutumbuliwa majipu
kuanzia Uhasibu, Ukaguzi na Manunuzi zikiwemo ofisi za mikoani akitolea
mfano Mkoa wa Kilimanjaro na makao makuu, Upanga, Dar es Salaam.
“Tutasafisha
nawahakikishia hata ikibidi kuanza upya, ikitulazimu pia kufukuza wote
ikithibitika mnakwenda kinyume na maadili yenu tutawafukuza ila
hatutamwonea mtu, kwani wako watu wengi wenye sifa wanaotaka kufanya
kazi,” alisisitiza Kairuki.
Alisema
kuanzia sasa, ofisi hiyo itawekewa malengo ya utendaji wake na
kufanyiwa tathmini hasa kwa kesi zilizoshindwa ifahamike aliyezifanya,
sababu za kushindwa, iwapo imetokana na uzembe au kama upo mkono wa
mtu.
Alisema
imefikia wakati sasa watumishi wa taasisi hiyo wanapaswa sasa wale
kiapo cha ahadi ya uadilifu na kukisaini ili watakaoshindwa wachukuliwe
hatua za kinidhamu.
Taarifa za mali
Aliwataka
watumishi wote wa taasisi hiyo, kurejea upya kuwasilisha taarifa za
mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema
taarifa hizo zitapewa kipaumbele cha kuhakikiwa mali moja baada ya
nyingine na endapo mtumishi atabainika kufanya udanganyifu wa mali
anazomiliki, atachukuliwa hatua.
Alihadharisha
kuwa chombo hicho cha kupambana na rushwa hakipaswi kutuhumiwa kwa
rushwa. Alisema kikituhumiwa kwa sifa hiyo, ni sawa na kuigeuza Takukuru
kuwa jipu badala ya vidole vya kutumbulia majipu.
Takukuru mpya
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kuhakikisha inazalisha chombo
kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa chenye maadili.
Aliwataka
wanaoona hawawezi kwenda na kasi hiyo, wawasilisha barua zao za
kujiuzulu kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna wa Polisi
Valentino Mlowola.
Hata
hivyo, alisema Serikali inatambua kuwa kazi ya upelelezi na uchunguzi
ni ngumu kutokana na kukabiliwa na vishawishi vingi, jambo ambalo
wanahitaji ujasiri. Alisisitiza watumishi hao kutunza heshima yao na
chombo hicho.
“Faraja
ya uchunguzi ni kufanikisha majalada kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) na baadaye watuhumiwa kufikishwa mahakamani. Sasa ili kufanikisha
faraja hii ni vyema kufanya kazi kwa weledi na tusiwe na pupa ili mradi
tupeleke kesi nyingi kwa DPP na kuziwasilisha mahakamani,” alisema Kairuki.
Aliendelea,
“Nasema haya kwa sababu nafahamu bado kwenye uchunguzi hapa Takukuru
kuna upungufu. Nafikiri mmemuona Mheshimiwa Rais anavyoshughulikia suala
la rushwa na ufisadi, ni wajibu wenu Takukuru kufanikisha azma hii kwa
kuja na matokeo ya utendaji chanya.”
Aidha,
waziri huyo aliitaka taasisi hiyo kutumia weledi, sifa yaa ukachero wa
kiupelelezi na kiuchunguzi kufuatilia matukio yenye shaka yanayoendelea
mitaani na si kusubiri taasisi kubwa kuyavumbua.
“Nyie
ndio makachero tumieni ukachero wenu kuibua ufisadi, kuna mtu mmoja
amebainishwa na Rais lakini jina lake kwa umaarufu na utajiri wake
linatumika kama kituo, alishajiuliza sababu na kuchunguza?” alihoji.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mlowola aliwataka wafanyakazi wa
taasisi hiyo kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Kasi ya Magufuli
Aliwataka
wahakikishe wanaendana na kasi ya Dk Magufuli na Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ya utendaji na utumbuaji wa majipu katika maeneo yenye
ubadhirifu wa fedha, rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
“Natarajia
tutafanya kazi kwa weledi na si nguvu, kwa mfano taarifa zilizotolewa
katika maeneo ya bandarini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), siye
ndio tulitakiwa tuziwasilishe juu (ngazi ya Rais). Naomba tusisubiri
kuletewa,” alisisitiza.
Aliwataka watumishi hao kujiepusha kuwa watuhumiwa wa rushwa. “Jamani
hii ni mbaya kwetu Polisi akituhumiwa ujambazi ni mbaya sana, lakini
ofisa wa Takukuru akituhumiwa rushwa ni dhambi kubwa. Sisi tuwe watu wa
mwisho kutuhumiwa kwa rushwa."
Aliwataka
watumishi hao kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanaisaidia
Serikali kwenye eneo la upotevu wa fedha kwa kufuatilia matumizi na
miradi ya maendeleo na fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri na kwenye
manunuzi ya umma.
Alisema
katika utekelezaji wa jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa nchini
kwa mwaka 2014/15 taasisi hiyo ilipokea malalamiko 4,675. Ilifanyia
uchunguzi na kukamilisha majalada 667, kupeleka kwa DPP majalada 278,
walirejeshewa majalada 172 yenye vibali vya kufungua mashtaka na
kufungua kesi mpya 314 nchini kote.
Aidha
alisema taasisi hiyo ilishinda kesi 132 mahakamani na washitakiwa
walihukumiwa vifungo mbalimbali ikiwemo faini. Ziliokolewa Sh bilioni
saba zilizokuwa ziingie kwenye mifuko ya wabadhirifu wachache.
Ndani
ya siku 100 za Rais Magufuli madarakani taasisi hiyo ilipokea
malalamiko 411 kutoka kwa wananchi, imefungua mafaili 146 ya uchunguzi.
Imepeleka kwa DPP mafaili 103, mafaili 65 yenye kibali cha DPP
yamerejeshwa kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, jumla ya kesi 72 mpya
zimefunguliwa mahakamani na imeshinda kesi 40 na kushindwa kesi 52.
“Ndani
ya siku 100 tumefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 11 akiwemo
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Kipallo Kisamfu,” alisisitiza.