Friday, 20 February 2026

PROGRAM JUMUISHI YA MALEZI,MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO YAENDELEA KUIMARIKA KISHAPU

Na Sumai Salum- Kishapu
Afisa Ustawi wa Jamii wilayani Kishapu mkoani Shinyanga  Mwajuma Abeid akizungumza wakati akifungua kikao cha utekelezaji wa PJT-MMMAM mwezi Oktoba-Disemba 2025, kwa niaba ya Mganga Mkuu wilayani humo chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), Changamoto zilizotambuliwa na njia za kutatua changamoto hizo zinazoikabili programu hiyo Februari 19,2026

Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeendelea kutekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata malezi bora tangu wakiwa katika hatua za awali za maisha. 


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 Mratibu wa PJT–MMMAM wilayani humo,Paul Lupolaso, kwenye kikoa chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), Changamoto zilizotambuliwa na njia za kutatua changamoto hizo Februari 19,2026.


Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo utoaji wa elimu ya afya na lishe kwa jamii, kampeni za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, jitihada za kukabiliana na udumavu, pamoja na utoaji wa elimu ya kuzuia ukatili dhidi ya watoto. 

"Katika kipindi hiki tumeweza kutoa vidonge vya madini chuma kwa wanawake wajawzito na kufikia 91%, elimu ya kinamama kujifungulia vituo vya afya 90%, Watoto kunyonya maziwa ya mama pekee wenye umri wa miezi 0 mpaka miezi 6 kwa 98%" ameongeza Lupolaso

Aidha,  ameongeza kuwa elimu ya usalama wa mtoto imeendelea kutolewa katika shule za msingi 128 zilizopo ndani ya Wilaya ya Kishapu. Hata hivyo, amebainisha kuwa utekelezaji wa programu hiyo umekumbana na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa watumishi katika kitengo cha lishe, ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya afya na lishe ya familia, pamoja na uhitaji wa kuimarisha usimamizi elekezi katika vituo vya kutolea huduma za afya. 

Kutokana na changamoto hizo, Halmashauri imeweka mikakati ya kuimarisha utekelezaji wake kwa kufanya kikao cha Kamati ya Lishe kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata, kuhimiza maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe (SaLiki), kufanya usimamizi elekezi katika vituo vya afya na zahanati, kuongeza uhamasishaji wa jamii kuhusu usafi wa mazingira na umuhimu wa kinamama kujifungulia katika vituo vya afya, pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa watoa huduma kuhusu huduma za dharura kwa mama na mtoto. 

Baada ya uwasilishaji wa taarifa hiyo, wajumbe walitoa maoni mbalimbali ya kuboresha programu hiyo, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza mikakati ya kuwahusisha wanaume katika kliniki za wajawazito na masuala ya lishe ili kuimarisha uwajibikaji wa familia, kuanzisha vikundi vya wazazi katika ngazi ya jamii vitakavyosaidia kutoa elimu ya malezi chanya, pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia katika upangaji na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya mtoto. 

Sambamba na hayo, Halmashauri pia imeendelea kutoa shukrani kwa wadau wanaoiunga mkono katika utekelezaji wa programu hiyo wakiwemo World Vision, THPS, Marie Stopes, AMREF, Kivulini na REDESO kwa mchango wao katika kuboresha ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa Serikali ilizindua rasmi programu hiyo mwezi Desemba 2021 ikiwa na dhamira ya kuimarisha mfumo jumuishi wa malezi ya mtoto unaojikita katika maeneo ya afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.
Mratibu wa PJT–MMMAM wilayani humo,Paul Lupolaso akizungumza kwenye kikao cha utekelezaji wa PJT-MMMAM mwezi Oktoba-Disemba 2025, chenye lengo la kupata uelewa wa kadi alama ya tathmini ya maendeleo ya awali ya Mtoto (ECD), mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoikabili programu hiyo na ku Februari 19,2026
















 
Share:

Thursday, 19 February 2026

SERIKALI YATOA FURSA KWA WASANII KAHAMA KUPITIA MIKOPO YA UTAMADUNI NA SANAA

 

Na Neema Nkumbi, Kahama

Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni tano kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa ajili ya kuwakopesha wasanii nchini, hatua inayolenga kuinua vipaji, kukuza sekta ya ubunifu na kuwawezesha vijana kiuchumi.

Akizungumza katika mafunzo ya uelimishaji kuhusu namna ya kupata mikopo hiyo yaliyofanyika leo februari 18, 2026 katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Afisa wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Jovita Godwin, amesema mfuko huo unatoa fursa kwa wasanii wa nyanja mbalimbali ikiwemo muziki, filamu, sanaa za maonyesho, fasihi na ufundi wa kazi za sanaa ili waweze kukuza kazi zao na kufikia malengo yao ya kisanaa na kibiashara.

Amesema serikali imekusudia kuona sekta ya sanaa inakuwa chanzo cha ajira na mapato kwa vijana wengi, hivyo amewahimiza wasanii wa Kahama kujitokeza kwa wingi na kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili wanufaike na mikopo hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama, Martha Kapela, amesema halmashauri imejipanga kuibua na kukuza vipaji kupitia matamasha, makongamano na ziara katika kata mbalimbali kwa lengo la kuwatambua wasanii na kuwaunganisha na fursa zinazotolewa na serikali.

Naye Meya wa Manispaa ya Kahama, Kaniki Mataluma, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuchumi kwa vijana, akiwataka wasanii kutumia mikopo hiyo kama chachu ya maendeleo yao binafsi na ya taifa.

Baadhi ya wasanii waliohudhuria mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kuanzisha mfuko huo wakisema utawasaidia kupanua shughuli zao za kisanaa, huku wakiiomba serikali kuendelea kuboresha masharti ya mikopo ili kuwafikia wasanii wengi zaidi.


Share:

SHUWASA YATWAA TUZO YA MDAU SHUPAVU KANDA YA ZIWA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeibuka mshindi wa Tuzo ya Mamlaka Bora inayosimamia upatikanaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika Tuzo za Wadau Shupavu Kanda ya Ziwa, zilizofanyika Jumatatu tarehe 16 Februari 2026.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya  Golden Crest, jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa utambulisho, Mhandisi Katopola alisema SHUWASA imetekeleza kwa vitendo jitihada za kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa majisafi kwa wastani wa saa 23 kila siku.

Aliongeza kuwa juhudi hizo, sambamba na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira, zimeifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa kinara wa usafi kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo.

SHUWASA inatoa huduma katika eneo lote la Manispaa ya Shinyanga pamoja na miji midogo ya Didia, Tinde na Iselamagazi, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. 

Mhandisi Katopola alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Mamlaka na wadau wake, hususan wateja na wananchi, kwa kulipia ankara za maji kwa wakati na kutoa taarifa za uvujaji au uharibifu wa miundombinu.

Aidha Mhandisi Katopola alimshukuru Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Hamidu Aweso kwa maelekezo yake ya mara kwa mara katika kuhakikisha Mamlaka za Maji nchini zinatoa huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi katika maeneo yao ya huduma.

Tuzo hii ni chachu ya kuendelea kuboresha huduma na kudumisha viwango bora vya maji safi na usafi wa mazingira kwa maendeleo ya wananchi wa Tinde, Didia, Iselamagazi na Manispaa ya Shinyanga.  












Share:

DOTTO EMANUEL MANUMBU ASHINDA TUZO YA TOP 100 AFRICANS GLOBAL 2026 KAMA GLOBAL YOUNG MALE POLITICAL LEADER


Kiongozi kijana katika masuala ya Elimu, Habari na Siasa, Dotto Emanuel Manumbu, ametangazwa rasmi kuwa mmoja wa washindi wa tuzo za Top 100 Africans Global 2026, akitambuliwa katika kipengele cha Global Young Male Political Leader.

Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wake mkubwa katika uongozi na juhudi zake za kuleta maendeleo chanya kwa jamii pamoja na Taifa kwa ujumla. 

Kupitia nafasi mbalimbali za kiuongozi, Manumbu ameonyesha uwezo, ubunifu na dhamira ya dhati katika kutumikia nafasi yake na jamii kwa ujumla. 

Akizungumzia ushindi huo, Manumbu ameeleza kuwa ni heshima kubwa kwake na kwa Tanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa tuzo hiyo ni motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii, unyenyekevu, na uadilifu kwa manufaa ya jamii.

“Tuzo hii ya heshima namrejeshea Mungu, ambaye ndiye mgawaji wa riziki na neema zote. Nawashukuru kwa dhati wazazi wangu kwa malezi yao mema, viongozi wangu walionilea na kuniongoza katika utumishi wangu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ukerewe kwa kuniamini na kunipa fursa ya kuwatumikia wananchi. Aidha, namshukuru DC Ngubiagai, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED), pamoja na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Tawi la Mwanza — kisima cha kuzalisha viongozi makini barani Afrika. Shukrani za pekee pia ziende kwa watumishi wenzangu wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa ushirikiano na malezi yaliyonifikisha katika hatua hii,” amesema Manumbu.

Hafla rasmi ya ugawaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika tarehe 28 Februari 2026 katika ukumbi wa Morena Hotel jijini Dodoma, ambapo washindi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika watatunukiwa tuzo hizo rasmi.

Ushindi huo umeendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa kwa kuonyesha mchango wa vijana katika uongozi na maendeleo ya Bara la Afrika.




Share:

Wednesday, 18 February 2026

TUJIFUNZE KWA VIJANA WA MAKUNDUCHI WALIOGEUZA TAARABU ASILIA KUWA ‘MIGODI’ YA FEDHA MTANDAONI




Wakati baadhi ya vijana wakiendelea kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira rasmi, kundi la vijana wanane kutoka Kijiji cha Makunduchi, Kusini Unguja, limeibuka na jibu la vitendo: Ubunifu ndio ajira ya kisasa.

Vijana hao, wakiongozwa na kijana mtanashati Ibrahim Suleiman, wameamua kutumia muziki wa Taarabu asilia—urithi ambao wengi waliuona kama kitu cha kizamani—na kuugeuza kuwa bidhaa adimu inayouzika kupitia mitandao ya kijamii. Wao badala ya kusubiri majukwaa makubwa, wameamua kutumia simu zao za mkononi kutengeneza maudhui yanayochanganya vichekesho na midundo ya jadi, jambo lililowafanya kuwa gumzo kote nchini na nje ya mipaka.

“Tumeamua kutumia kile tulichonacho mkononi. Hatukusubiri kuajiriwa, tuliamua kujiajiri kupitia kipaji chetu na utamaduni wetu,” anasema Ibrahim Suleiman, akisisitiza kuwa soko la sasa linataka kitu cha kipekee (Originality).

Ubunifu wa vijana hawa si tu unawaingizia kipato kupitia watazamaji wa mtandaoni (views) na matangazo, bali pia unalinda heshima ya muziki wa jadi wa Zanzibar usipotee.

Hii ni dhihirisho tosha kwa vijana wengine wa Kitanzania kuwa; uwe una ujuzi wa VETA, unalima parachichi, au unajua kuimba, nguvu ya kugeuza ujuzi kuwa utajiri iko kwenye ubunifu wako na matumizi sahihi ya teknolojia.

Huu ni ujumbe mzito kwa wale wanaopoteza muda kubeza juhudi za maendeleo: Wakati ninyi mkiandika vibaya mitandaoni, wenzenu wa Makunduchi wanatumia mitandao hiyo hiyo kuvuna fedha na kutangaza utamaduni wa nchi yao. Tanzania ya sasa inahitaji vijana wenye "misuli ya akili" kama hawa, wanaoona fursa pale wengine wanapoona matatizo.
Share:

Monday, 16 February 2026

MAVUNDE AZINDUA KISIMA CHA MAJI MSALATO, ASEMA NI UTEKELEZAJI WA AHADI YA 2025

Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mkoani Dodoma, Mhe. Anthony Mavunde, ambaye pia ni Waziri wa Madini amezindua kisima cha maji katika Mtaa wa Msalato, Ubalozi wa Catherine Mwajoka, kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kuhusu kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza na wananchi mara baada ya uzinduzi huo, Mheshimiwa Mavunde amewataka wakazi wa Msalato kulinda na kutunza miundombinu ya kisima hicho ili kiweze kudumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Aidha, ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya Msalato na Jimbo la Mtumba kwa ujumla, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Serikali.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mavunde amewashukuru wananchi wa Msalato kwa imani kubwa waliyoionesha kwa kumpigia kura Samia Suluhu Hassan, yeye kama Mbunge pamoja na Diwani wao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, akieleza kuwa ushindi huo unampa nguvu ya kuendelea kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger