Monday, 11 December 2023
Sunday, 10 December 2023
MBUNGE CONCHESTA LEONCE RWAMLAZA AGAWA MITUNGI YA GESI KAGERA
Na Mariam Kagenda _ Kagera
Mbunge wa viti maalum Mkoani Kagera Mhe, Conchesta Leonce Rwamlaza ametimiza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la ugawaji wa mitungi ya gesi kwa Wanawake wa kata za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba wanaokwenda kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Akizungumza kabla ya zoezi la ugawaji wa mitungi 75 kwa akina Mama waliofika na kuwakilisha wenzao kutoka baadhi ya kata hizo ikiwemo kata ya Kyaitoke, Kyamulaile Katoma Nyakato na nyinginezo Mbunge Rwamlaza amempongeza Rais Samia kwa namna alivyowaunga mkono wabunge wa Tanzania kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na kuwafanya wabunge hao kuwa waratibu wa ugawaji wa mitungi hiyo jambo litakalosaidia akina Mama hao kuondokana na madhara yanayoweza kutokana na kupika kwa kutumia kuni na mkaa.
Rwamlaza amesema yeye kama mbunge wa viti maalum kutoka mkoa wa Kagera kupitia CHADEMA anamuunga mkono Rais Samia kupitia mabadiliko ya Nchi kuongozwa na Mwanamke na kuwa ukiachana na itikadi za vyama Rais Samia amefanya jambo kubwa na la kihistoria.
"Rais Samia ni Mama mpambanaji nani asiyejua kuwa kawezesha miradi mingi na mikubwa hapa nchini tumeona katika sekta ya Elimu Barabara, afya na nyinginezo hivyo mimi siangalii mambo ya vyama ninachoangalia ni namna anavyowapigania wanyonge kama ambavyo amewainua Wanawake hawa", alisema Mbunge huyo.
Ameongeza kuwa huu ni muda wa akina Mama hao kupika kwa urahisi bila vikwazo kwani awali waliotumia kuni walihusishwa katika imani za kishirikina baada ya macho yao kuonekana mekundu huku akiwahimiza kuitumia mitungi hiyo kwa lengo lililokusudiwa kwani nia ya Rais Samia ni njema kwao.
Mitungi hiyo imegawiwa kidogo kwa watu wawili wawili kila kata ili wawe mabalozi kwa wengine kutumia na kuchochea matumizi sahihi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Naye Mgeni rasmi katika zoezi hilo ambaye ni mratibu wa miradi ya REA Wilaya ya Bukoba Bi Jamila Haroub Juma akitoa darasa na namna ya matumizi sahihi ya mitungi hiyo amesema mitungi hiyo imetolewa mahususi kuhamasisha kutumia nishati safi na salama ya kupikia na imetolewa na Wakala wa nishati Vijijini (REA) kwa kupata ruzuku kutoka Serikali kuu ambapo Rais Samia amewaondolea changamoto za kiafya zitokanazo na moshi kwani wengine ujikuta wanapata madhara kwenye mapafu, kifua kutokana na kuvuta hewa chafu.
Aidha Jamila amewahimiza akina mama hao kutunza, kutumia na kuendeleza mitungi hiyo wala si kwa matumizi mengine kwani watakuwa wamekwenda tofauti na dhamira ya Serikali.
"Mnatakiwa kurudisha shukrani kwa kutumia nishati hii ili kuepukana na madhara yatokanayo na moshi utokanao na mkaa na kuni tumeona watu wakipata shida kwenye mapafu kutokana na kuvuta hewa chafu hivyo nimpongeze Rais Samia kuwezesha zoezi hilo ambalo litakuwa endelevu kwa nchi nzima",amesema.
Hata hivyo akina Mama hao akiwemo Bi Winifrida Maxmilian wa kata Katoma, Hildagarda Ponsian wa kata Nyakato na Bi Ashura Jafari kutoka Kyaitoke Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba wamemshukuru Rais Samia kupitia mbunge huyo viti maalum Bi Rwamlaza na kuwa mradi huo utawasaidia kutunza Mazingira kwa kutokata miti ovyo kwa ajili ya kupata kuni na mkaa ambapo pia Rais Samia amewaweka katika maisha ya kati huku wakiahidi kutumia vyema mitungi hiyo.
Saturday, 9 December 2023
SERIKALI ITAENDELEA KUTAMBUA, KUHESHIMU NA KUTHAMINI MCHANGO WA KANISA KATOLIKI
Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina S. Mndeme amesema kuwa serikali itaendelea kutambua, kuheshimu na kuthamini mchango wa Kanisa Katoliki.
Hayo yamesemwa leo tarehe 9 Desemba, 2023 wakati aliposhiriki hafla ya Kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Paul wa pili Parokia ya Lubaga Jimbo Kuu Katoriki Shinyanga hafla iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es salaam Mwadhama Paolycarp Kardinali Pwngo.
RC Mndeme amesema kuwa, tunapoadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika, nchi imeweza kupiga hatua kubwa sana katika kuwatumikia wananchi wake hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matokeo yake yanaonekana chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Serikali itaendelea kutambua, kuheshimu na kuthamini mchango wa kanisa katoriki, na kwa kuzingatia kuwa nchi leo inaadhimisha miaka 62 ya Uhuru na maendeleo makubwa yanaoneka chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan", alisema RC Mndeme.
Kwa upande wake Mwadhama Kardinaly Pengo alisema kuwa, uzuri na upya wa kanisa hili halitakuwa na yoyote iwapo waumini wake hawataishi katika matendo ya upendo katika mioyo yao na maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na akawataka wananchi kuja kanisani hapa kwa ajili ya kuomba msamaha na ndiyo sehemu pekee ambayo unaweza kuomba msamaha kwa mungu.
Kando na hafla hii, pia RC Mndeme amewapa nafasi kufungua rasmi matumizi ya Kitabu cha Ibada ambacho kina mafundisho mbalimbali, sala, novena na nyimbo ambazo zitamuwezesha muumini kusali na kuelewa kwa urahisi zaidi kitabu hiki kitakuwa kinapatikana katika kanisa mbalimbali hapa Shinyanga.
LUHEMEJA: MAONESHO YA NGUVU KAZI/ JUA KALI KUFUNGUA FURSA ZA MASOKO KWA WAJASIRIAMALI
Na; Mwandishi Wetu – Bujumbura, BURUNDI
Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi/Jua Kali yameendelea kufungua fursa za masoko ya wajasiriamali nje ya nchi na hususan masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ameyasema hayo aliposhiriki ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika jiji la Bujumbura nchini Burundi ambayo yamefunguliwa rasmi leo Desemba 8, 2023 na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Prosper Bazombanza.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa maonesho hayo yamewezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kutambulika kimataifa huku ameshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wajasiriamali 259 kwenda Burundi kutangaza bidhaa na huduma zao.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amewahimiza Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu kutumia fursa ya maonesho hayo kujiajiri na kuondokana na umaskini.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa amewahamasisha wajasiriamali kutumia fursa ya maonesho hayo ili kutangaza bidhaa za Tanzania, kukuza ujuzi na masoko ya bidhaa zao pamoja na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wajasiriamali walioshirikia maonesho hayo wamesema wamepata masoko ya bidhaa wanazozalisha katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.