Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Ng'ombe 22 wenye thamani ya shilingi milioni 12 ,wamekufa baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua na upepo mkali katika kijiji cha Kaziramihunda kata ya Gwanumpu wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
Wakizungumzia tukio hilo wamiliki wa ng'ombe hao,akiwemo Abdu Kasungu,wamesema tukio hilo limetokea Septemba 1,2019 majira ya saa kumi na moja jioni wakati vijana waliokuwa wametoka kuwanywesha maji ng'ombe katika Kijiji cha Msenga lakini wakiwa njiani ulitokea upepo mkali ulioambatana na radi na kuwapiga ng'ombe 22 ambao walikufa papo hapo.
Kasungu amesema kati ya ng'ombe 20 alizokuwanazo amepoteza ng'ombe 16 na kwamba anashukuru Mungu kwa kuwa watu waliokuwa wakiwachunga walibaki salama kwa kuwa imetokea ni bahati mbaya hawana budi kulipokea hilo.
Naye Filbert Chibedese aliyepoteza ng'ombe sita amesema tukio hilo limewasikitisha kwa kuwa litawarudisha nyuma sana kiuchumi lakini hawana namna kwa kuwa ni majanga ya kiasili yanayojitokeza bila kutarajia.
Akizungumza na wananchi hao wakati alipofika katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko,Kanali Hosea Ndagala amesema tukio hilo ni kama matukio mengine halikutegemea litojee hivyo watu wanatakiwa kuwa wavumilivu na kujua kuwa mambo hayo ni mpango wa mwenyezi Mungu na kutoa pole kwa wote walioingia hasara katika kupoteza ng'ombe hao.
"Nitoe pole kwa wote mliondokewa na mifugo hii, ni kweli inaumiza sana na ni hasara kubwa mmeipata, jambo kubwa ni kumshukuru Mungu kwa kuwaponya watu waliokuwa wanawachunga ng'ombe hao, kikubwa ni uvumilivu msikate tamaa muendelee kupambana haya mambo yanatokea hatuna sababu ya kukata tamaa katika utafutaji poleni sana", amesema Kanali Ndagala.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi waliojitokeza katika tukio la ng'ombe kupigwa radi.Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akiangalia ng'ombe waliokufa kwa kupigwa radi.