Monday, 2 March 2020

Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga, Amchefua Waziri Mkuu...Aagiza Achunguzwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Bibi Judica Omari achunguze utendaji kazi wa Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga, Bibi  Juan Mening.

Amesema hajaridhishwa na utendaji wake kwa kuwa ameshindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na hata hicho kidogo kinachokusanywa hakifikishwi Serikali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo  (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkinga pamoja na wananchi baada ya kufungua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga akiwa katika ziara  ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu  na haitosita kuwachukulia hatua.

“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”

Waziri Mkuu aliwaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Pia, Waziri Mkuu amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuhakikisha wanakuwa wakali katika usimamizi wa makusanyo ya mapato pamoja na matumizi yake.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku 18 kuaznia leo Jumatatu, Machi 2, 2020 kwa watumishi wa halmashauri hiyo wanaoishi jijini Tanga wawe wamehamia katika kituo chao cha kazi na watakaoshindwa wabaki huko huko waliko.

Amesema Serikali inataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi. “Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi jijini Tanga wawe wamehamia hapa ifikapo Machi 20 mwaka huu na wasiohamia waendelee kubaki huko huko.”

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Share:

Katibu Mkuu CCM: Tusifurahie Benard Membe Kufukuzwa, Milango Iko Wazi Kama Atakiri Makosa na Tutampokea

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt Bashiru Ally, amemuomba aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, aache kutapatapa na kwamba anahitaji kufanyiwa ushauri wa kisaikolojia ili aweze kuwa sawa.

Dr Bashiru Ameyasema hayo wakati akizungumza  katika mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi leo tarehe 2 Machi 2020 jijini Dar es Salaam

Amesema CCM wamechukua hatua hiyo baada ya hatua za awali kushindwa kufanikiwa....

"Ndugu Membe alishawahi kupewa adhabu ya onyo kali ikiwa ni hatua ya kujaribu kumpa nafasi ya kujirekebisha, lakini ilishindikana,  huu ni uamuzi mgumu tuliochukua, na si kusherehekea na nisingependa WanaCCM kujitokeza hadharani kufurahia.

" Nadhani tumpe muda, ni binadamu ana haki zake,  anahitaji ushauri nasaha, maana siyo tatizo dogo hili na mimi sitaki kulizungumza kwa ushabiki hata lingenipata mimi ningehitaji marafiki zangu wa karibu niwashirikishe" amesema Dkt Bashiru.
 

Dk. Bashiru ameeleza kuwa, milango ya CCM  kupokea wanachama wanaokiri makosa yao na kuomba msamaha iko wazi, hivyo Membe anaweza kukata rufaa juu ya suala hilo.

“Mchakato huu ni kama wa kimahakama kuna rufaa, nikianza mimi kusema wakati mimi ndio nitapokea rufaa kama nipo ni kama naingilia mchakato wa haki. Na matarajio yangu ni kwamba atarudi CCM, nikiwa hai au nimekufa.

“Sababu milango ya kuwapokea wanachama iko wazi na kuondoka iko wazi, mimi nimesaini barua za misamaha 14 na niko tayari kusaini ya 15 ambayo ni ya Membe kurudi kama akitaka,” amesema Dk. Bashiru.


Share:

Wafungwa 150 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora Wapelekwa Gereza la Kwitanga Mkoani Kigoma Kulima Michikichi

Wafungwa 150 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepelekwa katika Gereza la Kwitanga Mkoani Kigoma ikiwa ni mkakati maalumu wa Serikali kuliteua gereza hilo kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la  mchikichi nchini.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mkakati huo uliotolewa maagizo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati ya mwaka 2018 alipofanya ziara gerezani hapo  ukiwa na lengo la kulifanya Jeshi la Magereza kuingia katika mfumo wa uzalishaji mali.

“Katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo ni agizo la serikali, wizara tumeongeza nguvukazi hapa kwa kuleta wafungwa 150 na muda si mrefu tutaongeza wafungwa wengine 300 kutoka magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuongeza uzalishaji huku eneo lenye ukubwa wa ekari 6000 linatarajiwa kulimwa zao hilo sambamba na kusambaza mbegu zinazozalishwa gerezani hapo kwenda Halmashauri za Mikoa, Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi,” alisema Masauni

“Lakini pia ili kuliwezesha gereza hili tumeliagiza Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza kulichukua Gereza la Kwitanga na kuliingiza katika kundi la magereza yanayowezeshwa na shirika ili kuweza kutatuliwa matatizo yao ya kifedha badala ya kusubiri bajeti kuu kutoka serikalini ambayo inakua haitoshi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Magereza mkoani Kigoma, Kamishna Msaidizi Leonard Bushiri aliunga mkono hoja ya Gereza Kwitanga kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali huku akikiri baadhi ya masuala kukwama kutokana na changamoto za kibajeti.

“Nafikiri hili suala la gereza kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali litatatua changamoto nyingi za kibajeti na kiuendeshaji maana gereza halina gari kubwa kwa ajili ya uvunajina usafirishaji wa mafuta kutoka gerezani kwenda kwa mtumiaji, hakuna bajeti ya uendeshaji kwa mfano kukamua lita 100 mpaka 120 za mafuta tunahitaji maji lita 1000 hivyo fedha kwa ajili ya kununulia umeme ili kusukuma maji ni changamoto, kwahiyo kuingizwa kwenye shirika itasaidia changamoto nyingi” alisema ACP Bushiri

Sambamba na kulima zao la mchikichi Gereza Kwitanga linalima pia mahindi, mpunga, mihogo, maharage na Bustani za mbogamboga.



Share:

Waziri Mkuu Majaliwa Asema hajaridhishwa na ujenzi wa jengo la kituo cha pamoja cha huduma ya forodha kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa jengo la kituo cha pamoja cha huduma ya forodha kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Horohoro, Tanga ambacho ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 7.6.

“Jengo hili kuta tayari zimeshaanza kuvimba, kwa nini majengo ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) yanajengwa kwa kiwango cha chini na kwa nini mmeruhusu majengo haya yatumike,” amehoji Waziri Mkuu.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amemtaka Afisa Miliki wa TRA, Bw. Haruna Sumwa, mkandarasi aliyejenga jengo hilo pamoja na wote waliohusika na ujenzi huo wafike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma Machi 11, 2020.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo  (Jumatatu, Machi 2, 2020) wakati akiwa katika ziara ya kikazi wilaya ya Mkinga mkoani Tanga. Amesema ni lazima majengo hayo yakidhi viwango.

“Hapa ni sura ya nchi ni lazima majengo yawe katika hali nzuri, haiwezekani mgeni anaingia na kuhudumiwa katika jengo chakavu, tutachukua hatua kwa yeyote aliyehusika, hizi ni fedha za umma lazima zitumike vizuri.”

Awali, Mkuu wa wilaya ya Mkinga Bw Yona Maki alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza Julai 2011 hadi Septemba 2014 na lilianza kutumika Agosti 2015 likiwa na taasisi 16 za Serikali zinazofanyakazi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa nyumba 62 za watumishi, maji safi na salama pamoja na upungufu wa watumishi.

Majukumu ya kituo hicho ni pamoja na kusimamia, kudhibiti uingiaji na utokaji wa raia wa Tanzania na wageni, kufanya doria na misako hasa kwenye vipenyo ambako wale wasiopenda kufuata taratibu hupenda kutumia.

Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza watu wote wanaoingia nchini kupitia mipaka mbalimbali wapimwe afya zao ili kulikinga Taifa na maambuki ya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Pia amewataka wananchi kutoa ushirikiano na Serikali kwa kutoa taarifa za watu wanaoingia nchini bila ya kufuata taratibu. “Lazima tulinde nchi yetu katika kupambana na kuzuia magonjwa mbalimbali kwa kuhakikisha watu wote wanaingia nchini wawe salama.”

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani Tanga kuimarisha doria katika maeneo ya mpakani ikiwa ni pamoja na kukagua maroli kwa kuwa yanahusika na ubebaji wa wahamiaji haramu.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi kutojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kuwa madhara yake ni makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema wananchi wakatae kutumika katika kupitisha dawa za kulevya na atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. “Usikubali gari lako likatumika kubeba wahamiaji haramu wala dawa za kulevya kwani ukikamatwa linataifishwa.”

Waziri Mkuu amesema mwaka jana dawa za kulevya aina ya heroine gramu 746, bangi kilo 485, mirungi kilo 880 zilipitishwa katika wilaya hiyo kiawango ambacho ni kikubwa, hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya aimarishe doria.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula alitaja changamoto zinazoikabili wilaya hiyo ikiwemo ya ukosefu wa maji safi na salama, ambapo Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imeshaanza kushughulikia suala hilo.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Share:

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini(TMA) Yatoa Angalizo la Mvua Kubwa Siku Tatu

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini(TMA), imetoa tahadhari ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha Machi 2 - 3, 2020, katika Mikoa ya Mara, Simiyu, Arusha,Kilimanjaro, Manyara, Singida,Dodoma, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Tanga, Dar es Salaam,Pwani pamoja na Visiwa vya Mafia,Unguja na Pemba.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo pia imeeleza kuwa mvua hizo pia zitanyesha Machi 4 kwa baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Njombe, Iringa, Arusha, Kilimanjaro,Manyara, Dodoma, Tanga, Morogoro, Dares Salaam, Pwani pamoja na Visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo Machi 2 hadi Jumatano ya Machi 4, 2020.
 
TMA pia imeeleza athari ambazo zinaweza kujitokeza kuwa ni pamoja na baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri,kusimama kwa muda kwa baadhi yashughuli za kiuchumi na kijamii na kuwataka wananchi kuzingatia na wajiandae.



Share:

Video Mpya : MR DEVI NG'WANA OBEDI - DUNIA

Hii hapa ngoma mpya ya Msanii wa Nyimbo za Asili Mr Devi Ng'wana Obedi inaitwa Dunia..Itazame hapa chini mtu wangu

Share:

Video Mpya : BEXY - BORA IWE

Ninao wimbo mpya wa Msanii Bexy unaitwa Bora Iwe.. 
Tazama video hapa chini

Share:

WAANDISHI WA HABARI WASHAURIWA KUWA WAZALENDO, KUTUMIA VYEMA KALAMU NA MIDOMO YAO KATIKA USTAWI WA TAIFA


Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Arusha, Bw. Charles Yamo, akisoma hotuba ya ufunguzi wa semina kwa waandishi wa habari za uchumi na fedha kwenye ukumbi wa BoT jijini Arusha Machi 2, 2020.
****
WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kuwa wazalendo kwa taifa kwa kutumia vyema kalamu zao, midomo yao na vyombo vyao vya habari kwa kuhabarisha umma vyema bila kuharibu uelekeo wa ustawi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha wakati akifungua semina kwa wanahabari kuhusiana na habari za Uchumi na Fedha Mkurugenzi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) tawi la Arusha Charles Yamo amesema kuwa umuhimu wa vyombo vya habari katika ujenzi wa taifa ni mkubwa sana hivyo ni lazima Wanahabari wawe chachu ya maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

"Kupitia mafunzo haya tunaamini umma utaelewa zaidi ni nini benki kuu inafanya na nini wategemee kutoka kwetu" Ameeleza.

Amesema kuwa kupitia mafunzo hayo wanahabari watapata fursa ya kufahamu zaidi kuhusiana na sera za fedha, masoko ya sekta ya fedha, usimamizi wa fedha na huduma za kibenki na kupitia maarifa hayo wananchi watapata fursa ya kupata elimu zaidi kuhusiana na majukumu yanayotekelezwa na benki kuu ya Tanzania.

Aidha Yamo amewashauri waandishi wa habari kujiendeleza kielimu ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

"Dunia imebadilika teknolojia inakua kwa kasi ni vyema wanahabari mkajiendeleza zaidi kielimu ili kuweza kutayarisha na kuandika habari zitakazowafikia wananchi kwa urahisi zaidi" Ameeleza.

Pia amesema kuwa umahiri kwa wanahabari ni jambo lisiloepukika hivyo ni vyema kwa kila mwanahabari kubobea katika sekta fulani kiuandishi na kuimakinikia.

"Ukiwa na sekta ambayo umeibobea utaitendea vyema kazi yako na sio kuandika kila kitu, ukiwa mahiri na mweledi katika sekta ya uchumi au kilimo itakupa nafasi zaidi ya kuitendea kazi vyema" amesema.

Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yatakwenda sambamba na kutembelea miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano jijini Arusha.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Uhusiano na Itifaki, BoT, Bi. Vicky Msina mwanzoni mwa semina hiyo, alieleza kuwa washiriki wa semina hiyo wanatoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo vya televisheni, radio, magazeti na mitandao ya kijamii na kwamba semina hiyo itadumu kwa siku tano ambapo wataalamu wa BoT watatoa elimu kuhusu shughuli za BoT.
Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Arusha, Bw. Charles Yamo, akisoma hotuba ya ufunguzi wa semina kwa waandishi wa habari za uchumi na fedha kwenye ukumbi wa BoT jijini Arusha Machi 2, 2020.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango, akiendelea kutoa ufafanuzi kuhusu ukuaji wa Uchumi nchini kwenye semina ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha inayofanyika jijini Arusha.
Meneja Msaidizi wa Uhusiano na Itifaki BoT, Bi. Vicky Msina (katikati) akitoa maelezo ya awali kuhusiana na semina hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa BoT tawi la Arusha, Bw. Charles Yamo na kulia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango.
Meneja Msaidizi wa Uhusiano na Itifaki BoT, Bi. Vicky Msina akitoa maelezo ya awali kuhusiana na semina ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha inayofanyika jijini Arusha.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango, akifafanua moja ya mada iliyohusu mapitio ya maendeleo ya uchumi nchini, kikanda na dunia na matarajio kwa mwaka 2020,Kwenye Semina ya Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali ikiwemo mitandano ya Kijamii iliyohusu Habari za Uchumi na Fedha,inayofanyika jijini Arusha
Wanahabari wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye semina hiyo inayoendelea jijni Arusha
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango, akitoa mada kuhusu mapitio ya maendeleo ya uchumi nchini, kikanda na Dunia na matarajio kwa mwaka 2020.
Baadhi ya Wanahabari wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Misango kuhusu mapitio ya maendeleo ya uchumi nchini, kikanda na dunia na matarajio kwa mwaka 2020.
Share:

TMA YATOA TAHADHARI YA MVUA KUBWA KUNYESHA LEO HADI JUMATANO TANZANIA ...."MJIANDAE MAJI"

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini(TMA), imetoa tahadhari ya mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha Machi 2 - 3, 2020, katika Mikoa ya Mara, Simiyu, Arusha,Kilimanjaro, Manyara, Singida,Dodoma, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Tanga, Dar es Salaam,Pwani pamoja na Visiwa vya Mafia,Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo pia imeeleza kuwa mvua hizo pia zitanyesha Machi 4 kwa baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Njombe, Iringa, Arusha, Kilimanjaro,Manyara, Dodoma, Tanga, Morogoro, Dares Salaam, Pwani pamoja na Visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo Machi 2 hadi Jumatano ya Machi 4, 2020.

TMA pia imeeleza athari ambazo zinaweza kujitokeza kuwa ni pamoja na baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri,kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii na kuwataka wananchi kuzingatia na wajiandae.

Share:

TAASISI ZA KIFEDHA NCHINI ZATAKIWA KUACHA URASIMU KATIKA MIKOPO

Na Salvatory Ntandu - Kahama

Serikali imezitaka Taasisi za kifedha nchini kuacha urasimu katika utoaji wa mikopo kwa wawekezaji wa viwanda wa ndani ili kuwasaidia kukuza mitaji yao hali ambayo itachangia kuongeza ajira.

Kauli hiyo imetolewa Machi mosi na Makamu wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Ali Idd wilayani, Kahama mkoani Shinyanga katika ziara yake ya kwanza baada ya kutembelea na kukagua eneo la ujenzi wa viwanda vitatu katika eneo la Chapulwa vinavyojengwa na KOM GROUP OF COMPANIES.

Alisema kuwa baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zitoa masharti magumu kwa wawekezaji wa ndani pindi wanapohitaji kukopeshwa fedha kwaajili ya kukuza biashara zao na kusababisha wengi wao kushindwa kuwekeza kwa tija.

“Nizitake taasisi hizi zitambue umuhimu wa wawekezaji wetu wa ndani kama vile kampuni hii ya KOM ambayo inaendelea na uwekezaji katika eneo hilo la Chapulwa,riba zikipungua nina imani watanzania wengi watanufaika kwa kupata mikopo ambayo itasaidia kukuza uwekezaji wao”,alisema Balozi Idd.

Alifafanua kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli imejikita katika uanzishwaji wa viwanda hivyo ni budi kwa taasisi hizo kuunga mkono juhudi za kuelekea katika uchumi wa kati na kuwawezesha wananchi wengi kupata ajira za kudumu sambamba na kuongeza uchumi wa taifa.

“Mkoa wa shinyanga mmetia fora katika uhamasishaji wawekeza wa ndani katika ujenzi wa viwanda nimekagua eneo hili ambako kunajengwa viwanda zaidi ya vitatu ambapo watanzania zaidi ya 2000 watapata ajira”,alisema Balozi Idd.

Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alitoa rai kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika mkoa wa Shinyanga kutokana na wingi wa fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa huo.

“Katika eneo hili la Chapulwa mkoa wa Shinyanga tumetoa viwanja bure kwa wawekezaji huyu wa kampuni ya KOM kama kuwapa motisha ya kuwahamasisha kuwekeza katika mkoa wetu sambamba na kuandaa mazingira rafiki kwao”,alisema Telack.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya KOM GROUP OF COMPANIES,Braison Edward alisema kuwa gharama za uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya dola milioni 10 za Kimarekani na viwanda vitakavyojengwa ni vya maji,soda na kusaga nafaka.

Balozi Seif Alli Idd yupo mkoani Shinyanga katika ziara ya siku tano akiwa ni mlezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga ,akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.
Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na kwa kutowapa mikono viongozi kutekeleza agizo la Waziri wa Afya Ummy mwalimu kuhusu Virusi vya Corona.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga  Mabala Mlolwa akiwa amekiti na mgeni wake Balozi Seif Ali Idd katika sofa katika eneo la Bukondamoyo
Mkuu wa mkoa wa shinyanga zainabu telack akiwa ameketi kwenye sofa na Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika eneo la viwanda vidogo la bukondamoyo katika eneo la halmashauri ya mji wa kahama.
Share:

Raia wanne wa kigeni walioingia na mafua Uganda watengwa Kwa Hofu Ya Virusi Vya Corona

Raia wanne wa kigeni waliowasili nchini Uganda na dalili za virusi vya corona wametengwa katika hospitali ya Entebbe, Waziri wa afya amethibitisha.

Bila ya kutaja uraia wao, afisa mahusiano wa waziri wa afya bwana Emmanuel Ainebyoona alisema kuwa raia hao wamechukuliwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe.

"Sampuli ya vipimo vyao vimepelekwa katika kituo cha utafiti wa virusi nchini humo (UVRI). Na tutaitaarifu umma " gazeti la Daily Monitor limemnukuu

Wizara ya afya imewataka wananchi kuwa watulivu na kufuata hatua za kujikinga na ugonjwa wa corona kwa sababu hakuna udhibitisho wa kuwa virusi hivyo vimeingia nchini humo.

-BBC


Share:

Korea Kaskazini Yafyatua Makombora Mengine Mawili

Korea Kaskazini  leo imefyatua makombora mengine mawili kuelekea baharini

Vyombo vya habari kutoka Korea Kusini vimeinukuu wizara ya ulinzi ya nchi hiyo ikitangaza kuwa, makombora hayo mawili yamefyatuliwa mapema leo katika mji wa Korea Kaskazini wa Wonsan kuelekea baharini.

Tarehe mosi Januari, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alitangaza kuwa, miradi ya nyuklia na majaribio ya makombora ya nchi yake yataanza tena endapo mazungumzo ya nchi hiyo na Marekani hayatoanza tena.

Mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini hivi sasa yameingia kwenye mkwamo baada ya kuvunjika mazungumzo kati ya pande hizo mbili yaliyofanyika Hanoi, Vietnam mnamo mwezi Februari mwaka 2019.


Share:

Uturuki yawauwa wanajeshi 19 wa serikali ya Syria

Mashambulizi ya angani ya ndege za Uturuki zisizoruka na rubani yamewauwa wanajeshi 19 wa serikali ya Syria katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Idlib, wakati mvutano ukiendelea kati ya Syria na Uturuki. 

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria limesema wanajeshi hao waliuawa baada ya msafara wao kushambuliwa katika eneo la Jabal al-Zawiya na kituo cha kijeshi karibu na mji wa Maaret al-Numan. 

Ripoti hiyo imekuja saa chache baada ya Uturuki kuzidungua ndege mbili za kivita za Syria, katika operesheni kali inayofanywa dhidi ya serikali ya Syria mkoani Idlib, ambako wanajeshi waasi wakisaidiwa na Uturuki wanaweka kizingiti kwa serikali ya Damascus kuchukua udhibiti wa nchi nzima. 

Uturuki imethibitisha kuanzisha operesheni kamili dhidi ya wanajeshi wa Syria wanaoungwa mkono na Urusi baada ya wanajeshi 34 wa Uturuki kuuawa wiki iliyopita katika shambulizi la angani lililodaiwa kufanywa na serikali ya Syria.


Share:

Watanzania Watakiwa Kuchangamkia Fursa Kili Marathon.

Na. Aron Msigwa - WMU, Moshi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Hamisi Kigwangalla ametoa wito kwa Watanzania hususani vijana wajitokeze kushirikimashindano mbalimbali  yanayofanyika nchini Tanzania yakiwemo ya Kilimanjaro Premium Lager  Marathon ili wanufaike wanufaike kiuchumi.

Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo mjini Moshi wakati  akizungumza na wakazi wa mji wa Moshi na maelfu ya wakimbiaji waliojitokeza kushiriki  Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon mwaka 2020 katika uwanja wa Michezo wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Dkt. Kigwangalla ambaye alikua mgeni rasmi na miongoni mwa washiriki wa mbio hizo kwa upande wa Kilometa 21 amesema ushiriki wa Watanzania katika mbio za KILI Marathon unachangia kuimarisha afya za washiriki na kutoa fursa ya ajira kwa wakimbiaji, kukuza kipato kwa wenyeji kufanya  biashara na kuuza huduma mbalimbali kwa wageni.

Dkt. Kigwangalla amewashukuru waandaji wa mbio hizo ambazo zimejumuisha washiriki zaidi ya elfu kumi na mbili (12,000) kutoka nchi zaidi ya 56.

Amesema ujio wa wageni hao kutoka mataifa mbalimbali ni fursa ya kiuchumi kwa Watanzania pia ni moja ya mkakati wa kukuza na kutangaza vivutio mbalimbali vya Utalii.

" Unapopata wageni kutoka nchi zaidi ya 56 kwa wakati mmoja ni jambo la kujivunia, sio jambo dogo sisi kama wizara tumelichukulia kwa uzito mkubwa na ndio maana niko hapa leo pamoja na watendaji kutoka Taasisi mbalimbali kama vile Bodi ya Utalii , TANAPA, KINAPA , Ngorongoro na wadau wengine wa utalii ili kwa pamoja tutangaze utalii uliopo nchini kwetu" Amesema Dkt. Kigwangalla.

Ameeleza kuwa washiriki wa mbio hizo pamoja na mambo mengine wanapata fursa ya kuzuru vivutio vya utalii ikiwemo kupanda Mlima Kilimanjaro , kutembelea eneo la Ngorongoro, Zanzibar, Mikumi Ruaha, Nyerere na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii na kuchangia katika kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa.

" Watalii hawa hufanya matumizi mbalimbali wanapotembelea vivutio vyetu na hii hukuza biashara mbalimbali, ni jambo la kuungwa mkono kwa nguvu zote natoa rai kwa waandaaji tuendelee kushirikiana pamoja na Wizara ya Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo ili tusukume gurudumu hili" Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.

Dkt.Kigwangalla ametoa wito kwa watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii.

" Tumeshusha viingilio kwa kiasi kikubwa ili Watanzania wengi zaidi wapate fursa ya kutembelea vivutio hivi na hii ni pamoja na wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo, Tutumie fursa hii vizuri na Wizara yangu itagakikisha vivutio vyote vinakuwa katika hali ya ubora unaotakiwa " Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.

Aidha, amewataka waandaaji wa mbio mbalimbali zinazovutia watalii wajitokeze na kuishirikisha Wizara ili isaidie kuweka mikakati mizuri ya matumizi ya fursa zilizopo.

Amesema Serikali itaendelea kuunga mkono mashindano hayo na kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili mashindano hayo yaendelee kuwa kivutio miongoni mwa washiriki, yakuze utalii na kuwa chanzo kikubwa cha mapato.

Kwa Upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza wakati wa utoaji wa Nishani na  zawadi mbalimbali kwa Washindi wa mbio hizo ametoa wito kwa waandaji wa mbio hizo wawahamasishe vijana wa Kitanzania washiriki mashindano hayo na kushinda Tuzo na zawadi mbalimbali zinazotolewa badala ya kuachia wageni.

Dkt. Mwakyembe ametoa rai hiyo kufuatia idadi kubwa ya washindi wa nafasi za juu katika mashindano hayo kuwa wageni kutoka nchi za jirani za Kenya na Uganda.

Amesema Tanzania ina vijana wazuri wenye uwezo wa kukimbia na kupeperusha bendera ya Tanzania Kimataifa akibainisha kwamba jambo hilo la ushiriki hafifu wa Watanzania katika mashindano ya Marathoni lazima litafutiwe ufumbuzi.

" Haiwezekani, Tanzania tunao vijana wazuri sana na wenye uwezo wa kukimbia kwa spidi kama ya pikipiki, hatuwezi kuendelea kuwaachia wageni ndio wakawa wanashika nafasi za kwanza na kuchukua fedha wakati vijana wa kitanzania miguu mnayo na uwezo wa kukimbia mkachukua fedha hizi upo" Amesisitiza.

Kufuatia hali hiyo ametoa agizo kwa viongozi wa mchezo wa riadha kutoka maeneo mbalimbali nchini kukutana naye mjini Dodoma ili waweze kufanya maamuzi juu ya hiyo hilo.

Aidha amesema kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweka miundombinu na mazingira wezeshi ya kuongeza idadi ya washiriki wanaojitokeza katika mashindano hayo ikiwemo ujenzi wa miundombinu na njia maalum zitakazoongeza idadi kubwa ya  wakimbiaji wa Kili Marathon kutoka katika mataifa mbalimbali.

MWISHO


Share:

Taasisi Za Kifedha Nchini zatakiwa Kuacha Urasimu Katika Mikopo

NA SALVATORY NTANDU
Serikali imezitaka Taasisi za kifedha nchini kuacha urasimu katika utoaji wa mikopo kwa wawekezaji wa viwanda wa ndani ili kuwasaidia kukuza mitaji yao hali ambayo itachangia kuongeza ajira.

Kauli hiyo imetolewa Machi mosi na Makamu wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Balozi Ali Idd  wilayani, Kahama mkoani Shinyanga katika ziara yake ya kwanza baada ya kutembelea na kukagua eneo la ujenzi wa  viwanda vitatu katika eneo la chapulwa vinavyojengwa na KOM GROUP OF COMPANIES.

Alisema kuwa baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zitoa masharti magumu kwa wawekezaji wa ndani pindi wanapohitaji kukopeshwa fedha kwaajili ya kukuza biashara zao na kusababisha wengi wao kushindwa kuwekeza kwa tija.

“Nizitake taasisi hizi zitambue umuhimu wa wawekezaji wetu wa ndani kama vile kampuni hii ya KOM ambayo inaendelea na uwekezaji katika eneo hilo la Chapulwa,riba zikipunguwa naimani watanzania wengi watanufaika kwa kupata mikopo ambayo itasaidia kukuza uwekezaji wao”alisema Balozi Idd.

Alifafanua kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli imejikita katika uanzishwaji wa viwanda hivyo ni budi kwa taasisi hizo kuunga mkono juhudi za kuelekea katika uchumi wa kati na kuwawezesha  wananchi wengi kupata ajira za kudumu sambamba na kuongeza uchumi wa taifa.

“Mkoa wa shinyanga mmetia fora katika uhamasishaji wawekeza wa ndani katika ujenzi wa viwanda nimekagua eneo hili ambako kunajengwa viwanda zaidi ya vitatu ambapo watanzania zaidi ya 2000 watapata ajira”alisema Balozi Idd.

Nae mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alitoa rai kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika mkoa wa shinyanga kutokana  na wingi wa fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa huo.

“katika eneo hili la chapulwa mkoa wa Shinyanga tumetoa viwanja bure kwa wawekezaji huyu wa kampuni ya KOM kama kuwapa motisha ya kuwahamasisha kuwekeza katika mkoa wetu sambamba na kuandaa mazingira rafiki kwao”alisema Telack.

Kwa upande wake meneja wa kampuni ya KOM GROUP OF COMPANIES,Braison Edwad alisema kuwa gharama za uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya dola milioni 10 za kimarekani na viwanda vitakavyojengwa ni vya maji,soda na kusaga nafaka.

Balozi Seif Alli Idd yupo mkoani shinyanga katika ziara ya siku tano akiwa ni mlezi wa chama cha mapinduzi mkoa,akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.

Mwisho.


Share:

Waziri Mkuu Majaliwa Afungua Kitengo Cha Kuchuja Damu Katika Hospitali Ya Bombo-Tanga

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua mradi wa huduma ya kuchuja damu  katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo na kupunguza gharama ya kuwasafirisha wagonjwa wenye matatizo ya figo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  kufuata hiduma hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amefungua mradi wa ujenzi wa barabara ya Makorora-Msambweni (km nne) iliyojengwa kwa thamani ya sh. bilioni 5.9 ambayo itarahisisha mawasiliano kwa wakazi wa kata za Msambweni, Makorora, Mzingani na watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Waziri Mkuu amezindua miradi hiyo kwa nyakati tofauti jana (Jumapili, Machi 1, 2020) wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara  ya kikazi mkoani Tanga, ambapo alisisitiza azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi wote.

Alisema sekta ya afya imepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka minne iliyopita na Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na maboresho ya stahili za watumishi. Amewataka watumishi waendelee kuwa watulivu wawe na Imani na Serikali yao.

Alisema ni vema kwa watumishi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanafanyakazi kwa uaminifu na uadilifu ili wagonjwa wenye matatizo ya figo pamoja na matatizo mengine ya kiafya wapate huduma bora  bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao kuandaa utaratibu wa kutoa elimu kila siku asubuhi juu ya umuhimu wa kujikinga na magonjwa yanayoambukiza na  yasiyoambukiza ambayo ni hatari na ya gharama kubwa.

“Suala la mazoezi ni tiba muhimu na nyie wataalamu ambao mnajua ugonjwa huu tunautibu vipi ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, hivyo  andaeni nafasi ya dakika tano hadi kumi za kutoa elimu na kuhamasisha watu wajenge tabia ya kufanya mazoezi. Magonjwa mengine yanaweza kutibika kwa kufanya mazoezi na kubadilisha mitindo ya maisha.”

Waziri Mkuu alisema Serikali imeboresha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi wake zikiwemo za afya, hivyo aliwaagiza viongozi katika ngazi mbalimbali wahakikishe hakuna mwananchi anayekwenda kwenye maeneo ya kutolea huduma na kukosa dawa au vipimo.

Akizungumza kuhusu barabara ya Makorora-Msambweni, Waziri Mkuu alisema mbali na kurahisisha mawasiliano pia itaboresha usalama na mazingira ya wananchi kutokana na uwepo wa taa za barabarani jambo litakaloongeza thamani ya makazi.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema huduma za figo nchini zilikuwa zinatolewa katika vituo 19 vya binafsi na hospitali tano za Serikali ambazo ni Hospitali za Kanda za Rufaa Muhimbili, Mbeya, Bugando, KCMC na Benjamin Makapa.

Waziri Ummy alisema hadi 2016 asilimia 90 ya huduma za kusafisha figo zilikuwa zinatolewa na sekta binafsi na asilimia 10 taasisi za umma. “Hali hii inasababisha huduma za usafishaji figo kuwa na gharama kubwa na kukosa uwiano wa huduma hasa kwa wananchi waishio mikoa ya pembezoni.”

Alisema Serikali imepanga kutanua huduma hizo ili ziweze kutolewa katika hospitali zote za rufaa za mikoa, ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo imeanza kwa hospitali za rufaa za mikoa ya minane ambazo ni Bombo-Tanga, Meru-Arusha, Mtwara, Iringa, Bukoba-Kagera, Maweni-Kigoma na Sekoutoure-Mwanza.

Waziri Ummy alisema uanzishwaji wa kituo kimoja cha kutolea huduma ya kuchujia damu hadi kuanza kufanya kazi kama kilivyo cha Bombo kinagharimu sh milioni 574,794,177, hivyo kwa vituo hivyo nane ambavyo mwezi huu vinataanza kutoa huduma vitagharimu sh. bilioni 4.5.

Kwa upande wao,wagonjwa wenye matatizo ya figo waliishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma ya kuchuja damu katika hositali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga kwa kuwa awali walilazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo katika hospitali ya Muhimbili.

Pia, Wagonjwa hao licha ya kuishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma, pia wameiomba iangalie uwezekano wa kupunguza gharama ili watu wengi waweze kumudu matibabu hayo kwani kwa sasa gharama ya session moja ni sh. 250,000.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne March 2


















Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger