Thursday, 12 March 2026

CCM SHINYANGA MJINI YAENDELEA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO, YATAKA IKAMILIKE KWA WAKATI

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe akipokea taarifa ya mradi

Na Mapuli Kitina Misalaba

Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imeendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa ya Shinyanga, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.

Ziara hiyo imefanyika leo Machi 11, 2026 ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe, na kuhusisha viongozi mbalimbali wa Manispaa na Wilaya.

Kamati imeanza ziara kwa kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo katika Shule ya Awamu na Msingi Mwengi iliyopo mjini Shinyanga ambapo Mwenyekiti Makombe amepongeza hatua za mradi huo.

Baada ya hapo, kamati imetembelea ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Kolandoto, Kata ya Kolandoto ambapo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe ameeleza kuwa zahanati hiyo ni muhimu kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa haraka na karibu na makazi yao.

Kamati pia imekagua mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi unaotekelezwa na SHUWASA katika Kata ya Kolandoto na kwamba Mwenyekiti Makombe amesisitiza kuwa maji safi ni muhimu kwa afya ya wananchi na maendeleo ya kijamii, hivyo mradi lazima ukamilike kwa wakati na bila dosari za kiufundi.

Ziara ilihusisha ukaguzi wa mradi wa TANESCO wa upanuzi wa umeme katika eneo la Ibadakuli ambapo Samweli Jackson Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini amepongeza juhudi za serikali na TANESCO huku Mwenyekiti Makombe akihimiza uwajibikaji wa mara kwa mara ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi wapate umeme wa uhakika.

Kamati pia imetembelea Shule ya Sekondari Rajani iliyopo Kata ya Ibadakuli ili kukagua ujenzi wa mabweni mapya huku Makombe akisema mabweni ni muhimu kwa kutoa hifadhi salama kwa wanafunzi na kuhamasisha malezi bora.

Ziara hiyo imemalizika kwa kukagua ujenzi wa jengo la wahandisi katika Manispaa ya Shinyanga ambapo Mwenyekiti Makombe ameridhika na hatua ya mradi huo.

Ziara hiyo imehusisha viongozi mbalimbali: Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Mhe. Anord Makombe; Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Mzee Fue Mrindoko; Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga; Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Salum Kitumbo; Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Doris Kibabi,
Samweli Jackson Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjinin a viongozi wengine wakiwemo kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga.

Mwenyekiti Makombe amesisitiza kuwa Kamati itaendelea kufuatilia kila mradi ili kuhakikisha malengo ya maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga yanatimizwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ambaye ni katibu wa jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini Bi. Doris Kibabi, amepongeza utekelezaji wa miradi inayotekelezwa katika Manispaa ya Shinyanga.

Doris amebainisha kuwa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema miradi hiyo, ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni na miundombinu ya majisafi, ni ishara ya dhahiri ya ahadi za chama kufikiwa na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Shinyanga huku akiwataka wananchi kushirikiana na viongozi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Ziara ya siku mbili ya Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini imehitimishwa leo ambapo viongozi wamesisitiza kuwa ufuatiliaji wa miradi hiyo utaendelea ili kuhakikisha kila mradi unakamilika kwa wakati, unaendana na viwango vya ubora na kwamba wananchi wanapata huduma zinazotarajiwa. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Mwenge Manispaa ya Shinyanga Hassan Hemed akisoma taarifa fupi ya mradi huo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Mwenge Manispaa ya Shinyanga Hassan Hemed akisoma taarifa fupi ya mradi huo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi katika shule ya msingi Mwenge mjini Shinyanga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko akizungumza.
Ziara ya kutembelea na kukagua mradi katika shule ya awali na msingi Mwenge ikiendelea.
Jengo la zahanati katika Kijiji cha Kolandoto, Kata ya Kolandoto ambapo ujenzi unaendelea.
Mwenyekiti Makombe akipokea taarifa ya ujenzi wa jengo hilo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Samweli Jackson akizungumza.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya.
Kaimu Mkurugenzi mamlaka hiyo Mhandisi Uswege Musa, akizungumza.
Kaimu Mkurugenzi mamlaka hiyo Mhandisi Uswege Musa, akisoma taarifa ya mradi huo.
Ziara ikiendelea.
Mradi wa TANESCO wa upanuzi wa umeme katika eneo la Ibadakuli.

Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Samweli Jackson akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi wa TANESCO katika Kata ya Ibadakuli.
wenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko akizungumza ambapo amepongeza hatua nzuri ya mradi huo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe akipongeza weledi na kasi ya mradi huo kuwa unaridhisha.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Said Kitinga, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya.
Mabweni mapya katika shule ya Sekondari Rajani iliyopo Kata ya Ibadakuli.

Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Kibabi akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa mujibu wa Ilani ya CCM.

Ziara ikiendelea.

Shule ya Sekondari Rajani iliyopo Kata ya Ibadakuli.

Mwenyekiti Makombe na kamati yake baada ya kuwasili katika mradi wa ujenzi wa jengo la wahandisi.


Share:

Wednesday, 11 March 2026

SAUTI ZA DHAHABU: RAIS SAMIA AFUNGUA UKURASA MPYA WA UTU KWA MAGWIJI BITCHUKA NA ZAHIR ZORRO



Katika ulimwengu wa muziki wa dansi nchini Tanzania, majina ya Hassan Bitchuka na Zahir Zorro si majina ya kawaida. Hizi ni tunu za taifa; ni sauti zilizobeba huzuni, furaha, na mafundisho ya jamii ya Kitanzania kwa zaidi ya miongo minne.

Wiki hii, tasnia ya sanaa imeshuhudia mguso wa kipekee wa kibinadamu kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kupitia kwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, amemfikia Hassan Bitchuka nyumbani kwake Sinza Mori, Dar es Salaam.

Hassan Bitchuka, fundi wa mashairi na mwimbaji aliyepata kutamba na bendi za DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’, Msondo Ngoma, na OSS, kwa sasa anapambana na maradhi. Rais Samia amemtumia kiasi cha Shilingi milioni 10 kama mkono wa pole na msaada wa matibabu.

"Rais anathamini mchango usiopimika ambao Bitchuka ametoa kuijenga sanaa ya Tanzania," alisema Mwana FA wakati akikabidhi msaada huo. Hili si jambo dogo; ni ishara kuwa serikali sasa inahamia kwenye falsafa ya "Kazi na Utu"—kutambua kuwa msanii ni binadamu anayehitaji kuthitimiwa wakati wa uhai wake.

Ukitaja Sikinde huwezi kumuacha Bitchuka. Ukitaja darasa la uimbaji lenye weledi, huwezi kumuacha mzee Zahir Zorro. Hawa ni watu walioweka misingi ya muziki wa dansi (Tanzania Rumba) ambao leo hii unarithishwa kwa vizazi vipya.

Bitchuka anajulikana kwa uwezo wake wa kutunga mashairi yenye falsafa nzito na sauti iliyokaa kimamlaka jukwaani wakati Zahir Zorro ni gwiji aliyebobea katika uimbaji wa sauti za juu na uandishi wa nyimbo zinazogusa hisia, huku akiwa ameacha mrithi kama Banana Zorro anayeendeleza kipaji hicho.

Hatua ya Rais kuwakumbuka magwiji hawa, inarejesha heshima ya taaluma ya sanaa ambayo kwa muda mrefu ilionekana kusahaulika pindi wasanii wanapostaafu au kuugua.

Katika mwendelezo huo huo wa kuthamini alama za wasanii, Rais Samia alitumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kumzawadia mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Bibi Flora Mtegoa, gari jipya aina ya Harrier (New Model).

Hii ni ujumbe tosha kwa jamii kwamba hata kama msanii ametangulia mbele za haki, alama aliyoiacha (Legacy) bado inatambulika na serikali yake, na familia yake haitaachwa pweke.

Tunapongeza hatua hii ya Rais Samia. Kuwajali magwiji wetu wakati bado wapo nasi ni kitendo cha kishujaa. Inatuma ujumbe kwa wasanii vijana kuwa ukifanya kazi kwa uaminifu na uzalendo, taifa lako litakukumbuka.

Tunamtakia Hassan Bitchuka nafuu ya haraka na tunazidi kuwaombea magwiji wetu wote maisha marefu yenye amani.
Share:

KANISA KATOLIKI LAJITENGA NA UOVU WA KISIASA


Na mwandishi wetu, Mara

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Mkoani Mara Michael Msonganzila amesema Kanisa hilo haliruhusu kikundi chochote kuingia Kanisani kikiwa kimevalia sare za Chama cha siasa kwani Kanisa hilo halifungamani na upande wowote wa kisiasa isipokuwa lina waumini ambao ni wanasiasa na wanachama wa Vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Askofu Msonganzila ametoa kauli hiyo mara baada ya Wanawake wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAWACHA) kuingia kwenye ibada ya Jumapili ya Machi 08, 2026 katika Kanisa Kuu la Jimbo la Musoma Mjini wakiwa wamevalia sare zao na baadae kutaka kufanya Mkutano na waandishi wa habari ndani ya eneo la Kanisa, suala ambalo lilisababisha mvutano kati yao na Jeshi la Polisi Mkoani Mara.

"Jumapili imefika hawa BAWACHA, bila sisi kufahamu kikanisa kama wamekuja pale Kanisani kwangu, wakaingia Kanisani na nadhani walibaini kuwa wanafuatiliwa na ninaambiwa hawakuingia getini na mavazi ya Kanisa, waliingia kawaida na wakaenda mafichoni ndani ya Kanisa wakavaa mavazi ya Chadema na baadae wakaingia kanisani na wameshiriki ibada."

"Kanisa tuna kanuni moja, haturuhusu mambo ya siasa yafanyike Kanisani lakini wakati mwingine tunaongozwa na busara na hekima ya hali ya juu na ndio maana aliyeongoza ibada hakusema ninyi mliovaa hivi ondokeni. 

Alishangaa baada ya misa wametoka halafu ghafla wanataka kufanya mahojiano na waandishi wa habari, kitu ambacho baadhi ya walei waliona si kitu cha kawaida." Amekaririwa akisema Baba Askofu Msonganzila.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari Jumanne Machi 10, 2026, Askofu Msonganzila amesema binafsi anaamini kuwa masuala au malalamiko ya kisiasa yalipaswa kutolewa ndani ya Ofisi ya Chadema tofauti na awali walivyokuwa wakitaka kufanyia Mkutano wao wa wanahabari ndani ya Viunga vya kanisa, akihoji kupatikana kwa Mwandishi huyo wa habari ikiwa aliandaliwa ama lah na ni kwanini aende kufanyia kazi zake ndani ya Kanisa Katoliki.

Akizungumzia kuhusu Kanisa kuruhusu Wanawake wa Chadema kufanya Kongamano lao katika Viwanja vya Matumaini kwa Vijana, uwanja unaomilikiwa na Kanisa hilo, Askofu Msonganzila amesema awali waliruhusu uwanja huo kutumika kwani hawakuwa wakifahamu kuhusu zuio la serikali kutokana na maamuzi ya Mahakama.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger