Na Mwandishi Wetu - Dodoma
SERIKALI imeihakikishia Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na madawa ya kulevya kuwa itaendelea kuboresha huduma kwa waathirika wa madawa ya kulevya kupitia tiba ya Methadone.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Dkt.Leonard Subi, alipokuwa akijibu hoja za wabunge wa kamati hiyo inayoongozwa na Mhe. Oscar Mukasa walipofanya ziara kwenye kituo cha kuhudumia waathirika hao cha Itega, jijini Dodoma.
Amesema pamoja na kuwepo na kituo hicho pia Serikali inatarajia kufungua kituo cha Methadone mkoani Tanga mwezi Aprili mwaka huu.
Dkt.Subi amesema madawa ya kulevya ni vita ambayo inahitaji ushirikishaji wa sekta mbalimbali na ndio sababu wanatumia asasi zisizo za serikali ili kuwafikia watumiaji hao na kuwaleta kwenye vituo hivyo.
“Imesaidia sana kuwajenga kijamii na ndio maana kuna wengine wanasema ndoa ziliisha lakini kwasasa wanaishi na wake zao” amesema Dkt Subi.
Awali, akitoa taarifa ya kituo hicho, Mkurugenzi wa Hospitali ya Mirembe na Kituo cha Itega, Dk.Erasmus Mndeme, amesema waraibu hufika kituoni hapo kupitia asasi zisizo za serikali kama MEFADA, YOVARIBE na YCR.
Amebainisha kuwa kwasasa kituo kina waraibu 479 ambapo 367 wanatumia dawa ya methadone kila siku.
Ameeleza kuwa waraibu 26 wanaishi na Virusi vya Ukimwi(VVU), wanne waligundulika na Kifua Kikuu.
“Wengine 176 walipimwa homa ya ini ambapo 64 sawa na asilimia 36 waligundulika kuwa na homa ya ini aina ya B na C,”amesema.
Dk.Mndeme ameomba kamati hiyo kuwa mabalozi katika upatikanaji wa ajira na ushirikishwaji wa waraibu katika shughuli za kijamii ili wajiongezee kipato.
Naye, Meneja wa asasi isiyo ya kiserikali inayopambana na madawa ya kulevya(MEFADA), Alex Chitawala, amesema kuanzishwa kwa Kituo cha Itega kimeondoa kwenye mzunguko kiasi cha Sh. Bilioni 2.7 zilikuwa zikitumika na waraibu 367 kila mwaka kununua dawa ya heroin.
Amesema asasi zisizo za serikali zina mchango mkubwa katika kupambana na madawa ya kulevya na wamekuwa wakiwafuata kwenye vijiwe ili kuwaondoa na matumizi hayo.
“Kete moja ya heroin Dodoma inauzwa kwa Sh.7,000 na kiwango cha chini cha matumizi kwa mtu mmoja ni kete tatu kwa siku, hivyo zaidi ya Sh.Milioni 7.7 zimeokolewa kwa siku na Sh.Milioni 231 kwa mwezi na kwa mwaka ni Sh.Bilioni 2.7 tumeiondoa kwenye mzunguko wa dawa za kulevya,”amesema.
Amesema vita ya madawa za kulevya ni kubwa kwasababu wameondoa fedha kwa wauzaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Oscar Mukasa, ameshauri Serikali kuangalia kwa makini maambukizi ya homa ya Ini kwa waathirika hao kutokana na kuwa kwa kiwango kikubwa.
“Pia Tunahitaji kipimo cha pamoja ili kujua kiwango cha madawa za kulevya kikoje nchini kwasasa kutokana na jitihada zilizopo, maana tunaona kuna takwimu za maralia, Ukimwi, Kifua kikuu lakini kwa madawa ya kulevya hazipo” amesisitiza.
Kadhalika, Mraibu, Baraka Mandai ambaye ni mwalimu, ametaja sababu ya baadhi yao kurudi kwenye matumizi ya madawa hayo kuwa ni kutokana na kukosa kazi za kujiingizia kipato.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment