Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024, Juni 9,2025 Jijini Dar es salaam - Picha na Kadama Malunde
*Yasisitiza Takwimu za Ukatili ni nyenzo muhimu kwa mipango na mikakati ya ulinzi wa watoto na vijana.
Serikali ya Tanzania imetangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024 (The 2024 Tanzania Violence Against Children and Youth Survey - VACS), ukionesha kupungua kwa viwango vya ukatili wa kingono, kimwili na kihisia kwa watoto wa kike na wa kiume ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 2009.
Matokeo hayo yametangazwa leo, Juni 9, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ambaye amesema utafiti huu ni wa pili kufanyika tangu mwaka 2009 na umefanywa kitaalamu kwa ushirikiano wa serikali na wadau wa maendeleo.
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza matokeo ya Utafiti wa Kitaifa wa Ukatili Dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024
Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa takwimu hizi zitasaidia serikali kufanya tathmini ya sera, sheria na programu za kisekta kupitia MTAKUWWA II (Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto), ili kuongeza ufanisi wa juhudi za ulinzi wa watoto na vijana.
Athari za ukatili – Hatari za muda mrefu
Waziri Gwajima amesisitiza kuwa ukatili dhidi ya watoto ni ukiukwaji wa haki za binadamu na huleta athari za muda mrefu za kiafya, zikiwemo matatizo ya afya ya akili, mawazo ya kujiua, matumizi ya dawa za kulevya, tabia hatarishi za ngono, maambukizi ya VVU, pamoja na kupungua kwa fursa za kimaendeleo kwa waathirika.
Amesema serikali itaongeza bajeti na rasilimali watu kuimarisha huduma kwa manusura wa ukatili na kuzuia ukatili kwa njia endelevu.
Takwimu ni za Kitaifa na Zinaaminika
Kwa mujibu wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, utafiti huu umefanyika katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kutumia sampuli wakilishi ya kitaifa, hivyo takwimu zake ni sahihi na zinafaa kutumika kupanga mikakati ya kitaifa.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa
Ushiriki wa Wadau wa Kimataifa
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS), Dkt. Redempta Mbatia, amesema kuwa THPS inajivunia kuratibu utafiti huu kwa weledi mkubwa kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (U.S. CDC), na kwa usimamizi mzuri wa Serikali ya Tanzania.
Dkt. Redempta Mbatia akizungumza na waandishi wa habari
“Utafiti huu umetupatia takwimu muhimu za kusaidia serikali kuongoza juhudi za kitaifa za ulinzi wa watoto na vijana kwa kushirikiana na wadau. THPS tumejidhatiti kuendelea kushirikiana na serikali na wadau katika kutekeleza afua hizi,” amesema Dkt. Redempta.
Ameeleza kuwa matokeo ya utafiti yanaonyesha maendeleo makubwa ya kitaifa katika kupambana na ukatili wa kingono, kimwili na kihisia, na kutoa mwongozo wa kisera na kimkakati kwa serikali na washirika wa maendeleo. 
Bi. Miranda Armstrong akizungumza na waandishi wa habari
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka UNICEF, Bi. Miranda Armstrong, amesema shirika hilo limekuwa sehemu ya ufanikishaji wa utafiti huu kama sehemu ya wajibu wao wa kuwalinda watoto.



















































































