Monday, 31 January 2022

RC MTAKA AAGIZA WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULE WAPEWE ADHABU YA KUSAFISHA VYOO VYA SHULE

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akivuka daraja la mto Buluku  lililotengenezwa kwa muda baada ya kuharibiwa na mvua za masika zinazoendelea Wilayani Kondoa na kusababisha wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo.


*******
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 blog-KONDOA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kondoa,Dk.Hamis Mkanachi kuwakamata   wazazi ambao watashindwa kuwapeleka wanafunzi shule kujiunga  kidato cha kwanza na kwamba mara baada ya kuwakamata wazazi hao  wanatakiwa kwenda kufanya usafi kwenye vyoo vya shule ili kuwaaibisha.

Mtaka amesema hayo mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Bukulu Kata ya Bukulu Wilayani Kondoa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Bukulu,Mkuu huyo wa Mkoa amemwagiza DC Mkanachi kuwakamata wazazi ambao watashindwa kuwapeleka shuleni watoto wao.

Licha hayo amewaagiza  Wakuu wa shule katika Wilaya hiyo kuanzisha Klabu za taaluma ili kuwasaidia wanafunzi waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.

“Mwanafunzi asipofika Jumatatu (31 Januari) chukua mgambo  kamata wote waje wafanye usafi, waje wasafishe vyoo wapelekeni pale shuleni ili watoto wao wawe wanawaona, Wazazi wao wanavyodhalilika kwa sababu yao”amesema.

“Anzisheni Klabu za taaluma za Sayansi,Arts,Mazingira na Takukuru anzisheni midahalo ya form one na form two na form three na four  ili wanafunzi waweze kupata ulewa pamoja na kujifunza.Wapeni mitihani ya mara kwa mara Mkuu wa Wilaya una PHD lakini hali ya elimu hapa sio nzuri,”amesema.

Kwa upande wake,Mkuu wa Wilaya hiyo,Dk.Mkanachi  amewataka wanafunzi wa shule hiyo  kusoma kwa bidii kwani Serikali imeishawapelekea miundombinu ikiwemo ujenzi wa madarasa na walimu.

Naye,Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kondoa,Mohammed Kova amesema kiujumla hali ya elimu Wilayani humo sio nzuri hivyo zinahitajika jitihada za pamoja ili kunusuru hali ya elimu.

“Nawaomba sana wanangu someni,someni mimi niliuza nyumba yangu Kondoa  ili nisomeshe watoto wangu sasa hivi wote wana kazi nzuri na mimi nakula matunda yao,tusomeshe,”amesema.


Share:

JESHI LA POLISI LASEMA ASKARI POLISI MAHEMBE ALIJIUA KWA KUJINYONGA


Gaitan Mahembe (kushoto), ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi anayedaiwa kujinyonga, Grayson Mahembe (kulia).
**

Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi kuhusu taarifa za upotoshaji zinazoendelea kuhusu tukio la kujinyonga hadi kufa kwa mkaguzi msaidizi wa jeshi hilo, Grayson Mahembe, tukio lililotokea Januari 22, 2022 mkoani Mtwara.

Taarifa iliyotolewa leo, Januari 31, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, SACP David Misime zinaeleza kwamba ushahidi ukiwemo wa picha na ripoti ya daktari, umethibitisha kwamba Mahembe alijiua kwa kujinyonga katika mahabusu ya peke yake aliyokuwa akishikiliwa kwa makosa yaliyokuwa yakimkabili yeye na wenzake.

Makosa hayo ni kudaiwa kushiriki kumnyang’amya fedha na kisha kumuua kijana aliyefahamika kwa jina la Mussa Hamis na kwenda kuutupa mwili wake vichakani katika Kijiji cha Namgogori mkoani Mtwara, tukio lililotokea Januari 5, mwaka huu.

Taarifa hiyo imeendelea kusisitiza kwamba wananchi hawapaswi kuamini taarifa za upotoshaji na mijadala inayoendelea na kuongeza kuwa askari huyo hakuzikwa kijeshi kwani kwa sheria za jeshi hilo, askari anapojitoa uhai, hawezi kupigiwa gwaride la mazishi linalochezwa na risasi au mabomu kwani anahesabiwa kuwa hajafa kishujaa.

Grayson Mahembe na wenzake saba, wanadaiwa kutekeleza mauaji ya kijana huyo Januari 5 mwaka huu na kisha mwili wa marehemu waliutupa katika kitongoji cha Majengo, kijiji cha Hiari wilayani Mtwara
Share:

HII HAPA RATIBA YA MGAO WA UMEME


Wakati ratiba ya mgao wa umeme katika baadhi ya maeneo nchini wa siku kumi ikiwa haijatoka, wananchi, wakiwamo wafanyabiashara wadogo na sekta binafsi wanahofu shughuli zao kwenda mrama.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) juzi Ijumaa lilitangaza kuwapo maboresho ya vituo vya kuzalisha umeme vya Kinyerezi l vinavyotegemewa kuzalisha megawati 185 na Ubungo lll megawati 112 kuwa vitasababisha mgao nchini.

Taarifa hiyo kwa umma inaeleza kuwa, upungufu huo wa umeme hautakuwa nchi nzima, isipokuwa kwa baadhi ya maeneo, lakini kila eneo litakaloathirika litapewa taarifa ni kwa muda gani kukosekana kwa umeme kutadumu.

“Lengo ni kuwawezesha wateja na wananchi kuweza kujipanga katika shughuli zao za kiuchumi na hata viwanda vikubwa vipange ratiba nzuri ya rasilimali watu kutokana na upatikanaji wa umeme,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande.

Pia, alisema Tanesco watatumia mwanya huo wa kukatika umeme kufanya matengenezo katika miundombinu ya usambazaji umeme, kwa kuwa kukatikakatika kwa huduma hiyo kunasababishwa na uchakavu.

Novemba 18, 2021 Tanesco ilitangaza kupungua kwa umeme, ikisema mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupungua kwa maji katika vyanzo vya uzalishaji wa umeme wa maji, hivyo kutakuwa na upungufu wa megawati 345.

Ilisema inachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kwa kuharakisha matengenezo ya baadhi ya mitambo ya Ubungo I inayozalisha megawati 25, ikisema itaendelea kutumia na vyanzo vingine mbadala kuhakikisha nishati hiyo inapatikana muda wote.




Share:

MISS MAREKANI AJIUA KWA KUJIRUSHA GHOROFANI




Cheslie Kryst (30) aliyekuwa mlimbwende wa Marekani mwaka 2019 amefariki dunia. Kwa mujibu wa Polisi, Cheslie alijirusha ghorofani jana Jumapili, Januari 30, 2022 majira ya asubuhi huko Manhattan, New York.

Kabla ya kujirusha aliweka bandiko la picha yake Instagram yenye ujumbe; “Siku hii ikuletee Pumziko la Amani” ambapo familia yake imethibitisha kutokea kwa kifo hicho. Cheslie alikuwa na Shahada mbili ikiwemo ya Sheria na Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara.

“Ni huzuni na mafadhaiko makubwa ambayo familia tumeyapata kutokana na msiba wa mpendwa wetu Cheslie, alikuwa mwema na mwenye ushawishi duniani kote hasa kwa urembo na umaridadi wake.

“Cheslie alikuwa na upendo wa dhati, kwa kutumia uwezo wake na ushawishi wake amewasaidiwa wengi hasa katika kazi zake za uanasheria ikiwemo kuhakikisha wanyonge wanapata haki zao. Lakini cha ziada alikuwa binti yetu, dada, rafiki, mwenzetu na mshauri pia,” imesema familia yake.


Kryst, alikuwa wakili wa mahakama ya Division I na North Carolina, alishinda taji la Miss USA, Mei, 2019, na kushiriki katika Mashindano ya Miss Universe mwaka huo huo.
Share:

WATU 13 WAUAWA KWA BOMU LILILOTEGWA ARDHINI WAKIWA KWENYE DALADALA



TAKRIBANI watu 13 wamefariki dunia kufuatia mlipuko uliotokea leo, Januari 31, 2022 asubuhi katika eneo la Mandera, Kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka wa Somalia baada ya gari la abiria (daladala) kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini ikiwa ni siku mbili tu baada Ufaransa kutoa tahadhari ya Shambulio.

Watu wengine kadhaa ambao idadi yao haijafahamika wamejeruhiwa. Gari hilo lilikuwa likisafiri kuelekea Mandera, Mji ulio katika eneo la mpakani, ambao umekuwa ukiathiriwa mara kwa mara na mashambulizi ya wanamgambo.

Picha kutoka kwa wanahabari wa eneo hilo zinazoshirikishwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha mabaki ya gari la umma, linalojulikana kama matatu, ambalo lilipuliwa baada ya kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa barabarani.

Hakuna aliyedai kuhusika, lakini waasi wa Al Shabaab wamekuwa wakiwalenga polisi na raia ndani na karibu na Mandera na vifo kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, na kuifanya Mandera kuwa moja ya maeneo hatari zaidi ya Kenya kuishi.

Shambulio hilo limetokea wiki moja tu baada ya balozi kadhaa za kigeni nchini Kenya, zikiwemo Marekani na Ufaransa, kuwaonya raia wake kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini humo.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATATU JANUARI 31,2022

Magazetini leo Jumatatu January 31 2022


 


Share:

Sunday, 30 January 2022

SERIKALI YAAHIDI MAZINGIRA BORA ZAIDI SHIRIKA LA POSTA


Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (katikati) akiwasili kwa ajili ya kufunga rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Macrice Mbodo na kulia ni Kaimu Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika hilo, Constantine Kasese. Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo (kulia) akimkabidhi zawadi Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto mara baada ya kufunga rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo kabla hajafunga rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo, katika ukumbi wa Jakaya kikwete Convention Center jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania mara baada ya kufunga rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akizungumza wakati akifunga rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.


***************************


*Kushughulikia malimbikizo madeni ya Sh bilioni 2*


Na Mwandishi Maalumu


SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Shirika la Posta nchini lengo ikiwa ni kuongeza uzalishaji na kutekeleza majukumu yake liweze kuendana na lengo la uanzishwaji wake kwa mujibu wa Sheria iliyounda Shirika hilo.


Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto wakati akifunga mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center, jijini Dodoma.


Msajili huyo wa Hazina amesema Serikali inatambua mchango wa Shirika la Posta katika kuwahudumia wananchi hasa katika sekta ya Mawasiliano, ndiyo maana inaendelea kuliongezea nguvu Shirika ili liendelee kutoa huduma stahiki na zinazoendana na mahitaji ya wakati ya wananchi.


Itakumbukwa kuwa mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliamua kulipunguzia mzigo Shirika wa kuwalipa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki baada ya Serikali kuchukua jukumu hilo na pia Serikali ililirejeshea Shirika kiasi cha Bilioni 7.9 ikiwa ni fedha lilizotumia kuwalipa wastaafu hao kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1994 2006 na 2015-2020 lengo likiwa ni kuliongezea ufanisi Shirika hilo.


“Serikali iliamua kurejesha Shilingi bilioni 7.9 ikiwa ni fedha walizolipwa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki ili kuweka mazingira wezeshi kwa Shirika kuongeza uzalishaji na kutekeleza majukumu yake”. Amesema Mgonya.


Aidha, Msajili wa Hazina amelitaka Shirika la Posta kuzitumia fedha hizo kwa kuzingatia maelekezo na malengo ya fedha hizo katika kuboresha vitendea kazi vya Shirika, pia amewataka watendaji wa Shirika hilo kuongeza ubunifu ili kuleta tija katika kuongeza pato la Taifa na hatimaye kuweza kutoa gawio kwa Serikali.


Sambamba na hilo, ameahidi Ofisi yake itaendelea kushirikiana na Shirika la Posta katika utatuzi wa changamoto za kiuendeshaji na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kushirikiana na Serikali ikiwemo suala la Mtaji kwa Shirika na malimbikizo ya madeni ya kodi ya muda mrefu (ya shilingi Bilioni 26 yanayotakiwa kuchukuliwa na Serikali).


Akizungumza wakati akimkaribisha Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Msaidizi Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Elisa Mbise kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema kuwa, Serikali iko tayari kuliboresha Shirika la Posta ili liongeze tija kwa Taifa na kuwataka watendaji wa Shirika kuonesha uwezo wa kutumia rasilimali walizonazo ili Serikali iendelee kuona umuhimu wa kuliimarisha Shirika hilo kiutendaji.


“Onesheni uwezo wa kutumia rasilimali mlizonazo ili Serikali ione umuhimu wa kuendelea kuwaongezea mtaji muweze kuboresha utendaji wenu ili wananchi waendelee kunufaika na huduma za Posta”. Alisema Mbise.


Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa TPC, Macrice Mbodo amesema katika mkutano huo, wajumbe wamepatiwa mafunzo ya huduma kwa mteja; wamepitia Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (2022/33 – 2025/26) unaojikita kuifanya “Posta ya Kidijitali kwa maendeleo endelevu” pamoja na kupitia Mapendekezo ya Mpango Mkakati mpya wa nane wa kibiashara wa miaka mitano (2022/23 - 2026/27).


Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Baraza Afisa Masoko Mwandamizi kutoka Zanzibar, Bi Halima Abdulla Hamad amemshukuru Msajili wa Hazina kwa kutenga muda wake kufunga Baraza hilo, na kuahidi kutekeleza yote waliyoyajadili katika kikao hicho ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Shirika Mkutano huo ulihudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalum (Wafanyakazi), Mhe. Dkt. Alice Karungi Kaijage, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kitaifa wa Bara na Zanzibar pamoja na Viongozi wa Shirika la Posta kwa ngazi ya Makao Makuu na Mikoa.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger