Thursday, 4 June 2026
Wednesday, 3 June 2026
TEMESA NA TOYOTA WAJADILI MAGEUZI YA HUDUMA ZA MATENGENEZO YA MAGARI NCHINI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania - TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, leo tarehe 02 Juni 2026 amekutana na viongozi wa kampuni ya TOYOTA Tanzania katika ofisi zao eneo la Posta, jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili kuhusu jitihada za Serikali katika kuendelea kuboresha huduma za matengenezo ya magari hapa Nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mahimbali amesema TEMESA imejipanga kuhakikisha huduma za ufundi na matengenezo ya magari ya Serikali zinatolewa kwa viwango vya juu kwa kutumia teknolojia za kisasa na za viwango vya kimataifa.

“TEMESA inaona fursa kubwa katika kuimarisha ushirikiano na TOYOTA kupitia miradi ya pamoja itakayowezesha taasisi hizi mbili kubadilishana utaalamu kwa mafundi na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wadau wetu,” amesema Mtendaji Mkuu.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TOYOTA Tanzania, Bw. Jatin Pandya amehakikisha utayari wa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na TEMESA katika mafunzo ya kitaalamu kwa mafundi, ushauri wa kiufundi, matumizi ya teknolojia mpya na kuimarisha mifumo ya usalama wa magari.

“Sisi TOYOTA tunatanguliza usalama wa watumiaji wa magari na ubora wa huduma. Tunaamini ushirikiano huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za matengenezo ya magari nchini na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani,” amesisitiza Pandya.

Aidha, mara baada ya kikao hicho, Mtendajji mkuu pia alipata fursa ya kufanya ziara fupi katika karakana za TOYOTA ili kujionea teknolojia mpya zinazotumika katika matengenezo ya magari.
Miongoni mwa mambo waliyojadili katika kikao hicho ni pamoja na uwezekano wa kuanzisha ushirikiano kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi - PPP. Hatua inayotarajiwa kuimarisha uwezo wa karakana na kuongeza ufanisi wa huduma katika sekta ya matengenezo ya magari.
Kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya TEMESA na TOYOTA, huku kikitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi makubwa katika sekta ya ufundi wa magari nchini.
VYUO VIKUU MALAYSIA VYAANZA MAONESHO YA ELIMU DAR
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tanzania na Malaysia zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika elimu ya juu kupitia ubia wa vyuo vikuu, tafiti za pamoja, ubadilishanaji wa wanafunzi na wahadhiri, ufadhili wa masomo pamoja na ushirikiano katika sayansi na teknolojia.
Akizungumza katika kikao cha Kuimarisha Ushirikiano wa Elimu ya Juu Kati ya Tanzania na Malaysia** kilichofanyika katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema ujio wa ujumbe wa elimu kutoka Malaysia ni wa wakati muafaka wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha na kutangaza kimataifa mfumo wake wa elimu ya juu.
Kikao hicho kiliandaliwa na kuratibiwa na Education Malaysia Global Services (EMGS), chini ya Wizara ya Elimu ya Juu ya Malaysia, kwa kushirikiana na Global Education Link Ltd (GEL).
Prof. Mushi amesema ujio wa ujumbe huo umevitambulisha vyuo vya Malaysia nchini Tanzania na kutoa nafasi kwa pande zote mbili kujadili maeneo ya ushirikiano yatakayowanufaisha wanafunzi, wahadhiri na taasisi za elimu ya juu.
Amesema Tanzania inatarajia kuona ushirikiano utakaoimarisha programu za pamoja, kubadilishana maarifa, tafiti, ubunifu na kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu nchini.
Kwa mujibu wa Prof. Mushi, Malaysia imepiga hatua kubwa katika kutumia elimu, teknolojia na ujuzi kama nyenzo ya mageuzi ya kiuchumi, jambo ambalo Tanzania inaweza kujifunza katika safari yake ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa na teknolojia.
Amesema kipaumbele kinapaswa kuwekwa katika kuwaandaa wanafunzi wa Tanzania kwenye maeneo ya sayansi, hisabati, kemia, sayansi ya takwimu, ujifunzaji wa mashine na akili mnemba.
Aidha, amesema wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya nchi wanapaswa kuandaliwa si kitaaluma pekee, bali pia kilugha na kitamaduni ili waweze kushindana na kufanikiwa katika mazingira ya kimataifa.
“Ushirikiano wa aina hii ni muhimu kwa sababu unawapa wanafunzi na taasisi zetu nafasi ya kupata maarifa mapya, mifumo mipya na njia mpya za kujenga rasilimali watu kwa maendeleo ya taifa,” amesema Prof. Mushi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Stephen Maluka, amesema kikao hicho kimetoa jukwaa la vitendo kwa taasisi za Tanzania na Malaysia kujadili namna bora ya kujenga ushirikiano rasmi.
Amesema majadiliano yamelenga kuanzisha mahusiano ya moja kwa moja kati ya vyuo vikuu, wizara na taasisi za elimu kutoka nchi zote mbili kwa lengo la kuendeleza elimu, sayansi na teknolojia.
Prof. Maluka amesema Tanzania inahitaji ushirikiano unaokwenda zaidi ya udahili wa wanafunzi na kuingia katika maeneo ya tafiti za pamoja, programu za pamoja, ufadhili wa masomo, ubadilishanaji wa wahadhiri, maboresho ya mitaala na ushirikiano wa kitaaluma.
Amesema ufadhili wa masomo utasaidia wanafunzi wa Tanzania wenye sifa kupata nafasi za masomo Malaysia, hususan katika maeneo ambayo nchi hiyo imepiga hatua kubwa.
Aidha, amesema ubadilishanaji wa wahadhiri unaweza kusaidia kuongeza ubora wa ufundishaji, usimamizi wa tafiti na kuwapa wanataaluma uzoefu wa mifumo tofauti ya elimu ya juu.
Prof. Maluka ametaja teknolojia, sayansi ya takwimu na akili mnemba kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya ushirikiano wa baadaye.
Amesema ushirikiano katika maeneo hayo unaweza kusaidia Tanzania kuongeza uwezo katika teknolojia chipukizi na kuwaandaa wahitimu kwa dunia inayoongozwa na ubunifu na mabadiliko ya kidijitali.
“Sasa ni muhimu kutoka kwenye mazungumzo ya jumla na kuingia kwenye mifumo ya utekelezaji itakayoongoza ushirikiano kati ya taasisi,” amesema Prof. Maluka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link Ltd, Bw. Abdulmalik Mollel, amesema GEL inajivunia kuratibu mpango huo unaounganisha taasisi za Tanzania na vyuo vikuu pamoja na mamlaka za elimu kutoka Malaysia.
Amesema mpango huo hauhusu kutangaza fursa za kusoma Malaysia pekee, bali pia kujenga daraja la muda mrefu la elimu kati ya Tanzania na Malaysia.
“Ushirikiano huu unalenga kujenga daraja la kweli kati ya Tanzania na Malaysia katika elimu ya juu. Tunataka kuona vyuo vya pande zote mbili vikishirikiana katika tafiti, programu za kitaaluma, ubadilishanaji wa wanafunzi, ubadilishanaji wa wahadhiri na mafunzo yanayotegemea teknolojia,” amesema Mollel.
BEI YA PETROLI YASHUKA, SERIKALI YAWEKA RUZUKU KWENYE DIZELI
Na mwandishi wetu
Watumiaji wa petroli wamepata afueni mwezi Juni 2026 baada ya bei ya mafuta hayo kushuka ikilinganishwa na mwezi uliopita. Kwa Dar es Salaam, petroli sasa itauzwa kwa bei kikomo ya shilingi 4,086 kwa lita, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama kwa watumiaji wa kawaida na baadhi ya shughuli za usafiri.
Kwa upande wa dizeli, watumiaji wanakabiliwa na ongezeko dogo la bei, ambapo kwa Dar es Salaam bei kikomo imefikia Shilingi 4,333 kwa lita. Ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia pamoja na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa hiyo.
Licha ya changamoto hizo za kimataifa, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kulinda uchumi na wananchi kwa kuweka ruzuku ya Shilingi 534.91 kwa kila lita ya dizeli. Hatua hiyo imelenga kupunguza athari za ongezeko la bei kwa sekta muhimu kama usafirishaji, viwanda na huduma za kijamii.
Mabadiliko haya yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, vinavyohusisha Marekani, Israeli na Irani. Mgogoro huo umeathiri uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji wa mafuta duniani, huku kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz kukiongeza gharama za usafirishaji na bima za meli za mafuta.















