Sunday, 31 December 2023

SHUWASA YATOA CHAKULA KWA WENYE UHITAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imewakumbuka watu wasiojiweza katika Manispaa ya Shinyanga kwa kuwapa zawadi za mwaka mpya ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Zawadi hizo zimejumuisha mchele, mafuta ya kupikia, sukari na sabuni ambapo jumla ya watu 13 wamepatiwa msaada huo ambapo zawadi hizo ni mchele kilo tano, sukari kilo mbili, mafuta ya kula lita tatu na sabuni miche miwili.

Aidha SHUWASA imekuwa ikiwasaidia watu hao wenye uhitaji ikiwa ni pamoja na kuwalipia bili za maji za kila mwezi.









Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI DESEMBA 31,2023. .... FUNGA MWAKA

 


Magazeti ya kufungia mwaka 2023

Share:

Saturday, 30 December 2023

KC HALMASHAURI YA WILAYA YA UBUNGO WACHAMBUA BAJETI YENYE MLENGO WA JINSIA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) Kupitia vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Ubungo wamekutana kuichambua bajeti ya 2023/2024 yenye mlengo wa Jinsia ambapo wameangalia katika upande wa miundombinu ya Elimu,  Afya, Maji,Kilimo na Miundombinu ya barabara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 30,2023 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kituo Cha Taarifa na Maarifa  kata ya Manzese Bi. Theresia Lehanjara amesema kuwa kwenye maeneo ya elimu wameangalia miundombinu ya shule, kupatikana kwa vyumba vya kujisitiri kwa wasichana, uwiano wa matundu ya vyoo pamoja na uwepo wa vyoo kwa wenye ulemavu.

Aidha wameipongeza halmashauri ya Wilaya hiyo kwani imekuwa ikileta matumaini mazuri hasa kwenye eneo la elimu, wamewekeza fedha za kutosha katika kuimarisha miundombinu ya shule kwenye maeneo mbalimbali.

“Licha yakuwa kuna maeneo ambayo bado kuna changamoto, tunaamini mpaka kufikia mwezi wa sita matarajio mengi yatakuwa yamefikiwa kama watakuwa wamewekeza nguvu kwa wale watendaji”. Amesema

Amesema kuwa katika Wilaya yao hakuna uwiano sawa wa walimu wakuu wakike na wakiume ambapo imechangia changamoto kubwa ya kutatua mahitaji ya mtoto wa kike anapokuwa shuleni,ambapo wamebainisha pia kuhusiana na Miundombinu ya madarasa kubadilishwa kuwa maabara ingawa madarasa hayajitoshelezi.

"Tunaomba basi kama Wizara inawaamini wanawake, inapaswa kuwawezesha hawa wanawake wanapochaguliwa kuwa wakuu wa shule, tusisikie habari ya kwamba mwanamke amechaguliwa amekataa kuitumikia ile nafasi, kwanini wanaume wakipata nafasi wanapata uhamisho wao na wenzi wao. Jambo jingine ni madawati na majengo wanataka kuboresha maktaba kwenye mashule yetu tulipokua tukiangalia bajeti tunaomba wasipunguze madarasa kuwa maktaba maana majengo yaliyopo hayajitoshelezi". Amesema 

Vilevile amesema kuwa  bado wanakabiliwa na changamoto ya wodi ya wakinamama wajawazito kwa ajili ya kujifungua wanapohitaji huduma hiyo ambapo serikali inatakiwa kushughulikia changamo hiyo kwa haraka.

Kwa upande wake Mwalimu wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe Bi.Lihoya Chamwali amesema kuwa Bajeti yenye mlengo wa kijinsia ni muhimu ili kuhakikisha maendeleo yanamfikia kila mtu ambapo amesema wamebaini kuhusiana na suala la taulo za kike kuwa zimepungua kutoka Milioni mbili hadi kufikia Milioni Moja.

"Tulipewa ufafanuzi kuwa kuna pesa nyingine imetengwa na  hiyo ni kwaajili ya mapato ya halmashauri ya ndani, kuna pesa nyingine ambayo imetengwa kutoka vyanzo vingine hadi kufikia Milioni Kumi". Amesema Bi. Lihoya.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kituo Cha Taarifa na Maarifa Kata ya Mabibo Bw.Msafiri Mwajuma ameeleza kuwa bila miundombinu rafiki kwa mwanamke, haitawezekana kumuinua kiuchumi hivyo kunahitajika kutengeneza mazingira wezeshi.

Share:

KONDOA DC NA TGNP WAJADILI MAFANIKIO YA BAJETI YENYE MTAZAMO WA KIJINSIA


Na Mwandishi Wetu, Kondoa

Halmashauri ya wilaya ya kondoa, mkoani Dodoma, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, imeandaa bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia kwa kujenga miundombinu ya vyoo vya shule vyenye kukidhi mahitaji ya wasichana wanapokuwa kwenye hedhi.

Hayo yalibainishwa na Afisa Mipango wa Halmashauri, Joshua Mnyang’ali, alipokuwa akijibu taarifa ya uchambuzi wa Bajeti ya Halmashauri kwa mtazamo wa Kijinsia iliyofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa Kata ya Haubi.

“Choo tulichojenga shule ya Msingi Mwisanga na shule mpya ya sekondari ya Ntomoko, vina vyumba maalumu ya kujisitiri wasichana wanapokuwa kwenye hedhi, kichomea taka kwaajili ya kuteketeza taulo za kike ambazo zimetumika. Pia katika vyoo tunavojenga sasa, tunaweka sehemu ya haja ndogo kwa wavulana, lengo ni kupunguza msongamano kwenye vyoo, ili wanafunzi wafurahie kuwepo shuleni. Kwa kufanya hivyo tunapunguza pia utoro na kuongeza ufaulu”, alisema Mnang’ali.

Aidha naye mganga mkuu wa halmashauri, Dkt. Nelson Kimolo, amesema kwamba, Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, imedhamiria kupunguza kabisa au ikiwezekana kutokomeza vifo vya mama na mtoto, kwa kutenga bajeti Zaidi ya shilingi Milioni 44 kwaajili ya kuwalipa madereva wa ngazi ya jamii watakaotumika kuwasafirisha Mama wajawazito kutoka zahanati kwenda Hospitali kubwa ili kurahisisha mfumo wa rufaa.

“Huu ni mradi unaojulikana kama M-MAMA ambao umeleta mabadiliko makubwa, unasaidia sana kuondoa tatizo la usafiri, magari tuliyo nayo ya kubeba wagonjwa hayatoshelezi, tumeona afadhal kuwa na utaratibu huu mpya wa kuingia mikataba na madereva waliko kwenye jamii, wahudumu wa Hospitali wawasilane nao muda wowote ili kuhakikisha Mama mjamzito anapata huduma ya haraka na kukokoa maisha yake”, alisema Dkt. Kimolo.

Awali akiwasilisha mapendekezo ya Jumla mwezeshaji wa Uchambuzi wa Bajaeti kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba, pamoja na halmashauri kuwa na vyanzo vichache vya mapato ya ndani, bado wamejitahidi kuangalia eneo la afya na elimu.

Temba, ameongeza kwamba, bado kuna mapengo ya kijinsia kwenye Bajeti ya Halmashauri hasa katka eneo la ustawi wa Jamii ambapo Bajeti ya kuzuia na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia imetengwa kidogo, sambamba na Idara ya Maendeleo ya Jamii inayotakiwa kuwajibika katika uhamasishaji wa jamii kushiriki katika shughuli na maendeleo kutengewa fedha kidogo sana.

“Eneo la Ukatili wa Kijinsia, ni muhimu kuliangalia,tukiwekeza kwenye miundombinu ya elimu, alafu tusipoweka mikakati ya kuwalinda watoto wa kike na kiume wasifanyiwe ukatili wa Kijinsia na udhalilishaji wakingono, hatutapata matokeo mazuri”,alisema Temba.

Pia, eneo lingine lenye mapungufu ambalo Halmashauri imeshauriwa kuboresha na kuongeza msisistizo kwa viongozi wa vijiji na kata kuwashirikisha wananchi kwenye mchakato wa kuandaa bajeti ili waweze kuibua fursa na vikwazo katika maendeleo (O&OD) ili waweze kushiriki vizuri katika kuisimamia na kuitekeleza miradi ya maendeleo.

Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutumia kiasi cha shs.milion 440 kuboresha vyanzo vya maji, sh. Milion 3, kujenga vichomea taka katika zahanati, sh. Million 23 kujenga mashimo ya taka mbichi (placenta pit) katika zahanati na vituo vya afya, ambapo Kituo cha afya mnenia kimetengewa bajeti ya sh. Milion 35 kwa ajili ya kujenga kichomea taka na vyoo.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), unatekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri ya Kondoa, inayolenga kujenga uwezo wa kwa jamii kupitia Kituo cha taarifa na Maarifa, kupata uwezo wa kuchambua masuala ya Kijinsia na kushawishi kuingzwa kwa masuala ya Kijinsia katika sera, mipango na miongozo.

 Sambamba na kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali wa Halmashauri kuhusu masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uongozi bora na ushiriki wa wanawake katika uongozi.







Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger