Thursday, 3 October 2019

MGANGA WA KIENYEJI ADAIWA KUBAKA MTOTO WA MIAKA 8 MAMA AKINUNUA WEMBE

...

Mganga wa kienyeji mkazi wa Ujiji, Venas Edward (48), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Kigoma kwa madai ya kumbaka mtoto msichana mwenye umri wa miaka minane.

Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Katoki Mwakitalu, mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana.

Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Raymond Kimbe, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba mahakama kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Akisoma maelezo ya awali Wakili wa Serikali Kimbe, alidai kuwa Aprili 23, mwaka huu majira ya asubuhi eneo la Kasoko-Ujiji, mshtakiwa huyo alimbaka mtoto huyo mwenye umri wa miaka minane na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.

Kimbe alidai siku ya tukio mtoto huyo alichukuliwa na mama yake mzazi (jina linahifadhiwa) na kwenda naye kwa mshtakiwa ambaye ni mganga wa kienyeji kwa ajili ya kupata matibabu.

Alidai baada ya kufika kwa mganga huyo mama wa mtoto aliambiwa aende kununua kiwembe dukani na kumuacha mtoto na mganga huyo, ambaye anadaiwa alitumia nafasi hiyo kumbaka mtoto huyo.

Kufuatia tukio hilo ilidaiwa mshtakiwa huyo alikamatwa na askari polisi na baada ya mahojiano alipelekwa mahakamani.

Wakili huyo alidai upande wa mashtaka unatarajia kupeleka mashahidi watano pamoja na kielelezo kimoja cha PF 3 na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikiliza mashahidi.

Hakimu Mwakitalu alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9 kwa kusikilizwa.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger