Wednesday, 15 July 2020

Serikali Kuendelea Kununua Mazao Ya Wakulima

...
Wakulima nchini wamehakikishiwa kuwa serikali itaendelea kununua mazao yao kwa ajili ya kuongeza hifadhi ya kutosha ili kuwa na uhakika na usalama wa chakula nchini.

Kauli hii ya serikali imetolewa jana wilayani Mbalali na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipotembelea kituo cha ununuzi zao la mpunga kijiji cha Uturo unaofanywa na Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula ( NFRA) kanda ya Makambako

“Serikali kupitia wizara ya Kilimo itaendelea kununua mazao ya wakulima hususan mahindi na mpunga kwa wingi hivyo wakulima msidanganywe kuwa muda umebaki mfupi wa kupeleka mazao yenu NFRA. Leteni hapa mpunga wenu tutaununua wote” alisema Kusaya.

Akiwa katika ghala la Ushirika Uturo Mbarali Katibu Mkuu huyo aliongea na wakulima wa mpunga na kuwahakikishia kuwa wizara imejipanga kuona nchi inaendelea kuwa na usalama wa chakula ndio maana anapita mikoani kujionea hali ya uzalishaji mazao

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Makambako Frank Felix alisema tayari wakala umeshanunua tani 1,700 za mpunga kati ya malengo ya tani 5,000 na mahindi tani 2,933.174 kati 25,000 msimu huu.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa mpunga Mbarali Said Nkenja alishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kununua mpunga kwani umesaidia kuongeza ushindani wa bei sokoni.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa uongozi wake unaowajali wakulima nchin.Leo Mbarali tunafurahia kuuza mpunga kwa NFRA tena bei ni nzuri .Tunaomba iendelee kununua zaidi mpunga upo mwingi tunavuna bado” alisema mkulima Said Nkenja.

Katika hatua nyingine  Katibu Mkuu Kusaya alitembelea  Chuo cha mafunzo ya Kilimo na Mifugo  ( MAMRE) cha Wanging’ombe mkoani Njombe  na kutoa agizo kuwa wanafunzi wanaoshindwa kulipa ada ya mafunzo wasifukuze badala yake utafutwe utaratibu rafiki.

Kusaya alitoa agizo hilo kufuatia malalamiko ya wanafunzi kusema baadhi yao wameshindwa kuendelea na masomo baada ya kushindwa kulipa ada na michango mingine.

“Vyuo vyote 29 ( 14 vya serikali na 15 vya binafsi) ni vyangu kwani vinalenga kuzalisha maafisa ugani watakaokwenda kuhudumia wakulima nchini.Nitaendelela kuvisaidia bila kuangalia nani  anakimiliki muhimu vitoe mafunzo bora kwa wanafunzi wa kitanzania” alisema Kusaya.

Kusaya aliusihi uongozi wa chuo cha MAMRE  kutafuta njia rafiki kuwasaidia wanafunzi wenye mazingira magumu yanayosababisha kutolipa ada kwa muda.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu huyo ameahidi kutoa kompyuta  ili kuwezesha kuanzisha maktaba mtandao ( e- learning) na kugharimia mwanafunzi mmoja kwenda kujifunza kanuni bora za ufugaji kuku kisasa katika vhuo cha Ihemi Iringa kwa gharama za serikali.

Katibu Mkuu amesema katika kuboresha mafunzo kwa vitendo atakipatia Chuo hicho Kitalu nyumba moja (Green House) ili wafundishe klimo cha mbogamboga na matunda ( horticulture).

Chuo cha MAMRE kina wanafunzi 103 wa ngazi ya astashahada na stashahada.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Geofrey  Mapesa alisema changamoto kubwa Kwa sasa ni kukosekana kwa mfumo wa udahili wa pamoja ( Central Admission System) hali inayopelekea upungufu wa wanafunzi.

Tayari wanafunzi 169 wamehitimu mafunzo ya kilimo na mifugo tangu chuo hicho kilipoanzishwa mwaka 2014 chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger