Wizara ya Afya, kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia Jumla ya shilingi bilioni 33.195 ili kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii hususani zilizopewa kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Akiwasilisha Hotuba ya Wizara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika mwaka wa fedha 2020/21 Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kuimarisha huduma na mafunzo kwenye Taasisi za Ustawi na Maendeleo ya Jamii, kukarabati makazi ya wazee, kujenga mahubusu za watoto na kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Alisema kuwa bajeti hiyo itasaidia kuimarisha Kujenga kumbi pacha na hosteli katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.7 zimetengwa, pia kuboresha utoaji wa mafunzo ya taaluma ya maendeleo ya jamii ili kukidhi mahitaji ya soko sambamba na kukuza ujuzi wa wahitimu ikiwemo kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa kutenga jumla ya shilingi bilioni 6.6.
Maeneo mengine yaliyotengewa fedha ni pamoja na ukarabati wa majengo na miundombinu katika makazi ya wazee kwa shilingi milioni 400, ujenzi wa Shule ya Maadilisho katika Mkoa wa Geita shilingi milioni 200, kuimarisha ujenzi wa mahabusu ya watoto katika mikoa ya Kigoma na Mtwara shilingi milioni 700 na kuwezesha Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuboresha utoaji wa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko shilingi milioni 250.
Aidha, jumla ya shilingi milioni 827.95 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Ili kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa kwa mwaka 2020/21, Wizara kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii imekadiria kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya Wizara ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa ofisi na miradi ya maendeleo” alisema.
Mhe. Ummy amesema Wizara imeendelea kukuza ari ya jamii kushiriki katika kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia nguvu kazi na rasilimali zinazowazunguka na kusimamia masuala yote ya ushirikishwaji wa jamii kwenye sekta mbalimbali.