Wednesday, 8 March 2023
Tuesday, 7 March 2023
SERIKALI YA TANZANIA YAPIGA MARUFUKU WATOTO MADARASA YA AWALI HADI LA TANO KWENDA BWENI
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepiga marufuku wanafunzi wa kuanzia madarasa ya awali hadi darasa la tano kusoma shule za bweni (boarding).
Kupitia waraka uliotolewa na Kamishna wa Elimu wa Wizara hiyo, Dk. Lyabwene Mtahabwa kwa wadau wa elimu nchini, serikali imezitaka shule zote zinazotoa huduma ya bweni kwa madarasa ya kwanza hadi la tano kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.
Dk. Mtahabwa amesema hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi kutoka mdau husika na kwamba utekelezaji wa waraka huo umeanza Machi 1, 2023.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji wa usajili wa shule uliotolewa na wizara Novemba 2020.
Via Global Publishers
MIKUTANO YA KAMATI ZA BUNGE LA AFRIKA (PAP) NA VYOMBO VINGINE VYA PAP YAANZA KUUNGURUMA
Rais wa Bunge la Afrika (Pan - African Parliament (PAP), Mhe. Chifu Fortune Charumbira akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mikutano ya Kamati za Kudumu za Bunge la Afrika (PAP) na vyombo vingine vya Bunge Afrika itakayofanyika kuanzia Machi 6, 2023 hadi Machi 17,2023 katika Makao Makuu ya Bunge la Afrika, Midrand Afrika Kusini vikiongozwa na Kaulimbiu ya Umoja wa Afrika (AU) ya 2023 "Mwaka wa AfCFTA: Kuharakisha Utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika".
Sherehe hizo za ufunguzi zilizofanyika Jumatatu Machi 6,2023 zimehudhuriwa pia na wageni wa ngazi za juu akiwemo Mhe. Candice Mashego-Dlamini, Naibu Waziri wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa.
Akizungumza, Rais wa Bunge la Afrika (PAP) Chifu Fortune Charumbira amesema Kamati za Kudumu ndizo waendeshaji wakuu katika kutoa matarajio ya raia wa Afrika hivyo kuziagiza Kamati hizo kueleza kikamilifu matarajio ya watu wa Afrika .
"Ili Kamati zetu ziweze kuchangia katika kurekebisha masuala yanayoikabili Afrika, tunapaswa kuwa wazi juu ya orodha kamili ya masuala ambayo yanaathiri vibaya watu wetu. Ni lazima, kwa hiyo, kutumia vikao hivi kufanya uchunguzi wa mazingira kwa hadubini, kuandaa orodha ya kina ya changamoto zinazowakabili wananchi wetu na kuandaa mipango kazi ambayo inatoa kipaumbele na kukabiliana na masuala yaliyoainishwa. Mtazamo wetu lazima ubaki thabiti juu ya mahitaji na matarajio ya raia wa Afrika na hapo ndipo tunaweza kusalia kuwa muhimu kama taasisi ya uangalizi na uwakilishi wa bara," amesema Chifu Charumbira.
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LIMEMUAGA ALIYEKUWA KAMISHNA MSTAAFU MARTIN MBAGO KIJESHI, JIJINI DAR ES SALAAM.

Dar es Salaam- 06 Machi, 2023
Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza akimwakilisha Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, leo tarehe 6 Machi, 2023 ameungana na Waombolezaji katika Misa ya Kuuaga Kijeshi Mwili wa aliyekuwa Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (1995-1996) Martine K. Mbago nyumbani kwa marehemu Chanika Zingiziwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kutoa salamu za rambirambi, Kamishna Semwanza alisema Marehemu Kamishna Mstaafu Mbago, alitumikia vyema na ni miongoni wa Waanzilishi ambao wamelitengeneza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa na mwonekano huu tunaouona hii leo, na kuongeza kuwa Marehemu alifanya kazi kwa Uaminifu na kwa Weledi na kuwatengeneza Maafisa na Askari ili kuja kulitumikia Jeshi katika Huduma za Kuzima Moto na Uokoaji.
"...Kwa Ujumla, Marehemu alifanya kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu, amewatengeneza Askari na Maafisa ili kuja kulitumikia Jeshi na Taifa kwa ujumla katika huduma za Kuzima Moto na Uokoaji katika dharura mabalimbali..." alisema Kamishna Semwanza.
Katika Misa hiyo ya Kuuaga mwili wa Kamishna Mbago, Viongozi mbalimbali walihudhuria ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Benard Mchomvu, Makamishna Wastaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania bara na Kamishna Mstaafu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar Ali Malimusy.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa shukurani za dhati kwa wote waliohusika katika kufanikisha zoezi la mazishi ya Mwili wa Marehemu.
(Picha zote na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)


NAIBU WAZIRI MASANJA AONGOZA KIKAO CHA TAASISI ZA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Watendaji (hawapo pichani) kuhusu kuboresha utendaji kazi katika kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kilichofanyika leo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Watendaji kuhusu kuboresha utendaji kazi katika kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kilichofanyika leo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha.**************************
Na Happiness Shayo
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameongoza kikao cha kimkakati cha kufanya mapitio ya taarifa mbalimbali za utendaji kazi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na hatimaye kukuza utalii na kuimarisha usimamizi wa Uhifadhi wa Maliasili nchini.
Kikao hicho kimefanyika leo Machi 6, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi za Ngorongoro zilizopo Jijini Arusha.
Mhe.Masanja ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Taasisi kuwa wabunifu kwa kutumia historia ya taifa na elimu ya viumbe hai kuwa fursa ya kujifunza na kuiongezea Serikali Mapato na kuongeza ajira na kipato kwa Mwananchi mmoja mmoja.
Aidha, kikao hicho kilijadili namna ya kutumia Makumbusho za Taifa kama eneo mojawapo la kuiongezea Serikali mapato kwa kuwa wana wigo mpana zaidi kuliko Taasisi nyingine katika kuibua fursa zilizopo nchini.
Katika hatua nyingine, Mhe.Masanja amekielekeza Chuo cha FITI kuandaa mpango utakaokiwezesha Chuo hicho kuwepo na miradi mbalimbali itakayokiwezesha kuongeza mapato kwa njia ya Mafunzo.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Makumbusho ya Taifa ( NMT) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.










































