Friday, 4 October 2019

Watumishi 42 wakiwemo watendaji wa Kata na Vijiji Wafikishwa TAKUKURU Rukwa

...
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amekabidhi watumishi 42 wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Rukwa kwa uchunguzi wa upotevu wa fedha wa zaidi ya shilingi milioni 916 baada ya kuonekana utetezi wao juu ya upotevu wa fedha hizo kutokuwa na vielelezo vya kutosha.

Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo baada ya kuitisha kikao cha Wakurugenzi, Wawekahazina, wahasibu na watendaji wa vijiji na kata wa halmashauri zote nne mkoani hapa ambao mfumo wa ukusanyaji mapato ngazi ya halmashauri (Local Government Revenue Collection Information System – LGRCIS) kuonesha kuwa fedha za makusanyo yao kubaki mifukoni mwao.

Aidha, Ametoa siku saba kwa wale wote ambao hawajawasilisha fedha za makusanyo yao benki kuhakikisha wanawasilisha fedha hizo ikiwemo wale waliokabidhiwa kwa TAKUKURU na kuonya kuwa endapo fedha hizo hazitawasilishwa kesi hiyo itatoka TAKUKURU na Kuhamia Jeshi la Polisi ili kuwafikisha mahakamani.

“Mimi natafuta fedha ukishindikana tutakufunga, na ndio maana nimesema jambo hili kwanza lishughulikiwe kwanza na TAKUKURU mpaka uturudishie hizo fedha kwa muda maalum ambao nimeutoa, nimeshatoa siku sita zimeisha leo hii natoa siku saba nyingine, wacha hawa ambao watakuwa wamerudisha, wale ambao watakuwa hawajakabidhisha fedha zao, nitatoa siku saba baada ya hapo kesi hii itatoka TAKUKURU na kuhamia polisi ili iende mahakamani,” Alisema

Katika kujadili sababu mbalimbali zinazopelekea fedha za makusanyo kutumiwa bila ya utaratibu maalum mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Joseph Sengerema amesema kuwa matatizo ya upotevu wa fedha hizo yanasababishwa kutokana na kukiuka sheria ya fedha za Serikali za Mitaa ambayo hairuhusu Mtendaji kufanya matumizi yoyote bila ya ridhaa ya mkurugenzi wa Halmashuri na kabla ya kuwasilisha fedha hizo benki.

“ Ukiangalia katika Halmashuri ya Wilya ya Nkasi mimi nishatahadharisha kwamba, kuna hatari kubwa mtendaji wa kijiji anapokusanya fedha halafu anapeleka fedha hiyo kwa mtendaji wa kata bila ya kuwa na nyaraka maalum inayokiri upokezi wa fedha hizo, kwa hali hiyo unawezaje kusimamia ili fedha hizi zisipotee? Na pia mtendaji wa kata anapozifikisha idara ya fedha anahakikishaje zinfishwa benki kwa wakati?” Alihoji.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda limshukuru Mh. Wangabo kwa kuwasaidia kupambana na upotevu wa mapato katika halmashauri jambo ambalo wamekuwa wakilitolea maelekezo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya bila ya matunda.

“Usikivu wa watendaji wetu ni mdogo sana lakini nikuahidi kwamba maelekezo uliyoyatoa ya siku saba nitayafanyia kazi na kesho Defaulters (wadaiwa) wote tukutane pale ukumbi mdogo wa halmashauri ili niweze kuwakabidhini kwa Halmashauri ili Mkaanze utaratibu wa uchunguzi,” Alisisitiza.

Mmoja wa Watendaji hao Lusilus Bruno wa Kata ya Kirando, Wilayani Nkasi alikiri kuwepo kwa makosa ya kufanya matumizi kabla ya fedha hizo kufikishwa kwenye halmashauri jambo linalokwamisha kupokelewa kwa fedha pungufu wakati wa kuzipeleka benki na kusema kuwa upungufu huo unatokana na matumizi wanayoyafanya katika shughuli za kila siku za vijiji na kata.

“ Mtendaji wangu wa kijiji Tarehe 15 alinikabidhi shilingi 439,500/= ambazo tulitoa matumizi ya shilingi 150,000/= ambayo tuliandika dokezo kama kawaida na kumpa Mkurugenzi akakataa na kusema kuwa matumizi hayo ni makubwa, hilo deni likafika shilingi 540,100 kwa maana kwamba ile bili ilikuwa bado inasubiri ile 150,000 ili iende benki lakini mpaka jana ilikuwa bado makusanyo ni shilingi 100,800/= ambazo alinikabidhi kwahiyo tulishindwa kusafisha bili kwasababu ya upungufu wa shilingi 150,000,” Alisema.

Kati ya hao waliokabidhiwa TAKUKURU watumishi 22 ni watendaji wa kata na vijiji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, na watumishi 18 ni watendaji wa kata na vijiji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na mmoja ni mweka hazina na mhasibu wote wa Wilaya ya Nkasi na wengine 16 kutoka halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga walitakiwa kuandika maelezo pamoja na kuambatanisha vielelezo vya kuwasilisha fedha zao kwa mweka hazina wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. 

IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger