Monday, 28 October 2024

SMAUJATA TANGA YAWATAKA VIJANA KUCHAGUA VIONGOZI WATAKAOKUWA SAUTI YA WANANACHI





Na Oscar Assenga, TANGA

VIJANA Mkoani Tanga wametakiwa kuhakikisha wanawachagua viongozi ambao watakuwa sauti ya wananchi kwenye maeneo yao na sio wachuma tumbo wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu .

Wito huo ulitolewa leo na Mkuu wa Idara ya Vijana Hamasa Smaujata Mkoa wa Tanga Athumani Sheria wakati akizungumza na mtandao huu ambapo alisema vijana ni muhimu kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi huo kwa wingi ili waweze kuwachagua viongozi ambao watawapa maendeleo.

Alisema kwa sababu lazima viongozi wanaowachagua wawe ambao wanajitokeza na kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maendeleo katika maeneo yao kwa kushirikiana na wananchi.

“Ndugu zangu vijana katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa tuhakikishe tunatumia haki yetu ya msingi kuwachagua viongozi ambao watakuwa sauti ya wananchi kwa kuchochea maendeleo na sio wachuma tumbo”Alisema Sheria

Hata hivyo aliwataka vijana kuhakikisha wanajitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi huo kutokana na kwamba mchango wao kwenye maeneo yao unaweza kuwa na tija kubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo

Aidha pia alisema kwamba wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa uwekezaji wa Bilioni 429.1 katika Bandari ya Tanga ambayo yamewezesha maboresho makubwa na hivyo kuufungua kiuchumi mkoa huo.

Alisema maboresho hayo yamewasaidia kupata ajira lakini Serikali kuongeza pato pamoja na kuwainua kiuchumi vijana wa bodaboda na mama lishe ikiwemo wafanyabiashara mbalimbali mkoani humo.
Share:

Sunday, 27 October 2024

HOFU YATANDA MATUMIZI YA KEMIKALI YA ZEBAKI KWA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU, WACHENJUAJI NA WAMILIKI WA LESENI NZEGA

WACHIMBAJI Wadogo wa madini ya dhahabu, wachenjuaji na wamiliki wa leseni wilayani Nzega mkoani Tabora wameeleza hofu yao juu ya matumizi ya kemikali ya zebaki (Mercury)  kwenye shughuli zao na kuishauri Serikali kuzuia matumizi yake baada ya kubaini athari zake kiafya na kimazingira.


Baadhi ya wachimbaji, wachenjuaji na wamiliki wa leseni walisema hayo baada ya kufuatwa kwenye mgodi namba tano wa Lusu uliopo kitongoji cha Mkwajuni, Kata ya Lusu wilayani Nzega mkoani Tabora na wataalam kutoka Maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, kanda ya kati.

Wadau hao walikuwa wakipewa elimu juu ya matumizi na utunzaji salama wa kemikali ya zebaki inayotajwa na shirika la afya duniani kuwa miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya za binadamu na mazingira.


Mmoja wa wachimbaji Aboubakar Nuru alisema baada ya kugundua madhara hayo makubwa ya Zebaki hawaoni haja matumizi yake kuendelea hata kama kuna tahadhari badala yake anashauri ni vyema ikapatikana na kuhamasishwa kemikali nyingi Mbadala ili kuwanusu wachimbaji na watu wanaowazunguka.


Aidha Salum Ngozani akasema bado ni ngumu kuiondoa haraka kemikali hiyo kabla ya kuweka namna bora ya kulinda kemikali nyingine mbadala aina ya Sodium cyanide ambayo ufungashaji wake huwa ni kwa kipimo kikubwa na kuwa rahisi kuwatamanisha wezi tofauti na ZEBAKI ambayo ni rahisi kufichika ambapo kiwango kidogo huweza kufanya kazi kubwa 


“Lakini kuna wanyonge hawawezi kumudu hii kemikali Mbadala, hawawezi kununua Wala kuilinda wakiwa migodini, Hawa watasaidiwaje?kuna watu wanaitwa manyani huku, wanaingia maduarani wakati wowote na hawawezi kuiacha, wataiba tu na ni miongoni mwa sisi, tutawezaje kuulinda?”Alisema Ngozani.

Aidha Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo TABOREMA, wilayani Nzega na mjumbe wa mkutano mkuu wa FEMATA taifa, Joseph Mabondo, akaishukuru maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kutoa elimu hiyo na kuwasihi kuendelea kuelimisha na wachimbaji  wa maeneo mengine ya wilaya hiyo juu ya matumizi mazuri na salama ya zebaki, namna ya kuiingiza katika maeneo yao, namna ya kuitumia, kujisajili kuuza kemikali na mambo mengine muhimu.
 
Mwenyekiti huyo akasema hata wao wameendelea kuelimisha wachimbaji wadogo juu ya madhara ya zebaki na wengine wamekubali kuachana nayo na kutumia kemikali Mbadala huku ambao bado wanatumia zebaki akitaka waendelee kuelimishwa.

 "Tumekuwa pia tukiwahimiza kujenga makaro ili kuzuia utiririshaji ovyo wa maji wanayotumia kuchenjua madini Ili wasisababishe athari kiafya na kimazingira" Alisema Mabondo.

Kwa upande wake Meneja wa mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali kanda ya kati, inayohusisha mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida, Tabora na Morogoro Bw Gerald Meliyo alisema kemikali ya zebaki sio salama kiafya na kimazingira ndio maana wanaendelea kutoa elimu ya kujikinga na athari zake wakati wa kuitumia.

Meliyo akasema kimataifa kemikali hiyo iko mbioni kuondolewa na baadhi ya maeneo ikiwemo hospitali na viwandani tayari wamesitisha matumizi yake huku mkakati wa Serikali ikiwa ni kuiondoa kabisa kemikali hiyo sokoni katika matumizi yake ndani ya miaka michache ijayo.

Akasema hawawezi kuzizuia kwa mara moja na ndio maana wanaendelea kutoa mafunzo ili wachimbaji watumie ila kwa tahadhari, "Ndio maana tunawahimiza kutumia vifaa kinga ili kujilinda na madhara yanayoweza kuwapata hata kama hayaonekani sasa, hata baadaye, huwa inaharibu mapafu, inakwenda kwenye ubongo, inafanya watu kutetemeka na hivyo kushindwa kufanya majukumu yao, lakini miaka michache ijayo huenda upatikanaji wake ukawa mgumu”Alisema Molel.

Akawahimiza wachimbaji hao kujiunga vikundi ili kutumia kemikali mbadala ya zebaki aina ya Sodium cyanide ambayo haina madhara makubwa tofauti na zebaki madhara yake ni makubwa kiafya na kimazingira.

Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Bi Fatuma Kyando akasema kama Serikali ama wasimamizi wa wachimbaji wadogo huwa wanaangalia zaidi afya ya watu wao kwa kutamani wachimbe kutafuta fedha huku wakiwa salama kiafya ili waweze kutumia fedha zao wanazotafuta hata baada ya kazi.

 
Akasema elimu hiyo kwa wachimbaji ni muhimu na itasaidia kwani inawagusa wahusika wenyewe moja kwa moja kwa kujua madhara na namna ya kuyaepuka wao na jamii inayowazunguka.
 
Katika hatua nyingine Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Mkwajuni kata ya Lusu yalipo machimbo hayo akiwemo Bi Dotto Ramadhani na Charles Patrick wameomba kuondolewa kwa migodi jirani na makazi na kudhibitiwa usafirishaji holela wa udongo utokanao na madini ili kunusuru afya za wakazi kwani wasafirishaji wamekuwa wakipeperusha ovyo mchanga bila kujali na kutengeneza njia katikati ya makazi na viwanja vya watu.

 "Mara vumbi, mara makemiko haya, Hawa wenye mialo (mashimo ya madini) inabidi wasogezwe waende mbali kabisa, kwanza hayo makrasha yenyewe ni kelele tupu, tunaomba Serikali itusaidie",alisema Charles Patrick.
Afisa madini mkazi mkoa wa Tabora Fatuma Kyando
Gerald Meliyo, meneja wa Maabara ya mkemia mkuu wa Serikali, Kanda ya kati

Share:

MRADI WA BAHARI MAISHA KUONGEZA USHINDANI KATIKA SOKO LA MAZAO BAHARI KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu.

Mradi wa Bahari Maisha unaotekelezwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) unatarajiwa kuongeza ushindani katika soko la mazao bahari kimataifa. 

Hayo yamebainishwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa Tanzania (UNDP), Shigeki Komatsubara katika hafla ya kukabidhi makaushio na mashine za kusaga zao la mwani, pamoja na vifaa vya kuwawezesha wakulima wa mwani, na wafugaji wa jongoo bahari na kaa iliyofanyika juzi, jijini Dar es salam.
 
Komatsubara amesema kupitia Mradi wa Bahari Maisha changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa mazao bahari kupitia mradi huo, (UNDP) limechukua hatua kwa kufadhili mafunzo ya uendeshaji wa kilimo, usimamizi wa vikundi, usimamizi wa fedha, kuongeza thamani ya mazao pamoja na masoko kwa vikundi vya wanawake na vijana.

“Leo tunatoa mashine nne zenye uwezo wa kusaga zao la mwani tani moja kwa saa na makaushio manne yenye uwezo wa kukausha mwani tani moja kwa mara moja pamoja na bando elfu mbili za kamba na bando elfu tatu za taitai,

"Hii ni katija kuwawezesha wakulima wa mwani na wafugaji wa kaa na jongoo bahari katika maeneo ya Tanga, Bagamoyo, Unguja na Pemba kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao haya Kimataifa" sema Komatsubara.

Aidha amebainisha kuwa Shirika linaendelea kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau mbali mbali wa maendeleo kuinua Uchumi wa Bluu hususani kwa makundi ya wanawake na vijana.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mkazo wa Uchumi wa Bluu, ambapo amebainisha kuwa Mkoa wa Tanga unaendelea kuimarisha uvuvu salama.

'Sambamba na hilo, pia kuhamasisha kilimo cha mwani pamoja na ufugaji wa jongoo bahari na unenepeshaji wa kaa, lakini pia tujiweka zaidi kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa katika zao la mwani ili kupata bidhaa mbali mbali zenye ubora" amesema.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kepteni Hamad Hamad amelishukuru (UNDP) pamoja na Chuo cha Mipango kwa mradi huo kwani unawagusa moja kwa moja kiuchumi wananchi wa Zanzibari.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Edwin Mhende amebainisha kuwa uzalishaji wa zao la mwani unaendele kukua kutoka tani elfu tatu mwaka 2021 hadi kufikia tani elfu tisa kwa mwaka huu 2024 ikiwa ni ongeezeko la asilimia 166.67, hivyo kwa niaba ya serikali ameahidi ushirikiano madhubuti kwa wadau wa maendeleo.

Awali akitoa taarifa ya utakelezaji wa Mradi huo wa Bahari Maisha Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Juvenal Nkonoki amesema mradi huo unaotekelezwa na Chuo ni matokeo ya tafiti iliyofanywa kwa wakulima wa mazao bahari na kubaini changamoto kadhaa zinazowakabili wakulima hao. 

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mbinu duni na ukosefu wa vifaa vya kisasa, hivyo chuo kwa kushirikiana na UNDP waliandaa programu maalumu ya mafunzo elekezi ya uendeshaji wa kilimo cha kisasa, usimamizi wa vikundi.

"Lakini pia programu hiyo iliandaa usimamizi wa fedha, kuongeza thamani ya mazao pamoja na masoko ambapo zaidi ya wakulima na wafugaji 350 wa mazao bahari katika maeneo ya Unguja, Pemba, Tanga, na Bagamoyo wamenufaika na mafunzo hayo" amesema.
Share:

OUT YATOA MAFUNZO KUIMARISHA UFUATILIAJI NA USIMAMIZI WA MIRADI SERIKALINI


Mafunzo ya ufuatiliaji na tathmini yanayoendeshwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa pamoja tawala za mikoa yanatarajiwa kuimarisha usimamizi pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi inayowekezwa na serikali katika kupeleka shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa kuwa watumishi katika idara hizo watakuwa wameimarika vyema.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ndg. Mussa Otieno, wakati akifungua mafunzo ya awamu ya pili ya Ufuatiliaji na Tathmini akimuwakilisha Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mh. Adolf Ndunguru, jijini Dodoma.

“Serikali inatumia bajeti kubwa katika mamlaka za serikali za mitaa, baada ya mafunzo haya tunaamini kila mmoja atakuwa ameimarika na atakuwa na uwezo wa kutimiza malengo yanayotakiwa katika maswala ya ufuatiliaji na tathmini ili miradi ya serikali iendane na malengo yaliyopangwa. Tukatumie vyema utaalam tutaopata hapa na tukawashirikishe na wenzetu tunaofanya nao kazi pamoja ili kuwa na timu nzuri kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika halmashauri tunazotoka,” amesema Ndg. Otieno.

Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Utendaji wa serikali, ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Sakina Mwinyimkuu, amesema serikali za mitaa ndiyo mtekelezaji mkubwa wa shughuli za serikali, karibu 70% ya shughuli zote za serikali zinatekelezwa na mamlaka ya serikali za mitaa hivyo washiriki wa mafunzo haya ya ufuatiliaji na tathmini wanatarajiwa kuiongezea uwezo serikali kufikia malengo yake ya kitaifa ikiwemo dira ya maendeleo.

“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni mdau anayetusaidia kujengea uwezo taasisi za umma katika ufuatiliaji na tathmini, serikali za mitaa ndiyo watekelezaji wa shughuli za serikali na ndiyo wanaotoa picha ya utendaji wa serikali kwa jamii. Hili ni eneo linaloweza kuwabadilisha mitizamo ya wananchi na kuwajengea imani kwa serikali yao kwa kuona inasimamia vyema utekelezaji wa sera, miradi na mipango. Hivyo mafunzo haya yatawasidia simamia vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoibuliwa na halmashauri na mingine ya kitaifa inayotekelezwa katika halmashauri,” amesema Bi. Mwinyimkuu.

Mratibu wa Mafunzo na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Emmanuel Mallya amesema chuo hiki kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri mkuu kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmni nchini hivyo kinaendesha mafunzo haya ili warudipo basi serikali ishuhudie mabadiliko makubwa ambayo yanalenga kuimarisha utendajikazi hasa katika upande wa ufuatiliaji na tathmini.

Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo na Katibu Tawala msaidizi sehemu ya Usimamizi, Ufutiliaji na Ukaguzi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Ndg. Pius Ngaiza, amekipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kuitendea haki nafasi waliyopewa ya kutoa mafunzo haya kwani wengi walikuwa wanafanya tathmini na ufuatiliaji katika namna ambayo ilileta shida hasa katika ukaguzi, mafunzo haya yamewaimarisha na wanaamini kazi sasa itafanyika kwa kufuata mfumo unaotakiwa kiofisi na hata kitaifa.

Mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo ya awali yaliyoendeshwa katika jiji la Arusha kanzia Oktoba 7, 2024 hadi Oktoba 11, 2024, ambapo baada ya mafunzo haya yaliyohudhuriwa washiriki 90 kutoka mikoa takriban 13 ambayo kiujumla inakuwa 70% ya halmashauri, manispaa na majiji yote nchini kupata mafunzo haya ya ufuatiliaji na tathmini.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI OKTOBA 27,2024

 
Share:

Saturday, 26 October 2024

MBUNGE UMMY-KAZI YA MAENDELEO ILIYOFANYWA NA RAIS DKT SAMIA SULUHU MKOANI TANGA SIO YA KUTAFUTA KWA TOCHI




Na Oscar Assenga,TANGA

MBUNGE wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema kazi ya Rais Dkt Samia Suluhu anayoifanya ya Maendeleo katika Mkoa wa Tanga sio ya kutafuta kwa Tochi.

Ummy aliyasema hayo leo wakati akitoa salamu katika Kongamano la Samia Challenge 2024 ambalo limeandaliwa na African Anti-Violence Journalist lililofanyika Jijini Tanga kwenye ukumbi wa Samia Business Centre Kange.
Ambapo alisema  kuna miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya Afya,Umeme,Elimu,Maji na Vitega Uchumi karibia kila kona ambayo imechangia kuinua uchumi wa mkoa wa Tanga.

Alisema kwa sababu katika kila eneo la maendeleo utamkuta Rais Samia na kubwa zaidi ambalo wanajivunia nalo ni maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga ambapo uwekezaji uliofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu ni wa Bilioni 429.1

“Kutokana na hili sasa tunatembelea kifuata mbele kutokana na uwekezaji huo ambao umeufanya mkoa huo kuanza kupokea meli kubwa zinazoleta shehena za magari na hilo linaonyesha matunda ya uwekezaji katika Bandari kwa kuchimbwa kina na meli kutia nanga gatini “Alisema
Share:

TAASISI ZA UMMA ZITUMIE MIFUMO RASMI YA SERIKALI MTANDAO: MH.MACHANO




Na Mwandishi wetu,Dodoma

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Watendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ), wametembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mtumba jijini Dodoma.

Ujumbe huo, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mh.Machano Othman Said, umetembelea e-GA ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika kuendeleza eneo la Serikali Mtandao Tanzania Bara na Visiwani.

Sambamba na wajumbe hao, ugeni huo uliongozana na Mhe. Ali Suleiman Ameir - Waziri wa Nchi Afisi ya Raisi Ikulu, Zanzibar pamoja na Ndg. Saleh Juma Mussa - Katibu Mkuu - Afisi ya Rais, Ikulu Zanzibar.

Katika ziara hiyo kamati ilipata taarifa ya utekelezaji wa hafua mbalimbali za Serikali Mtandao kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh.Machano Othman Said ametoa wito kwa Taasisi za Umma nchini kutumia mifumo rasmi ya TEHAMA ili kuendeleza utawala bora,kudhibiti mapato ya serikali na kulinda usalama wa nchi katika zama hizi za sayansi na Teknolojia.

Mh. Machano amesema kuwa, Serikali zote mbili zina utayari wa mageuzi ya TEHAMA katika uendeshaji wa shughuli za serikali za kila siku katika kuwahudumia Watanzania.

" Kila tukiwasikia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Dkt.Hussein Mwinyi wamekuwa vinara katika kuleta mapinduzi ya kidijiti na kuonesha umuhimu wa TEHAMA katika utendaji, hivyo tusisitize Taasisi zote kutumia mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi wao wa kila siku" ameeleza Mh.Machano.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba, ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanziba (eGAZ) ili kuhakikisha Serikali Mtandao inaimarika kote Bara na Visiwani.




Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger