Waangalizi wa Kimataifa ambao wamekuwa wakifuatilia Uchaguzi Mkuu nchini Afrika Kusini, katika ripoti yao ya awali, wanasema Uchaguzi huo ulikuwa huru, haki na wa amani.
Ripoti hii imekuja siku mbili baada ya raia wa nchi hiyo kupiga kura tarehe nane ,na matokeo ya awali yanaonesha kuwa chama tawala ANC kinaongoza na kinaelekea kupata ushindi.
Mwenyekiti wa waangalizi wa Umoja wa Afrika, rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete, amesema kuwa zoezi la upigaji kura liliendelea kwa amani na utulivu katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa waangalizi wa Umoja wa Afrika wanasema Tume ya Uchaguzi ilijiandaa vema, kufanikisha Uchaguzi huu, huku maafisa wa usalama wakitoa ushirikiano wa kuhakikisha kuwa usalama unakuwepo kipindi chote cha upigaji kura.
Hata hivyo, Kikwete amesema vijana wengi hawakuonekana wakipiga kura licha ya kuwa ndio wengi nchini humo, suala ambalo Umoja wa Afrika unataka wadau kuliangazia.
“Licha ya mambo mengine, kwenda vizuri, tuliona kuwa vijana wengi hawakujitokeza kupiga, hili ni suala ambalo linastahili kupewa ufumbuzi wa haraka,” alisema Kikwete.
Waangalizi wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC pia walitoa ripoti yao ambayo pia imeeleza kuwa Uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.
Wachambuzi wa siasa barani Afrika, wamekuwa wakisema miaka ya hivi karibuni, waangalizi wa Uchaguzi wamekuwa wakitumia mbinu za kidiplomasia, kutuliza joto la kisiasa katika mataifa mbalimbali ya Afrika.
Chama cha ANC ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1994, kinatarajiwa kushinda Uchaguzi huo kwa kati ya asilimia 55-59 huku kile cha EFF kikitarajiwa kumaliza katika nafasi ya tatu.
Tume ya Uchaguzi inatarajiwa kutangaza matokea ya mwisho, mwishoni mwa wiki hii.
Chanzo - RFI
0 comments:
Post a Comment