Tuesday, 3 October 2023

WATUMISHI MADINI WATEMBELEA MGODI WA NORTH MARA



Kundi jingine la Watumishi wapatao 14 kutoka kada mbalimbali za Wizara ya Madini ikihusisha Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu na Wahudumu wametembelea Mgodi wa North  Mara uliopo Mkoani Mara.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa  kutembelea migodi katika utekelezaji wa maazimio na ahadi alizotoa Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo lililofanyika mwezi Mei, 2023, jijini Dodoma ambapo kundi la kwanza lilitembelea migodi mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha, ziara hiyo inalenga kuwajengea uelewa wa pamoja  watumishi wote wa Wizara kuhusu shughuli zinazofanywa katika  Sekta ya Madini hususan shughuli za uchimbaji wa madini  katika migodi mikubwa, ya kati na midogo  ili kuwezesha malengo mahususi ya wizara kutekelezwa kwa pamoja kama familia moja ya Madini. 

Watumishi hao wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali katika mgodi huo ikiwemo mgodi wa chini ( underground mining), sehemu  ya uchenjuaji (processing plant) bwawa la huifadhi tope sumu ( TSF) , sehemu ya upokeaji na utunzanji wa vifaa vinavyotumika katika mgodi pamoja na kutembelea miradi ya jamii inayotekelezwa na migodi hiyo kupitia  Mpango wa Uwajibikaji wa Migodi kwa Jamii (CSR).

Hili ni kundi la pili la watumishi wa kada hizo kutembelea maeneo ya migodi ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa.
Share:

KUELEKEA TAMASHA LA 15 LA JINSIA, TGNP YAJIVUNIA MAFANIKIO YA KAMPENI, SHERIA



Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
KUELEKEA tamasha la 15 la jinsia Novemba 7-10, 2023 na Tapo la Ukombozi wa mwanamke Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unajivunia mafanikio ya baadhi ya sheria kurekebishwa hapa nchini na kampeni mbalimbali kushika hatamu na kuwa ajenda ya serikali.


Akizungumza na Mwandishi wetu wa Michuzi Blog, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Nguvu ya Pamoja na Harakati, Florah Ndaba amesema kuwa mabadiliko ya Sheria, ambazo zilifanyiwa marekebisho na nyingine zimeundwa na zimebeba masuala ya kijinsia na hata TGNP isipokuwepo sheria hizo zitakuwepo.


Florah amesema kutimiza miaka 30 ya TGNP, wanajivunia kutangaza na kusambaza bajeti yenye mrengo wa kijinsia. "Tunaona serikali imeanza kutenga bajeti zenye mrengo wa kijinsia na tunajivunia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali kupata mafunzo ya juu bajeti ya mrengo wa kijinsia.
Amesema kuwa TGNP ndio mwanzilishi wa Kampeni ya Mtue Mama Ndoo Kichwani ambayo enaendelea kutekelezwa na Wizara ya Maji inayoongozwa na Jumaa Aweso mbapo mikoa mbalimbali wamenufaika na kampeni hiyo.


Amesema kuwa kampeni hiyo iliungwa mkono na taasisi, Mashirika na kampuni kwa kuchimba visima, kutengeneza matenki ya kuhifadhia maji pamoja na usambazaji mabomba ili kuisaidia jamii kupata maji kwa urahisi.


Hata hivyo kampeni hiyo imekuwa mkombozi kwa Mwanamke ambaye alionekana kuwajibika zaidi katika majukumu ya nyumbani.


Pia amesema kuwa Kampeni hiyo imeweza kumsaidia mwanamke kupunguza muda na umbali wa kutafuta maji hivyo nguvu imeelekezwa kujiinua kiuchumi kwa mwanamke.


Amesema pia mafanikio mengine ni kuwa na vuguvugu la kubadilisha sheria ya Ndoa. Marriage Act katika katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ni kitu kilichoanza tangu zamani juu ya kutetea mtoto wakike kutokuolewa akiwa chini ya miaka 18.


Sheria hiyo pia imekuwa ikipigiwa kelele na Taasisi pamoja na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za mtoto.


Mswada wa mabadiliko ya sheria hiyo yalifika mpaka bungeni na kujadiliwa, hiyo ni moja ya kampeni zilizoanzishwa na TGNP.
“Mabadiliko ya sheria ya likizo ya uzazi nayo ni mafanikiao ambayo wanapata watu wengine ingawa waliopigania mabadiliko ya sheria likizo ya uzazi kwa wanaojifungua ni kitu ambacho hakikuwepo lakini leo hii akinamama wanafaidika juu ya sheria hiyo.”


Pia amesema kuwa kulikuwa na kampeni ya rasilimali ziwanufaishe wanachi, kwa sasa kweli tunaona rasilimali zinawafikia wananchini kwa njia mbalimbali.


Rasilimali zinawafikia wananchi kwa uwepo wa hosptali, zahanati na shule katika mikoa yote hapa nchini.


Ingawa kampeni nyingine hazikuendeshwa na TGNP peke yake lakini wadau mbalimbali walisukuma kampeni hizo mbele mpaka kufikia malengo endelevu ya Milenia.


Licha ya kuwa na Mafanikio hakukosi changamoto Florah amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa sheria ambazo hazitekelezwi, kwani kazi kubwa imefanyika katika marekebisho ya sheria lakini hazitekelezwi.
Pia amesema Mila na destuli mbaya nazo ni changamoto inaendelea kushikiliwa na baadhi ya makabila na zinarudisha nyuma kazi kubwa inayofanywa na wadau mbalimbali pia zinakwamisha kujikwamua Mwanamke kiuchumi.


Changamoto nyingine ni 'nani anabeba ajenda’, ajenda inabebwa na mtu au na watu, kuna wakati ajenda inabebwa na watu ambao sio wengi ambayo inafanya kutokuwa na mabadiliko ya haraka ya Mtazamo, fikra na kitabia za watu.


Pia Mabadiliko ya uongozi. Amesema kuwa viongozi wanaukuwa katika sekta flani wanatofautiana vipaumbele na kushindwa kubeba ajenda iliyopo na kuanza na ajenda nyingine.


Frola amesema kuwa Changamoto nyingine ni Ukuaji wa Sayansi na Teknolojia, mabadiliko ya teknolojia yameleta shida ukilinganisha na zamani ambapo mtoto alikuwa anajifunza kwa jamii inayomzunguka peke yake, lakini kwa sasa mafunzo yanatoka katika kila pande ya dunia.


"Kwahiyo lazima tueleze kinagaubaga kuwa kunachangamoto za dunia kuwa kijiji na mafanikio ya dunia kugeuka kuwa kijiji, hasa kwenye utetezi wa haki za watoto, ulinzi wa watoto na utetezi wa jinsia unakuta kunakuwa na changamoto katika kutetea...."
Ongezeko la Ukatili; Frola amesema kuwa changamoto hii inasura mbili
i) Uelewa wa jamii ndio unapelekea kuoongezeka kwa matukio ya ukatili, isingekuwa mchango wa wadau mchango wa TAPO(Vuguvugu) kuibua changamoto, hata mikakati ambayo Serikali inafanya kujenga madarasa, Madawati, kutengeneza mikakati mbalimbali ya kupambana na ukatili.


Amesema ukatili usingekuwepo kama kusingekuwepo na TAPO na wadau kuibua na kueleza kinagaubaga ili kuwepo na njia za kukemea na kuzuia zisiendelee kujitokeza.


Kwahiyo ni kitu cha kufurahia kwamba kazi za TAPO zinaibua changamoto katika jamii na zinachukuliwa hatua.


Pia amesema Changamoto hiyo bado ipo kwani matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ni mengi pia amesema mashirika yaliyopo nchini inawezekana hayatoshi katika utatuzi wa changamoto hizo zote zinawezesha kuibua fursa au mbinu mbadala ya jinsi ya kutatua changamoto za kijinsia.


"Mabadiliko sio ya siku moja, mabadiliko ya kifikra ni ya kila siku." Amehitimisha Florah.
Share:

CHONGOLO AWATAKA WANANCHI KATAVI KUACHANA NA IMANI ZA KISHIRIKINA


Na Mwandishi Wetu, Katavi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo amewataka wananchi wa Mkoa wa Katavi kuachana na imani za kishirikina maarufu kwa jina la Kamchape kwani ni chanzo cha uasikini.

Chongolo ameyasema hayo Oktoba 2,2023 wakati akizungumza na wananchi na wana CCM baada ya kuwasili Mpanda ambako atakuwa na ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na kutatua kero za wananchi.

“Nimeambiwa huku kuna kamchape , hawa jamaa mnawapa nguvu kubwa , mnawapa kichwa , mnawapa fursa ya kufanya mambo yanayokiuka sheria za nchi

“Imani za kishirikina ni umasikini na ukitaka kujifunza angalia watu wanaonamini katika ushirikina uone maisha yao.Wanaamini katika ndoto ambazo kutekelezeka kwake ni ngumu.

“Achaneni na kuendekeza mambo yanayoleta taaswira ya umasikini kwa. Mkoa wa Katavi ni mkubwa na mmeshajenga historia kubwa ,huu ni mkoa wa Mhandisi Kamwelwe, Mkoa wa Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, ni mkoa wa watu wazito katika nchi hii,”amesema.

Chongolo amesema haiwezekani mpaka leo Mkoa wa Katavi kuendekeza ushirikina kama daraja la kufanikiwa katika mambo yao , hivyo ni lazima watoke katika kufikiri mambo kirahisi.

Amesisitiza maendeleo hayapatikani kwa ndumba, kwa kupuliza, kwa kuagua , kupiga ramli na kutengeneza mambo rahisi bali maendeleo ni mambo yanayotaka kufuata utaratibu.

“Ukiona watu wa namna hiyo wewe usipate shida angalia maisha yao, mtu anaweza kuwa na ng’ombe 1000 lakini anakula nyama nusu kilo kwa wiki, sababu ya masharti.Achaneni na maisha hayo , afadhali uwe na ng’ombe 10 lakini uwe na uhuru wa kula nyama.

“Ni afadhali uwe na shamba heka tatu lakini uwe na uhuru wa kula mchele wako, achaneni na mila potofu , mila potofu zinawagombanisha , mila potofu zinawatenganisha…

“Mila potofu zinawatengenezea uadui usio na maana , zinawakwamisha kwenye shughuli za maendeleo.Akija mtu kapiga kamchape yake akawaambia ukilima shamba hili hutavuna mwaka huu, unaacha kwasababu unaamini alichosema.”


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mpanda Oktoba 2, 2023, tayari kuanza ziara ya siku tano mkoani Katavi. Akiwa mkoani humo atafanyakazi ya kuimarisha uhai wa chama, kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.Pichani kushoto ni Mwenyekiti wa CCM MKoa wa Katavi Ndugu Idd Kimanta












Mkuu wa Mkoa wa Katavi akisoma Taarifa ya Chama na Serikali mbele ya Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo.

Share:

Video : BEXY - JUU

 
Hii hapa video mpya ya Msanii Bexy inaitwa Juu... Tazama hapa chini

Share:

Monday, 2 October 2023

VIFAA VYA USHONI, TEHAMA VYAONGEZA UFANISI BOHARI KUU YA JESHI LA POLISI



Na Abel Paul, Jeshi la Polisi- Dar es salaam.

Jeshi la Polisi kupitia Bohari kuu imesema imeendelea kusimamia uzalishaji wa sare za maafisa na askari wa Jeshi la Polisi nchini Pamoja na kufunga mifumo ya Tehama na vifaa vya kisasa vya ushoni Bohari kuu ya Jeshi la Polisi.

Akitoa taarifa hiyo leo Octoba 02, 2023 Boharia Mkuu wa Jeshi la Polisi Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Moses Mziray amesema pamoja na kufanyika maboresho makubwa ndani ya Jeshi hilo Bohari kuu pia imepata vifaa vya kisasa vitakavyowezesha kuongeza uzalishaji wa sare za Jeshi hilo huku akimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anawezesha kiwanda hicho kufanya uzalishaji mkubwa.

ACP Mziray ameongeza kuwa kikosi hicho kimeendelea kushona sare za Jeshi hilo kwa kasi kubwa ili kuondoa upungufu wa sare ambapo amebainisha kuwa mashine za kisasa zilizopo zimeongeza ufanisi mkubwa wa utendaji wa kazi kiwandani hapo huku akimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Camillius Wambura kwa namna ambavyo ameendelea kukiangalia kwa karibu na kukiwesesha kiwanda cha Jeshi hilo.

Naye Mkuu wa kiwanda cha ushonaji Bohari kuu ya Jeshi la Polisi Mkaguzi msaidizi wa Polisi A/INSP Jenitha Mtayoba amesema wanaendelea na ushonaji kwa kasi kubwa kutokana na vifaa vya kisasa vilivyopo kiwandani hapo.

Share:

BENKI YA CRDB YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (kulia) akipokea fomu ya uwekezaji katika hatifungani ya kijani ya "Kijani Bond" kutoka kwa kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Afisa Mkuu wa Bishara Benki ya CRDB, Boma Raballa wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2023 iliyofanyika katika tawi la benki hiyo la Azikiwe lililopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo (wapili kulia) akipokea kadi yake ya 'TemboCard' kutoka kwa kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Afisa Mkuu wa Bishara Benki ya CRDB, Boma Raballa wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2023 iliyofanyika katika tawi la benki hiyo la Azikiwe lililopo jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wakwanza kulia), na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo (wapili kushoto).
Dar es Salaam Octoba 2, 2023 - Benki ya CRDB imewaahidi wateja wake kuendelea kutoa huduma na bidhaa bunifu zitakazowawezesha kufikia malengo yao ya kifedha.


Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu na Afisa Mkuu wa Biashara wa benki hiyo, Boma Raballa wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2023 uliofanyika katika tawi la benki hiyo la Azikiwe.


Akitoa ahadi hiyo, Raballa alisema Benki ya CRDB ikiwa kinara katika soko inaamini katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wake na Watanzania kama njia ya kusaidia wateja kufikia malengo yao.
“Tunapoadhimisha wiki hii tumejipanga kuendelea kutoa huduma bora na kuziboresha kadri ya matakwa ya wateja wetu ili tuendelee kuwaridhisha na kufanya huduma zetu kuwa na viwango zaidi,” alisema Raballa.


Raballa alisema Benki hiyo sasa hivi imetilia mkazo katika uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji kwa wateja. Benki hiyo pia imeendelea kutanua wigo wa huduma kupitia matawi zaidi ya 260, na “CRDB Wakala” ambao wamefikia zaidi ya 28,000 kote nchini.
“Malengo yetu ni kuona tunawafikia wateja kwa urahisi na kutoa huduma zinazoendana na mahitaji halisi ya wateja. Tunaendelea kuwekeza katika ubunifu wa huduma na bidhaa, na hivi karibuni tumezindua hatifungani ya kwanza ya kijani “Kijani Bond” nchini inayotoa fursa ya uwezeshaji wa miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira,” alisema.


Aidha, Raballa aligusia kuwa Benki hiyo pia imewekeza vyakutosha katika mafunzo kwa wafanyakazi ili kuwajengea weledi na kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wateja.
Akizindua Wiki hiyo ya Huduma kwa Wateja, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia huduma na bidhaa bora zinazotolewa na benki hiyo.


Mhe. Mpogolo ameiomba Benki ya CRDB kuendelea kuwekeza katika huduma za kidijitali ili kuendana na mahitaji ya wateja ambayo yamekuwa yakibadilika kila uchwao. Amewataka wananchi pia kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB ikiwamo mikopo ili kuboresha maisha yao.
Mkuu wa Wilaya huyo alitumia fursa hiyo kuwekeza katika hatifungani ya kijani ya Benki ya CRDB “Kijani Bond” ambayo imebaki siku tano tu dirisha la uwekezaji kufungua. Mhe. Mpogolo aliwahimiza wananchi kuchangamkia fursa hiyo na kunufaika na riba shindani ya asilimia 10.25 kwa mwaka.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo alisema Wiki ya Huduma kwa Wateja ni fursa kwa Benki hiyo kuwashukuru wateja wake kwa kuichagua Benki ya CRDB na hivyo kuifanya kuendelea kuwa Benki bora, huku akiwakaribisha kupata huduma katika matawi ya Benki ili kupata huduma bora, na kutoa maoni au ushauri.
Aidha, Yolanda alisema katika Wiki hii ya Huduma kwa Wateja Benki ya CRDB pia imejipanga kutembelea wateja wake katika maeneo yao kuwashukuru, kusikililiza mahitaji yao na kutoa elimu juu ya huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB.










Share:

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUTANGAZA UTALII KUPITIA MICHEZO, YAZIDI KUNG'ARA MASHINDANO YA KAMBA - SHIMIWI

Na Mwandishi Wetu, IRINGA.

Timu ya wanaume ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeibuka  mshindi kwenye mchezo wa kamba  kwenye mashindano ya Shirikishio la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani Iringa.

Akizungumza mara baada ya ushindi huo, Kapteni wa timu hiyo, Faraja Mmasa amesema ushindi uliopatikana umetokana na maandalizi mazuri ambayo yameisaidia timu hiyo kushinda kwa seti mbili kwa sifuri dhidi ya wapinzani wao TARURA. 

"Nianze kwa kuupongeza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa namna ambavyo walituandaa toka maandalizi mpaka kutuwezesha kufika hapa na kushiriki . Timu imejiandaa vizuri na kama unavyoona leo tulikuwa tunacheza mechi dhidi ya TARURA na tumeshinda ushindi wa seti mbili kwa bila." Amesema Mmasa


Ameongeza kuwa timu hiyo ina uwezo wa kusonga mbele kwa  hatua zinazofuata kwani wao kama wachezaji  wamejipanga vizuri kushindana na hatimaye kusinda kwa  hatua zinazofuata.


‘’ Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii tumeona ni timu ambayo ipo Kwa ajili ya ushindani. Tumejipa kuendelea kusonga mbele kuchukua kikombe " Aliongeza Mmasa.

Naye mchezaji wa timu hiyo Paul Shayo amesema, mashindano hayo yanayoendelea mkoani Iringa ni njia moja wapo ya kuutangaza utalii wa ndani na hivyo wanatumia fursa hiyo vilivyo kuhamasisha  utalii wa ndani

Kwa upande wa mchezaji  Chamganda Hamis amesema, kwa ushindi walioupata wanamshukuru Mungu kwani utawasaidia  katika safari yao ya kuelekea kunyakua vikombe.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger