Tuesday, 2 December 2025
TUTAPONYA WAATHIRIKA WA MATUKIO YA OKTOBA 29, 2025
RC KUNENGE KUZINDUA MBIO MAALUMU ZA ADEM BAGAMOYO
Monday, 1 December 2025
MOTO WA CHUKI WAKEMEWA: WATANZANIA WATAKA UMOJA NA UTULIVU UTUNZWE
Watanzania, hasa vijana, wamehimizwa kukataa vikali moto wa chuki na mgawanyiko, wakisisitizwa kuwa maendeleo hayawezi kustawi bila amani na umoja. Ujumbe mkuu unaojirudia katika jumbe mbalimbali za wananchi ni: “Maendeleo hayawezi kustawi kama kuna moto wa chuki na mgawanyiko. Amani si tu ukosefu wa vita, bali ni hali ya utulivu, heshima, na umoja inayotuwezesha kujenga pamoja.”
Vijana wanakumbushwa kwamba wao ndio Nguvu ya Sasa na Taifa la Kesho, na hivyo wanapaswa kuthamini amani ya Tanzania ambayo imebarikiwa kuwa "kisiwa cha amani" katika ukanda huu.
Wananchi wanatoa wito wa wazi wa kukataa mgawanyiko: “Kataa kabisa fikra, matendo, au kauli zinazotaka kutugawa kwa misingi ya dini, kabila, au siasa. Sisi ni Watanzania Kwanza! Umoja wetu ndio silaha yetu kubwa.”
Ili kudumisha amani, wanahimizwa kujenga maridhiano kwa kutumia lugha ya staha, kusikiliza wengine, na kutatua tofauti kwa mazungumzo na upendo.
Wananchi mitandaoni wamesema kwamba amani ndiyo tunu, msingi, na dira ya maisha bora na maendeleo. "Amani ni dira ya maendeleo na maendeleo ndio safari yetu," ilisema moja ya jumbe za wananchi, ikionya kwamba vurugu sio njia ya kudai haki bali ni njia ya kuvunja amani moja kwa moja.
“VIJANA ACHENI GHASIA, MTATUUA KWA NJAA” — MACHOZI YA MACHINGA KARIAKOO
Katika hali ya wasiwasi inayoendelea nchini, hasa kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa vurugu zingine, kuanzia Desemba 9 sauti ya wazazi na wafanyabiashara wadogo inazidi kupaaa ikihimiza watoto wao waepuke vurugu, wakisisitiza kwamba maisha yao yanategemea amani na utulivu.Akizungumza kwa hisia, Mama Zawadi alieleza: “Mimi ni Mama Zawadi, mchuuzi wa soko la Kariakoo, na naongea kwa niaba ya maelfu ya Watanzania ambao maisha yetu hutegemea kupata riziki ya kila siku. Ninaposikia wito wa maandamano yenye vurugu, moyo wangu unajawa na hofu isiyoelezeka.”
Woga wake mkubwa unahusu jinsi ghasia zinavyokwamisha shughuli za kiuchumi. "Maandamano yanamaanisha masoko kufungwa, biashara kusimama, na uwezekano wa kupoteza kipato ambacho ndio mlo wa watoto wetu," alifafanua.
Alitoa onyo kali kwa vijana: "Tunaweza vipi kupata chakula kama hatuwezi kufanya kazi? Kusimamisha nchi ni sawa na kutuhukumu kifo kwa njaa.”
Aidha, Mama Zawadi aliweka bayana athari za machafuko kwa kundi la wagonjwa sugu, kama wa UKIMWI na Kisukari, ambao maisha yao yanategemea upatikanaji wa huduma za afya bila kukosa.
Alisimulia maelezo ya mmoja wa wagonjwa alisema, "Kukiwa na machafuko, hospitali zinasita kufanya kazi, usafiri unakwama. Tutapata wapi dawa zetu? Bila dawa, afya yetu inazidi kuzorota. Tunaomba huruma!’”
Mama Zawadi alimalizia kwa kuwataka vijana kutafuta suluhu kupitia mazungumzo na kuonya: "Kuna ndugu zetu tayari wamepoteza wapendwa wao... maandamano yenye ghasia yataacha majonzi ya kudumu."
DKT. MWIGULU AWATOA WASIWASI WATANZANIA: “AMANI YETU HAIUZWI!”
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema serikali imeendelea kufanya mikutano na viongozi wa taasisi mbalimbali za dini, ikiwemo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), na viongozi wa kimila ili kuwaeleza hali halisi ya usalama nchini na kuwataka kuendelea kudumisha amani.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na wananchi wa Arusha katika ziara byake ya kikazi ambayo poia ameitumia kuangalia uharibifu uliofanywa katika vurugu ya Oktoba 29.
Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa amani kama msingi mkuu wa maendeleo ya taifa.
Katika ziara hiyo pia aliwapa wananchi salamu za pole zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia athari za vurugu zilizotokea hivi karibuni.
Waziri Mkuu alitembelea na kukagua uharibifu uliotokea wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025, ambapo Kituo cha Polisi cha Kikatiti, Mahakama ya Mwanzo ya Maji ya Chai, na kituo cha mafuta cha Total Energies vilichomwa moto. Aidha, alibaini kuibwa kwa mali katika soko kuu na kubomolewa kwa sefu ya kutunzia fedha.
Waziri Mkuu amewaonya wananchi kuwa kuchagua vurugu ni sawa na kuchagua kufukuza maendeleo na kuongeza umaskini kwa mtu mmoja mmoja, akisisitiza kuwa ahadi za maendeleo kama maji na barabara zitafanyika endapo tu nchi itakuwa na amani.
DKT. MWIGULU AFICHUA NJAMA: ‘WANAHARAKATI WANALIPWA MAMILIONI KUIVURUGA TANZANIA’
Serikali imefichua kuwa chokochoko na vurugu zinazoendelea nchini zimeletwa na wanaharakati wanaolipwa kwa lengo la kuharibu uchumi wa nchi na kurudisha nyuma maendeleo.
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kukataa kushawishiwa na wanaharakati hao.
Waziri Mkuu ameeleza kuwa baadhi ya vijana walio nje ya nchi wamebainika kupokea kiasi cha Dola za Marekani milioni mbili (sawa na takribani shilingi bilioni 4.5) ili kuchochea vurugu nchini.
Alihimiza watanzania kujiuliza maswali kuhusu maslahi na ajenda ya watu wanaotoa malipo hayo kwa nchi.
Kulingana na maelezo ya Waziri Mkuu, lengo kuu la wachochezi hawa ni kunyakua rasilimali adimu za Tanzania. Alitaja ugunduzi wa Uranium (Tanzania ikiwa nchi ya tisa duniani na ya kwanza Afrika kwa tani za ujazo 890,000) na maendeleo ya miradi ya gesi asilia kama vivutio vikubwa vinavyowafanya waivuruge Tanzania.
"Hawa watu wanalenga tugombane ili wachukue madini adimu (rare earth minerals)... Wanajua Tanzania ina gesi asilia nyingi na inakaribia kuanza," alionya Waziri Mkuu.
Amesisitiza kuwa mbinu hizi zimetumika katika nchi zingine barani Afrika, ambapo chokochoko huanzishwa ili kuruhusu uvurugaji na uchukuaji wa rasilimali, kabla ya wachochezi kuondoka baada ya rasilimali kuisha.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania "kuamka na kuchukua tahadhari" dhidi ya mchezo huu, akisisitiza kuwa ajira na uondoaji wa umaskini utapatikana tu nchi ikiwa na amani.























