Na Lydia Lugakila _ Misenyi.
Katika risala iliyosomwa na mtendaji wa kata ya Bugandika Nassoro Mswadiko katika sherehe za Bugandika day amesema siku hiyo maalum ya kuchangia maendeleo ya kata Bugandika(Bugandika Day) wameamua kuchangia maendeleo ya kata ikiwa ni pamoja na kuanza kuwanusuru watoto wa kike wanaopitia changamoto wawapo njiani kwani hukumbana na vishawishi vingi vinavyoweza kuleta madhara makubwa ikiwemo kupata mimba.
"Utoro,kukosa muda wa kujisomea na kushindwa kutimiza ndoto zao ni mambo yaliyokuwa yakiumiza roho zetu hivyo kwa kuanza tutaweza bweni litabeba watoto 120 wa kike tutakuwa tumesaidia pakubwa" ,amesema Mswadiko.
Ameongeza kuwa wanalazimika kujenga bweni ili kuwasaidia wanafunzi kuboresha ufaulu wao na kuchochea nidhamu bora,kujitegemea na kujiamini.
Naye Diwani wa kata ya Bugandika Amudi Migeyo alisema kuwa shule ya Sekondari Bugandika ilianzishwa mwaka 2007 ambapo licha ya Wananchi kujitoa kujenga vyumba vya kutosha vya shule changamoto kubwa ilikuwa ni bweni la shule.
Migeyo amesema wana Bugandika waishio nje ya Bugandika wamekuwa chachu kubwa ya kuleta maendeleo ndani ya shule hiyo.
"Bugandika Day iliyoanzishwa ilikuwa inahusisha kanisa (Bugandika Parish) ambapo sisi tumeomba tuwe na Bugandika Day yah pamoja ndani ya vijiji 7 tayari Wananchi wamejitoa kwa nguvu kubwa", amesema diwani huyo.
Naye Mgeni rasmi katika sherehe hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge Frolent Kyombo amewapongeza wadau hao kwa nguvu zao kwani wamewezesha kupatikana kwa kiasi cha ya shilingi milioni 20.6 ikiwemo ahadi na taslimu kupitia harambee ya kuchangia ujenzi wa shule hiyo.
Naye Profesa Hosea Rwegoshora akitoa neno la hamasa amewapongeza waasisi wa Bugandika day kwa wazo hilo la muda mrefu ambalo limeanza kwa hatua kubwa huku akiomba mshikamano ili kusonga mbele.
Naye Naibu Kamishina wa Polisi mstaafu Adrian Rweikiza Magayane kutoka Wilayani Misenyi amesema kuwa baadhi ya watu ambao wanakuwa hawachangii maendeleo wanakuwa hawapapendi nyumbani kwao hivyo wao wamerudi kwa kuunga mkono juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajat Fatma Mwassa za Ijuka Omuka.
Mwenyekiti wa bodi ya shule Bugandika Harun Said amewashukuru wadau hao na kuwa suala la kuanzisha bweni linahitaji mshikamano, nguvu huku akiomba vijana na wazee kuchangamka kwani shule ni yao na watoto ni wao hivyo wajivunie maendeleo ya Bugandika kwa kujitoa kwa moyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Steven Ndyakoa amesema kupitia kikundi cha Whatsapp cha Bugandika mpya fukuto la maendeleo lilianzia hapo hadi wakafikia hatua ya kupendekeza na kushauri Desemba 26 iwe siku maalum ya Bugandika ili kukutana na kufahamiana kwa waishio ndani na nje ya jamii huku akiwapongeza Wananchi na Serikali kwa kuzidi kujitoa kwa ajili ya maendeleo.
Aidha amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Nkenge Wilayani Misenyi mkoani kagera Florent Kyombo kwa kutoa Mamilioni ya pesa kuijenga kata hiyo.
Hata hivyo Mbunge wa jimbo la Nkenge Florent Kyombo amesema wataendelea kuboresha kila wakati ili Bugandika day iweze kufana zaidi ya hiyo iliyofanyika.
"Niwapongeze kwa nguvu nyingi mfuko wa Mbunge imeishatanguliza Milioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa bweni leo Ofisi ya Mbunge tutaongeza milioni 3 ambapo Desemba 30 Mwaka huu tutaidhinisha fedha hizo ambazo ni jumla ya shilingi milioni 5.
Hata naye Dr. Auson Simeon Rwehumbiza ambaye ni Mwenyekiti wa Bugandika Mpya alisema miaka miwili iliyopita walianzisha kusomba mawe eneo la mradi ambayo gharama yake ni Shilingi milioni 2.3 hivyo chimbuko la Bugandika Mpya limefanya Bugandika day hivyo ushirikiano mshikamano uendelee ambapo ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau mbali mbali wa maendeleo kuweka nguvu ili Bugandika iwe na manufaa kwa wote huku akiwaomba Wananchi kuilinda miundo mbinu inayotolewa na wadau.
Ikumbukwe kuwa kata ya Bugandika ndiyo kata yenye mtaji mkubwa kuliko kata nyingine zote ikilinganishwa na kata Kasambya kutokana na wingi wa kuwa na vijiji 7 ambapo kata Bugandika ina wasomi wakubwa ikiwa ni pamoja na kuwepo Maprofesa 4 ndani ya kata hiyo na Maprofesa 2 wanaotokea katika familia moja.