Wednesday, 12 February 2025

BARAZA LA MADIWANI TUNDURU LAJADILI NA KUPITISHA MAKADIRIO YA BAJETI KWA MWAKA 2025/26


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Hailu Hemed Mussa akitoa taarifa ya Rasimu ya makadirio ya bajeti hiyo


Na Regina Ndumbaro-  Tunduru.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru limekutana kujadili rasimu ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26.


Rasimu ya Bajeti hiyo imepitishwa katika Baraza hilo la Madiwani kwa mwaka 2025/26 ni kiasi cha bilioni 7.6.

Baraza hilo limeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mhe. Hairu Hemed Mussa, ambapo imewasilishwa na Afisa Mipango wa halmashauri hiyo, Bosco Mwingira kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri.

Mwingira amesema kuwa bajeti hiyo inalenga kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, kilimo, na sekta nyingine kwa maendeleo ya wilaya.

Madiwani wa kata ya Mchoteka na Kata ya Ligoma katika baraza hilo wameiomba serikali kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa kata zao, ikiwemo ukosefu wa huduma za afya, barabara na maendeleo ya kilimo.

Wamesema hali ya miundombinu katika kata zao inahitaji maboresho makubwa ili kuinua kipato na maisha ya wananchi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando, alisema wanaendelea kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Mtangashari, ukarabati wa mabwawa ya samaki, pamoja na kuboresha kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao.


Aidha, Marando ameeleza kuwa Wilaya ya Tunduru imebarikiwa kuwa na rasilimali za madini aina ya shaba (copper) yanayopatikana katika Kata ya Mbesa ambayo pia yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri.


Mkurugenzi wa Halmashauri ameomba ushirikiano kutoka kwa madiwani na wananchi katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kushirikiana katika ujenzi wa madarasa mapya katika Kata ya Ligoma ili kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa wilaya hiyo.


Kwa upande wake, Makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ametoa mchango wake akisisitiza uboreshaji wa mapato ya ndani ya halmashauri.

Ameeleza kuwa ukamilishaji wa kilomita 1,206 za barabara unakadiriwa kuchukua takribani miaka nane, hivyo ni muhimu kuweka mkazo katika usimamizi wa fedha na rasilimali zilizopo.

Hata hivyo amesema kuwa bajeti ya fedha kuhusu ukarabati wa barabara kwa upande wao wameiachia Mamlaka ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Tarura kushughulikia changamoto hizo.

Katika hitimisho la kikao hicho, madiwani walikubaliana kuwa asilimia 40 ya kiasi cha fedha zilizotengwa zitumike katika uboreshaji wa barabara ndani ya halmashauri.

Kwa ujumla wamehimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo ufanyike kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wa Tunduru wananufaika na bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Hailu Hemed Mussa akitoa taarifa ya Rasimu ya makadirio ya bajeti hiyo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando akiongea na madiwani kuhusu rasimu ya makadirio ya bajeti ya mapato ya Halmashauri hiyo ya Tunduru
Afisa wa serikali za mitaa mkoa mhe Amandusi Chilumba akizungumza na Madiwani wilayani Tunduru
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Hailu Hemed Mussa akizungumza kwenye kikao hicho
Madiwani wakimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando
Madiwani wakimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando
Madiwani wakimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando
Share:

BARRICK NORTH MARA KIDEDEA MECHI YA SOKA YA KIRAFIKI NA TIMU YA CHUO CHA MWALIMU NYERERE

Wachezaji wa timu ya Barrick North Mara na Chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere wakipata mawaidha kabla ya kuanza mechi ya soka ya kirafiki iliyofanyika katika viwanja vya North Mara ambapo North Mara iliibuka na ushindi wa bao 1-0
Kikosi cha timu ya Barrick North Mara katika picha ya pamoja kabla ya mchezo wa soka wa kirafiki na timu ya iliyofanyika katika viwanja vya North Mara ambapo North Mara iliibuka na ushindi wa bao 1-0
Wachezaji wa timu ya Barrick North Mara wakifanya mazoezi kabla ya kuanza mechi ya soka ya kirafiki iliyofanyika katika viwanja vya North Mara ambapo North Mara iliibuka na ushindi wa bao 1-0
Wachezaji wa timu ya Barrick North Mara na Chuo kikuu cha Mwalimu Nyerere wakipambana vikali uwanjani wakati wa mechi ya soka ya kirafiki iliyofanyika katika viwanja vya North Mara ambapo North Mara iliibuka na ushindi wa bao 1-0

***
Timu ya soka ya wafanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara imeonyesha umahiri wake wa kutandaza kabumbu baada ya kuichapa bao 1-0 timu ya Chuo kikuu cha Mwalimu J.K. Nyerere (MJNUAT) katika mechi ya kirafiki iliyofanyika katika viwanja vya mgodi huo.

Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa ambapo kila timu ikitafuta kuibuka na ushindi na mpaka kufikia mapumziko timu zote zilikuwa hazijafungana. Katika kipindi cha pili timu mwenyeji ya North Mara ilifanikiwa kupata bao ambapo timu pinzani haikufanikiwa kusawazisha bao hilo.

Mgodi wa Barrick North mara mbali na kuwa na timu nzuri ya soka unazo timu za wafanyakazi ambazo zimekuwa zikitamba katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa netball ,mpira wa kikapu (Basketball) na timu ya riadha ambayo imefanikiwa kushiriki katika riadha mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Pia mgodi imekuwa ukidhamini michezo mbalimbali katika jamii ikiwemo mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana – yajulikanayo kwa jina la Mahusiano Cup yanayojumuisha timu za vijana kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka.

Kwa kushiriki katika mashindano haya kila mwaka, vijana wanapata fursa ya kuonesha na kukuza vipaji vyao vya michezo, kujenga afya zao kimwili na kiakili, kufahamiana, kujifunza ushirikiano na nidhamu, kubadilishana mawazo na hata uzoefu kwa upendo.

Aidha, mamia ya wananchi wanaokutanishwa na mashindano ya Mahusiano Cup wanapata pia fursa ya kuelimishwa jinsi mgodi unavyochangia maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.
Share:

RC RUVUMA AIPONGEZA EWURA, KUDHIBITI SEKTA YA MAFUTA KWA WELEDI




Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mha. Karim Ally (kushoto), akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed, mara alipo wasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huyo leo 11.2.2025, Ruvuma.

........

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali. Ahmed Abbas Ahmed, ameipongeza EWURA, kwa kuwadhibiti wafanyabiashara wajanja waliokua wakitishia kuficha mafuta kwa kisingizio cha kusubiri bei mpya ya mafuta itangazwe.

Ameyasema leo Tar.11.2.2025, wakati alipotembelewa na Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mha. Karim Ally, kwa lengo la kuzungumzia shughuli mbalimbali zinazofanywa na ofisi hiyo ya kanda.

“Hongereni sana EWURA, kuweza kuwadhibiti wafanya biashara wa mafuta wasio waaminifu. Huduma zimekua nzuri wakati wote, pia nawapongeza kwa huu mfumo wenu wa NPGIS, ambao unawasaidia kujua kiasi cha mafuta kilichopo katika vituo vya mafuta” alisema

Pia Kanali Ahmed alitoa rai kwa EWURA kutoa elimu zaidi ya matumizi ya gesi ya kupikia majumbani na gesi asilia kwenye magari ili wananchi wengi wachangamkie fursa hizo mara moja.

Mhandisi Ally alisema ni jukumu la EWURA ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za nishati na maji kwa wakati na kwa gharama sahihi.

Ofisi ya EWURA nyanda za Juu Kusini ina ofisi zake katika jengo la NHIF, Ghorofa ya 6 Mbeya na inasimamia mikoa mitano ukiwepo mkoa wa Ruvuma, Mbeya, Njombe, Songwe na Rukwa
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO FEBRUARI 12, 2025

Share:

Tuesday, 11 February 2025

Video Mpya : NG'WANA KANG'WA - SIMBA

 

Share:

NYAMBARI NYANGWINE FOUNDATION YATOA VITABU 3,380 KWA SHULE ZA SEKONDARI MASASI

Maboksi ya vitabu vilivyotolewa na Nyambari Nyangwine Foundation kwa shule za Sekondari Wilayani Masasi


Baadhi ya Walimu wakipanga Vitabu hivyo

Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara. 

 Taasisi ya Nyambari Nyangwine Foundation imechangia vitabu 3,380 kwa shule za sekondari katika wilaya ya Masasi, ikiwa ni juhudi za kusaidia kuboresha elimu kwa wanafunzi na walimu. 

Msaada huo unalenga kuinua kiwango cha ufundishaji na kujifunza shuleni.


Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Nyambari Nyangwine Foundation, Dk. Leonard Akwilambo, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa taasisi hiyo, amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya dhamira ya Nyambari Nyangwine Foundation katika kusaidia maendeleo ya elimu nchini. 


Amesisitiza kuwa vitabu hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa walimu katika kufundisha na kwa wanafunzi katika kujifunza.


Dk. Akwilambo ametoa wito kwa walimu na wanafunzi kuhakikisha kuwa vitabu hivyo vinatunzwa vizuri ili viweze kutumiwa na vizazi vijavyo. 


Amewataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kwa kujifunza kwa bidii na kuhakikisha kuwa elimu wanayoipata inawasaidia katika maisha yao ya baadaye.



Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bi. Chikunja Kamwela, akizungumza kwa niaba ya walimu, ameishukuru Nyambari Nyangwine Foundation kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunza. 


Amesema vitabu hivyo vitawasaidia walimu katika ufundishaji na kuwafanya wanafunzi kuelewa masomo kwa urahisi zaidi.


Mchango wa vitabu hivi unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya kwa shule zilizopokea msaada huo, huku walimu na wanafunzi wakihimizwa kutumia rasilimali hizo kwa ufanisi.


 Uwekezaji katika elimu kupitia misaada kama hii unaonyesha mshikamano wa jamii katika kuboresha sekta ya elimu nchini.


Nyambari Nyangwine Foundation imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia sekta ya elimu kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vitabu, vifaa vya kujifunzia, na programu za kukuza ujuzi kwa walimu na wanafunzi. 


Taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa elimu inaboreshwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Msaada huu wa vitabu kwa shule za sekondari Masasi ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata nyenzo bora za kujifunzia, hali inayoweza kusaidia kuongeza ufaulu na kuimarisha kiwango cha elimu wilayani humo.


Share:

Monday, 10 February 2025

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE FEBRUARI 11, 2025

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger