Saturday, 14 February 2026
RC KANALI KIDO RASMI AKABIDHIWA OFISI KAGERA

Na Mbuke Shilagi Kagera.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa amemkabidhi rasmi Ofisi Kanali Yahaya Ramadhan Kido leo Februari 13,2026 katika ukumbi wa ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera uliopo Manispaa ya Bukoba.
Akizungumza baada ya makabidhiano Hajjat Fatma Mwassa amesema kuwa Mkoa umefanikiwa kuboresha sekta za huduma zikiwemo sekta za Afya na Elimu.
Amesema kuwa katika Halmashauri zote saba za Mkoa wa Kagera tayari zipo hospitali za Wilaya ambapo zote zinatumika.
Aidha amemuomba Rc Kanali Kido kutupia jicho la karibu katika hospitali ya Wilaya ya Muleba kutokana na changamoto ya mkandarasi na ubora wa ujenzi.
Akipokea rasmi ofisi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Yahaya Ramadhani Kido amesema kuwa kwa kuwa Mkoa wa Kagera upo mpakani hivyo suala la ulinzi na usalama litakuwa ni kipaumbele namba moja katika Taifa na katika uongozi wake.
"Nitashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuendeleza kwa kuendelea kuimarisha usalama kwakua Mkoa wetu unapakana na Nchi jirani", amesema RC Kanali Kido.
Aidha ameongeza kuwa atasimamia miradi yote inayoendelea kutekelezwa na ile inayopangwa kutekelezwa ili iendane na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali na kukamilika kwa wakati.
Amesema kuwa amepokea rasmi dhamana ya uongozi ya Mkoa huo akiwa na dhamira thabiti ya kuendeleza yaliyofanywa na mtangulizi wake na yale yote yaliyoelezwa na Mkuu wa Mkoa mstaafu Hajat Fatma Mwassa yatafatiliwa kwa kina na kuhakikisha yanakamilika kwa wakati.




Friday, 13 February 2026
DKT. GWAJIMA AZINDUA MKAKATI WA KITAIFA WA KISEKTA WA KUTOKOMEZA UKEKETAJI
Na Saidi Saidi WMJJWM ,Arusha
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua Mkakati wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji Nchini (2025/2026–2029/2030) katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji yaliyofanyika Februari 12, 2026, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Uzinduzi wa mkakati huo unalenga kuimarisha juhudi za kitaifa za kulinda haki, afya na ustawi wa wanawake na watoto wa kike.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Gwajima amesema mkakati huo utaimarisha uratibu na ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii katika kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukeketaji. Ameeleza kuwa mikoa ya Arusha na Manyara ina viwango vya juu vya ukeketaji, hali inayohitaji hatua madhubuti na ushiriki wa kila mdau.
Dkt. Gwajima amesema kuwa katika kutokomeza ukeketaji ni muhimu sana kuwashirikisha wanaume kwa kuwapa elimu, kwani wao ndio wahamasishaji wakuu wa vitendo hivyo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Gwajima pia ameongoza maandamano ya wanaume kama ishara ya kuwataka kupinga ukeketaji.
Aidha, amewashukuru wadau mbalimbali wanaoiunga mkono Serikali ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), C-SEMA, SOS Children’s Village, Compassion International Tanzania na mashirika mengine kwa mchango wao katika mapambano dhidi ya ukeketaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana Kimathi, amemshukuru na kumpongeza Waziri Dkt. Gwajima kwa kuichagua Wilaya ya Monduli kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, akisema kuwa ujio wake na kufanyika kwa maadhimisho hayo umeamsha ari kubwa ya mapambano dhidi ya ukeketaji.
Ameongeza kuwa Wilaya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutokomeza ukeketaji.
Naye Katibu wa Viongozi wa Mila Wilaya ya Monduli (Laigwanan), Natuli Letema, amesema viongozi wa mila wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mkoa katika kutoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na ukeketaji.
Ameeleza kuwa juhudi hizo zitazaa matunda kutokana na ari mpya iliyoamshwa na Waziri Dkt. Gwajima ya kuendelea kupambana na mila hatarishi, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa jamii kubadilika na kulinda watoto wa kike.





Magazeti
