Tuesday, 9 July 2019

Rais Magufuli Aitaka Wizara ya Maliasili Iweke a mikakati kuongeza watalii

Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza watalii nchini ambao ametaja baadhi ya malalamiko ambayo amekuwa akiyapata kupitia ripoti ya robo mwaka na kiitaka wizara hiyo kuhakikisha inafanya kazi masuala hayo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 9, wilayani Chato mkoani Geita katika uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,702.

“Ninatoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kujipanga na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza watalii nchini, miongozi mwa malalamiko ambayo nimekuwa nikiyapata ni pamoja na gharama za utalii kuwa juu, usafi kwenye hoteli na mengine mengi hivyo hamna budi kufuatilia mambo hayo,” amesema.

“Ninawasihi kuwa na utaratibu wa kufanya kaguzi mara kwa mara lakini pia wekeni mikakati ya kujenga uwezo wa waongoza watalii na kuhakikisha wote wanatambuliwa rasmi maana kuna wengine wanadanganya watalii, hakikisheni hifadhi zetu zinakuwa na mchanganyiko mzuri wa vivutio,” amesema.

Aidha amewataka watanzania kujega utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani hasa katika maeneo ya hifadhi zinazowazunguka ili kuiongezea nchi kipato na kukuza uchumi wa nchi ambapo ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka gharama nafuu kwa watalii wa ndani ili kuwezesha zoezi hilo.

“Ninahimiza Wizara kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani ikiwemo kwa kuweka gharama za nafuu pia kwa watanzania ninawasihi kujenga utamaduni wa kutembelea vituo vyetu vya utalii pia tuanzisha hifadhi ndogo ndogo za kufuga wanyama pori,” amesema.

“Mimi ninafikiria kuanzisha hifadhi ndogo lakini nitafuga wale wanyama ambao ni wapole nisije nikajikuta nimekuwa kitoweo huko ndani, ninasisitiza Wizara hakikisheni mnaangalia gharama kwa wazawa zinakuwa chache,” amesema.


Share:

Mwakyembe Atoa Onyo Kwa Wanaosambaza Picha za Ajali Mitandaoni

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewaonya watu wanaopiga picha kwa simu mara tu zinapotokea ajali na kusambaza mitandaoni.

Mwakyembe ametoa onyo hilo leo Jumanne Julai 9, wakati wa shughuli ya kuaga miili ya wafanyakazi wa Azam Media waliofariki jana Julai 8, katika ajali ya gari kati ya Shelui na Igunga na kuongeza kuwa Sheria ya Makosa ya Mitandao inazuia kufanya hivyo.

"Niwaombe Watanzania tuendeleze utamaduni wa utu ndugu zetu wanapopata ajali, niwaombeni acheni tabia ya kupiga picha na kurusha kwenye mitandao, sheria ya mitandao inakataza, hatutazungumza tena hili ni onyo la mwisho" - Waziri Mwakyembe


Share:

Rais Magufuli .Ampongeza Faru Rajabu

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amempongeza faru Rajabu, ambaye ni mtoto wa Faru John, kwa juhudi zake za uzalishaji na kuzidi kuongeza idadi ya faru hadi kufikia faru140, katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Julai 9, wakati wa Uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi, iliyopatikana mara baada ya mapori matatu ya akiba kuunganishwa, likiwemo pori la Burigi, Biharamulo na Kimisi Wilayani Chato Mkoani Geita.



"Mwaka 2014 kulikuwa kuna tembo 43,330 lakini hivi sasa baada ya kuanzisha kikosi cha kupambana na ujangili wamefikia zaidi ya 60,000 faru hawakuwepo kabisa ila sasa wamefikia 163 ", amesema Magufuli.
 
''Hakuna budi kupongeza kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na faru rajabu, mtoto wa faru John naambiwa kwasasa amezalisha watoto 40, nadhani wajina wangu john alikuwa hajitumi vizuri'


Share:

Iran Yasema Italipa Kisasi kwa Uingereza

Mnadhimu mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini Iran Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesema leo kwamba, hatua ya Uingereza kuikamata meli yake ya mafuta nje ya eneo la Gibraltar haitapita bila majibu. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim Bagheri amesema kukamatwa kwa meli hiyo ya mafuta ya Iran chini ya misingi ya visingizio vya kutengenezwa, hakuta pita bila kujibiwa na itakapolazimika Tehran itatoa jibu sahihi. 

Jeshi la majini la Uingereza liliingia katika meli hiyo, Grace 1, nje ya pwani ya Gibraltar siku ya Alhamis na kuikamata kuhusiana na shutuma kwamba inavunja vikwazo kwa kupeleka mafuta nchini Syria. 

Iran imetaka kuachiwa mara moja kwa meli hiyo ya mafuta, wakati kamanda huyo wa jeshi la mapinduzi la Iran ametishia siku ya Ijumaa kukamata meli za Uingereza kwa kulipa kisasi.


Share:

RAIS MAGUFULI AMPONDA KIAINA WA JINA WAKE 'JOHN' KWA UZEMBE KUZALISHA

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema tangu kuanzishwa kwa kikosi kazi cha kupambana na ujangili mwaka 2016 idadi ya wanyama hapa nchini imeongezeka.

Magufuli amesema hayo leo Jumanne Julai 9 mwaka 2019 wakati wa uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato mkoani Geita.

"Mwaka 2014 kulikuwa kuna tembo 43,330 lakini hivi sasa baada ya kuanzisha kikosi cha kupambana na ujangili wamefikia zaidi ya 60,000 faru hawakuwepo kabisa ila sasa wamefikia 163 hatuna budi kumshukuru Faru Rajabu mtoto wa Faru John," amesema Magufuli.

"Inaonekana yule Faru wajina wangu (John alikuwa hajitumi vizuri) huyu mtoto wake nimeambiwa mpaka sasa amekwisha zalisha 43," amesema Rais Magufuli huku akitabasamu.
Na Ephrahim Bahemu, Mwananchi
Share:

Waziri Lugola aagiza Polisi kuwakamata wanaowapa mimba Wanafunzi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amelitaka Jeshi la Polisi  wilayani Bunda, mkoani Mara, kuwakamata wazazi wanaowatumia wanafunzi katika shughuli za kilimo na mifugo na kuwasababishia kukatisha masomo yao.

Pia Waziri Lugola amewaagiza Polisi hao kuwakamata watu wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kuwasababishia kukatisha masomo kwa kuwapa mimba.

Waziri Lugola, ametoa kauli hiyo akiwa wilayani Bunda katika  ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake la Mwibara, ambapo amesema kuwa lazima Watoto waendelezwe kielimu ili iwaletee manufaa kwao na kwa taifa.

“Nina taarifa baadhi ya wazazi uwatumikisha Watoto wao kufanya shughuli za kilimo, kulima dengu, pamoja na kuwatumia katika kuchunga mifugo, hii haikubaliki, wazazi lazima muwajibike kwa kutowatendea vema watoto,” alisema Lugola na kufafanua;

“Kuvunja sheria za nchi kwa kutompa elimu mtoto ni kosa, hivyo, wazazi wanaotumikisha Watoto shughuli za uchumi wa wazazi hao,hakika tutawakamata, OCD (Kamanda wa Polisi Wilaya), akikisheni mnawakamata wazazi ambao wanawatumia Watoto katika shughuli zao binafsi na pia kusababisha utoro katika shule zetu.”

Pia Lugola aliwahoji wanafunzi wa Shule ya Msingi Karukekere, Kata ya Namuhura, Wilayani humo, kuwa wanataka Serikali iwafanyie nini wazazi wao ambao wanawakatisha masomo, hata hivyo,wanafunzi hao walisema wazazi wao washitakiwa kwa kutowapa haki zao za msingi.

Alisema ili kupunguza utoro ndani ya Jimbo hilo, aliwataka wazazi kufuatilia elimu ya watoto wao, kwa kuhakikishe wanakua na daftari ambalo wanafunzi hao wataenda nalo shuleni, na Mwalimu atasaini baada ya mwanafunzi huo kufika shuleni na pia atasaini kabla ya muda wa kuruhusiwa kwenda nyumbani, hatua hiyo itapunguza zaidi utoro katika jimbo lake.


Share:

Taasisi Za Kidini Na Jumuiza Kijamii Katika Mikoa Ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa Na Songwe Kuhakikiwa Kuanzia Tarehe 15 Julai, 2019




Share:

Tanzania Kuendelea Kunufaika Kiuchumi na SADC

Na Frank  Mvungi- MAELEZO- Morogoro
Katibu Mkuu Mstaafu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Mussa Uledi amesema kuwa Tanzania inanufaika kiuchumi  kama mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na jumuiya nyingine ambazo Tanzania ni mwanachama.
 
Akizungumza wakati akiwasilisha mada leo mjini Morogoro ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo  kwa waandishi  wa habari ya kuwajengea uwezo wa kuandika na  kuripoti   habari za SADC, Bw. Uledi amesema kuwa  nchi yetu imenufaika na utekelezaji wa miradi ya miundomnbinu,  biashara, uwekezaji  na viwanda.
 
“ Mkakati wa maendeleo wa SADC unafafanana kwa kiwango kikubwa na ule wa Tanzania ambao pia unazingatia haja ya utekelezaji wa viwanda na miundombinu hapa nchini hali itakayochangia katika kuimarisha maendeleo na kukuza uchuni na ustawi wa wananchi” Alisisitiza Bw. Uledi
 
Akifafanua amesema kuwa vipaumbele vya Tanzania vimejikita katika upanuzi wa Mauzo nje na uongezaji wa michepuo yake lengo likiwa ni kukuza na kuendeleza biashara hali inayowezesha uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani katika malighafi za ndani hususan mazao ya kilimo na madini.
 
Aliongeza kuwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli  katika baadhi ya nchi wanachama wa SADC imeonesha kuwa Tanzania imejipanga vizuri kimkakati inaweza kuwa ghala la Chakula kwa kukuza zaidi uzalishaji kuendana na mahitaji katika soko la jumuiya hiyo na hata nje ya jumuiya.
 
 Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na  uendelezaji miundombinu kama barabara, reli, usafiri wa anga, uzalishaji na usambazaji huduma za umeme ambayo ni nyenzo muhimu sana katika kuyaunganisha masoko ya nchi wanachama wa SADC.
 
Aliongeza kuwa vipaumbele vingine ni utafutaji wa rasilimali na utekelezaji wa miradi ya Kikanda kwa kuundwa kwa kikosi kazi cha Mawaziri wenye dhamana ya Fedha na uendelezaji miundombinu, Amani na Usalama umeendelea kuimarika ndani ya SADC.
 
Tanzania inatarajiwa kuleta msukumo mpya kwa nchi wanachama wa SADC katika utekelezaji wa miradi na program za maendeleo za Jumuiya hiyo kwa kuwa itakuwa na dhamana kubwa ya kukidhi matarajio makubwa ya nchi wanachama wakati wote wa uenyekiti wake.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Brigedi ya Magharibi ya Jeshi  la Ulinzi la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  Kanali Wilbert  Ibuge akiwasilisha mada katika mafunzo hayo amesema kuwa  Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa Barani Afrika zilizotoa mchango mkubwa na kuratibu kuanzishwa kwa mtangamano wa  SADC.
 
“Hadi sasa hali ya amani na usalama imeendelea kuimarika katika SADC kama inavyojidhihirisha kwa takribani nchi zote za SADC  ambapo nchi wanachama ziliazimia kusimamia maendeleo ya kiuchumi ya Kanda kwa kuzingatia malengo ikiwemo kukuza uchumi, kuondoa umasikini, kuboresha hali ya maisha ya wananchi.
 
Msingi wa SADC ni kusimamia malengo yake ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na yale ya ulinzi na usalama unabainishwa katika Ibara ya 2 ya mkataba wa SADC ( Article 2 of SADC Treaty).


Share:

TARURA Kuanza Kutumia Mfumo Mpya Wa Malipo Serikalini

Na. Geofrey Kazaula, TARURA, Morogoro
Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) umeanzishwa na wataalamu wa ndani ili kuunganisha mifumo mingine iliyopo, lengo likiwa ni kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za fedha.

Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Francis Mwakapalila, ambaye alikuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mafunzo ya Mfumo wa Ulipaji Serikalini- MUSE kwa wahasibu na wahandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA mkoani Morogoro.

Bwana Mwakapalila alisema kuwa mfumo huo umetengenezwa na wataalam wa ndani kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na utaanza kutumiwa na TARURA kisha kutumiwa na Taasisi zote za Serikali pamoja na Wizara baada ya kujiridhisha na ufanisi wake.

 “Nitoe wito kwa washiriki wote wa mafunzo haya kuhakikisha wanauelewa vizuri mfumo na kuwa tayari kuutumia mara tu baada ya mafunzo kukamilika kwa kuwa mfumo huu ni muhimu kutoka na mabadiliko ya teknolojia katika mifumo ya fedha duniani”, alisema Bw. Mwakapalila .

Naye Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amewataka wataalam wa Wakala huo wanaoshiriki mafunzo, kutokuwa na mtazamo hasi kuhusu mfumo na badala yake changamoto watakazo kutana nazo waziwasilishe mahali husika ili kuweza kutafutiwa ufumbuzi kwa kuwa mfumo huo ndio suluhisho la matumizi bora ya fedha za Serikali.

Aidha ameeleza kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imetoa wataalam wa kutosha ili kuhakikisha wahasibu wote wa TARURA wanapatiwa mafunzo na kuuelewa mfumo kwa kina.

Kwaupande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, alieleza kuwa mfumo huo utaiwezesha Serikali kuangalia malipo yanayofanyika Katika Taasisi, Kampuni na wadau wengine wanaotoa huduma Serikalini .

Alisema kuwa mfumo huo ulianza baada ya kukusanya mahitaji kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi Ishirini za Serikali na kwamba Taasisi ya TARURA itakuwa ya kwanza kutumia mfumo huo kupitia wahasibu wake na wahandisi watakao kuwa wakiidhinisha malipo.

Bwana Sausi, alisema mafunzo hayo yanawahusisha wahasibu na wahandisi wa TARURA nchi nzima kuanzia ngazi ya Halmashauri lengo likiwa ni kumwezesha Mtendaji Mkuu wa TARURA kuona malipo yote yanayofanyika na Wakala huo katika sehemu mbalimbali kwa wakati.

Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikitumia Mifumo ya Fedha tangu miaka ya Sitini na kutokana na ukuaji wa teknolojia imeamua kufanya maboresho ya mifumo hiyo ili kuendana na mahitaji ya sasa na kurahisisha kupata hesabu sahihi za fedha kwa wakati.

Mwisho


Share:

Katazo La Mifuko Ya Plastiki Nchini Limesaidia Kuweka Mazingira Safi.

Na Faidha Jumanne-Maelezo.
Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya mazingira imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa mifuko bora mbadala kwa wananchi. 

Hii imetokama na jitihada za serikali za kupiga marufuku mifuko hiyo, kuanzia tarehe 01 Juni 2019 na kupelekea kupatikana kwa mifuko mbadala,  kwa wananchi inayoimarisha afya zao kuongeza ajira na kupunguza uchafuzi wa mazingira. 

Akihojiwa na Idara ya Habari - MAELEZO, Afisa Habari Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Lulu Musa, alianza kusifia juhudi zilizopatikana kwa muda mfupi, huku akirejea Siku ya Maazimisho ya Usafi Kitaifa Jijini Dodoma, yaliyofanyika Juni 5, 2019. 

``Tumetoa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa wananchi, kazi hii inafanywa na Halmashauri za Serikali za Mitaa- TAMISEMI kwa kusimamia maeneo yao kwa kutotumia mifuko ya plastiki hakika wanastahili pongezi, nasema hongereni sana”. 

Uamuzi wa Serikali kuhusu kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki lengo lake ni kuboresha usafi wa mazingira na kuwaweka wananchi katika hali ya kuepuka magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara damu. 

“Lengo ni kuimarisha afya.  Kadhalika, mazingira salama ambapo, sote tunatambua umuhimu wa mtu kuwa na mazingira mazuri na yenye usalama kiafya kwa kushiriki katika shughuli za kijamii na za kitaifa”. Amesisitiza Lulu. 

Ameongeza  serikali itaendelea kuwa macho kufuatilia mwitikio mzuri wa wananchi kutoendelea kutumia mifuko ya plastiki, na kutotegemea watu wengine kusimamia mazingira ya Watanzania, kadhalika akasema bali iwe ni zoezi la kawaida kwa wananchi.  

Lulu akazidi kufafanua kuwa, serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutunza mazingira kwa lengo  la kuboresha afya zao na kufahamu kwa kina mifuko ya plastiki kwa kiasi gani imeleta madhara na kusababisha magonjwa ya aina mbalimbali yakiwemo nyemelezi,  kuteketeza uhai wa viumbe kama vile samaki na mifugo. 

Aidha, Tanzania ni nchi miongoni mwa nchi zilizoonekana katika orodha ya matumii makubwa ya mifuko uya plastiki. Hii ilitokana na kuongezeka kwa kasi kwa matumizi hayo kadiri siku zilivyozidi kwenda, amesema Lulu.  

Imeelezwa pia, Serikali kwa kushilikiana na wadau kama Shirika la Viwango Tanzania -TBS limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwenye sekta ya afya na mazingira yenye lengo la kuboresha matumizi ya mifuko mbadala na kuimalisha afya za wananchi. 

Mfano, TBS imeweka viwango vya ujazo kwenye mifuko ya plastiki ambayo bado inatumika kama vifungashio kuepusha kuzagaa kwa mifuko ya plastiki na kusababisha uchafuzi wa mazingira. Pia, imebainisha  viwango vya mifuko ambayo imeruhusiwa kwa kutumika kwa kufungashia chakula pamoja na madawa ya kilimo kwa kuangalia uzito/ujazo wa bidhaa, aina za bidhaa ambazo zitatumia mifuko hiyo ili kuweza kusaidia katika utunzaji wa mazingira. 

Vilevile,  Lulu aliongezea kuwa shirika la viwango, TBS litakua na uwezo wa kuwasiliana na wananchi kwa njia yoyote ile hata ikiwa kimtandao kwa kuwapa taarifa ya matumizi ya mifuko iliyo bora na yenye viwango  ili kuweza kusaidia kutoa huduma bora kwa wanainchi. 

Akielezea mfumo wa matumizi ya kidigitali Lulu amesema kuwa, Tanzania ilishaingia mfumo wa matumizi ya kidigitali katika utoaji huduma kwenye maeneo mengi, na imekuwa msaada mkubwa katika shirika la viwango TBS. 

Hata hivyo Tanzania imekua na matumizi mazuri ya mfumo wa kidigitali kwa kutoa mawasiliano kwa wananchi katika mambo mbalimbali ya kijamii na kuleta mafanikio chanya katika mwitikio wa jambo kama hili la katazo ya mifuko ya pllastiki, Lulu akasema, “Kupitia mfumo huu wa kutoa mawasiliano katika mitandao ya kijamii utasaidia kuongeza uwingi wa watu katika kupata taarifa kwa uharaka na sisi kutupelekea ufanyaji kazi wetu kutoa taarifa haraka kwa umma”.
`` … tutaendelea kuwa na utaalamu wa hali ya juu kwa kuhakikisha taarifa tutakazo zitoa zitakuwa taarifa sahihi zenye viwango sahihi kwa kutoa msaada mkubwa sana kwa kuwa hizi taarifa ni za muhimu sana kwa wananchi’’.   

Akiongea mmoja wa wananchi waliohojiwa,  Hashim Chikwaya ambaye ni mkulima amesema, “  Kutokana na kusitishwa  kwa mifuko ya plasiki,  hakika hili ni jambo jema sana kwa wananchi kwa kuwa wananchi walikuwa wakitumia mifuko hiyo kwa kuhifadhia chakula ambacho chakula hicho ni chenye joto” alisema Chikwaya.  

Akaendelea Chikwaya ambaye anaonekana kuwa na uzoefu wa kujua athari za mifuko, kuwa Kutokana na joto la kwenye mfuko linasababisha kutoa mvuke wenye majimaji ya tindikali ambayo imetumika kutengenezea mfuko huo na kuingia kwenye chakula, iwapo chakula hicho kikiliwa na mtu, hupata athari kubwa za kiafya.   

Vilevile, akielezea zaidi adhari za kiafya Chikwaya alisema “Kulikuwa na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima pale mtu anapochukua mfuko wa plastiki kwa matumizi ya kuwashia moto, hususani jiko la mkaa, kitendo hicho kinapofanyika mtu huyo anavuta hewa ya mfuko unaoyeyuka na kumsababishia madhara ya kupata ugonjwa wa kansa”. 

Akimalizia, Chikwaya alisema, mbali na uchafuzi wa mazingira mara nyingi, mfano hospitali madaktari walikuwa wakishauri kuepukana na matumizi ya vifaa vya plastiki kuhifadhia chakula chenye joto na kusema kuwa plastiki hizo huchubuka zipatapo joto na kusababisha athari ya upatikanaji wa magojwa pinde ulapo chakula hicho, akaongeza, “hata hivyo si rahisi kuona michubuko hiyo kwa macho”.  

Zoezi la katazo la Mifuko ya Plastiki limeanza Juni mosi, 2019 ambapo mpaka sasa kwa tafiti imeonyesha mafanikio, mfano katika Jiji la Dar-es-salaam wengi waliohojiwa mitaa ya Kariakoo wamesema mitaa yao inaonekana safi kwa kuondolewa mifuko hiyo na hivyo wanaishukulu serikali.      


Share:

UWT MANISPAA YA IRINGA WANAWAKE KOPENI KWA MALENGO


Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Manispaa ya Iringa (UWT) Ashura Jongo akizungumza wakati wa baraza la UWT manispaa ya Iringa akiwaasa wanawake kukopa kwa malengo.

Mwenyekiti wa CCM manispaa ya Iringa Said Rubeya akitoa neno kwa wanawake wa UWT manispaa ya Iringa. 


Na Fredy Mgunda,Iringa. 

Kukosekana kwa elimu ya matumizi bora ya mikopo kwa wanawake kumetajwa kuwa sababu ya wanawake wengi wa manispaa ya Iringa kushindwa kurudisha mikopo katika taasisi za kifedha.

Akizungumza kwenye baraza la UWT manispaa ya Iringa,mwenyekiti wa umoja huo Ashura Jongo  amesema kuwa wananwake wamekuwa wanakopa bila ya kuwa na elimu ndio maana wanashindwa kurejesha mikopo ambayo wamekopa kwenye taasisi za kifedha.

“Changamoto za wanawake kutokuaminika katika vyombo au taasisi za kifedha ni kutokana na hali ngumu,wanawake wanaweza wakakopa wakiwa na malengo lakini wakirudi nyumbani wanakutana na matatizo mengi yanahitaji matumizi ya fedha” aliema Jongo

Jongo alisema kuwa wanawake wanatakiwa kuendelea kuwawezesha kwa kuwa wanauwezo wa kutmia vizuri fedha ambazo zinapatikana hivyo ukimuwezesha mwanamke umewawezesha watu wengi kwa kuwa wanawake ndio nguzo ya familia hasa kwenye maswala ya kiuchumi.

Kwa upande wake mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi Rose Tweve amezitaka taasisi za kifedha kutoa elimu kwa wakopaji ili waweze kuzitumia vizuri fedha hizo.
“Shida moja wapo ya wanawake kushindwa kurudisha mikopo ni kutokana na kutokuwa naelimu ya matumizi ya fedha kwa kuwa pesa hiyo inahitaji nidhamu na matumizi bora ya fedha hizo za mikopo” alisema Tweve

Tweve alisema kuwa tasisi za kifedha zinatakiwa kutoa elimu kwanza kabla ya kutoa mikopo kwa wanawake ili waweze kuzirejesha kwa wakati kwa kuwa tayari ameshapata elimu ya matuzi bora ya mikopo waliyokopa.

“Pale wanapokopa lazima wajue matumizi ya hizo pesa la sivyo watazitumia bila nidhamu fedha hizo na kushindwa kuzirejesha na kujikuta wakiwa matatani kutokana na kushindwa kulipa mkopo huo” alisema Tweve

Naye mgeni rasmi kwenye baraza hilo mwenyekiti wa CCM manispaa ya Iringa Said Rubeya amewataka wanawake kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha ili kufikia malengo waliyojiwekea kabla ya kwenda kukopa.

“Kwa kwali wanawake wa CCM manispaa ya Iringa wengi mnakopa mikopo lakini hamrejeshi kwa wakati na hili ni bomu kubwa kwa chama hivyo mnatakiwa kuwa na nidhamu ya matumizi ya mikopo hiyo” alisema Rubeya
Share:

Live : RAIS MAGUFULI ANAZINDUA HIFADHI MPYA YA TAIFA YA BURIGI CHATO

LIVE:Rais Magufuli anazindua Hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi Chato


Share:

Upandaji holela wa miti katika njia za umeme Kahama watajwa kusababisha nishati ya umeme kukatika.

NA SALVATORI NTANDU
Upandaji holela wa miti katika njia kuu za Umeme Wilayani kahama mkoani Shinyanga umetajwa kuchangia kusababisha Nishati hiyo kukatika mara kwa mara kutoka na miti hiyo kugusa nyanya za Umeme.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Kahama Mhandisi King Fokanya wakati akizungumza na waandishii wa habari ofini kwake kuhusiana namna walivyojipanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa miundombinu ya umeme.

Amesema katika maeneo mengi wilayani humu wananchi wamepanda miti mikubwa katika karibu na nguzo za umeme jambo ambalo linaweza kuleta madhara makubwa pindi nguzo zinapo anguka ama kuguswa na miti hiyo.

Amefafanua kuwa pindi Shirika hilo linapotaka kuikata baadhi yao wamekuwa wakilaumu juu ya ukataji wa miti hiyo katika njia za umeme na watumishi wake katika oparesheni za kuhakikisha miundombinu hiyo inakuwa salama.

Katika Hatua nyingine Mhandisi Fokanya amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 Ofisi yake imepokea shilingi milioni 847 kwa ajili ya kupeleka huduma ya nishati ya umeme kwenye kata 10 ambazo hazina umeme zilizopo Halmashauri ya Mji wa Kahama na Msalala.

Amefafanua kuwa  shilingi Milioni 847 zimegawanya katika makundi mawili ambapo shilingi milioni 402 zitatumika kupeleka huduma ya nishati ya umeme kwenye kata 10 msalala na kahama mjini huku Milioni 445 zinatumika kwenye mategenezo ya kubadilisha nguzo,vikombe, maboresho ya Transfoma na vifaa vilivyoharibika.

Kata ambazo zinapelekewa huduma hiyo ni pamoja  kata ya Muhungula, Nyakato, Mbulu, Mhongolo, Nyashimbi, Nyihogo sekondari, Kagongwa, Mwendakulima Isaka na Kakola.

Mwisho.


Share:

Makamu Wa Rais Mhe. Samia Ahudhiria Mkutano Wa 12 Wa Dharura Wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kuhusu Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,  ameshiriki katika Mkutano wa 12 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) unaofanyika jijini Niamey nchini Niger.
 
Makamu wa Rais Mhe. Samia ameipongeza Serikali ya Ghana kwa kuchaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya AfCFTA na kuisihi Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuharakisha ukamilishaji wa muundo, wa bajeti na mpango kazi  wa Sekretarieti hiyo ili ianze kufanya kazi haraka.
 
Mkutano huo wa Wakuu wa nchi na Serikali umepokea taarifa ya Mheshimiwa Mahamadou Issoufou, Rais wa Jamhuri ya Niger kuhusu utekelezaji wa AfCFTA ambayo imepokelewa na kupishwa na viongozi hao. Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) umeanza kazi rasmi tarehe 30 Mei, 2019 na unahusu uasili wa bidhaa zitakazouzwa katika soko la Afrika, kufungua biashara ya bidhaa kwa asilimia 97 na uanzishwaji wa Sekretarieti ya kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA.
 
Aidha, alimpongeza Mheshimiwa Mahamadou Issoufou, Rais wa Jamhuri ya Niger kwa jitihada zake za kuhakikisha azma ya Umoja wa Afrika ya kuanzisha Soko Huru la pamoja la Afrika inafikiwa. 

Makamu wa Rais pia alizipongeza nchi 27 wanachama wa Umoja huo zilizoridhia mkataba wa uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kati ya nchi 54 zilizotia saini mkataba huo na kuahidi kwamba Tanzania itaungana nao baada ya kukamilisha taratibu za ndani.
 
Kwenye mkutano huo Makamu wa Rais amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo alitoa salam za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wakuu wa Nchi na Serikali waliohudhuria mkutano huo.
 
Wakati huo huo Waziri wa Fedha na Uchumi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa amesema kwa upande wa Afrika Mashariki  Tanzania imepiga hatua zaidi kutokana na kuwepo katika Jumuiya za Afrika Mashariki na SADC, hivyo Tanzania imefaidika sana kutokana na kupanuka kwa Soko hilo.
 
Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiao wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro amesema Tanzania imenufaika na mkutano huo kutokana na kuendelea kujifunza zaidi kuhusiana na Biashara ya pamoja katika Afrika pamoja na kuweza kushiriki kuchagua Muwakilishi wa Bara la Afrika katika nafasi mbalimbali ndani ya Afrika na Duniani kote wakati Tanzania imepata nafasi moja ambapo Bethabina Seja Afisa wa Takukuru amechaguliwa katika Bodi ya kudhibiti Rushwa Barani Afrika.


Share:

Bunge la Tanzania kuwa mwenyeji wa vikao vya Kamati ya Uongozi na ya Bajeti za Chama cha Wabunge wa Nchi za Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika

Bunge la Tanzania linatarajia kuwa mwenyeji wa vikao vya Kamati ya Uongozi na ya Bajeti za Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika (CPA-AFRICA REGION) vitakavyofanyika tarehe 9 hadi 14, Julai, 2019 katika Ofisi Ndogo za Bunge la Tanzania, Jijini Dar es Salaam.

Kamati hizo zitakutanisha Wajumbe kutoka Mabunge zaidi ya Kumi (10) ya nchi za Afrika ambapo mbali na Wajumbe hao vikao hivyo pia vinatarajiwa kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Kenya Mhe. Justin Muturi, Spika wa Bunge la Sierra Leone Mhe. Dkt. Abbas Bundu, Spika wa Bunge la Uganda Mhe. Rebbeca Kadaga na Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai ambaye ndiye mwenyeji wao.
 
Aidha, mbali na Maspika hao, vikao hivyo vitahudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge la Cameroon Mhe. Emilia Lifaka, Naibu Spika wa Bunge la Namibia, Mhe. Bernard Sibalatani na pia Mnadhimu Mkuu wa Bunge la Ghana Mhe. Dkt. Osei Mensah Bonsu.
 
Mbali na vikao vya Kamati, kutakuwa pia na kikao cha Bodi ya Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola-Kanda ya Afrika ambacho kitafanyika tarehe 11 Julai, 2019.
 
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai anatarajiwa kuhudhuria na kuongoza kikao cha Bodi ya Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika na pia kutoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Uongozi wa chama hicho.
 
Wajumbe wengine ambao ni Waheshimiwa Wabunge wanaotarajiwa kuhudhuria katika vikao hivyo wanatoka katika Mabunge ya nchi za Malawi, Kenya, Nigeria, Ghana, Sierra Leone, Afrika kusini, Uganda, Namibia, Zambia, Lesotho, Mauritius na wenyeji Tanzania. Kwa hivi sasa Bunge la Tanzania ndiyo Sekretarieti ya Chama Chama cha Wabunge wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola–Kanda ya Afrika.
 
Imetolewa na;
KATIBU WA CPA-KANDA YA AFRIKA
8 Julai, 2019


Share:

TETESI ZA SOKA ULAYA JUMANNE


Atletico Madrid imeanzisha mchakato wa kumuadhibu mshambuliaji wa Ufaransa Antoine Griezmann, 28, ambaye anatarajiwa kuhamia Barcelona kwa dau la £107.5m . (Guardian)

Real Madrid inafikiri kumuuza mshambuliaji wake raia wa Colombia James Rodriguez, 27, ili kukusanya £150m kumnunua kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba, 26. (Mail)

Napoli ina hamu ya kumsaini James kutoka Real Madrid, pamoja na mshambuliaji wa Argentina na Inter Milan Mauro Icardi, 26. (Goal.com)

Bayern Munich inataraji winga wa Ujerumani Leroy Sane, 23, kuamua wiki ijayo iwapo anataka kujiunga na mibabe hao wa Ujerumani kutoka Manchester City. (Mail)

Arsenal, Manchester United na Paris St-Germain wana hamu ya kumsaini kiungo wa kati wa Ufaransa Tiemoue Bakayoko, 24, kutoka Chelsea. (RMC Sport - in French)

West Ham wanafikiria kulipa dau la £43.5m na kuishinda Valencia ili kumsajili mshambuliaji wa Celta Vigo na Uruguay 22. (Evening Standard)

Mshambuliaji wa Manchester United na Ubelgiji Romelu Lukaku, 26, anatumai kuwa mchezaji wa Inter Milan kufikia wakati ambapo ataikabilia Man United tarehe 20 mwezi Julai.. (Mirror)

Aston Villa wamewasilisha ofa ya dau la £7m kumnunua kipa wa Burnley na Uingereza Tom Heaton, 33. (Sun)

Arsenal inakaribia kumsajili beki wa Saint-Etienne William Saliba, huku mchezaji huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 8 akidaiwa kugharimu £25m. (Evening Standard)

Beki wa kushoto wa Liverpool, 27, raia wa Uhispania Alberto Moreno anakaribia kuhamia Villarreal. (ESPN)
Gareth Bale alikuwepo wakati wachezaji wa Real Madrid waliporudi katika maandalizi ya msimu mpya siku ya Jumatatu , baada ya wachache kutomtarajia mshambuliaji huyo katika timu hiyo. (Marca)

Manchester City inakaribia kumsaini kinda wa Uingereza anayechezea timu ya Uingereza ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 Morgan Rogers kutoka West Brom, (Mail)

Everton inakaribia kuwasilisha ofa ya dau la £35m kumnunua mshambuliaji wa Barcelona na Brazil Malcom.
Arsenal pia inamnyatia mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23. (RMC Sport - in French)

Watford ina hamu ya kumsajili winga wa Ufaransa Allan Saint-Maximin, 22, kutoka klabu ya Nice kwa dau la rekodi la £25m. (Sky Sports)

Aston Villa ina hamu ya kusalia kwa mkopo beki wa Man United Axel Tuanzebe baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 kuhudumu msimu wake uliopita akichezea klabu hiyo. (Telegraph)

CHANZO.BBC SWAHILI
Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne 9 July























Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger