Saturday, 2 November 2024

DC MKUDE AAGIZA ELIMU YA ULIMAJI WA PAMBA KWA WANACHAMA WA AMCOS KISHAPU

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mkoani Shinyanga, Mhe. Joseph Mkude

Na Sumai Salum - Kishapu

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mkoani Shinyanga, Mhe. Joseph Mkude, amevitaka Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu kutoa elimu kwa wanachama kuhusu ulimaji sahihi na kanuni bora za utunzaji wa pamba katika msimu wa kilimo wa 2024/2025.

Akizungumza katika kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu kilichofanyika Novemba 1, 2024, katika ukumbi wa SHIRECU, Mkude amesema  pamba ni zao la kimkakati na matarajio ni kuongeza pato la wilaya, mkoa, na taifa kupitia zao hilo.

"Kishapu tunasifika kwa ulimaji wa pamba, lakini kuna baadhi ya wakulima wameonekana wakimwaga pamba chini. Hii inadhihirisha kuwa hawajui thamani ya zao hilo. Natoa maelekezo kwa Afisa Ushirika na viongozi wa vyama vyote kuhakikisha wanatoa elimu kwa wanachama kuanzia kwenye maandalizi ya mashamba hadi kuvuna," amesema Mkude.

Aidha, Mkude ameeleza kuwa ataunda tume ya uchunguzi kuhusu madai ya uwepo wa mchanga kwenye pamba zinazopelekwa viwandani, akimtaka Afisa Ushirika kuitisha kikao baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba, ikijumuisha AMCOS, SHIRECU, kampuni zinazonunua pamba, na Wakala wa Vipimo.

Amesema pia ipo changamoto ya wakulima kupewa malipo pungufu, akitoa ushauri kwa wanachama kununua mashine za kisasa za kuhesabia fedha ili kuboresha usimamizi wa fedha zao.

"Ni muhimu kuwa na uwazi katika matumizi ya fedha," ameongeza Mkude.

Katika hatua nyingine, ameweka wazi kwamba serikali imeanzisha mipango ya kuwasaidia wakulima kwa kutoa pembejeo, viuatilifu, na matrekta 16, ambayo tayari yanatumika katika maeneo yasiyolimika wakati wa mvua. 

"Tunatoa wito kwa wakulima kuendelea kulima na kuandaa mashamba mapya," amesema.

"Tunaanza na maeneo chepechepe na sehemu zote zilizoomba kulimiwa zitafikiwa ikiwemo Bubiki na Bunambiyu kisha tutapeleka maeneo mengine, nitoe wito endeleeni kulimia ng'ombe kabla hatujafika huko na baadaye tutayagawa kwa mujibu wa sheria ili yawanufaishe na pia wawekezaji wasaidie kuinua zao la pamba kwa kutuletea zana za kilimo", ameongeza Mkude.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu, amemtaka Afisa Ushirika Faraji Kimwaga kukusanya takwimu za wale walikatwa fedha kwa madai ya pamba kuwa na mchanga, na kwamba tume itakayoundwa itafuatilia madai hayo kwa vielelezo maalumu.

Meneja wa SHIRECU, Kanda-Mhunze Ramadhani Kato, amesisitiza umoja kati ya wanachama wa AMCOS ili kupunguza changamoto mbalimbali, huku akiiomba serikali kuleta wanunuzi wengi wa pamba ili kuwepo kwa ushindani mzuri.

Katika kikao hicho, wanachama walieleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya makampuni ya pamba kuwakata kilo kadhaa kwa madai ya mchanga, jambo linalopelekea hasara kwa vyama vya msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Joseph Mkude akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu Novemba 1,2024 katika ukumbi wa SHIRECU- Picha na Sumai Salum 
Meneja SHIRECU Kanda-Mhunze Ramadhani Kato akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi AMCOS Ishosha-Basami, Cosmos Marco akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Katibu AMCOS Mihama, Bi.Mary Ndaki akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Shija Ntelezu akizungumza kwenye kikao chaVyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira na Diwani wa kata ya Mwamashele Wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Lucas Nkende akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Willium Jijimya Novemba 1,2024 katika kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Mzee Mathius Lembo mwenyekiti wa AMCOS Lwagalalo akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Katibu wa Siasa na Uenezi Chama Cha Mapinduzi CCM Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Jiyenze Seleli akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Katibu AMCOS Gimaji, Raphael Sospeter akizungumza kwenye kikao cha uVyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Wenyeviti na makatibu wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wakisiliza na kuchangia mada kwenye kikao
Katibu wa AMCOS Komagililo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga ,Joseph Ally akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu
Afisa Ushirika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Faraji Kimwaga akizungumza kwenye kikao cha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilaya ya Kishapu







Share:

SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 2 KUENDELEZA MIRADI YA REA




Na mwandishi wetu, Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipa kipaumbele sekta binafsi kutekeleza miradi ya nishati ya umeme kwa kuwekeza katika sekta hiyo na kuwezesha fedha ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mha. Advera Mwijage alipotembelea mradi wa umeme wa Ijangala (Ijangala Mini Hydropower Plant 360 kW) uliopo katika wilaya ya Makete mkoani Njombe.

Amesema kuwa Rais Samia amefanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na muda wote katika maeneo yenye miradi hiyo.

"Tunatoa shukrani kwa Rais Samia kwa kutambua mchango wa sekta binafsi katika kushirikiana na Serikali kuendeleza vyanzo vya umeme na kuhakikisha wananchi wanapata huduma," amesema Mha. Mwijage.

Vile vile ameishukuru Wizara ya Nishati na Bodi ya Nishati Vijijini kwa miongozo na maelekezo mbalimbali ya kuhakikisha REA inatekeleza majukumu yake ipasavyo katika kuwahudumia wananchi.

Vile vile, amesema kuwa, utunzaji wa mazingira katika miradi hiyo umepewa kipaumbele kwa kuwa inazalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu.

"Tunapata fedha kupitia mifuko inayofadhili miradi ambayo haizalishi hewa ya ukaa hivyo, mradi huu ni mojawapo ya mradi ambao hauzalishi hewa ya ukaa, ni rafiki kwa mazingira, " ameongeza Mha. Mwijage.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Umeme Ijangala, Daudi Sanga amesema kwa kiasi kikubwa mradi huo umefadhiliwa na REA na wadau wengine wa maendeleo. Mradi huo unazalisha kilowati 360.
Share:

TANESCO YAACHANA NA MKATABA WA MIAKA 20 WA UNUNUZI WA UMEME NA SONGAS


TANESCO imeachana na Mkataba wa Miaka 20 wa Ununuzi wa Umeme na Songas: Hii ni hatua muhimu kuelekea kujitegemea kwa Nishati chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Katika hatua muhimu, TANESCO imetangaza kumalizika kwa mkataba wa miaka 20 wa kununua umeme kutoka Songas, kampuni inayozalisha umeme kwa njia ya gesi asilia. Hii ni hatua ya kihistoria kwa Tanzania, kwani nchi yetu inachukua hatua zaidi za kuhakikisha kujitegemea katika nishati.

Kwa mafanikio ya maendeleo ya Mradi wa Bwawa la Umeme wa Julius Nyerere, ambao tayari unaongeza megawati 940 kwenye gridi ya taifa, Tanzania sasa iko katika nafasi nzuri zaidi ya kukidhi mahitaji yake ya nishati. Uamuzi huu unaakisi dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kuaminika, wa bei nafuu, na endelevu kwa Watanzania wote.


Chini ya uongozi wake, serikali imeweka kipaumbele kwenye miradi mikubwa ya nishati, ikiiwezesha TANESCO kuongoza katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme imara kote nchini. Hatua hii ya kimkakati inalenga kulinda maslahi ya taifa, kuunda nafasi za ajira, na kukuza uchumi.


Kwa pamoja, tunasonga mbele kuelekea mustakabali mwangavu na kujitegemea

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI NOVEMBA 2,2024

 



Magazetini leo
     
Share:

Friday, 1 November 2024

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA NISHATI ATEMBELEA UJENZI WA KITUO MAMA CHA GESI ASILIA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amefanya ziara ya kutembelea eneo la ujenzi wa Kituo mama cha Kushindilia na Kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG) ambacho kijapatikana Ubungo Jijini Dar es Salaam ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 01,2024 Ubungo Jijini Dar es salaam Naibu Katibu wizara ya Nishati Dkt.Mataragio amesema,Kituo hicho kinalenga kuhudumia magari yote ambayo yanatumia gesi asilia ambayo ni chanzo Cha nishati safi ukilinganisha na Petroli na dizeli.

Aidha Maragio amesema Kituo hicho kinatarajiwa kutoa huduma kwa wafanyabiashara wadogo ambao nao watawasogezea watu huduma hiyo kwa ukaribu, kwasababu watakuwa na sehemu ya kuchukuliwa nishati hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta,TPDC,Mhandisi Emmanuel Gilbert amesema kituo hicho kitatoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo ambao watahitaji kuwekeza katika biashara ya Gesi kwa ajili ya kujaza kwenye magari.

Amesema kutokana na ukubwa wa kituo hicho kinahimili kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwasiku kinaweza kuhudumia magari zaidi ya Elfu moja.

Aidha Mhandisi Gilbert. amesema Gesi itakayo patikana katika kituo hicho itatumika kwa matumizi mbalimbali yakiwemo matumizi ya shule,hospitali,pamoja na viwandani.

Aidha amebainisha kuwa hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH)pamoja na kiwanda cha Kairuki tayari wameishaingia makubaliano na TPDC kwa ajili ya kuwapelekea gesi kwa aili ya matumizi yao.

Kituo hicho chakushindilia na kujaza gesi kinatarajiwa kuwa mbadala wa petroli na disel kwani kitatumika kuzalisha nishati ya Gesi kwa ajili ya magari,nishati ya viwandani ambapo katika hospitali ya Muhimbili watatumia nishati hiyo kwa ajili ya kuzalisha mvuke wa kufanyia usafi
Share:

MAANA YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KUIFUNGUA NCHI


Tangu aingie madarakani Machi 2021 hadi Agosti 2024, Rais Samia Suluhu Hassan ameufungua  uchumi wa Tanzania kwa dunia na kujenga mazingira bora ya biashara za kimataifa. 

Matokeo ya juhudi hizi yanaonekana wazi katika ukuaji wa biashara yetu kimataifa, kutoka USD 17.4 bilioni (Mauzo nje - $8.4bn, Uingizaji bidhaa - $9bn) hadi kufikia USD 31.4 bilioni (Mauzo nje - $15bn, Uingizaji bidhaa - $16.4bn). Hii ni sawa na ongezeko kubwa la 84%! 📈 

Huku tukishuhudia ongezeko hili la kibiashara, deni la nje limeongezeka kwa asilimia 33%, kutoka $24.4 bilioni hadi $32.6 bilioni, ambalo ni jambo la kawaida kwa nchi zinazopiga hatua za kimaendeleo kupitia uwekezaji wa kimkakati. 

Kwa kufanya hivyo, Rais Samia amefungua milango ya fursa mpya kwa Watanzania na kukuza uchumi kwa kuhakikisha Tanzania inakuwa sehemu ya ushindani wa kibiashara duniani. 

Twende pamoja na Mama kwa maendeleo zaidi!

Chanzo benki kuu ya Tanzania monthly Economic Review May2021 and Monthly Economic Review for October 2024
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger