Sunday, 10 August 2025
Saturday, 9 August 2025
IAA TAWI LA DODOMA YATOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU KOZI ZINAZOTOLEWA NANENANE

MENEJA wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) – Tawi la Dodoma Dkt. Grace Temba, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 8,2025 katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni, jijini Dodoma.

MENEJA wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) – Tawi la Dodoma Dkt. Grace Temba, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 8,2025 katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni, jijini Dodoma.
Na Alex Sonna-DODOMA
CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA) – Tawi la Dodoma, kimeendelea kuwa kinara katika kutoa elimu ya vitendo kwa vijana nchini, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 kwa kuanza na programu tatu za diploma.
Akizungumza leo Agosti 8,2025 katika banda la Chuo hicho katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (NaneNane) yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni, jijini Dodoma, Meneja wa tawi hilo, Dkt. Grace Temba, amesema kuwa chuo hicho ni sehemu ya mtandao wa kitaaluma unaojumuisha kampasi mama iliyopo Dar es Salaam, pamoja na matawi mengine yaliyopo Babati, Songea, Bukombe, Arusha, na Dodoma yenyewe
“Tunapokea wanafunzi kuanzia ngazi ya kidato cha nne ambao husoma kwa miaka mitatu, wakijifunza kupitia mitalaa ya kisasa inayolenga kuwaandaa kwa soko la ajira la sasa na la baadaye,” amesema Dkt. Temba.
Kwa sasa, IAA inatoa jumla ya programu 38 katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uhasibu, Usimamizi wa Fedha, Uhasibu wa Kodi, Uongozi na Utawala wa Biashara, Masoko, na Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi. Kozi hizi zimebuniwa kwa uangalifu ili kumwandaa mwanafunzi kuwa mtaalamu mahiri na mwenye ushindani katika mazingira ya kazi.
Dkt. Temba ameeleza kuwa mafunzo ya diploma yanayotolewa chuoni hapo yanazingatia mfumo wa elimu shirikishi unaowapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo, jambo linalowajengea uwezo wa kujitegemea na kuwa na ujasiri wanapoendelea na shahada au kuingia kwenye soko la ajira.
“Tunajivunia kuwalea vijana wanaoweza kushindana kitaifa na kimataifa kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na hali ya soko la ajira,” ameeleza Dkt. Temba.
Kwa mujibu wa Dkt. Temba, amesema kuwa ushiriki wa IAA katika maonesho ya Nanenane ni wa kila mwaka, ambapo chuo hutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kozi mbalimbali, taratibu za kujiunga, na nafasi zilizopo kwa vijana kujiendeleza kielimu.
Aidha ameongeza kuwa kupitia banda la chuo hicho katika maonesho hayo, wananchi wamekuwa wakipata maelezo ya kina kuhusu huduma na fursa zinazopatikana, sambamba na ushauri wa kitaaluma.
“Tunatumia jukwaa hili pia kuhamasisha vijana wa maeneo ya karibu na Dodoma kujiunga na kozi zenye tija, hasa zinazokidhi mahitaji ya sekta za fedha, biashara, utawala na TEHAMA,” amesema Dkt. Temba.
Kwa upande wa mikakati ya baadaye, chuo hicho kinaendelea kuimarisha mitaala yake, kuongeza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji, pamoja na kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali kwa lengo la kuongeza fursa za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.
Amesema kuwa Chuo pia kinatumia fursa hiyo kuonyesha namna kinavyotekeleza mkakati wa Serikali wa kuimarisha elimu na taaluma kwa vitendo, jambo linalosaidia kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa taifa.
Dkt. Temba ametoa wito kwa wazazi, walezi na wanafunzi kutembelea banda la IAA katika maonesho ya Nanenane ili kupata taarifa muhimu na kujifunza namna ya kuchagua kozi zenye mwelekeo bora wa ajira.
Friday, 8 August 2025
TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO KWA WANANCHI MAONESHO NANENANE MBEYA
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) kanda ya Nyanda za juu Kusini limetoa elimu ya viwango kwa wananchi, na wajasiriamali walioshiriki katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo Bw. Peter Namaumbo, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi amesema TBS imefika katika maonesho haya kutoa elimu ya uelewa wa masuala matakwa ya viwango kwa wazalishaji wa bidhaa na watumiaji wa bidhaa hizo
Bw. Namaumbo amesema kuwa elimu hii imetolewa kwa wajasiriamali walioshiriki maonesho haya ambapo TBS imewatembelea katika mabanda yao kuwaeleza taratibu za kupata alama ya ubora kwa wale ambao hawakuwa na elimu hiyo lakini pia kuzungumza nao na kujua changamoto wanazozipitia zinazowakwamisha kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TBS inatoa huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali wadogo na wa kati bila gharama yoyote, mjasiriamali atahitajika kuanzia SIDO ambapo ataandikiwa barua inayomtambulisha kama mjasiriamali mdogo au wa kati na baada ya kupata barua hiyo basi atahudumiwa na TBS bure kabisa kwa muda wa miaka mitatu.
“Tunatoa wito kwa wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuongeza wigo wa masoko yao ndani na nje ya nchi Kwani huduma ya uthibitishaji hutolewa bure na TBS mjasiriamali anatakiwa kuanzia SIDO tu ili kupata barua ya utambulisho basi”
Aidha ameongeza kuwa TBS imetoa elimu kwa wananchi kuwakumbusha kutotumia bidhaa za vipodozi vilivyopigwa marufuku kwani bidhaa hizo zinamadhara makubwa sana kiafya kitu ambacho kisipozingatiwa kinaweza kupelekea Taifa kupoteza nguvu kazi.
“Tunawakumbusha wananchi hasa dada, mama zetu na watoto wetu kutotumia vipodozi vilivyopigwa marufuku kwani bidhaa hizi zina viambata sumu vyenye madhara makubwa sana katika afya za watumiaji kwani hupelekea kansa ya ngozi, vizazi na wakati mwingine mvurugiko wa homoni, madhara yote haya mengine hupelekea kifo na mengine hupelekea kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa”
Bw. Peter amesema kuwa maonesho haya yamekuwa fursa kubwa ya kutoa elimu hii sababu vipodozi vingi vilivyopigwa marufuku vinaingia nchini kupitia njia za panya kutoka nchi jirani zinazopakana na mikoa inayopatikana katika Kanda ya Nyada za Juu Kusini.
Amesisitiza kuwa elimu hii inalenga kuwafanya wananchi kuelewa madhara ya bidhaa hizo na hatimaye kuacha kabisa kutumia bidhaa hizo na kama uhitaji wa bidhaa hizo utaisha basi hata soko la bidhaa hizo litaisha kabisa.
TBS inatoa wito kwa wananchi kuhakikisha wananunua bidhaa zilizokidhi matakwa ya Viwango ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kwa kutumia bidhaa hafifu.


















