Sunday, 30 October 2022
BIBI MWENYE JINO MOJA AENDELEA KUTINGISHA MITANDAO YA KIJAMII
Bibi kizee Mkenya anayefahamika kwa jina la Shosh Wa Kinangop amewafurahisha mashabiki wake kwa lugha ya mtaani ya shembeteng. TAZAMA Mambo yake <HAPA>
Bibi huyo anayejaribu bahati yake katika ulimwengu wa mitandaoni kuunda maudhui hivi majuzi alijiunga na TikTok, na anapiga hatua kubwa.
Akiwa na video chache tu kwenye akaunti, amezidi likes 221k, ambapo ni mwanzo tu kwa mama huyo mkongwe. Mashabiki wake wanakisia kuwa huenda ni mmoja wa wajukuu zake wanaomsaidia kuendesha akaunti hiyo.
Akiwa amevalia sweta ya kijivu na kitambaa cha rangi ya samawati ya turquoise kichwani bibi huyo alionesha wazi hakuja kucheza mitandaoni.
Aliwaambia mashabiki wake kwamba kwa sababu alikuwa mzee haimaanishi kuwa haelewi lugha ya vijana ya sheng.
"Msinione mimi ni shosho, me najua sheng, nawalambotove."
'Shosh' ni jina la Kikuyu kumaanisha bibi au ajuza, na Kinangop ni eneo nchini Kenya anakotoka, kwa hivyo zinapowekwa pamoja inakuwa 'Shosh Wa Kinangop.
Haya ni baadhi ya maoni ya wafuasi wake;
@dinahmwenda933 alisema: "Lakini shosh ni mrembo na ni bayana alikuwa anang'aa siku zake za ujana....anapendeza."
@Delia poppy alisema: "Kila wakati naingia tik tok napatana na video zako zikiwa za kwanza shosh nifanyie video moja shosh."
@amazinghope0 alidokeza; "Kongole shosh, tunakupenda."
Hivi majuzi, bibi mmoja ambaye amekuwa kipenzi cha Wakenya wengi baada ya kuagiza kwa mzaha mafuta ya KSh 70,000 aliwafurahisha watu mitandaoni kwa kuzungumza kwa lugha ya sheng.
BUNGE LA AFRIKA KUANZA KUUNGURUMA RASMI KESHO... HII HAPA RATIBA
Ufunguzi Rasmi wa Mkutano wa Kwanza wa Kawaida wa Bunge la Sita wa Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) unatarajiwa kufanyika kesho Jumatatu Oktoba 31,202 katika Makao Makuu ya Bunge la Afrika Midrand, Johannesburg Afrika Kusini.
Sherehe za ufunguzi wa Mkutano huo wa Bunge la Afrika utaongozwa na Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Mhe. Chief Fortune Charumbira ambapo pamoja na mambo mengine Wabunge kadhaa kutoka nchi mbalimbali wataapishwa kuwa Wabunge wa PAP kufuatia chaguzi zilizofanyika katika majimbo kadhaa barani Afrika.
Tazama ratiba hapa
WAZIRI NDALICHAKO AWAPONGEZA WAWEKEZAJI KWA KUTOA AJIRA KWA WATANZANIA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako(kulia) akizungumza na mwekezaji wa kiwanda cha vinywaji cha U-fresh Food Limited (Wapili kushoto) wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya kazi katika Mkoa wa Pwani akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri, Viongozi wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na watendaji wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na mwakilishi wa uongozi wa kiwanda cha Kutengeneza bidhaa mbalimbali za usafi cha Keds Tanzania Ltd (wakwanza kulia) pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho (hawapo pichani) katika ziara yake iliyolenga kufuatilia mrejesho wa utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi Mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (aliyesimama) akizungumza na viongozi wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan Choice Ltd wakati wa kikao cha kutoa tathmini baada ya viongozi wa taasisi zilizochini ya Waziri Mkuu alioambatana nao kukamilisha ukaguzi katika kiwanda hicho.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda (mwenye miwani) akitoa mrejesho wa ukaguzi ulifanywa na wakaguzi wa OSHA katika kiwanda cha vinywaji cha U-fresh Food Limited mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wawekezaji wa kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wengine kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (mbele), Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri (wapili kushoto) Viongozi mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na watendaji wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakielekea katika maeneo ya kiwanda cha Tan choice yanayofanya uzalishaji wakiongozwa na mwakilishi wa uongozi wa kiwanda hicho kwa lengo la kukagua mifumo ya usalama na afya katika kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akifanya ukaguzi wa shughuli za uzalishaji katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za usafi cha Keds Tanzania Ltd.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha vinywaji cha U-fresh Food Limited wakati wa ziara yake iliyolenga kufuatilia mrejesho wa utekelezaji wa Sheria mbalimbali za kazi ikiwemo Sheria Na 5. Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
************************
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewapongeza wamiliki wa viwanda wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania kupitia uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi.
Ametoa pongezi hizo alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku mbili (2) katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo ametembelea viwanda na maeneo ya kazi sita (6) yanayozalisha bidhaa mbali mbali vikiwemo vifungashio, vyombo vya majumbani, mabomba, vinywaji, taulo za kike na nyama.
Maeneo yaliyotembelewa na Waziri Ndalichako ni pamoja na Lake Oil Group, Tanzania Ruidar Co. Ltd vya Kigamboni pamoja na Tanchoice Limited, U-fresh Food Limited, Keds Tanzania Ltd na Global Packaging Limited.
Katika ziara hiyo, Waziri Ndalichako ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya (OSHA), Khadija Mwenda, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, watendaji wengine wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Wilaya za Kigamboni na Kibaha.
“Nimehitimisha ziara yangu ya siku mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Lengo la ziara hii ilikuwa ni kupata mrejesho wa utekelezaji wa Sheria za Kazi ikiwemo kuangalia ajira zinazozalishwa na wawekezaji wetu. Jambo la kufurahisha ni kwamba katika maeneo yote sita niliyotembelea nimeona zaidi ya ajira 3,000 zimezalishwa,” amesema Prof. Ndalichako.
Aidha, amesema wengi wao kati ya idadi hiyo yote ni vijana jambo ambalo linadhihirisha kwamba serikali ya awamu tano inatekeleza ipasavyo wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.
Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo kwa wawekezaji, Prof. Ndalichako amebainisha kwamba kumekuwa na dosari ndogo ndogo katika maeneo ya kazi aliyoyatembelea ikiwemo baadhi ya waajiri kutotoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, kutowasilisha michango katika mifuko ya hifadhi kwa jamii pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa kufanya ziara katika Wilaya ya Kibaha na kuwakumbusha waajiri kuzingatia Sheria za Kazi ambapo ameahidi kushirikiana na wawekezaji katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewataka wawekezaji kushirikiana kwa karibu na Ofisi yake katika kuboresha mazingira ya kazi.
“Wakati wote sisi tupo tayari kushirikiana nanyi kutengeneza mifumo ya usalama na afya kwenye maeneo yenu ya kazi ili ajira hizi mnazozizalisha kwa wingi ziwe endelevu na zilete tija kwenu, kwa wafanyakazi wenyewe na Taifa kwa ujumla,” amesema Mkaguzi Mkuu wa maeneo ya kazi nchini.
MRADI WA MAJI WA SH.BILIONI 1.6 KWENDA KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI HIFADHI YA TAIFA RUAHA
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV- Ruaha
HIFADHI ya Taifa ya Ruaha imesema kwa sasa kuna mradi mkubwa wa maji ambao unaendelea katika eneo la Malumbe Kijiji cha Tungamalenga kwa lengo la kuhakikisha maji hayo yanafika kwenye eneo la ndani ya hifadhi hiyo, ili kuondokana na adha ya kukosa maji safi na salama.
Imeelezwa kwamba ili kufanikisha mradi huo kiasi cha Sh.bilioni 1.6 kimepangwa kutumika kuanzia mwanzo wa ujenzi hadi kukamilika kwake na kwamba ulianza Septemba na unatarajia kukamilika Desemba mwaka huu na hivyo kutaondoa adha ya kukosekana kwa maji safi na salama iliyoko kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Godwell Ole Meing’ataki amesema kuwa kwa sasa wanaendelea na ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ambao unatekelekezwa kwa ushirikiano wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na wananchi wa Tungamalenga na Msembe na maji hayo yatakwenda ndani ya hifadhi hiyo.
“Maji haya yanaelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hasa eneo la Msembe lakini pia maji haya yatapelekwa kwenye tenki lililopo Kingamalenga kwa ajili ya jamii ya watu wa pale , ikumbwe kwamba Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa miaka 58 tangu ianze kumekuwa na changamoto kubwa ya maji na maji yaliyokuwepo katika eneo hili hayana ubora na sio salama , mara nyingi haya maji hayafai kwa ajili ya kupikia , kunywa kwani ni maji ambayo yana chumvi chumvi hata ukijaribu kuoga hautakati hata ukitumia sabuni maji haya hayafai.
“Na pia viwango vya madini mbalimbali kwenye maji haya yako juu na sio mazuri haishauri kwa binadamu kunywa wala kupikia.Hata ukitaka kupikia utakuta sufuria inabadilika kutokana na chumvi nyingi, sasa Hifadhi yetu ya Taifa ya Ruaha kwa kushirikiana na kijiji cha Kingamalenga walibuni mradi huu na sasa utakwenda kuhakikisha uhakika wa maji safi na salama yanapatikana katika kijiji cha Msembe kwa ajili ya matumizi ya watumishi ,familia zao lakini na idadi kubwa ya wageni ambao wanatembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha
“Huu mradi umetoka hapa mpaka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha eneo la Msembe takribabani kilometa 36, mitaramo na mabomba yameshatandazwa katika kilometa hizo , kazi ambayo inafanyika hapa ni kujenga eneo la dakio la maji na baada ya hapo tutaunganisha mabomba na kupeleka maji eneo la Msembe.Pia tumejenga tenki kubwa kwa ajili ya kutunza haya maji halafu tutakwenda kuyasambaza hadi hifadhini,”amesema.
Hivyo amesema kwa hiyo mradi huo ni wa kipekee ambao unaonesha manufaa ya ushirikiano kati ya wananchi wanaoishi jirani na hifadhi kwani bila ya mahusiano mema kati yao na wananchi wasingeruhusiwa kuchukua maji ambayo hata wao wananchi wanayahitaji.Pia wasingeruhusu mitaro na mabomba kupita kwenye mashamba yao, maeneo ya makazi kwa ajili ya kupela maji kwenye Hifadhi ya Taifa Ruaha.
“Tunashukuru kwa ushirikiano ambao tumeupata na huu ni mradi mkubwa ambao unakwenda kunufaisha hifadhi lakini na wananchi nao kwa upata maji safi na salama, huu mradi ni mkubwa na umetumia takribani Sh.bilioni 1.6 ambazo ndio zimetumika kwenye huu .Lakini kubwa zaidi katika kipindi cha kutekeleza mradi wananchi hawa wamekuwa waaminifu.Tunachohurahia maji yapo ya kutosha.
Kwa upande wake Ofisa Uhifadhi wa Taifa Ruaha Kitengo cha Uhusiano kwa Jamii Priscus Mrosso amesema hifadhi hiyo makao makuu yake yapo Msembe ambacho ni kitongoji cha Kijiji cha Kingamalenga kwa hiyo wameuchukua mradi huo katika Kijiji cha Malunde.“Ni sehemu ya ujirani mwema na ni mradi ambao unakwenda kutunufaisha sisi wote.
“Kwa awamu hii ambayo mradi unatekelezwa sasa hivi Tungamalenga watapata maji kidogo lakini kwenye awamu ya pili ya mradi ambayo hayajatolewa la maji lakini awamu ya pili watapata maji mengi , kwani tutaongezea nguvu kwenye tanki lao kubwa la maji ambalo liko hapa kwenye kijiji. Mahusiano kati ya hifadhi na kijiji cha Kingamalenga yako vizuri ndio maana waliliridhia hifadhi kupitisha mabomba katika maeneo yao ya mashamba, pia waliahidi mabomba hayo watayalinda kwani wanajua watanufaika na hayo maji ambayo yanatakiwa kutoka Kijiji cha Malumbe mpaka hifadhini,”amesema.
Wakati huo huo Ofisa Mtendaji Kijiji cha Tungamalenga Linuss Mweluka amesema mahusiano kati yao,TANAPA na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hayajaanza leo ni muda mrefu na wamekuwa wakipata wa kujengewa majengo mbalimbali taasisi hasa Elimu na Afya .
“Lakini kwa mradi huu wa maji tunasema umefika kwa wakati kwasababu kijiji chetu kilikuwa na changamoto sana ya maji ya bomba , kwa mahusiano tuliyonayo na TANAPA hadi sasa tumeshaambiwa tunaletewa maji hayo na tutawekewa kwenye tenki ambalo lipo hapa kwa ajili ya kutumia sehemu kubwa kwa taasisi mbili elimu na afya kwa awamu hii ya kwanza
“Kwa awamu ya pili tutatoa maombi kwa ajili ya huduma kwa ujumla ya kijiji kizima kwa hiyo kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Kijiji cha Kinamalenga napenda kutoa shukrani zangu za awali kwa TANAPA , ahadi yetu sisi ni kutoa ushirikiano hasa katika ulinzi wa mradi kwasababu mara nyingi kwenye miradi kama hii ya maji ambapo kumepita mabomba huwa kunatokea uharibifu lakini tumejipanga ili kulinda vizuri mradi huo.”
Kuhusu ushiriki wao kwenye kulinda hifadhi hiyo amesema kupitia elimu ambazo zimekuwa zikitolewa wananchi wamekuwa na uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa hifadhi na ndio maana hata ujangili kwa sasa umepungua.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Godwell Ole Meing’ataki alipokuwa akizungumza mambo mbalimbali kuhusu hifadhi hiyo ukiwemo mradi mkubwa wa maji ambao unaendelea katika eneo la Malumbe Kijiji cha Tungamalenga mkoani Iringa kwa lengo la kuhakikisha maji hayo yanafika kwenye eneo la ndani ya hifadhi hiyo, Ambapo katika Mradi huo kiasi cha Sh.bilioni 1.6 kimepangwa kutumika kuanzia mwanzo wa ujenzi hadi kukamilika kwake na kwamba ulianza Septemba na unatarajia kukamilika Desemba mwaka huu na hivyo kutaondoa adha ya kukosekana kwa maji safi na salama iliyoko kwa muda mrefu.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Godwell Ole Meing’ataki akiwa eneo unapojengwa mradi mkubwa wa maji ambao unaendelea katika eneo la Malumbe Kijiji cha Tungamalenga mkoani Iringa kwa lengo la kuhakikisha maji hayo yanafika kwenye eneo la ndani ya hifadhi hiyo, Ambapo katika Mradi huo kiasi cha Sh.bilioni 1.6 kimepangwa kutumika kuanzia mwanzo wa ujenzi hadi kukamilika kwake na kwamba ulianza Septemba na unatarajia kukamilika Desemba mwaka huu na hivyo kutaondoa adha ya kukosekana kwa maji safi na salama iliyoko kwa muda mrefu. PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-RUAHA.
Ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ambao unaendelea katika eneo la Malumbe Kijiji cha Tungamalenga mkoani Iringa kwa lengo la kuhakikisha maji hayo yanafika kwenye eneo la ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruahahiyo kuondokana na adha ya kukosa maji safi na salama.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Tungamalenga ambaye pia mmoja wa mafundi wanaoshiriki kwenye ujenzi wa Mradi huo akieleza manufaa makubwa watakayoyapata mara baada ya kukamilika kwa mradi huo,ambao pia utanufaisha vijiji vya jirani
Ofisa Uhifadhi wa Taifa Ruaha Kitengo cha Uhusiano kwa Jamii Priscus Mrosso akizungumza na Ofisa Mtendaji Kijiji cha Tungamalenga Linuss Mweluka kuhusu kuendelea kuimarisha mahusiano yao ya ujirani mwema kati yao,TANAPA na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha,lakini pia kuhakikisha wanashiriki kulinda miradi mbalimbali inayoratibiwa na Hifadhi ikiwemo Elimu na Afya.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-RUAHA.
Saturday, 29 October 2022
MTOTO WA MIAKA MITATU ADAIWA KUBAKWA UCHOCHORONI SHINYANGA
NA HALIMA KHOYA,SHINYANGA
Mtoto mwenye umri wa miaka 3 (jina limehifadhiwa) mkazi wa mtaa wa dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, amedaiwa kubakwa mtu ambaye hakufahamika mara moja katika maeneo ya uchochoroni jirani na nyumbani kwao.
Tukio hilo limetokea jana Oktoba 28, 2022 majira ya saa 4 asubuhi katika mtaa huo wa dome.
Akieleza tukio hilo kwa njia ya simu Mwenyekiti Mtaa wa dome Solomoni Najulwa, amesema taarifa a kubakwa kwa mtoto huyo alipigwa simu na mama yake mzazi, lakini kutokana na yeye kuwa safarini ikabidi atume wajumbe wa mtaa ili wafike eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.
Amesema baada ya wajumbe kufika eneo la tukio hawakumkuta mtoto huyo ambapo mama yake mzazi alikuwa tayari ameshampeleka hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu, kutokana na kuumizwa vibaya sehemu zake za siri pamoja na kutoa taarifa Polisi.
Aidha, Najulwa amelaani tukio hilo na kubainisha kuwa katika mtaa wake kumekuwepo na wimbi la vijana wengi wakizurura mtaani na hawana kazi, na ndiyo wamekuwa wakifanya matukio hayo ya ubakaji pamoja na uhalifu, na kuahidi atakomesha vitendo hivyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
“Majira ya saa 6 mchana nilipigiwa simu na mmoja wa wakazi katika mtaa wangu ambapo aliniambia mtoto wake amebakwa na mtu asiyefahamika, ndipo nilipowatuma wajumbe wafike eneo hilo haraka, ili kutoa msaada kwa mhanga ikiwamo kumpeleka hospitali, lakini walikuta mama yake ameshampeleka,”amesema Najulwa.
“Mimi kama kiongozi wa ulinzi na usalama mtaa wa dome naahidi kushirikiana na wananchi wote kumsakana kwa hali na mali aliyehusika na kitendo cha kikatili kama hiki na tutahakikisha atakayekamatwa anajibu tuhuma zote zilizowahi kutokea kipindi cha nyuma ili kukomesha tabia hii isijitokeze tena”ameongeza.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga ACP Janeth Magomi, amesema bado hajapata taarifa ya tukio hilo na kubainisha kuwa analifuatilia.
WABUNGE WAPYA WA BUNGE LA AFRIKA 'PAP' WAPEWA MAFUNZO ELEKEZI
Sekretarieti ya Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) imeendesha semina elekezi kwa Wabunge 11 wapya wa Bunge la Afrika wakiwemo kutoka Burundi, Morocco, Msumbiji, Somalia na Tanzania kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Kawaida wa Bunge la sita wakati wabunge hao wapya wakitarajiwa kuapishwa.
Semina hiyo imefanyika leo Jumamosi Oktoba 29,2022 katika Makao Makuu ya Bunge la Afrika Midrand Johannesburg Afrika Kusini ambapo wamepewa taarifa muhimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa PAP, kazi za Bunge, majukumu yao kama wabunge pamoja na masuala ya fedha, Utawala na Rasilimali Watu.
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na Mhe. Anatropia Theonest, Mhe. Toufiq Salim Turkey na Mhe. Ng’wasi Kamani, kutoka nchini Burundi ni Mhe. Bernardine Nduwomana, Morocco ni Mhe. Hannaa Benkhair, Msumbiji ni Mhe. Sarfina Filipe Franco Chindaculema na kutoka Somalia ni Mhe. Seneta Prof. Abdi Ismael Samatar, Mhe. Mohamed Jamal Mursal, Mhe. Abdulrahman Mohamed Hussein, Mhe. Aden Mohamed Nur na Mhe. Zamzam Muhumed Omar.
Kaimu Naibu Karani anayeshughulikia Biashara na Mikutano ya Bunge la Afrika (PAP), Galal Nassir akizungumza kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) kwa Wabunge wapya wa Bunge la Afrika kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa PAP, kazi za Bunge, majukumu yao kama wabunge pamoja na Masuala ya Fedha, Utawala na Rasilimali Watu. Picha na Kadama Malunde - Midrand Afrika Kusini
Kaimu Naibu Karani anayeshughulikia Biashara na Mikutano ya Bunge la Afrika (PAP), Galal Nassir akizungumza kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) kwa Wabunge wapya wa Bunge la Afrika kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa PAP, kazi za Bunge, majukumu yao kama wabunge pamoja na Masuala ya Fedha, Utawala na Rasilimali Watu.
Kaimu Naibu Karani Mfawidhi wa Fedha, Utawala na Rasilimali Watu Bunge la Afrika (PAP, Vivian Abii akizungumza kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) kwa Wabunge wapya wa Bunge la Afrika kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa PAP, kazi za Bunge, majukumu yao kama wabunge pamoja na Masuala ya Fedha, Utawala na Rasilimali Watu.
Kaimu Naibu Karani Mfawidhi wa Fedha, Utawala na Rasilimali Watu Bunge la Afrika (PAP, Vivian Abii akizungumza kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) kwa Wabunge wapya wa Bunge la Afrika kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa PAP, kazi za Bunge, majukumu yao kama wabunge pamoja na Masuala ya Fedha, Utawala na Rasilimali Watu.
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anatropia Theonest na Mhe. Ng’wasi Kamani (kushoto) wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (Pan - African Parliament - PAP ) kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu kuhusu kanuni za uendeshaji wa PAP, kazi za Bunge, majukumu yao kama wabunge pamoja na masuala ya fedha, Utawala na Rasilimali Watu.
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP)
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP)
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP)
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP)
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP)
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP)
Wabunge wapya wa Bunge la Afrika wakiwa kwenye semina elekezi iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Bunge la Afrika (PAP) leo Jumamosi Oktoba 29,2022 katika Makao Makuu ya Bunge la Afrika Midrand Johannesburg Afrika Kusini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
JE UMEWAHI KUSIKIA HABARI ZA MWANAMALUNDI?? YULE MSUKUMA MWENYE MIUJIZA?? ....SOMA HAPA
Mwanamalundi ni jina ambalo lilikuwa maarufu sana karne ya 18 na 19 (enzi za mkoloni) maeneo ya kanda ya ziwa; hususani Mwanza na Shinyanga. Habari za huyu mtu zimewahi kuandikwa kwenye kitabu kiitwacho "MWANAMALUNDI: Mtu maarufu katika Historia ya Usukuma". Ni kitabu ambacho kiliingizwa kwenye mtaala wa elimu ya msingi miaka ya 1970-80. Wazee wenzangu watakuwa wanakumbuka. Hivi sasa habari za mtu huyu ni Kama vile zimepotea kabisa.
Mwanamalundi ni jina la mtu wa miujiza kutoka kabila la Wasukuma. Matamshi sahihi ya jina hili Ni "Ng'wanamalundi" na sio "Mwanamalundi" kama ambavyo wengi hutamka.
Mwanamalundi alizaliwa kijiji cha Ng'wakwibilinga, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mwaka 1892. Baba yake aliitwa Bugomola na mama yake aliitwa Ngolo.
Wazazi hawa wawili hawakujaaliwa kupata watoto kwa muda mrefu sana. Uzee uliwakaribia bila hata kupata mtoto. Jambo hili liliwakosesha sana raha, hasa Mzee Bugomola ambaYe alitamani sana japo apate mrithi wa mali zake. Hali hii ilimfanya Bugomola kuwa mtulivu na mpole muda mwingi katika maisha yake.
Katika jamii ya wasukuma wakati huo, mwanamke asiposhika mimba ndani ya kipindi cha miezi 6 hadi 12 tangu aolewe, ilikuwa ni lazima aende kwa mganga kujua kinachomsumbua.
Ni nyakati ambazo hakukuwa na makanisa ya maombezi kama ilivyo leo hii, misikiti ya kuomba dua wala hospitali. Waganga ndio watu pekee waliotatua matatizo mbalimbali ya jamii zao.
Mzee Bugomola na mke wake Ngolo wakaamua kwenda kwa mganga upande wa mashariki ya kijiji walichokuwa wakiishi (Ng'wakwibilinga) ili wapate ufumbuzi wa tatizo lao.
Mganga aliwaambia ujio wao hata kabla hawajajieleza wenyewe. Mganga akawatengenezea dawa kisha akawaambia kuwa Ngolo (mama/mke) atashika mimba na atazaa mtoto wa kiume ambaye atakuja kuwa mashuhuri siku za hapo baadaye lakini kwa bahati mbaya Bugomola (baba/mume) hatoweza kumuona mtoto huyo; yaani Bugomola atafariki kabla mtoto hajazaliwa.
Habari hii ilimfurahisha sana Bugomola pamoja na kwamba aliambiwa atakufa bila kumuona mtoto. Mkewe pia alifurahi kusikia kuwa atashika mimba. Bugomola hakujali kifo chake sababu hata umri wake ulikuwa umeenda kidogo.
Furaha yake kubwa ilikuwa ni kumpata mrithi wake. Walirudi nyumbani wakiwa na furaha kubwa. Bugomola hakuweza kuificha furaha yake. Muda mwingi alionekana ni mwenye tabasamu na vicheko vingi tofauti kabisa na vile watu walivyozoea kumuona.
Baada ya wiki kadhaa Ngolo alishika mimba. Mimba ilipotimiza miezi mitatu tu, Bwana Bugomola aliaga dunia bila hata kuugua. Ngolo ambae alikuwa mjane wakati huo aliilea mimba hiyo hadi ilipofikisha miezi 9.
Siku moja kabla Ngolo hajajifungua mtoto, wingu kubwa lilitanda angani. Mvua kubwa na yenye radi kali ikaanza kunyesha. Mtoto aliyekuwa tumboni akaruka mruko usio wa kawaida na kisha ikaskika sauti ya kitoto kutoka tumboni ikisema, "Mayu nibyalage, yaani mama nizae!"
Ngolo akashtuka na kuingiwa hofu baada ya kusikia sauti hiyo, hivyo akamuita mama mkwe wake na baadhi ya majirani ili nao waweze kuwa mashahidi wa sauti hiyo.
Kwa bahati nzuri sauti ile ikajirudia tena na ghafla uchungu ukamshika Ngolo. Ilikuwa ni mwaka 1892 Ngolo alipojifungua mtoto wa kiume mwenye maajabu tangu akiwa tumboni mwake. Mtoto huyo akaitwa Igulu, yaani Mbingu.
Igulu (Mwanamalundi) alizaliwa akiwa mwenye afya njema kabisa isipokuwa tu miguu yake ilikuwa myembamba na yenye nyayo kubwa tangu alipozaliwa. Kutokana na wembamba wa miguu yake, jamii ikampa jina la utani "Mamilundi" likimaanisha "mamiguu membamba".
Igulu alikuwa ni mtu mwenye aibu sana enzi za utoto wake. Alikuwa akiwakimbia wageni wasimuone na kuuficha uso wake kwa aibu. Pamoja na aibu alizokuwepo nazo, alipenda sana kuzurura mitaani akiwa ameambatana na marafiki zake.
Baadhi ya wazazi hawakupendezwa na tabia yake ya uzururaji akiwa ameambatana na watoto wao. Mara kadhaa wazazi wa marafiki wa Igulu walimtamkia Igulu (Mwanamalundi) maneno mabaya kila Igulu (Mwanamalundi) alipotoka kuzurura na watoto wa majirani zake, walimwambia, “Mamilundi galyo lilihumbura bana bise”, ikiwa na maana "mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”.
Katika ujana wake Igulu, alipenda sana kucheza ngoma aina ya Kahela. Kila aliposhiriki kucheza ngoma hiyo, alipenda sana kuuficha uso wake kwa kitambaa cheusi. Katika mashindano ya kucheza ngoma hiyo, Igulu na marafiki zake walishindwa kuwa washindi.
Watu kama SamÃke, Ng'wanikinga, Ng'wanilong'ho na GÃndù NkÃma walikuwa si rahisi kuwashinda katika uchezaji wa ngoma. Ni watu ambao walijua kucheza ngoma kwa umahili kuliko Igulu (Mwanamalundi). Mara nyingi matumizi ya uchawi yalihusika katika kuwapa ushindi wa kucheza ngoma hiyo na kukubalika kwa watu mbalimbali.
Kutokukubalika kwa Igulu (Mwanamalundi) na marafiki zake mbele ya jamii hasa katika uchezaji wa ngoma kulipelekea achukue uamuzi wa kwenda kwa mganga. Igulu aliwashawishi vijana wenzie waende kwa mganga atakayewapa dawa ya mvuto kwa watu na kuwa washindi nyakati zote za mashindano ya ngoma. Vijana wenzie walikubali sababu kwa nyakati zile suala la kwenda kwa mganga lilikuwa ni jambo dogo sana.
Safari ya kuelekea mashariki zaidi mwa kijiji chao ikawadia. Mganga alikuwa ni mwanamke, mwenye umri ufaao kuitwa bibi ndani ya kijiji cha Nyaraja, wilaya ya Iramba mkoa wa Singida. Walipokelewa vizuri na mwenyeji wao. Iliwachukua wiki moja bila kuhudumiwa chochote kile, siku ya nane mganga akawaamuru wachukue panga na majembe kuelekea porini ili wakachimbe dawa itakayowasaidia kupendwa na watu.
Wakiwa porini, yule bibi mganga alitafuta vinyonga watatu kwa idadi ya vijana hao wanaotaka dawa kisha akawaambia wachimbe mashimo yenye nusu ya urefu wao. Vijana wakachimba mashimo hayo huku wakiwa na vinyonga vichwani mwao. Walipomaliza kuchimba, bibi mganga akawaambia wafunike mashimo hayo kwa kuni kavu.
Vijana hao wakatii maagizo ya bibi mganga na kisha bibi akawatoa vinyonga waliokuwa wameng'ang'ania kwenye vichwa vya vijana hao watatu na kisha akawatia dawa midomoni vinyonga hao na kisha akawaweka juu ya kuni zilizofunika mashimo yale yaliyochimbwa na vijana wale watatu. Mara baada ya kuwaweka vinyonga hao juu ya kuni zile, moto ukawashwa ili kuwachoma vinyonga hao.
Hazikupita dakika kadhaa wakiwa wanashuhudia kuteketea kwa vinyonga hao, ghafla akatokea kifaru katika mazingira ya kutatanisha na akaanza kuwafukuza watu wote, akiwemo yule bibi mganga. Igulu (Mwanamalundi) ilimlazimu apande juu ya mti kujinusuru na madhira hayo. Wale vijana wawili walitimka mbio na hawakurudi tena.
Bibi mganga akararuliwa na yule kifaru mpaka akapoteza maisha na kisha kifaru akamjia Igulu (Mwanamalundi) aliyekuwa juu ya mti na kuanza kuudhuru ule mti kwa pembe yake. Kifaru hakufanikiwa kuuangusha mti aliopanda Igulu zaidi ya kuubandua magome yake. Kifaru alipochoka akaamua kuondoka na kutokomea kusikojulikana.
Igulu (Mwanamalundi) akashuka juu ya ule mti na kumwendea bibi mganga ambaye muda huo alikuwa ni marehemu. Igulu akaubeba mwili wa yule bibi mganga na kuurudisha nyumbani.
Akiwa njiani, ule mwili wa bibi mganga uliokuwa mabegani mwake ukaonesha kuwa ni kama vile unavuta pumzi mapafuni. Ghafla yule bibi akapiga chafya na kuamka kisha akamuuliza Igulu (Mwanamalundi), "Bhaja hálà abhayanda abhalaha" akimaanisha kuwa wako wapi vijana waliokuwa hapa? Igulu akamwambia kuwa wale vijana wenzie wamekimbia baada ya kumuona yule kifaru.
Bibi mganga ambaye muda huu alionekana kuwa ni mzima kabisa na hana majeraha tena akaomba warudi eneo la tukio ili wachukue dawa. Wakiwa njiani kurudi eneo la tukio, yule bibi mganga akamsifia sana Igulu kwa kumuita "Ni mwanaume kamili" aliyekuja kweli kutafuta dawa.
Bibi akaokota yale magome yaliyobanduliwa na kifaru na kisha kuondoka nayo.
Walipofika nyumbani, yule bibi akaamua kumwambia ukweli Igulu (Mwanamalundi) kuwa yule kifaru ni yeye mwenyewe bibi. Aliamua kujibadili ili kuwapima uwezo wao wa kuvumilia magumu. Kwa kuwa Igulu pekee ndio alionesha yuko imara, bibi yule alimtunuku dawa nzuri zitakazompa mvuto na nguvu katika ngoma zake.
Wale vijana wawili walipitiliza hadi kwao bila kurudi tena kwa mganga. Bibi mganga alimpa masharti Igulu baada ya kumpa dawa. Bibi mganga alimzuia Igulu (Mwanamalundi) kumparaza mtu yeyote au kumnyooshea kidole. Iwapo atafanya hivyo basi alieparazwa au kunyooshewa kidole atakufa hapohapo.
Igulu (Mwanamalundi) aliporudi kijijini kwake na kisha kucheza ngoma ya kwanza baada tu ya kurudi kutoka kwa mganga, alishinda.
Kuna nyakati Igulu aliamua kucheza ngoma akiwa juu ya jiwe kubwa. Wakati akicheza ngoma hizo, nyazo zake zilionekana juu ya mawe aliyokuwa akitumia kucheza ngoma.
Ni alama za nyayo ambazo zipo mpaka leo pale kijiji cha Nyandekwa, wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga. Ni kama km 10 tu kutoka makao makuu ya wilaya.
Kuna nyakati Igulu alitengeneza mashimo ya mchezo wa bao juu ya jiwe kwa kutumia kisigino chake. Ni alama ambazo pia bado zipo kijiji cha Nyandekwa, Kahama-Shinyanga.
Igulu aliposhinda mashindano ya ndani ya kijiji, akaamua kuomba kushindana na wapinzani wakubwa zaidi walioishi kijiji cha Ng'wagala wilaya ya Maswa; yaani akina SamÃke, Ng'wanikînga, Ng'wanilog'ho na mwanamke mwenye nguvu za kiganga aitwae GÃndü NkÃma. Hawa watu wanne walikuwa hawana mpinzani katika ngoma lakini Igulu (Mwanamalundi) akajitosa kushindana nao kwa mara nyingine.
Mwanamalundi alipofika kwenye mashindano, akafanya miujiza kwa kujirefusha kama ngongoti asiye na magongo yoyote yale na kisha akaanza kucheza huku akiwa ameficha uso wake kwa kitambaa cheusi kama kawaida yake.
Wakati anacheza ngoma akiwa ana urefu wa ngongoti, baadhi ya watu walijaribu kugusa na kuifunua miguu yake ili wajue kulikuwa kuna nini. Wote waliothubutu kuigusa walikufa baada ya muda mfupi.
Katika ngoma hiyo, GÃndü NkÃma akatumia nguvu zake za kiganga kumrudisha Igulu (Mwanamalundi) kama alivyokuwa awali; yaani pasipo kurefuka kama ngongoti. Kwa kufanya hivyo, Mwanamalundi alipoteza pambano hilo.
Mwanamalundi akaondoka Maswa na kwenda kijiji cha Nela ambako lilipangwa shindano jingine. Shindano hili Mwanamalundi alishinda.
Kwa kuwa katika safari zake zote huambatana na jopo la wapishi wa chakula, ushindi huu ulimkwaza GÃndü NkÃma, mpinzani wake mkubwa ambaye aliamua kuloga chakula anachoandaliwa Mwanamalundi ili kisiive hata kikipikwa wiki nzima.
Ni kweli kabisa, wapishi wa Mwanamalundi walilalamika kuhusu chakula kutoiva kabisa kwa muda mrefu na kuni zinakaribia kuisha. Hivyo wapishi wakaomba msaada wa kuni kwa Mwanamalundi. Baada ya wapishi kulalamika, Mwanamalundi akasonta/akanyoosha kidole kwenye pori fulani eneo hilo na kuwaambia wapishi waende wakakate kuni alikonyooshea kidole.
Kwa bahati mbaya wakati ananyoosha kidole hicho hakujua kama ndani ya pori hilo kulikuwa kuna mifugo na wachungaji kadhaa ambao wote walikufa na kukauka kama kuni.
Tukio hili la kukausha miti na kuua ng'ombe na wachungaji wake lilimuudhi sana Mtemi Masanja wa III ambaye aliamuru askari wake waende kumkamata Mwanamalundi haraka iwezekanavyo ili awajibishwe.
Askari wa Mtemi Masanja waliogopa sana kumkamata Mwanamalundi wakihofia kufa. Iliwalazimu kumkamata tu sababu walimuogopa zaidi mtemi kuliko Mwanamalundi.
Kabla Mwanamalundi hajakamatwa, alijua jambo hilo lingetokea. Hivyo akaenda haraka kumuaga mama yake mzazi na kumuachia maagizo.
Mwanamalundi alikamua maziwa kiasi fulani kwenye kikombe na kisha akampa mama yake na kumwambia, "Iwapo maziwa haya yataanza kuganda, ujue kuwa nipo katika hali mbaya, iwapo yataganda kabisa, ujue kuwa nimekufa!"
Mwanamalundi akachukua shoka isiyo na mpini kisha akaiegamisha ukutani na kumwambia mama yake, "Iwapo nitakamatwa na kupelekwa kuuliwa, shoka hii itakuwa ikipanda ukutani nikiwa napelekwa kuuliwa, tukifika eneo nitakalouliwa, basi hii shoka itapandisha hadi mwisho wa ukuta kuonesha kuwa tumefika mwisho wa safari!" Mama yake alipokea maagizo hayo na haikuchukua muda Mwanamalundi akakamatwa na askari wa Mtemi Masanja.
Mtemi Masanja III aliamua kupeleka shauri hilo kwa watawala wa kizungu (Wajerumani) ili wamchukulie hatua Mwanamalundi.
Uchunguzi ukafanyika na Mwanamalundi akaonekana ana hatia ya mauaji ya watu wasio na hatia. Adhabu ya kosa hili ilikuwa ni kunyongwa.
Katika safari hii ya kunyongwa, Mwanamalundi aliambatana na Makongoro Igana ambaye alikuwa ni Mtemi wa Ilemela.
Mtemi huyu alikuwa ana hatia ya kuwachapa fimbo wajerumani baada ya kupita upande usio sahihi katika njia kadiri ya utaratibu wa utawala wake.
Mtemi Makongoro Igana kila alipokuwa akisafiri juu ya punda, mkono wake wa kuume ulikuwa umeshika fimbo ndefu. Fimbo hiyo hutumika kumchapia kila atakaepita upande wa kuume katika safari zake. Kwa bahati mbaya wajerumani hawakujua utaratibu huo wa Mtemi Makongoro.
Siku wajerumani walipopishana safarini na Mtemi Makongoro, walipita upande wa kuume wenye fimbo. Mtemi Makongoro akawachapa fimbo wazungu hao kama ilivyo jadi yake. Wazungu hao walishindwa kumvumilia, wakamkamata na kumfungulia mashtaka yaliyoamuru Mtemi anyongwe.
Kaliyaya ni mtu wa pili aliyeambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa. Huyu Kaliyaya alikuwa ni mtu aliyeonekana ni mwenye ushawishi mkubwa kwa watu wa jamii yake. Kukubalika kwake kulimfanya apate wafuasi wengi ambao walihofiwa kumpindua mjerumani.
Hivyo wajerumani wakaona ni bora wamfungulie mashtaka ili wamnyonge kabla hajawapindua. Kaliyaya alikuwa ni mtu wa kawaida tu ila ni mwenye ushawishi na kipenzi cha watu wengi.
Mtu wa tatu aliyeambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa ni Mtemi Italange wa Bugando. Mtemi huyu aliingia mgogoro na Wajerumani baada ya kuhodhi eneo kubwa la pwani ya ziwa Victoria na bandari zake kisha akakataa kuwapa Wajerumani. Ili kumnyang'anya utajiri huo, wajerumani wakaamua kumfungulia mashtaka ili wamnyonge.
Zoezi la kunyongwa lilipofika, Mwanamalundi alikuwa ndio mtu wa kwanza kuvishwa kitanzi. Kamba ilipofyatuliwa tu ili kumuua, kamba ikakatika yenyewe. Zoezi la kumuua likaahirishwa, badala ya kunyongwa akabadilishiwa adhabu.
Ikaja zamu ya Mtemi Makongoro Igana. Mtemi alipowekewa tu kitanzi shingoni na kisha kuifyatua kamba hiyo ili kumuua, ghafla kukatokea mfano wa sinema kwenye ukuta. Ni sinema ya kimiujiza iliyoonesha matukio ya kivita miaka ya nyuma.
Askari wakageuka kuitazama sinema hiyo. Sinema haikuchukua zaidi ya dakika moja, ikaisha. Walipomgeukia yeye (Mtemi Makongoro Igana) wakaona hana kamba shingoni. Huyu naye akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu.
Akaja Mtemi Italange. Huyu alipowekewa kitanzi shingoni, nae pia kamba ilifyatuka. Akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu. Ilipofika zamu ya Bwana Kaliyaya, kitanzi kilipofyatuliwa ili kumnyonga, hakika kitanzi kilimuua. Huyu hakuwa mwenye ulinzi wowote ule kishirikina; yaani alikuwa ni mtu wa kawaida tu.
Ndipo mamlaka za mjerumani zikaamuru askari wawapeleke watu hao watatu Tabora. Wakiwa njiani kuelekea Tabora, walifika Nzega na kuamua kupumzika kidogo chini ya mti mkubwa nje ya Shule ya Sekondari Chama.
Askari wakijerumani wakawa wakimuuliza maswali Mwanamalundi kuhusu nguvu zake na kisha wakamuomba afanye muujiza wa mwisho kabla hajafikishwa gerezani.
Mwanamalundi akawaambia askari kuwa bado ana uwezo mkubwa, hata huo mti waliopumzikia anaweza kuukausha.
Aliongea maneno hayo huku akiupigapiga mti huo. Kabla hajamalizia sentensi yake kuwa anaweza kuukausha, mti ulikauka palepale na majani makavu yakaanza kudondoka. Askari wa kijerumani waliogopa sana tukio hilo.
Walipofika Tabora mjini, Mwanamalundi na wale watemi wawili waliunganishwa na watu wengine wenye makosa ya uhaini na uhujumu uchumi na kisha kupelekwa kisiwa cha Mafia kutumikia kifungo cha miaka mitatu.
Akiwa gerezani, Mwanamalundi aliwekwa chumba kimoja na mtemi Makongoro Igana. Mtemi Makongoro akamuuliza Mwanamalundi, "Hivi huna namna ya kujiokoa mahali hapa?" Mwanamalundi akamjibu kuwa kwa wakati huo hangeweza kujiokoa, ila kuna miujiza ya shoka na maziwa amemuachia mama yake nyumbani. Mtemi akamuuliza, "Una miujiza mingine yoyote?" Mwanamalundi akamwambia Mtemi Makongoro kuwa yeye (Mwanamalundi) anaweza kupanda viazi na mihogo na ikavunwa ndani ya dakika kadhaa tu na ikawa tayari kabisa kwa chakula.
Wakiwa kisiwani hapo, wakakubaliana kwenda ng'ambo ya kisiwa (bara) kisha wakachukue mbegu za viazi na mihogo ili washuhudie miujiza hiyo ya kupanda na kuvuna ndani ya dakika kadhaa.
Kwa kuwa nyakati hizo wafungwa wa visiwani walikuwa wakiachwa huru sababu hawataweza kutoroka, Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walienda mpaka baharini ndani ya kisiwa hicho.
Makongoro akiwa ameshika jiwe na Mwanamalundi akiwa ameshika fimbo. Makongoro aliporusha jiwe umbali mrefu baharini, Mwanamalundi aliyapiga maji kwa fimbo na kisha maji yakajitenga na kuacha njia mpaka pale lilipotua jiwe. Walifanya hivyo mpaka walivyofika bara (mainland). Wakatafuta mbegu za mihogo na viazi na kuonesheana miujiza.
Kila walipokuwa wakitoroka gerezani, waliacha vivuli vyao vilivyoonekana kama watu halisi. Kuna nyakati Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walionekana wakiwa Mwanza au Shinyanga na gerezani pia muda huo huo. Jambo hili liliwachanganya sana wajerumani.
Walipomaliza kifungo chao walirudishwa nyumbani kwao kwa ndege. Jamii ya Mwanamalundi ilipoona ndugu yao amerudishwa kwa ndege wakaamua kumpa jina jipya, "Ng'wenhwa ndege", wakimaanisha "aliyerudishwa kwa ndege". Mwanamalundi anaaminika kuwa ndiye msukuma wa kwanza kupanda ndege.
Wakati anarudishwa nyumbani baada ya kumaliza kifungo chake, mama yake alifurahi sana. Mama yake alifurahi kwa sababu maziwa hayakuganda kwa miaka mitatu jambo ambalo lilionesha kuwa huko aliko alikuwa hai.
Maziwa yalibaki katika ubora uleule kwa miaka mitatu. Shoka ilianza kuteremka taratibu kwenye ukuta kadiri Mwanamalundi alivyokuwa akikaribia kufika nyumbani. Alivyofika tu, shoka ilikuwa tayari imefika ardhini kuashiri kuwa muda wowote Mwanamalundi atafika hapo. Na ndivyo ilivyokuwa.
Aliporudi mtaani, Mwanamalundi hakuacha asili yake. Aliendelea kucheza ngoma maeneo mbalimbali. Mtemi Masanja ambaye ndiye aliesababisha Mwanamalundi kunusurika kunyongwa na hatimae kufungwa, aliamua kumfukuza Mwanamalundi katika himaya ya utawala wake.
Mwanamaundi akaamua kuhamia kijiji kiitwacho Seke kwa Mtemi Mahizi ambako aliendelea kucheza ngoma na kufanya miujiza yake.
Akiwa Seke wilayani Kishapu ,mkoani Shinyanga; Mwanamalundi alifanya muujiza uliomuongezea heshima kijijini Seke.
Wanakijiji cha Seke waliibiwa ng'ombe wengi sana na Wamasai kutoka Tabora. Wanakijiji wakataka kwenda kufuatilia ng'ombe hao usiku huo huo jambo ambalo Mwanamalundi alikataa.
Mwanamalundi aliwahakikishia wanakijiji kuwa ng'ombe hao wapo salama na watarudishwa salama tu kesho asubuhi na sio usiku huo. Wanakijiji walikubali kutokana na kumuamini Mwanamalundi.
Usiku wa siku hiyo, Mwanamalundi akatuma nguvu zake zilizowazingira Wamasai na kisha kuwafanya wasinzie na mifugo hiyo. Hata walipofuatwa asubuhi, walikutwa wamelala fofofo. Wanakijiji wakawaua Wamasai hao na kisha wakarudi na mifugo yao.
Mwanamalundi akapewa jina jingine ugenini na kuitwa "Kishosha mang'ombe ga Seke", ikimaanisha "Aliyerudisha ng'ombe za Seke".
Kuna kipindi, Mwanamalundi alivamia pori la Mtemi wa Ng'hung'hu aitwae Chalya ili achimbe mizizi fulani ya dawa.
Mtemi Chalya alipata machale kuwa kuna mvamizi katika mapori yake anachimba mizizi ya dawa. Mtemi akaondoka na kuelekea kule ambako machale yalimuelekeza. Ni kweli, akamkuta Mwanamalundi akichimba mizizi ya dawa fulani.
Mtemi akamuuliza Mwanamalundi, "ni kwanini umeingia katika utemi wangu bila kunijulisha?" Mwanamalundi akajibu, "Wewe ni mtemi wa watu wote ila mimi ndiye mtemi wa miti yote!" Jibu hilo lilimkwaza Mtemi Chalya ambaye aliamua kurudi kwenye himaya yake kwa ghadhabu na kuwaamuru askari wake wamkamate Mwanamalundi ili aadhibiwe.
Askari wakiwa wameambatana na Mtemi Chalya walipofika porini eneo alilokuwepo Mwanamalundi, hawakumkuta.
Badala yake waliwakuta simba wengi wakiwa wamelala eneo hilo. Ilibidi watimue mbio kujiokoa wenyewe dhidi ya simba hao walioanza kuwafukuza. Walipofika kwenye himaya ya Mtemi wakiwa salama, walimkuta Mwanamalundi amemaliza kula chakula chao na anaondoka.
Ilibidi mtemi amuache tu Mwanamalundi aondoke bila kumbughudhi kwa lolote.
Mwanamalundi alifariki mwaka 1936 kwa maradhi ya kawaida na kuzikwa Ididi Jihu huko kijiji cha Seke wilaya Kishapu mkoa wa Shinyanga akiwa ana umri wa miaka 44.
Tukio la kifo chake liliitwa "hang'witulo gwa shigela" ikimaanisha "Vita ya kuwakimbia wamasai". Hii ni kwa sababu wakati Mwanamalundi anakata roho, kulitokea kishindo kikubwa kama tetemeko la ardhi. Watu wengi walikimbia ovyo kwa hofu kuwa labda wamasai wamevamia eneo lao ili kuwaua.
Baada ya kishindo hicho, giza likaingia ghafla, giza ambalo hata kuku wakaanza kurudi nyumbani, fisi wakaanza kutembea mitaani wakidhani ni usiku. Hata baada ya mazishi yake, kaburi lake lilifuka moshi mwingi sana uliopanda mpaka juu mawinguni na kutengeneza giza la muda mfupi.
Mwanamalundi anakumbukwa pia kwa kuweza kutembea hewani bila kukanyaga ardhi, kujibadili na kuwa kiumbe tofauti kama mnyama, ndege, majani, mti au jiwe na uwezo wake wa kutembea juu ya maji au kuwa ndani ya maji kwa muda mrefu.
Mwanamalundi ni mmoja tu wa watu mashuhuri katika tawala za Kisukuma. Kuna watu mashuhuri kabla yake kama akina NÃndwa, Italange na Sïta. Hawa wote walikuwa ni watu wa miujiza kama alivyokuwa Mwanamalundi.
Makala hii inasimuliwa na Msukuma halisi na mwanahistoria ya Wasukuma Ngh'wana Ibengwe Shileki Mazege katika kitabu chake kiitwacho "Miujiza ya akina NG'WANA MALUNDI", toleo la kwanza 2015. Huyu Bwana ana vitabu vingi sana kuhusu historia ya wasukuma.
Kwa maswali yoyote kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana nae kupitia:
+255 763 379 387