Monday, 28 April 2025

RAIS SAMIA SULUHU AHAMASISHA HUDUMA BURE ZA SARATANI KWA WANANCHI WA KILWA


Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Ocean Road wakiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Wilayani Kilwa Mkoani Lindi katika hatua ya kupeleka huduma ya ugonjwa wa Saratani kutokana na maagizo ya Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Mkoani Lindi

Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi.

Timu ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Ocean Road, wakitimiza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wametembelea Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo. 

Mazungumzo hayo yamehusu maandalizi ya zoezi la utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya saratani kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa, zitakazotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga kwa muda wa siku tatu kuanzia leo, tarehe 28 hadi 30 Aprili 2025.

Huduma hizo, ambazo zitatolewa bure, zinalenga kupambana na kuikomboa jamii dhidi ya magonjwa hatari ya saratani kama vile saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya tezi dume, saratani ya ngozi na aina nyinginezo. 

Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia wananchi wa maeneo ya vijijini bila gharama, huku pia likiwa na lengo la kutoa rufaa za moja kwa moja kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya ngazi ya juu zaidi katika hospitali kubwa nchini.

Akizungumza na madaktari hao, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Kilwa, Ndg. Yusuf Mwinyi, ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo huo muhimu wa afya kwa wananchi. 

Amesisitiza kuwa msaada huo utawezesha jamii kupata huduma za kibingwa bila malipo, tofauti na hapo awali ambapo ilihitajika kuwa na  safari ndefu na gharama kubwa kupata huduma hizo. 

Ameahidi ushirikiano wa ofisi yake kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Hemedi Magaro, amewapongeza madaktari hao kwa kujitokeza kutoa huduma kwa wananchi wa Kilwa.

 Amewataka watumishi wa umma na wananchi wote wa Wilaya ya Kilwa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo adhimu ya kupima afya zao bure. 

Aidha, ameeleza kuwa viongozi wa Wilaya wapo tayari kushirikiana kikamilifu na timu ya madaktari kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa kiwango cha juu.

 

Share:

ELIMU YA GESI ASILIA KWENYE MAGARI YAWAVUTIA WENGI MAONESHO YA WIKI YA USALAMA MAHALA PA KAZI, SINGIDA.

Katika kuadhimisha Wiki ya Usalama Mahala pa Kazi, kampuni ya GASCO imeendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi salama na nafuu ya gesi asilia, hasa kwenye vyombo vya moto. 

Katika banda la GASCO, wananchi walijitokeza kwa wingi kujifunza zaidi kuhusu teknolojia ya kutumia Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) kama mbadala wa mafuta ya petroli na dizeli. 

Akizungumza mbele ya wageni mbalimbali waliotembelea banda hilo, Mhandisi Hassan Temba alifafanua faida nyingi za matumizi ya gesi asilia kwenye magari ikiwemo kuokoa gharama.

"Gesi asilia ni salama zaidi kwa mazingira, inapunguza gharama za uendeshaji wa magari kwa zaidi ya asilimia 50, na inapunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa mazingira," alisema Temba. 

Aidha Temba, alisisitiza kuwa usalama wa matumizi ya gesi asilia umepewa kipaumbele, ambapo magari yanayofungwa mifumo ya gesi hupitia taratibu za ukaguzi wa kina na zinazozingatia viwango vya juu vya usalama vya kitaifa na kimataifa. 

Mhandisi Temba akitoa ufafanuzi  wa matumizi ya gesi kwenye magari kwa wannachi waliotembelea banda la GASCO

Wananchi wamehimizwa kutokuwa na hofu juu ya upatikanaji wa gesi asilia kwa magari yao, kwani TPDC imejipanga vizuri kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa uhakika ikiwa ni pamoja na kushirikisha  sekta binafsi na taasisi nyingine ili kupanua mtandao wa vituo vya kujaza gesi nchini.

Katika hatua muhimu ya kuendeleza matumizi ya nishati safi na salama nchini, Afisa Maendeleo ya jamii Bw. Oscar Mwakasege ameeleza kuwa TPDC  imekamilisha ujenzi wa kituo mama cha gesi asilia eneo la Chuo kikuu Dar es salaam kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya vyombo vya moto.  

‘‘Kituo hiki kitaongeza unafuu kwa watumiaji hali itakayochochoea kukua kwa uchumi na kuongeza tija kwa wananchi katika sekta ya usafirishaji.

Kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia magari zaidi ya 1000 kwa siku na kusambaza bidhaa hiyo kwa vituo vingine ni dhahiri kitasaidia kupunguza kero waliyokuwa wanapata watumiaji wa vyombo vya moto. Ujenzi wa kituo hiki ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi asilia kama mbadala wa nishati ya mafuta. Alisema Oscar. 

Muonekano wa Kituo mama cha gesi asilia kwenye Vyombo vya moto, eneo la Chuo kikuu Dar es salaam.

 Hatua hii ni fursa kwa wananchi, wafanyabiashara, na sekta ya usafirishaji kupunguza gharama za uendeshaji na kuchangia katika kupunguza uchafuzi wa mazingira. 

Kwa sasa, TPDC inaendelea na ujenzi wa kuongeza idadi ya vituo vidogo vinavyopokea gesi kutoka kituo hiki mama na kusambaza kwa watumiaji katika maeneo mbalimbali ya mijini na pembezoni, hivyo kuongeza urahisi wa kupata huduma hiyo popote walipo.

Share:

WAZIRI KIKWETE AIPONGEZA BARRICK KWA MATUMIZI TEKNOLOJIA ZENYE USALAMA MIGODINI


Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira , Kazi na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete akipata maelezo moja ya kifaa cha kukaa kinavyofanya kazi kwenye migodi ya Barrick North Mara
Mtaalamu wa Afya na Mazingira kutoka Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Aristides Medard (Kushoto) akifafanua jinsi mgodi huo wa Barrick unavyofanya shughuli za uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu , vifaa na mitambo ya kisasa na akili mnemba kwa Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa Maonesho yanayoendelea na Afya na Usalama mahali pa kazi yanayoratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama wa Mahali pa kazi (OSHA) katika viwanja vya Mandewa mjini Singida
Mrakibu Mwandamizi wa Usalama wa Mgodi wa North Mara, Bw. Meshack Issack (kushoto) akitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu akili mnemba inavyotumika kwenye uchimbaji wa madini kwenye migodi ya Barrick kwa Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira , Kazi na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete kwenye maonesho ya usalama mahali pa kazi yanayoendelea kwenye viwanja vya Mandewa mjini Singida

***
Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu) , Mhe Ridhiwani Kikwete ameipongeza migodi ya Barrick yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga nchini kwa kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia Akili Mnemba (AI) na vifaa, mitambo ya kisasa ya kijiditali na kulinda usalama na afya za wafanyakazi wake mahali pa kazi.

Amesema hayo alipotembelea banda la Barrick kwenye maonesho ya OSHA yanayoendelea kwenye viwanja Mandewa mjini Singida na kusisitiza umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa teknolojia ili kulinda afya za wafanyakazi kwenye sehemu zote za kazi kama vile migodi, viwandani na sehemu zingine.

“Huko nyuma mlikuwa mnakwenda wenyewe chini kwenye uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi lakini sasa mnatumia mitambo ili kuweza kufanikisha kazi hii, hongereni sana kwa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi,” amesema Kikwete alipokuwa kwenye Banda la Barrick Bulyanhulu.

Mhe. Kikwete aliongeza kwamba juhudi za Barrick nchini kwa kushirikiana na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) zimefanikisha kuwepo mazingira rafiki ya ufanyaji kazi ambayo ni chachu katika kuleta mabadiliko Chanya katika sekta ya uchimbaji wa madini,

“Natoa wito kwamba elimu hii ya afya na usalama mahali pa kazi inayoendelea kutolewa kupitia maonesho haya iendelee kutolewa nchini nzima ili kupanua wigo wa uelewa kwa watanzania hasa wafanyakazi katika sekta mbalimbali hapa nchini katika kukabiliana na ajali na majanga sehemu za kazi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Aristides Medard, Mtaalam wa Afya na Mazingira kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu amemweleza Waziri Kikwete na ujumbe wake kuwa kwa kutumia akili mnemba mgodi huo unaendesha shughuli zake kwa ufanisi na usalama zaidi hali ambayo inawapa motisha wafanyakazi kufanya kazi kutokana na mazingira kuwa rafiki.

Naye Mrakibu Mwandamizi wa Usalama, Bw. Meshack Issack kutoka Mgodi wa North Mara amesema mgodi huo ni kinara wa matumizi ya kidigitali na akili mnemba na mifumo ya kimataifa katika uchimbaji wa madini na afya na usalama nchini.

Ameongeza kwamba mgodi huo na migodi mingine yote ya Barrick inatekeleza program ya “Journey to Zero” ambayo inalenga kuhakikisha kila mfanyakazi anakuwa salama kazini hadi anaporudi nyumbani na kupaza sauti kunapokuwepo na viashiria vya mazingira hatarishi kwenye maeneo ya kazi.

“Hii programu ya “Journey to Zero” ni DNA ya kampuni inawahusu pia wakandarasi wa Barrick ,wageni wanaotembelea migodi yetu na jamii nzima kwa ujumla”, amesisitiza.
Share:

MKURUGENZI JAMII AFRICA : UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NI HAKI, SI HISANI...ATAHADHALISHA MATUMIZI MAKUBWA YA AKILI MNEMBA WAKATI WA UCHAGUZI

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo amesema uhuru wa vyombo vya habari si hisani bali ni haki ya msingi ambayo kila mwananchi anapaswa kuipata na kuitetea akisisitiza kuwa dunia ya leo inahitaji zaidi uwezo wa kuchambua, kutathmini na kuelewa taarifa kwa undani, kuliko wakati mwingine wowote.

Akizungumza leo Aprili 28, 2025 katika mjadala maalum kuhusu Athari za Akili Mnemba (AI) katika Mustakabali wa Uandishi wa Habari wakati maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayoendelea katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha, Melo amesema mapambano ya kulinda uhuru wa habari hayawezi kuachiwa waandishi peke yao bali ni jukumu la jamii nzima.

“Uhuru wa habari hauwezi kuonekana kama zawadi inayotolewa kwa neema. Ni haki yetu ya kuzaliwa kama binadamu huru. Katika enzi ya taarifa nyingi, akili mnemba ndiyo silaha kuu ya kulinda uhuru huu,” amesisitiza Melo.

Mageuzi ya Vyombo vya Habari

Melo ameelezea kuwa tasnia ya habari imepiga hatua kubwa, kutoka kwenye magazeti, redio na televisheni hadi kwa watengeneza maudhui wa kidijitali kama wanablogu, vloggers na podcasters.

Katika hali hii mpya, amesema, uhuru wa habari haupaswi kulindwa kwa vyombo vya habari vikuu pekee, bali kwa wote wanaoshiriki kusambaza taarifa kwa umma.

“Kila mmoja anayeshiriki katika mnyororo wa mawasiliano ya kisasa waandishi huru, wapiga picha, vloggers , anapaswa kuheshimiwa na kulindwa chini ya kanuni za uhuru wa habari,” amesema.

Umuhimu wa Akili Mnemba

Kaulimbiu ya mwaka huu, "Uhabarishaji katika Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba kwenye Uhuru wa Vyombo vya Habari", inaangazia hitaji la kutumia akili mnemba kuchuja taarifa za kweli dhidi ya propaganda na habari potofu.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNESCO ya mwaka 2023, uwezo wa kupima ubora wa taarifa umetajwa kama "ujuzi muhimu zaidi katika karne ya 21".

Melo alisisitiza kuwa bila akili mnemba miongoni mwa wanahabari na wananchi, tasnia ya habari iko katika hatari ya kudhibitiwa na taarifa za kupotosha zinazochochewa na maendeleo ya teknolojia kama AI.

Athari za AI katika Mustakabali wa Uandishi wa Habari

Mkurugenzi huyo wa JamiiAfrica ameonya kuwa tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa 2025, matumizi ya teknolojia ya kidijitali na Akili Bandia (AI) yatashika kasi kubwa kuliko wakati mwingine wowote nchini.

Amesema tayari katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, matumizi ya AI yalishuhudiwa na sasa JamiiAfrica kwa kushirikiana na wadau kama Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) inaendelea kuwajengea uwezo wadau wa siasa kutumia teknolojia kwa njia salama na yenye uwajibikaji.

"Tunapopokea fursa ya teknolojia mpya, lazima tuwe na uelewa wa kina kuhusu athari zake kwa uhuru wa kujieleza. AI inaweza kutumiwa kuharakisha kazi za habari, lakini pia inaweza kuwa chombo cha kusambaza taarifa za uongo ikiwa haitasimamiwa kwa makini," ameonya Melo.

Uhuru wa Vyombo vya Habari Katika Kipindi cha Uchaguzi

Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu, Melo ametoa wito kwa vyama vya siasa, mamlaka na jamii kulinda mazingira ya kazi za waandishi wa habari.

“Ni kipindi kama hiki ambapo uhuru wa vyombo vya habari hupimwa kwa vitendo si maneno. Lazima tuheshimu haki ya kila mwananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati,” amesema.

 Hatua Tunazopaswa Kuchukua

Katika dunia inayoongozwa na data na teknolojia za kisasa, ujumbe wa Maxence Melo unaacha somo muhimu: uhuru wa habari hautegemei huruma ya watawala au mitandao ya kijamii, bali unalindwa kwa uwezo wetu wa kufikiri kwa kina, kuchambua kwa makini, na kusimamia ukweli bila woga.

"Akili mnemba ndiyo silaha yetu dhidi ya taarifa za uongo. Na uhuru wa habari si zawadi — ni haki yetu ya kuzaliwa,” amesema Melo.

Ushirikiano wa Kimataifa

Katika maadhimisho hayo, viongozi wengine akiwemo Balozi wa Sweden nchini Tanzania, H.E. Charlotta Ozaki Macias, na mwakilishi wa UNESCO, Michael Toto, wameelezea umuhimu wa kulinda uhuru wa habari katika enzi ya teknolojia mpya kama AI.

 
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, H.E. Charlotta Ozaki Macias

Balozi Macias amekumbusha kuwa maendeleo ya AI yanapaswa kudhibitiwa kwa misingi ya kulinda faragha, kupambana na upendeleo, na kuimarisha usawa, huku akitoa mfano wa juhudi za Sweden katika kuhakikisha AI inatumikia binadamu.

Kwa upande wake, mwakilishi wa UNESCO, Michael Toto, amekumbusha kuwa mwaka 2024 pekee, zaidi ya waandishi 90 waliuawa ulimwenguni kote kwa ajili ya kuhabarisha ukweli. Alisisitiza kuwa uandishi wa habari ni nguzo ya demokrasia, uwajibikaji na amani duniani.

Maadhimisho haya ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2025 yanaendelea Arusha hadi Aprili 30, yakiratibiwa na JamiiAfrica kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO, na wadau mbalimbali wa habari ikiwemo MISA Tanzania.
Wazungumzaji wakijadili kuhusu Athari za Akili Mnemba(AI) katika Mustakabali wa Uandishi wa Habari​ - Picha na Kadama Malunde



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger