Wednesday, 10 July 2019

Picha : MKUU WA JESHI LA POLISI 'IGP SIMON SIRRO' AKAGUA NYUMBA ZA KISASA ZA MAKAZI YA POLISI SHINYANGA

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro ametembelea na kukagua nyumba 10 za kisasa za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la Kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga na kugharimu shilingi milioni 225.

Mkuu huyo wa jeshi la polisi amekagua nyumba hizo leo Jumanne,Julai 10,2019 na kueleza kuridhishwa jinsi zilivyojengwa kwa umaridadi na ubora wa hali ya juu. 

Nyumba hizo 10 ni sehemu ya nyumba 114 ambazo ujenzi wake umekamilika nchi nzima ikiwa ni sehemu ya nyumba 400 zinazojengwa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya makazi ya askari polisi.

"Ujenzi huu umegharimu shilingi milioni 225,ni kweli nyumba hizi ni nzuri sana,nimpongeze sana Mhe. Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mhe.Zainab Telack na kamati yake ya ulinzi na usalama,kamati ya ujenzi na wadau wote walioshiriki kwa kazi hii nzuri"

"Sasa tunamsubiri Mhe. Rais,Dkt.John Pombe Magufuli muda siyo mrefu atazindua hizi nyumba 114 nchi nzima. Pesa zilizotolewa ni kwa ajili ya kujenga nyumba 400,lakini mpaka sasa zilizokamilika sasa ni 114",alisema IGP Sirro. 

Kwa upande wake,Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Zainab Telack alimshukuru Rais Magufuli kwa kutoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya askari polisi huku akimuomba IGP Sirro kutafuta pesa kwa ajili ya ukarabati wa baadhi ya nyumba za askari ambazo hali yake siyo nzuri.

ANGALIA PICHA
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Zainab Telack akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro alipowasili mkoani Shinyanga kukagua nyumba 10 za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la Kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga leo Jumanne Julai 10,2019. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akizungumza wakati akikagua nyumba 10 za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la Kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga leo Jumanne Julai 10,2019.Kulia ni Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,ACP Richard Abwao,kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Zainab Telack.
Muonekano wa nyumba 10 za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Nyumba 10 za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la Kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Muonekano wa nyumba 10 za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Zainab Telack akimuonesha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akikagua nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akikagua nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Awali Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akisamiliana na askari polisi alipowasili mkoani Shinyanga kukagua nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akisamiliana na askari polisi alipowasili mkoani Shinyanga kukagua nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akisamiliana na askari polisi alipowasili mkoani Shinyanga kukagua nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akisamiliana na askari polisi alipowasili mkoani Shinyanga kukagua nyumba za makazi ya askari polisi zilizojengwa katika eneo la kambi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini Tanzania Simon Sirro akisamiliana na waendesha bodaboda katika eneo la nyumba za makazi ya polisi Kambarage Mjini Shinyanga na kuwakumbusha kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwasihi kuacha kubeba mishikaki,wavae kofia ngumu na wawe na leseni. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

Serikali yaanzisha utalii wa fukwe ziwa Viktoria

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangala amesema wameanzisha utalii wa fukwe katika ziwa Viktoria na kwamba tayari Mamlaka ya hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) inajenga kivuko kitakachokuwa na uwezo wa kupakia magari manne hadi sita na abiria wasiopungua 100.

Kigwangala ameyasema hayo jana Jumanne Julai 9, wilayani Chato mkoani Geita katika hafla ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,702 ambapo amesema kuwa kuna wanyama waliokuwepo katika hifadhi hiyo na baadae wakatoweka hivyo watafanya jitihada za kuwarudisha katika makazi yao ya asili.

“Katika mapori haya kulikuwa na Faru lakini walitoweka na tunajua aina ya Faru waliokuwepo hapa hivyo tutafanya jitihada za kuwarudisha katika makazi yao, pia tunatarajia kupokea faru 10 wenye asili ya Tanzania kutoka nchi za nje kuja kuongeza idadi ya faru katika nchi yetu,” amesema.

Aidha amesema kuwa walipopandisha hadhi mapori hayo uwindaji umekoma na matumizi yatabadilika na kwamba kiwango cha ulinzi na uhifadhi kitaongezeka kwa kiwango cha juu.

“Katika kipindi ambacho uvamizi ulikuwa umetamalaki wanyama wengi walitoweka lakini tangu tumepandisha hadhi mapori haya idadi imeanza kurudi,” amesema.


Share:

Aliyelazwa Mwaka Mmoja Mloganzila Apatiwa Mashine Ya Kupumua

Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, imempatia msaada wa mashine ya kusaidia kupumua (Oxygen Concentrator) Bw. Hamad Awadhi kutokana na matatizo yake ya afya ambayo yanamlazimu kutumia mashine ya oxygen muda wote ili aweze kupumua.
 
Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH-Prof. Charles Majinge amesema hospitali imempatia msaada Bw. Awadhi kwa lengo la kuokoa maisha yake sanjari na kuimarisha afya yake lakini pia kumuwezesha kuendelea na shughuli zake za kawaida ili kutokua tegemezi kutokana na hali yake.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru ameeleza kwamba mashine hiyo inathamani ya shilingi milioni tatu na nusu imenunuliwa na Hospitali ya Mloganzila ambapo wataalam wamempatia mafunzo Bw. Awadhi namna ya kuitumia na kuitunza ipasavyo.
 
Prof. Museru amemtaka Bwan. Awadhi kuitunza na kuitumia vema mashine hiyo kama ambavyo ameelekezwa na wataalam ili afya yake itakapoimarika iweze kusaidia watanzania wengine.
 
“Hospitali imekupatia msaada wa mashine hii ya kukusaidia kupumua- kwa lengo la kuhakikisha afya yako inaimarika zaidi hivyo tunaomba uitunze na utakapopona kabisa utairejesha hospitali ilituwasaidie wengine” amesema Prof. Museru.
 
Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani MNH- Mloganzila Dkt. Patricia Munseri amesema, Bw. Awadhi kwa muda wote aliokuwepo hospitalini ameishi kwa kutegemea mashine ya oxygen ambayo inamsaidia kupumua ambapo kwa siku alikua akitumia gesi wastani wa lita 5,760.
 
Bw. Hamad Awadhi alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Julai 9 mwaka 2018 na kuruhusiwa Julai 9 mwaka 2019 baada ya afya yake kuimarika.


Share:

Wazungu Watatu Waliokamatwa na Madini ya Dhahabu Warudishwa Rumande

Watu watatu raia wa kigeni kutoka nchi za Ireland na Uingereza wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na madini aina ya dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 98 kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Akisoma Shtaka Mwendesha Mashitaka wakili Msomi wa Serikali Mwandamizi Jacqueline Nyantori, anasema washtakiwa hao kwa pamoja wametenda kosa hilo la uhujumu uchumi July 3, 2019 na kukamatwa katika uwanja wa Ndege  Songwe uliopo Mkoani Mbeya ambapo walikutwa na madini aina ya yenye uzito wa gram 1043.33 yenye thamani ya shilingi milioni 98.5 .

Wakili huyo amewataja washtakiwa hao kuwa ni Clive Rooney (62) raia wa Irish ambaye ni Meneja wa fedha, Ross Harris (34) na Robert Wheedon (59)ambao ni raia wa Uingereza ambapo wamekamatwa na madini hayo wakiyasafirisha kuelekea Jijini Dar es Salaam.

Mwendesha mashtaka wa Serikali amesema washtakiwa hao wamekamatwa na Madini kinyume cha Sheria ya Uhujumu uchumi namba 18 (1) na 4 kifungu cha (1a) na kifungu cha sheria ya madini namba 14 cha mwaka 2010, ikiwa ni pamoja na aya ya 27 ya jedwali la kwanza na kifungu namba 57 kifungu kidogo.

Aidha Kaimu Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya Venance Mulingi amesema Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shtaka hili ambapo washtakiwa wamerudishwa wamerudishwe rumande hadi July 22 mwaka huu.


Share:

Magonjwa 8 Yanayoshambulia KUKU Pamoja na Tiba Zake

Hivi Karibuni tuliona namna unavyoweza kuwa milionea kupitia ufugaji wa kuku. Tulisimulia namna unavyoweza anza na mtaji wa 250,000 tu na ndani ya miaka miwili tukaona unavyoweza  kujipatia milioni 390 kupitia ufugaji wa kuku wa kienyeji.

Leo tutazungumzia magonjwa yote yanayosumbua kuku ili sasa uyajue na ukabiliane nayo na hatimaye uweze kutimiza ndoto zako za kuwa milionea.

 1.Rangi ya kinyesi
==>>Mharo mweupe(pullorum bacilary diarrhoea)
ugonjwa huu huathiri zaidi vifaranga kabla ya wiki nne
huharisha mharo mweupe,

Tiba
Usafi  kwenye banda na kuepusha maji yasimwagike ovyo

2.Kipindupindu cha kuku(fowl cholera)
-Kinyesi cha kuku ni njano
-Tumia dawa za salfa, eg Esb3 au amprollium

3.Coccidiuosis
mwanzo kinyesi cha kijivu na baadae huharisha damu iliyochanganyika. Tumia dawa ya VITACOX au ANTICOX

4.Mdondo(Newcastle)
-kuku hunya kinyesi cha kijani (NB; sio kila kijani ni newcastle)
-HAKUNA TIBA. (Kuku wapewe  chanjo  tangu  vifaranga wa  umri wa  siku 3,  baada ya  wiki 3  – 4,  na baadaye  kila baada  ya miezi 3)

5.Typhoid
-Kinyesi cheupe
-kinagandia sehemu za nyuma au hulowana sehemu za haja
-dawa ni Eb3

6.Gumboro
-Huathiri zaidi vifaranga
-kinyesi huwa ni majimaji
-Dawa hakuna, tumia vitamini na antibiotic

7.Kideri
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao hushambulia aina zote za spishi za ndege, ijapokuwa kuku ndio aina inayoathirika zaidi

Dalili
•Vifo vya ghafla bila kuonesha dallili zote
•Kuvimba kwa kichwa na shingo
•Kuhalisha uharo wa kijani
•Utagaji wa mayai kushuka kwa kiasi kikubwa au kusimama kabisa
•Kutetemeka, kichwa kugeuzwa upande mmoja
•Kupooza kwa mabawa na miguu.

Jinsi unavyoenea
•Chanzo cha maambukizi ni maji, chakula kill Hoxha fulls a na kinyesi cha kuku wagonjwa.
•Pia maambukizi huweza kupitia mfumo wa hewa ktoka kwa kuku wagonjwa
•Kuku, vifaa vya kazi na bidhaa zitokanazo na kuku ( nyama, mayai, manyoya na mbolea) kutoka mashamba yenye ugonjwa zinaweza kueneza ugonjwa
•Faranga anaweza kupata maambukizi kutoka vituo vya kutotolea vifaranga kutokana na maganda ya mayai yaliyochafuliwa
•Kuku kuzubaa na kuacha kula
•Kuku kukohoa, hupiga chafya na kupumia kwa shida

Matokeo Kwa Kuchunguza Mzoga Aliyeathirika
Ugonjwa huathiri zaidi mfumo wa hewa na njia ya chakula, hivyo mabadiliko yanayoonekana kwenye mzoga ni pamoja
•Madoa ya damu kwenye mfumo wa hewa
•Kamasi nzito zenye Tangu ya njano kwenye koromeo
•Utandu mweupe kwenye mfumo wa hewa
•Bandama kuvimba
•Uvimbe kwenye kichwa na eneo la shingo
•Madoa madogo madogo ya damu kwenye kifua, mafuta na utandu wa tumboni
•Damu kuvia kwenye mfumo wa usagaji chakula, juju, firigisi, tumbo na utumbo.

NB:
Haya matokeo yatakusaidia wakati pale kuku amekufa banda bila kujua nini tatizo, kabla ya kumtupa mchinje na kumkagua tatizo lilikuwa nini.

Kudhibiti
Kuna namna za kuchanja kuku wako dhidi ya ugonjwa wa kideriI.Kudondoshea tone moja jichoniII.Kwa kidonge

Kudondoshea tone moja jichoni
•Pata chanjo kutoka kwa wakala au duka la mifugo lililokaribu nawe. Chanjo inayopendekezwa ni chanjo ya kideri 1-2 (1-2 NEWCASTLE VASSINE)
•Kamata kuku kwa uthabiti huku ukiwagemeza upande
•Dondoshea tone moja la chanjo ya kideri kwenye jicho moja
•Subiri kuku achezeshe kope ndipo umuachie.
 
Kwa kidonge
•Pata chanjo kutoka wakala au duka la mifugo lililo karibu nawe, hakikisha hifadhiwa kwenye barafu ili isiyeyuke kabla ya kutumika
•Kidonge hicho kimoja kitatumika kwa kuwekwa kwenye kiasi cha maji Lita 20
•Ukisha changanya kidonge na maji, hakikisha inatumika ndani ya Masaa 2 baadaya masaa hayo kupita haitafaa tena kwa matumizi.

Muhimu:
Chanja kila baada ya miezi 3 kwa kuku umri zaidi ya miezi mitatu na kuendelea tofauti na vifaranga
Chanja kuku kwenye afya tuu. ( uki chanja mgonjwa atakufa)

Sababu za kuku kula mayai
Kuku hula mayai kwa sababu nyingi sana ambazo zingine au zote zinaweza kuzuilika,
1.Tabia yao tu- Hapa utakuta ndo uzao wao wanatabia ya kula mayai hivyo kuku hufanya muendelezo wa kula mayai,
2.Kuto kupata chakula cha kutosha- Hii ni moja ya sababu kubwa kabisa inayo pelekea kuku kula mayai.
3.Kukosa madini joto- Hii inaweza kuwa ndo sababu kuu ya kwa nini kuku wanakula mayai, kuku wakikosa madini joto ni lazima wale mayai na hata kulana wao wenyewe, na jua kwamba kwenye yai kuku huwa anatafuta lile ganda la juu pekee sema anapo donoa na kulipasua yai hujukuta anakula na ute na kiini ila yeye lengo lake hasa ni ganda la juu
4.Kuku kutagia sehemu nyeupe sana yenye mwanga mkari hupelekea kuku kula mayai.
5.Mayai kukaa muda mrefu bila kukusanywa baada ya kutaga- Hapa ni kwamba mayai yanapo kaa muda bila kukusanywa na kama yapo sehemu ya wazi sana hupelekea kuku waanze kutest na some time kushangaa nini hiki cheupe? katika kushangaa ni kitu gani hiki cheupe cha mviringo hujikuta wanatest kudonoa na matokea yake ni kupasua yai.
6.Lishe mbaya
7.Nafasi ndogo
8.Vyombo havitoshi
9.Kukosa shughuli
10.Banda chafu (Manyoya)
11.Ukoo

Namna ya kuzuia kuku kudonoana au kula mayai
1.Chakula cha kutosha ni muhimu sana, ili kuwafanya wasitake kula mayai ili kushiba.
2.Mayai yakusanywe mara tu anapo taga na usiyaache muda mrefu bandani.
3.Sehemu ya kutagia iwe na giza la kutosha ili kufanya kuku ashindwe kuona yai alilo taga.
4.Madini joto ni muhimu sana.
5.Kuku wenye tabia za kula mayai unaweza chinja au kuuza.
6.Kuweka idadi ya kuku inayolingana na sehem ulionayo.
7.Usizidishe mwanga.
8.Banda liwe safi.
9.Weka vyombo vya kutosha.
10.Wape lishe bora.
11.Wape kuku shughuli kwa kuwawekea bembea na sehemu ya uwazi kwa ajili ya mazoezi.
12.Kata midomo ya juu.
13.Epuka ukoo wenye tabia hizo.


Share:

Hii Ndio Sababu Kwanini Kama Hauna Kipimo Cha Kupimia Sukari ( Blood Test Kit ) Basi Unashauriwa Usitumie Baadhi Ya Dawa Z A Asili Zinazo Tibu Tatizo La Sukari Ya Kupanda.

Sukari  ( Ya Kupanda )   ni  tatizo  linalo  wasumbua  na  kuwatesa  mamilioni  ya  watu  duniani.

Habari  njema  ni  kwamba  zipo   dawa  mbalimbali  za  asili  ambazo  zina  uwezo  mzuri tu  wa kushusha  sukari  iliyo  panda sambamba  na  kudhibiti  kiwango  cha  sukari  kwenye  damu  kwa  ufanisi  mkubwa.

Kati  ya  dawa  hizo  zipo  zinazo  shusha  sukari  taratibu  na  zipo  zinazo  shusha  sukari  kwa  haraka  sana.

Mada  yangu  ya  leo  inahusu  dawa  za  asili  ambazo  zinashusha  sukari  kwa  haraka  sana  na  tahadhari  ya  kuchukua  kwa  mtu  anae  taka  kutumia  dawa  hizo.

Mtu mwenye  tatizo  la  sukari  ya  kupanda  anapokuwa  anatumia  dawa  za  asili kwa  ajili ya  kutibu tatizo  lake  anatakiwa  kujua  aina  ya  dawa  anazo  tumia.

 Anatakiwa  kujua  kama  dawa  anayo  tumia   inashusha  sukari  kwa  taratibu  au  inashusha  kwa  haraka.

Kwa  dawa  za  asili  zinazo  shusha  sukari  kwa  taratibu  mhusika  anaweza  kuwa  anatumia  dawa  usiku  na  mchana  na  kwenda  kupima  sukari  kila  baada  ya  wiki  ili  kujua  sukari yake  imepungua  kwa  kiasi  gani. Hizi  hazina  risk sana  kwa  sababu  zinashusha  sukari kwa  taratibu. Mhusika  kulingana  na  kiwango  cha  sukari  alicho  nacho  anaweza  kutumia  dawa  zilizopo  katika  kundi  hili kwa  muda  wa  kuanzia  mwezi  mmoja  hadi  miezi  mitatu  kulingana  na  dawa  husika.

Lakini  kwa  dawa  zinazo  shusha  sukari  kwa haraka, mhusika  anatakiwa  kuwa  karibu sana  na  kipimo  cha  sukari  ( Blood Sugar   Test  Kit )

Hii  ni  kwa  sababu  mhusika  anatakiwa  kuwa  anapima  sukari  yake  kila  siku.   Yani akitumia  dawa  usiku  basi  asubuhi  atatakiwa  kupima  sukari  yake  ili  kujua  imeshuka  kwa  kiwango  gani  na  akitumia  asubuhi  anatakiwa  kupima  tena  usiku  ili  kujua  sukari  imeshuka  kwa  kiwango  gani.

Kwa  sababu  asipo  fanya  hivyo  sukari  inaweza  kushuka  sana   ( below  normal ) jambo  linalo weza  kumsababishia  madhara makubwa  kwa  sababu  sukari  below  normal  ni  hatari  sana  kwa  mhusika.

Asubuhi   kabla  haujala  chakula  sukari  inatakiwa  kuwa  4  na  baada  ya  kula  chakula  inatakiwa  isizidi  7.  Sasa  akitumia  dawa  zikashusha  sana  sukari  yake  ni risk  kubwa  sana  kwake  kwa  sababu  sukari ikiwa  chini  ni  hatari  sana.

Lakini  akiwa  na  kipimo  cha  sukari ni  rahisi  kwake kujua  sukari  imefikia  kiwango  gani jambo  ambalo  litamuepusha  na  kuendelea  kutumia  dawa  ya  kushusha  sukari  wakati  sukari  yake  tayari  imekuwa  normal.

Ndio  maana  tunasema  mtu  anae tumia  dawa za  asili  kwa  ajili  ya  kushusha  sukari  anatakiwa  ajue  dawa  anazo  tumia  zipo  kwenye  kundi  gani.

Kwa  ushauri  na  kujua  aina  ya  dawa  za  asili  za  sukari  ambazo  zinashusha  sukari  kwa  haraka  pamoja  na  zile  ambazo  zinashusha  sukari  kwa  taratibu, wasiliana  na  duka  la  kuuza  dawa  za  asili  la  NEEMA  HERBALIST.  Tunapatikana UBUNGO  jijini  DAR  ES  SALAAM  kwa  namba  0693  005 189.

Tutembelee  kwenye  tovuti yetu : www.neemaherbalist.blogspot.com


Share:

Wanachama 13 CCM Wajitosa Kumrithiu Tundu Lissu

Wanachama 13 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamejitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho, kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge Jimbo la Singida Mashariki,baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kupoteza sifa.

Waliochuku fomu, ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu na Mkuu wa Mkoa wa  Songwe, mstaafu Luteni Chiku Galawa.

Wengine ni Mwanahamisi Mujori, Moris Mukhoty, Shilinde Kasure, Jeremia Ihonde, Lazaro Msaru, Hamisi Maulidi, Mariamu Nkumbi, Martini Lissu, Sylivester Meda, Thomasi Kitima na Emmanuel Hume.

Akitoa taarifa wilayani Ikungi jana, Katibu CCM Wilaya hiyo, Noverty Kibaji alisema leo wanachama hao wataanza kuchuana katika kura za maoni za ndani ya chama na watakaoshinda nafasi tatu za juu, majina yao watawasilishwa vikao vya juu kwa uamuzi.

“Leo (jana), nimekaa nao na kuwasisitiza wahakikishe wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za chama. Tofauti na hivyo, watasababisha CCM kichukue maamuzi magumu kwa yule atakayeenda kinyume,”alisema Katibu huyo.


Share:

Bilioni 40 Kujenga Vyuo Vipya 40 Katika Wilaya 25

NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI imesema katika bajeti yamwaka huu wa fedha imetenga bilioni 40 kwa ajili ya kujenga  Vyuo ha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA) vipya katika wilaya 25 nchini. 

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa uzindizi wa Chuo cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi wilayani Urambo.

Alisema lengo la ujenzi wa vyuo hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali iliyopo madarakani ya kuhakikisha kuwa inajenga walau Chuo cha Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA) katika wilaya zote ambazo hazina.

Profesa Ndalichako alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha vijana wengi wapate elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kuwawezesha kushiriki katika uchumi wa viwanda hapa nchini badala ya kuwa watazamaji.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema chuo hicho kimegharimu milioni  217.2 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Alisema kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi milioni 198.8 zilitolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kiasi kilichobaki cha milioni 18.3 zimechangiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Dkt Bujulu alisema ili kukamilisha huduma za msingi Chuoni, VETA pia imekusudia kujenga bwalo kwa ajili ya mikutano na wanafunzi kulia chakula kwa gharama ya Shilingi Milioni 20.

Alisema kwa kuanzia Chuo kitaanza kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kozi ndefu katika fani za ushonaji nguo, umeme wa majumbani, uashi na uhazili na komputya.

Kozi za muda mfupi ni matumizi ya komputya, uhazili, ushonaji nguo, uashi, umeme wa majumbani  na udereva wa awali wa magari.

Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Peter Maduki aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kuwaongezea eneo lilibaki ambalo lilikuwa likitumiwa na Mkandarasi ili waweze kuongeza  fani nyingi ambazo zinalingana na sifa za Chuo cha VETA ngazi ya wilaya.

Alisema kuwa eneo la sasa ni dogo na linaruhusu kozi nne na hivyo  kuongezwa kwa eneo kutawawezesha kutoa fani sita hadi saba kwa mwaka.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey aliwataka wakazi wa Urambo kuhakikisha wanatumia Chuo hicho kama fursa ya kuwapatia watoto wao elimu ili waweze kushiriki vema katika ujenzi wa Taifa badala  ya kuwa Watazamaji.

Alisema wasipotumia Chuo hicho vizuri nafasi za ajira zitawapita kwa sababu ya kukosa ujuzi unaostahili kuajirika.

Naye mbunge wa Jimbo la Urambo Margaret Sitta ameahidi kusomesha watoto 62 kutoka Vijiji 62 vya Wilaya ya Urambo kwa gharama za shilingi 60,000/- kila mmoja.

Alisema lengo ni kuwahamasisha wazazi wengi wa eneo hilo kuhakikisha wanatoa fursa kwa watoto wao wanaomaliza elimu ya msingi na wale wa sekondari kujiunga na fani mbalimbali


Share:

Basi Lingine La Abiria Lakamatwa Likiwa Na Abiria Zaidi Ya 90

Na Gasto Kwirini wa Polisi Arusha
Katika operesheni ya ukaguzi wa magari ambayo bado inaendelea leo tarehe 10.07.2019 muda wa saa 06:00hrs asubuhi Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP)Joseph Bukombe akiwaongoza Askari katika barabara ya Arusha – Kiteto walifanikiwa kukamata Basi lenye Namba za Usajili T. 735 AEM mali ya Kampuni ya COAST LINE likiwa limepakia abiria 95.
 
Basi hilo ambalo linafanya safari zake kati ya Arusha na Kiteto lilikua limepakia abiria 67 ambao walikua wamekaa kwenye siti, 25 walikua wamesimama,  kati yao Abiria wa kawaida walikua 10  na Wanajeshi 15. Pamoja na hao walikuepo Dereva, kondakta, fundi na Msindikizaji wa basi hilo ambapo wanafanya  idadi yao kuwa 95.
 
Akizungumza na  Abiria wa Basi hilo Mkuu huyo wa Usalama Barabarani amewataka kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi wanapoona Basi limezidisha abiria, mwendo mkali na kutokubali kupanda basi ambalo limejaa.
 
Aidha ametoa wito kwa wamiliki wa Mabasi kuwasimamia Wafanyakazi wao hasa madereva na Makondakta ili waweze kufuata sheria bila kushurutishwa.
 
“Wamiliki tokeni majumbani, fanyeni ukaguzi wa kushtukiza kuliko kulaumu kila mara tunawakamata kwa kuwaonea, mmiliki atakapowasimamia watu wake Jeshi la Polisi halitaangaika na mtu kumkamata” Alisisisitza RTO Bukombe.

Meneja wa Mabasi ya Coast Line Bwana Petro Amsi Stanley amepongeza Operesheni hiyo inayoendelea kufanywa kwani itasaidia kuwadhibiti Madereva na Makondakta wanaofanya kazi bila kufuata sheria  kwa sababu Wamiliki na Mawakala wanakua hawana taarifa za abiria kuzidi kwenye mabasi yao.
Pia amempongeza Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Arusha kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa ufasaha.
 
“RTO huyu anajiamini na anafanya kazi yake kwa ufasaha mkubwa, na hii imebabishwa na kutokua na ushirika na  Mtu hasa  wamiliki wa Vyombo vya moto, hivyo tunampongeza kwa Opereshini hii anayoendelea kuifanya”. Alisema bwana Esto.
 
Basi hilo limefikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa ajili ya kufanyiwa  Ukaguzi zaidi.
 
Aidha Mkuu wa  wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha ameamuru wakala wa basi hilo awatafutie abiria  wote waliozidi usafiri mwingine.
 
Sambamba na hilo, Dereva na Kondakta wa basi hilo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano, mara baada ya Upelelezi kukamilika watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.


Share:

Ofisa Utumishi Tanesco mbaroni kwa kuomba rushwa ya ngono

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Mtwara imemkamata ofisa Utumishi  wa Shirika la umeme Tanzania (Tanesco), Jumanne Songoro kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mtumishi mwenzake ili ampangie majukumu mengine ya kazi Katika kitengo cha kudumu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jumanne Julai 9, kamanda wa Takukuru mkoa wa mtwara Stephen Mafipa amesema afisa huyo amekamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa mlalamikaji na baada ya uchunguzi waliweka mtego na kufanikiwa Kimkamata mtuhumiwa.

Mafipa amesema katika mtego huo walifanikiwa kumkuta mlalamikaji akiwa na afisa huyo kwenye moja ya nyumba za wageni ambapo uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa alianza kushawishi rushwa ya ngono tangu Desemba 2018 hadi juni 4 mwaka huu ambapo mlalamikaji aliwasilisha malalamiko hayo Takukuru kwa lengo la kupata msaada.

“Kwa majibu wa mlalamikaji mtuhumiwa alitaka rushwa hiyo kutoka kwa mtmishi mwenzake ili ampangie majukumu mengine ya kazi Katika kitengo cha kudumu kulingana na kiwango cha elimu baada ya kubadilishiwa majukumu ya awali kufuata maagizo kutoka makao makuu ya Tanesco,” amesema Mafipa.

Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.


Share:

Mbunge atoa angalizo uuzaji wa mahindi Njombe

Na Amiri kilagalila-Njombe
Mbunge wa jimbo la Wanging’ombe mkoani Njombe mhandisi Gelson Lwenge ametoa wito kwa wananchi mkoani humo kuacha kuuza kiholela mazao ya chakula hususani mahindi ili kuondokana na balaa la Njaa litakaloweza kutokea kutokana na uuzaji holela wa zao hilo.

Lwenge amesema mwaka jana soko la mazao hususani mahindi lilikuwa limeyumba ukilinganisha na mwaka huu hivyo baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakiongezeka mkoani Njombe kufuata mahindi.

Mbunge huyo ametoa wito huo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lulanzi kilichopo Igima wilayani Wanging’ombe.

“Mwaka jana tumeyumba sana kwenye soko la mazao hasa mahindi lakini mwaka huu bei ni nzuri na inaendelea kupanda,maeneo mengine kwenye nchi hii hakuna mahindi ndio maana wote wanakimbilia Njombe, sasa nitoe angalizo tuwe waangalifu kwenye eneo la kuuza mahindi mwaka huu ili tusiwe na Njaa”alisema Lwenge

Kuhusu swala la Mbolea na pembejeo ambalo limelalamikiwa na wananchi wa kijiji hicho,Lwenge amesema serikali imejipanga kuleta bei ilekezi na naafuu badala ya kutoka kwa walanguzi ambapo walikuwa wakinufaika wachache.

Diwani wa kata ya Igima Paulina Samatta amesema zao la mahindi kwa kata hiyo limekuwa kubwa huku bei zikifikia shilingi 7000 kwa debe moja na kuungana na mbunge wa jimbo la Wanging’ombe kuhamasisha wananchi kuwa waangalifu katika biashara ya zao hilo la chakula.

“Mahindi katika kata yangu tumepata kwa wingi lakini bei pia zimefumuka,sasa hivi debe moja walanguzi wamepita wananunua mpaka shilingi 7000,na mimi ninahamasisha wananchi kutulia kwasababu kama tutauza mahindi yote tunaweza kuingia kwenye Njaa”alisema Samatta

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Lulanza akiwemo Fredy Kilasi na Blasto mpolya wamekiri kupanda bei kwa zao hilo na kuongezeka kwa wateja huku wakiahidi kutekeleza wito wa mbunge huyo.


Share:

Kunambi:Ujio Wa Dodoma Football Club Simba Na Yanga Wataisoma Namba.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Halmashauri ya jiji la Dodoma  imeichukua na kuanza kuimiliki rasmi timu ya Dodoma Football  Club  ambayo ilikuwa inamilikiwa na wananchi hapo awali.
 
Akizungumza na waandishi wa Habari jana Julai 9,2019  katika hafla fupi ya kumtambulisha kocha mpya  atakayekinoa kikosi hicho,mkurugenzi wa jiji hilo Godwin Kunambi amesema timu  Dodoma FC   itakuwa na umuhimu mkubwa katika jiji hilo ambapo jiji la Dodoma lipo tayari kuihudumua na kuigharamikia timu hiyo.
 
Kunambi amesema”lengo  kubwa ni kuwatanabaisha WanaDodoma na Watanzania kwa ujumla kuwa jiji la Dodoma limeichukua rasmi na kuimiliki timu ya Dodoma FC  ili iweze kupaa  kimataifa zaidi,Mpira ni taaluma kama taaluma  zingine na hatutaingilia masuala ya ufundi katika timu itakuwa na bodi yake ya wataalam na washauri kuhusu Masuala ya Soka”
 
Aidha ,Kunambi ameongeza”Kuhusu kuimarishwa na kuanza kusimamiwa timu ya Dodoma FC   kufika hadi ligi  kuu  na si ligi kuu tu mpaka Simba na Yanga wataisoma Namba tayari tumeshampata kocha Mbwana Makata  kwa mkataba wa mwaka mmoja “Alisema.
 
Naye Kocha atakayekinoa kikosi hicho Mbwana Makata amesema atajitahidi katika kuhakikisha Dodoma FC inasonga mbele katika Mafanikio ya Soka.
 
“Nina imani kubwa tutakuwa na ushirikiano katika kukuza vipaji vya soka  jiji la Dodoma,Bajeti  ipo ,nimefundisha zaidi ya timu 20 nimepandisha vilabu vinne Twiga Sports,Mji Mpwapwa,Alliance na JKT Oljoro kikubwa ni Ushirikiano”alisema.
 
Katibu  wa  timu ya Dodoma FC Fourtnastus  Johson  amesema watahakikisha wanaisimamia vyema timu hiyo huku  Bakari Fundikila  Diwani wa Chang’ombe akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa jiji hilo akisema uzalendo na ushirikiano ni nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu.
 
Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Dodoma Ester Bula amesema mchezo wa mpira wa Miguu unahitaji kuwa na kocha bora na wachezaji bora na ana mkakati wa kuanzisha timu ya  mpira wa Mguu ya wanawake  kwani kufanya hivyo inaweza kupatikana  vipaji ambao pia wanaweza kuchezea timu ya Taifa.
 
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe amesema jiji la Dodoma litakuwa kitovu cha wachezaji hivyo ni jambo la kila  mwanadodoma kuhakikisha anatoa Support  katika timu hiyo.


Share:

Serikali Yakaribisha Wawekezaji Wa Viwanda Vya Ngozi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Misri ikiwemo kampuni ya Cairo for Investment and Development inayoshughulika na usimamizi wa kiwanda cha ngozi waje kuwekeza nchini Tanzania.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Julai 9, 2019) alipotembelea kiwanda kikubwa cha ngozi cha Robbiki kilichoko katika mkoa wa Sharkianchini Misri, ambapo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao waje wawekeze nchini kwani kuna malighafi za kutosha.

Waziri Mkuu ambaje jana alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi nchini Misri alisema Tanzania inamifugo mingi hivyo inahitaji wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na mifugo hiyo ikiwemo ngozi.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeboresha mazingira ya biashara na ya uwekezaji pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo Tanzania ni mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kampuni ya Cairo for Investment and Development ya nchini Misri, ambayo inasimamia kiwanda cha ngozi cha Robbiki, Yasser Mohamed Ahmed Al Maghraby alisema kiwanda hicho kinauhitaji mkubwa wa ngozi kutoka Tanzania.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea mradi mkubwa wa mabwawa ya kufugia samaki, mradi wa upanuzi wa awamu ya pili ya mfereji wa suez canal, ambapo aliipongeza Serikali ya Misri kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha za ndani (Dola bilioni 8.2).

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Ziara Ya Rais Magufuli Namibia, Yawaibua Wawekezaji Katika Sekta Ya Mifugo Nchini

Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kufuatia ziara yake ya kikazi ya siku mbili aliyofanya nchini Namibia kuanzia Mei 27 hadi 28 Mwaka 2019, kuanza kuonesha mafanikio baada ya kupokea ugeni kutoka Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia iliyoonesha nia ya kuwekeza hapa nchini. 

Akizungumza (09.07.2019) ofisini kwake katika mji wa serikali eneo la Mtumba Jijini Dodoma na mmoja wa wakurugenzi katika kampuni hiyo Bw. Hendrick Boshoff, Prof. Gabriel amesema lengo la ziara yake ni kupata taarifa za awali, kutoka kwa wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili waweze kuwa na njia sahihi ya uwekezaji ambao utakuwa na tija kwa watanzania kupitia Sekta ya Mifugo.

“Mheshimiwa rais alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Namibia akiambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina na viongozi wengine, nichukue fursa hii kwa niaba ya wizara kumshukuru mheshimiwa rais kutuanzishia suala la soko la mazao ya mifugo hususan nyama, tumetembelewa na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia ili kukutana na wataalam baada ya rais kuonesha muelekeo na wao wakaitikia.” Amesema Prof. Gabriel

Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, amesema wameuhakikishia ugeni huo kutoka Namibia kuwa wizara iko tayari kupitia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kwa kuhakikisha nia ya kampuni hiyo kuanzisha kiwanda kingine cha kuchakata nyama hapa nchini inafikia katika utekelezaji kufuatia ziara ya mheshimiwa rais nchini Namibia.

Prof. Gabriel amefafanua kuwa ujio wa ugeni huo unaratibiwa na wizara nne zikiwemo za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo la Uwekezaji na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Sekta ya Mifugo ambapo Prof. Elisante Ole Gabriel ndiye Katibu Mkuu anayeshughulikia sekta hiyo na kwamba ameupokea ugeni wa mkurugenzi wa kampuni hiyo kutoka Namibia kwa niaba ya makatibu wakuu kutoka katika wizara nyingine tatu.

Aidha, ametoa wito kwa watanzania kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali hususan zinazolenga kuongeza masoko ya kutengeneza na kuuza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

“Viwanda kama hivi vikija ajira nyingi zitaongezeka na pia pato la taifa litaongezeka, bado tuko chini katika ulaji wa nyama takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) zinaonesha walau mtu wa kawaida anatakiwa kula kilogramu 50 kwa mwaka, bado kwa watanzania tunakula kilogram 15 kwa mwaka mzima, tunaleta wenzetu waongeze bidii katika hilo ili wazalishe na soko la ndani liwepo tuuze na nje ya nchi.” Alifafanua Prof. Gabriel

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia Bw. Hendrick Boshoff amwemambia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa, kampuni hiyo ilianza kuendesha shughuli zake miaka 40 iliyopita na  wamekuja nchini Tanzania wakilenga zaidi uwekezaji wa kuyaongezea thamani mazao ya mifugo hususan nyama.

Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo na Kati (DSME) Dkt. Consolata Ishebabi, amesema ugeni huo utafahamishwa pia fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) ili kufahamu mazingira mbalimbali ya uwekezaji yakiwemo ya sekta binafsi.

Aidha, Dkt. Ishebabi amefafanua kuwa ugeni huo utafikishwa pia katika Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) ambapo watafikishwa katika Ranchi ya Kongwa ambayo ipo chini ya NARCO kuweza kuona aina ya mifugo iliyopo nchini na waweze kupata taarifa za jumla ambazo zitawapatia mwanzo mzuri wa kuwekeza hapa nchini katika Sekta ya Mifugo.

Kikao hicho kiliwahusisha wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mwisho.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger