Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema mfanyabiashara Abdul Nsembo maarufu kama Abdukandida ni papa (kinara) katika mtandao wa biashara ya dawa hizo na anajulikana katika nchi mbalimbali zikiwamo Brazil na Marekani.
Nsembo alikamatwa na DCEA Mei Mosi mwaka huu, usiku wa manane akiwa amejificha juu ya dari nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam, mpaka sasa anaendelea kushikiliwa na mke wake Shamim Mwasha kwa kudaiwa kukutwa na gramu kati ya 560 hadi 700 za heroin zilizopatikana baada ya kupekuliwa nyumbani kwao kwa muda wa saa sita kuanzia saa nane usiku hadi saa moja asubuhi.
Akizungumzia sakata hilo, Kamishina wa Operesheni wa DCEA, Luteni Kanali Fredrick Milanzi, amedai Nsembo ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokuwa wakiwachunguza na kuwatafuta kwa muda mrefu.
“Nyinyi mnamuona Nsembo ni mtu mdogo, Nsembo si mdogo katika mtandao wa dawa, ana network (mtandao) kubwa, ukiwauliza wenyewe watakwambia ni mjanja na amekuwa akifanya biashara hii kwa muda sasa, na huyu kijana pia tuliomkamata juzi sio mdogo ni mkubwa, yeye ndio anatumiwa na wakubwa, hawa watu kuwakuta na kilo mbili tatu si kitu cha ajabu, ingekuwa tunawakuta na gramu tatu mbili ndiyo tungesema wadogo,” amesema Luteni Kanali Milanzi.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment