Friday, 4 October 2024
RAIS SAMIA AJA NA HATUA MPYA KATIKA MABORESHO YA MFUMO WA KIKODI TANZANIA
HATMA YA KOMBO MBWANA KUJULIKANA OCTOBA 31
Na Oscar Assenga, TANGA
MAAMUZI ya Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Kombo Mbwana Twaha kupelekwa mahakamani Kuu kwa ajili ya kupewa haki zake ama la itabainika Octoba 31 mwaka huu.Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama baada ya shauri hilo kuhairishwa Wakili wa Upande wa Utetezi Paul Kisabo alisema kwamba wanaamini mahakama itatenda haki na kutafsiri sheria kama ilivyo watasikia na kukiwa na maamuzi tofauti sheria zitawaelekeza nini cha kufanya .
Shauri hilo lililetwa mahakamani hapo na lilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa mbele ya Mhe.Jaji Happiness Ndesamburo ambapo kesi hiyo msingi wake waliifungua kwa ajili ya kuomba Kombo Mbwana Twaha aweze kupelekwa mahakamani ili aweze kupewa haki zake.
Aidha alisema kwamba Kombo anashikiliwa tokea 15 June 2024 alipokamatwa nyumbani kwake Handeni na mpaka leo bado anashikiliwa.
Alisema kesi hiyo msingi wake waliifungua kwa ajili ya kuomba kombo apelekwe mahakamni ili aweze kupewe haki zake kupitia maombi ya kuiomba mahakama kuu itoe amri mtu aletwe Yule aliyeshikiliwa kunyume cha sheria.
Wakili huyo alisema kwamba walifungua kesi hiyo na ilipangwa kusikiliza pande zote mbili wao upande wa mleta maombi Kombo Twaha Mbwana alikuwepo yeye na upande wa wajibu maombi ambaye ni kamansa wa RPC ,IGP,DPP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliwakilishwana mawakili wawili waliwasilisha hoja zao mahakamani hapo.
Awali akizungumza Katibu wa Chadema wilaya ya Tanga Shabani Ngozi alisema kwamba wamekuja Mahakam kuu kusikiliza kesi hiyo kwa mwenendo wa kesi wanawashukuru mawakili wao kwa kazi kubwa na ngumu wanayoendelea kuifanya kuhakikisha Kombo anapata haki yake ya msingi awe nje kwa dhamana .
Alisema kwa hiyo binafsi wanaendelea kushirikiana na mawakili wao na familia ili mwenzao awe huru waweze kuendeleza gurudumu la kuendeleza Taifa.
WANANCHI WA SHINYANGA WATAKIWA KUTUMIA ELIMU KAMA SILAHA YA UKOMBOZI WA MAENDELEO
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili Julius Mtatiro akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka wananchi kutumia elimu kama silaa ya ukombozi wa maendeleo.
Amesema hayo Jana Oktoba 03, 2024 wakati akifungua maadhimisho ya juma la wiki ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya stendi ya mabasi Iselemagazi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mhe. Wakili Mtatiro pia amewataka wazazi na walezi wa Mkoa wa Shinyanga kusimamia maadili ya watoto na vijana kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha wanapata elimu bora na kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na vijana shuleni na Nyumbani.
"Mzazi atakae sababisha kukatishwa masomo kwa mtoto wake atachukuliwa hatua", amesema Mhe. Mtatiro
Pia Wakili Mtatilo mewapongeza wazazi na walezi waliotoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha vijana wao wanaenda shule wakiwemo wasichana waliokatishwa masomo wamerejea tena shuleni kuendelea na masomo ili watimize ndoto zao.
Aidha, Mhe. Wakili Mtatiro alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kushiriki zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024.
Katika hatua nyingine, Mgeni Rasmi alipata fursa ya kutembelea banda ya Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga na taasisi mbalimbali.
Wednesday, 2 October 2024
WANAHARAKATI WATAKA MIFUMO YA ELIMU IBORESHWE KUPUNGUZA WATOTO KUKATISHA MASOMO
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wamewasilisha ombi kwa serikali kuhusu kuboresha mifumo ya elimu ili kukabiliana na changamoto ya watoto wanaokatiza masomo.
Katika semina iliyofanyika leo, Oktoba 2, 2024 Jijini Dar es Salaam, , Mwanaharakati wa Jinsia, Kennedy Anjelita, alisisitiza umuhimu wa kubadilisha mfumo wa elimu ili uwe rafiki kwa kila mwanafunzi, akiongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaoshindwa kumaliza masomo yao.
Anjelita amesema kupitia semina hiyo wamesisitiza kurudishwa kwa elimu ya stadi za kazi shuleni, akisema kuwa inaweza kuwa njia ya kusaidia wanafunzi kujipatia kipato na kuleta manufaa katika shule, ikiwemo kusaidia na masuala ya chakula badala ya kutegemea michango ya wazazi.
Pamoja na hayo Angelita alipendekeza pia uundaji wa utaratibu wa kukutana kati ya wazazi, walimu, na wanafunzi ili kujadili matatizo yanayowakabili watoto wanaokatisha masomo.
Aidha, Anjelita amesema wameshauri kuhusu adhabu zinazotolewa shuleni, akitaka zirekebishwe ili zisihamasishe wanafunzi kuacha shule.
Vilevile wadau hauo wamesisitiza umuhimu wa sera itakayoshughulikia watoto wanaoacha shule bila sababu, waakipendekeza kwamba wapelekwe katika magereza ya watoto kwa ajili ya kujifunza.
Kwa upande wake Theodosia Stephano ambaye pia ni mdau wa semina za Jinsia na maendeleo, ameeleza kuwa miundombinu ya shule, ikiwemo ukosefu wa madawati na vyoo ni miongoni mwa sababu zinazowafanya watoto kukatisha masomo.
Amesema kuwa uhaba wa chakula shuleni kutokana na hali duni ya kiuchumi ya wazazi ni sababu nyingine inayowakatisha tamaa watoto.
Theodosia ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu ili iweze kuwasaidia watoto wenye changamoto na kuwapa fursa sawa za elimu kama wenzao.
UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA ZANZIBAR KUFANYIKA OKTOBA
Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi Kisiwani Pemba, Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk amesema uboreshaji huo wa daftari utajumuisha mikoa ya Mjini Magharibi, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Pemba Kaskazini na Pemba Kusini.
Akizungumza wakati akifungua mkutano kama huo Kisiwani Unguja, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari ameongeza kuwa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024, Tume itawaandikisha watanzania waliopo Zanzibar ambao wametimiza umri wa miaka 18 na zaidi au watakaotimiza umri huo wakati au kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Amefafanua kuwa mtanzania huyo atakeyandikishwa ni lazima awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yeyote na awe anastahili kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
“Kwa lugha nyepesi ni kwamba, Tume itamwandikisha mtanzania yeyote aliyopo Zanzibar ambaye amekosa sifa za kuandikishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Hivyo, atakayeandikishwa kwenye Daftari la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi atapiga kura moja tu ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Asina.
Uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari ulifanyika tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma na mpaka sasa uboreshaji umeshafanyika kwenye mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Singida na sehemu ya mkoa wa Dodoma.
Tuesday, 1 October 2024
ASAKWA NA JESHI LA POLISI TANGA KWA TUHUMA ZA KUMUUA MKEWE NA BINTI YAO WA KAZI
Na Oscar Assenga, TANGA
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linamtafuta Alii Mohamed Bagidadi (60) mkazi wa Barabara ya 4 Jijini Tanga kwa tuhuma za kumuua mke wake Saira Ali Mohamed (50) na binti wa kazi anayejulikana kwa jina la Aisha (20) kwa kuwanyonga na kamba aina ya katani shingoni kisha kuwatoboa macho.
Akithibitisha kutokea tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (ACP ) Almachius Mchunguzi alisema kwamba tukio hilo lilitokea Septemba 30 saa moja usiku na kwamba baada ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho alitorokea kusikojulikana.
Kamanda Mchunguzi alisema kwamba Jeshi hilo linatoa wito wa wananchi kushirikiana na nao kutoa taarifa mahali popote atakapoonekana ili akamatwe na sheria iweze kuchukua mkondo wake.
“Kwa sasa tunamtafuta mtuhumiwa huyo lakini pia nitoe wito kwa wananchi kutoa taarifa mahali popote atakapoonekana ili akamatwe na sheria iweze kuchukua mkondo wake “Alisema Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga.
Hata hivyo aliwaasa wananachi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.