Friday, 8 November 2024

WALENGWA WA TASAF SHINYANGA WAPONGEZA MRADI WA BARABARA YA TANESCO - SANJO, WAPATA FAIDA ZA KIUCHUMI NA HUDUMA BORA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Walengwa wa Mpango Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wameeleza kupata manufaa makubwa kutokana na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mashema (Mtaa wa TANESCO) katika kata ya Chamaguha.

Mradi huu, uliofadhiliwa na TASAF kupitia ajira za muda mfupi, umeweza kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa mtaa huo kwa kuwapa malipo kwa kazi walizofanya, huku baadhi yao wakijiongezea mapato kupitia shughuli za kilimo na biashara.

Barabara hii yenye urefu wa kilomita 2 inayoanzia Mtaa wa TANESCO na kuunganisha mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha imesaidia kupunguza usumbufu wa usafiri ambao awali ulilazimu wakazi kutafuta njia ndefu.

Katika mahojiano na waandishi wa habari Novemba 8, 2024, walengwa wa TASAF wamesema, ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 2 umewezesha wakazi wa mtaa wa TANESCO na Sanjo kuepuka umbali mrefu wa kupita maeneo mengine, jambo ambalo lilikuwa linawaathiri hasa kwa upande wa usafiri.
Martha Daniel Chacha, mmoja wa wakazi wa mtaa huo, amesema kuwa kabla ya mradi, eneo hilo lilikuwa na majaruba, lakini sasa ni rahisi kufika kwenye huduma muhimu kama zahanati ya Chamaguha hivyo imewezesha wakazi kuepuka vikwazo vya usafiri.

Aidha walengwa wameeleza furaha yao kwa kupata malipo mazuri ya kazi walizofanya na wameomba miradi mingine kama hiyo iendelee ili kuboresha hali ya maisha yao zaidi.
Tabu Buganga Malaba 

"Ufuatiliaji wa mradi ulikuwa mzuri, tulilipwa kwa wakati. Tunashukuru TASAF kwa kuturahisishia maisha yetu, tunaomba mradi mwingine uje ili tuendelee kunufaika," amesema Tabu Buganga Malaba na Gigwa Masingija, miongoni wa walengwa.

Fundi Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi huo, Paul Ramadhani, pia amepongeza usimamizi mzuri wa mradi, na kusema kwamba ufanisi ulioonekana unatoa picha nzuri kwa miradi ya baadaye.

Mwenyekiti Mstaafu wa Mtaa huo Suleiman Mzee, ameiomba serikali iendelee kutekeleza miradi mingine ya barabara kwani mahitaji bado yapo.
Octavina Kiwone

Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Octavina Kiwone, amesema kuwa barabara hiyo imejenga daraja la kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Chamaguha na kuunganisha jamii na huduma muhimu.

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa TANESCO, Bundala Shija, amefafanua kuwa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mashema, wenye urefu wa mita 2,000, ulianza kutekelezwa tarehe 7 Desemba 2022 na kukamilika kwa asilimia 100 tarehe 12 Mei 2023.

Mradi huu uligharimu jumla ya shilingi 13,860,500/- kwa ajili ya kuanzisha mradi, kulipa walengwa, na kununua vifaa vya ujenzi.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi, Shija amesema, “Mradi huu wa barabara ni sehemu ya ajira za muda zilizofadhiliwa na TASAF, ambapo utekelezaji ulisimamiwa na Kamati ya Usimamizi ya Jamii kwa kushirikiana na mtoa huduma au fundi ngazi ya jamii, kwa niaba ya serikali ya mtaa. Walengwa 114 walishiriki katika ujenzi, ingawa baadhi yao hawakujitokeza."
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa TANESCO, Bundala Shija

Ameongeza kuwa kutokana na ubora wa kazi iliyoonyeshwa, TARURA ilichukua hatua ya kuiboresha barabara zaidi kwa kuweka moramu na kalvati, hivyo kuhakikisha barabara inapitika muda wote, hata katika hali mbaya ya hewa.

Shija pia ameomba TARURA kuendelea kuboresha barabara zingine katika eneo hilo na maeneo mengine, ili kuendelea kuboresha miundombinu na maisha ya wananchi.

“Tunaiomba TARURA iendelee kutufikishia maendeleo kwa kuboresha barabara nyingine zinazohitaji msaada. Hii itasaidia sana katika kukuza uchumi wa eneo letu,” amesema Shija.

Kwa jumla, mradi huu umeonyesha jinsi miradi ya miundombinu inayofadhiliwa na TASAF inavyoweza kuwa chachu ya maendeleo, hasa kwa walengwa wa Mpango Kunusuru Kaya Maskini, na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Octavina Kiwone akiwaelezea waandishi wa habari kuhusu barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Octavina Kiwone akiwaelezea waandishi wa habari kuhusu barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Octavina Kiwone akionesha miti iliyopandwa na Walengwa wa TASAF pembezoni mwa barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha.
Martha Daniel Chacha akielezea faida wanazopata kupitia barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Waandishi wa habari, maafisa kutoka TASAF wakitembelea barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa TANESCO, Bundala Shija akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha
Mwenyekiti Mstaafu wa Mtaa wa TANESCO kata ya Chamagusa Suleiman Mzee akiomba serikali iwapatie miradi mingine ya barabara
Fundi Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha, Paul Ramadhani akielezea namna walivyojenga barabara hiyo kwa ufanisi mkubwa
Gigwa Masingija akielezea namna alivyoshiriki ujenzi wa barabara ya Mashema inayounganisha Mtaa wa TANESCO na Sanjo katika kata ya Chamaguha
Share:

AKO TANZANIA COMMUNITY SUPPORT LAVUTIWA NA MIRADI YA TEA


Shirika la AKO Tanzania Community Support limeonyesha nia ya kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ili kuboresha utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya elimu nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa AKO, Bi. Hilda Kimath, alieleza dhamira hii alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, ofisini kwake Dodoma tarehe 8 Novemba 2024.

Bi. Kimath alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo ili kuongeza ufanisi katika miradi yao na kupunguza changamoto za gharama na ucheleweshaji.

‘‘Naamini tukitekeleza hii miradi kwa pamoja, tutakuwa na uhakika wa usimamizi lakini pia kuinua ubora wa miradi tunayotekeleza kwani TEA ambayo ni Shirika ni Serikali ina uzoefu wa kufanya miradi kama hii amesema” Bi Hilda

Dkt. Kipesha alieleza furaha yake kwa hatua hiyo na kupongeza juhudi za wadau kuchangia maendeleo ya elimu. Aliongeza kuwa TEA iko tayari kufanya kazi na wadau wote kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Alitaja faida za wadau kuchangia maendeleo kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ikiwemo kutambuliwa rasmi na kupewa Cheti cha Utambuzi, ambacho kinaweza kusaidia katika kupata nafuu ya kodi kutoka TRA.

TEA, iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001, ina jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa ajili ya kugharamia miradi inayolenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora na yenye usawa nchini.

Share:

TOSCI YATEKELEZA PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP) KWA VITENDO.

 Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na wataalam kutoka Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu wametembelea Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) Mkoani Morogoro.

Mfuko huo wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unajenga maabara ya kisasa ya uchambuzi wa Ubora wa Mbegu kwa ajili ya Taasisi hiyo kwenye makao makuu yake yaliyopo katika chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA).

 Kufika Kwa Ujumbe huo Mkoani Morogoro, ni sehemu ya ziara  ya kikazi ya kutembelea maeneo yanayotekeleza Programu hiyo,Tarehe 8 Novemba 2024.



Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)
Share:

Thursday, 7 November 2024

SERIKALI YAKUTANISHA WADAU KUANDAA MPANGO WA UHIMILIVU NA UENDELEVU WA UKIMWI


Dkt. Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, akifungua kikao cha Wadau wa Maendeleo na washirika wanaotekeleza afua za mwitikio wa UKIMWI, kilicholenga kujadili Mpango wa Uendelevu wa Kudhibiti UKIMWI nchini. Kikao hicho kinafanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 7 Novemba, 2024.

Na Mwandishi Maalum,Malunde Blog-ARUSHA

SERIKALI kwa Ushirikiano na wadau wa Maendeleo na watekelezaji wa shughuli za Mwitikio dhidi ya UKIMWI wamekutana Mkoani Arusha kwa siku mbili kuandaa Mpango wa uhimilivu na uendelevu wa wa UKIMWI nchini (HIV Response Sustainability Roadmap) kwenye Kikao kinachoratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Mpango huu unalenga kuweka mikakati itakayoiwezesha nchi yetu kuweza kutekeleza afua za UKIMWI kwa fedha za ndani pale ambapo fedha kutoka kwa wafadhili zitapungua zaidi au kukoma kabisa. Mikakati inayowekwa ni ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu baada yamwaka 2030 ambapo inatazamiwa kuwa UKIMWI utakuwa siyo janga la kiafya duniani.

Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela amesema kuwa kupatikana kwa Mpango huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na uwezo wa kutekeleza afua za UKIMWI nchini ikiwemo kuziba mwanya wa upungufu wa raslimali za Mwitikio wa UKIMWI nchini, baada kuendelea kupungua kwa raslimali za kutekeleza afua hizo.

“Mpango wa uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na upungufu wa rasilimali za kutekeleza Afua za Mwitikio wa UKIMWI nchini, nawashukuru sana wadau wote mlioshiriki na kufanikisha maandalizi ya Mpango huu, ni matumaini yangu kuwa wote tutashiriki siku ya uzinduzi utakaofika Mkoani Ruvuma tarehe mosi Disemba, 2024 ili tushuhudie kazi tuliyoifanya kwa kipindi chote hiki inazinduliwa tayari kwa matumizi” alisema Dkt Kamwela.

Dkt. Kamwela ameongeza kuwa kazi ya mapambano dhidi ya VVU bado kubwa kwani pamoja na kiwango cha kitaifa cha ushamiri wa maambukizi kupungua, ushamiri katika baadhi ya makundi umeongezeka hasa miongoni mwa makundi ya wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, madereva wa masafa marefu pamoja baadhi ya mikoa nchini.

 Hivyo, ni lazima tuongeze juhudi hadi hapo tutakapoona tunaondoa kabisa maambukizi mapya, watu wote walioambukizwa wanajitambua na kutumia dawa na kuhakikisha kunakuwa hakuna ubaguzi na unyanyapaa kwa WAVIU na wote walioathirika na UKIMWI.

Naye Mkurungenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) Dkt. Martin Odiiti akizungumza katika kikao hicho ameshukuru jitihada za Serikali kuona umuhimu wa kutoa kipaumbele katika maamdalizi ya Mpango wa uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI nchini.

Dkt. Martin amesema kuwa hii ni nyenzo muhimu sana kwa nchi kwani huu ni mwanzo mzuri wa kuiwezesha nchi kuweza kutekeleza mwitikio wa UKIMWI kwa fedha zake za ndani. Hata hivyo, aliwahakikishia wajumbe wa kikao kuwa kuandaliwa kwa mpango huu hakumaanishi kuwa wafadhili na wadau wa maendeleo wataondoka nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau kutoka Wizara,wadau wa wamaendeleo na watekelezaji wa Afua za Mwitikio wa UKIMWI.










Share:

WANAHARAKATI WASISITIZA UUNGWAJI MKONO KWA WANAWAKE WALIO TEULIWA NA VYAMA KUGOMBEA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WANAHARAKATI wa Jinsia na Maendeleo wameshauri kuwaunga mkono wanawake ambao wameteuliwa na vyama vyao kutokana na kukatwa majina ya  wanawake wengi katika mchakato wa ndani wa vyama vyao.

Akizungumza jana Novemba 06,2024 Mabibo-Jjijini Dar es Salaam katika ofisi za Mtandao wa jinsia TGNP kwenye semina za jinsia na Maendeleo (GDSS)zinazofanyika kila Jumatano, Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Nobart  Dotto amesema wao kama wanahaharakati wamedhamiria kwa dhati kuwaunga mkono wanawake walioteuliwa na vyama vyao kuanzia kipindi cha kampeni hadi katika kipindi cha kura.

Aidha Nobart ameeleza kuwa wanatamani kuona usawa wa kijinsia katika jamii ambapo wao kwa  kuonesha dhamira ya nia yao wamewaahidi wagombea hao kuwaunga mkono katika  kampeni pale zitakapo anza.

Kwa Upande wake ,Mwanaharakati wa Jinsia, Bi.Jackline Msafiri ameshauri wanawake ambao wameteuliwa na vyama vyao watambue kwamba hata kama wasipopitishwa, kura ndio zitakazo amua  hivyo wawe wavumilivu.

Aidha Jackline amewaasa wanawake waliojitoa kugombea katika uongozi, majina yao yakikatwa katika awamu hii wasikate tamaa kwani hata yeye aliwahi kugombea awali lakini alipofikia katika hatua ya uteuzi alionekana hajakidhi sifa.
Share:

DK. SAMIA KUZINDUA MFUKO WA MIKOPO YA UBUNIFU KWA VIJANA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Waziri Wa Elimu, Sayansi Na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan atazindua rasmi mfuko wa mikopo kwa ajili ya kusaidia bunifu na teknolojia zinazobuniwa na vijana wa Kitanzania

Aidha kupitia Uzinduzi huo atakabidhi hundi ya Shilingi bilioni 6.3 kwa watafiti 19 na atawatambua na kutoa tuzo maalumu kwa wanasayansi na wabunifu ambao matokeo ya kazi zao yamechangia kuleta mabadiliko ya kiuhumi na kijamii, ndani na nje ya nchi.

Prf. Mkenda ameeleza hayo leo November 6,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano hilo ambapo amefafanua kuwa mbali na hayo Rais Samia pia atakuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Tisa la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linalofanyika kila mwaka chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 2 hadi 4,2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam,linalokwenda na Kauli mbiu ya Kongamano kwa mwaka huu kuwa ni"Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ununifu katika Kuhimili Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi na Kuchangia kwenye Uchumi Shindani”.

Prof.Mkenda amesema Kongamano hilo linalenga kuwaleta pamoja watafiti, wabunifu, na wadau kutoka sekta mbalimbali, ndani na nje ya nchi ili kujadili kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mchango wa Sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema kupitia Kongamano hilo Serikali itapata michango ya kisera na kitaalamu ambayo itasaidia kuimarisha sera, mikakati, na juhudi nyingine zinazolenga kuimarisha mchango na mshikamano baina ya taasisi, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo katika kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama nyenzo kuu ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watanzania.

"ili kufanikisha na kufikia malengo yaliyokusudiwa, nitumie fursa hii kuwaalika Watanzania wote pamoja na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, ndani na nje ya nchi, kushiriki Kongamano hili la STICE na hata wale watakaoshindwa kuhudhuria kwasababu tofauti tofauti wafuatulie kongamano hili kwenye luninga kwasababu litakuwa mubashara,"amesema





Share:

Wednesday, 6 November 2024

WAANDISHI WA HABARI WA REDIO JAMII WAPEWA MAFUNZO MKOANI KATAVI


Na Mwandishi Wetu, Mpanda

Waandishi wa Habari wa redio jamii Mkoani Katavi wametakiwa kuchagiza urithi wa utamaduni usioshikika ili kuchochea fursa za ajira kwa Wanawake na vijana.

Carol Steven, Afisa Michezo, Utamaduni na Vijana Mkoani Katavi ametoa wito huu leo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa redio jamii Mkoani humo.

Mafunzo hayo yameandaliwa na shirika la Tanzania Media for Community Development kwa ufadhili wa mradi wa UNESCO- Alwalweed Philanthropies ili kujenga uwezo wa kutumia taaluma zao ili kuchagiza utamaduni wa urithi usioshikika na kuchochea fursa za ajira kwa Wanawake na vijana Mkoani Katavi.

Bwana Steven alisisitiza kuwa nchi ya Tanzania ni nchi ya kipekee ambayo imeendelea kulinda utamaduni wake na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani Mkoa wa Katavi una fursa nyingi zinazohitaji kutangazwa.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Leah Gwaza aliwataka waaandishi hao kutangaza urithi wa utamaduni usioshikika ili kuvutia wawekezaji Mkoani na kutengeneza fursa za kiuchumi kwa Wanawake na vijana,

“ Ukimsaidia Kijana umesaidia taifa la kesho na ukimsaidia mwanamke umeisaidia jamii nzima,” alisema Gwaza ambae alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Jamila Kimaro.

Mkoa wa Katavi ni moja wa mikoa mitano inayosifika na kuongoza kwa uzalishaji wa chakula ambapo pia ina vivutio vingi vya utalii na madini.

Mafunzo hayo pia yamejumuisha wasanii kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.
Share:

BENKI YA EQUITY TANZANIA YASAINI MKATABA WA KUWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI


BENKI ya Equity Tanzania imesaini mkataba na Taasisi ya ADC Tanzania, washauri wabobezi wa biashara, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi maalum wa kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Meneja Mkuu wa Biashara wa benki hiyo, Leah Ayoub amesema mradi huo unafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya African Guarantee Fund(AFAWA).

Amesema lengo kuu la mradi huo ni kuwajengea wanawake uwezo katika biashara zao waweze kufikia vigezo vya kupata huduma mbalimbali za kifedha, ikiwemo mikopo inayotolewa na benki hiyo kuboresha maisha yao kijamii na kiuchumi.

Leah amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mkakati wa beki hiyo kuongeza wigo wa huduma kwa wateja wadogo na wa kati (MSMEs), kwa lengo la kufikia asilimia 65 ya mikopo yote ifikapo mwaka 2030.
“Tunakuwa na dhamira ya kuwawezesha wanawake katika biashara, ushirikiano huu ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kufikia ukuaji wa kiuchumi endelevu,” amesema Leah.

Mradi huu unalenga kuwawezesha zaidi wanawake nchini kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha, mikopo nafuu, na ushauri maalum wa biashara.

Kwa hatua hiyo, Benki ya Equity Tanzania inaendelea kujitolea kuimarisha uimara wa kiuchumi na ujumuishi wa kijamii nchini.

Naye Ofisa Biashara wa ADC, Laura Vedasto amesema wanatarajia kuja na programu isemayo ‘Jifunze utoke’ itakayowasaidia wanawake kujua mbinu zitakazowawezesha kupata biashara na kukua.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger