Thursday, 6 June 2019

Mama Maria Nyerere alazwa hospitali baada ya kuugua ghafla akiwa Uganda

Mke wa baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amelazwa katika Hospitali jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili nchini jana Jumatano Juni 5, 2019 akitokea Kampala Uganda alipokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.

Mtoto wake Makongoro Nyerere amesema, baada ya kuwasili nchini mama yake alipumzishwa kwa muda wakati madaktari wakiendelea na uchunguzi kabla ya kufikia uamuzi wa kumlaza.

Makongoro alisema alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam akitokea Kampala nchini Uganda alikokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.
 
Mama Maria Nyerere alikuwa nchini Uganda kwa ajili ya ibada maalum ya kukumbuka mchango wa hayati Mwalimu juliasi Nyerere kwa Afrika na Ukristo.

Tangu mwaka 2009, waumini wa kanisa katoliki wamekuwa wakifanya ibada katika hekalu la Namugongo kwa ajili ya kumkumbuka mwalimu Nyerere.

Nyerere alitoa mchango mkubwa sana kwa ajili ya kuung'oa madarakani utawala wa rais Idi Amin..


Share:

Rais Magufuli Kukutana na Wafanyabiashara Watano Kutoka Kila Wilaya Kesho Ijumaa

Rais wa Tanzania, John Magufuli kesho Ijumaa Juni 7, 2019 atakutana na wafanyabiashara watano kutoka kila Wilaya kujadili mambo mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Juni 6, 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema mkutano huo utafanyikia Ikulu kuanzia saa 3.30 asubuhi.

Msigwa amesema wafanyabiashara hao watawawakilisha wenzao ambapo wataambatana na wajumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC).

“Mkutano huu utaanza saa 3:30 asubuhi hivyo wajumbe wote wanatakiwa kuwasili katika ukumbi wa Kikwete kuanzia saa 2:00 hadi saa 2:30 asubuhi,”  amesema Msigwa



Share:

Kuahirishwa Kwa Zoezi La Ajira Za Watumishi Wa Muda Kwa Ajili Ya Uboreshaji Wa Daftari La Kudumu La Wapiga Kura

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuwataarifu Wananchi wote kuwa tarehe 30 Mei, 2019 iliwatangazia nafasi za kazi za muda kupitia tovuti yake ya www.nec.go.tz na kuwaalika watanzania wenye sifa zilizo ainishwa kwenye tangazo hilo kuomba nafasi hizo za kazi.
 
Hivyo, Tume inapenda kuwataarifu wananchi wote ya kwamba mchakato wa ajira za muda kwa ajili ya zoezi hilo umeahirishwa hadi hapo itakapotangazwa tena.
 
Aidha, Tume inapenda kutoa shukrani zake kwa wale wote walioleta maombi yao ya kazi na inaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.
 
Dkt. Athumani Kihamia
MKURUGENZI WA UCHAGUZI


Share:

Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa Awataka waislamu kote nchini waendeleze utulivu, amani na uadilifu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka waislamu kote nchini waendeleze utulivu, amani na uadilifu waliouonesha katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwani kwa kufanya hivyo, watasaidia kukuza umoja wa kitaifa, uchumi na kuboresha huduma za jamii.

Amesema ni vema wakatambua kwamba uadilifu waliouonesha ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni silaha muhimu hususan katika kuimarisha maendeleo na kudumisha haki, umoja, usawa, upendo na utulivu.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Juni 5, 2019)kwenye Baraza la Eid El Fitri, lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Tanga Beach Resort jijini Tanga.“Nawashi sana kuyaenzi mema yote mliyoyafanya kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan’’.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezipongeza taasisi za Kiislamu na imani nyingine ambazo zimejenga shule ili kuchangia maendeleo ya elimu kitaifa lakini amesisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza shule nyingine na vyuo zaidi pamoja na kuziboresha zile zilizopo ili kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za jamii nchini

Amesema licha ya juhudi inazozichukua, Serikali peke yake haina uwezo wa kueneza huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji katika kila pembe ya nchi hivyo, inapotokea taasisi za Kiislamu au madhehebu mengine yakaweka mikakati ya kueneza huduma hizo, basi bila shaka Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo na kuchangia ufanisi wake.

Wakati huo huo, ameitaka BAKWATA ichukue hatua za makusudi katika kuhakikisha huduma nyingi za maendeleo na za kijamii zinaifikia kwenye mikoa mingi zaidi ya pembezoni. “Huu ni wakati muafaka sasa wa kutafakari ni namna gani Watanzania wa maeneo mengine nao watanufaika na uwepo wa huduma mbalimbali kama vile elimu, afya na nyinginezo.“

Kwa upande wake,Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally ametumia fursa hiyo kuwataka waislam wote nchini wabadilike na waache mazoea ili waweze kusonga mbele kielimu na kiuchumi.

Sheikh Zubeir amesema ni vema kwa waislamu wakajiimarisha kiuchumi kwa sababu kutawaondolea changamoto za kuendesha shughuli zao mbalimbali na hivyo watakuwa wamejiletea maendeleo na kuboresha maisha yao.

Mbali na wito huo pia amewataka waislamu wote wahakikishe wanatii mamlaka yaliyo juu yao , viongozi waliopo madarakani wawe wa kiserikali na wa kidini kama ilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa [TAKUKURU], Diwani Athuman amesema ili nchi iweze kuendelea kuwa na amani,  utulivu na usalama watanzania wote hawana budi kuungana pamoja katika kupiga vita vitendo vya rushwa.

"Rushwa ni dhambi kubwa na hukumu yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni moto kwa sababu rushwa ni kipingamizi kikubwa cha maendeleo, hivyo tuungane pamoja kupinga rushwa ndani ya nchi yetu kama Rais Dkt. John Magufuli anavyotuongoza."

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Wanafunzi watano wazama ziwa Victoria Wakisoma

Wanafunzi watatu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Makurugusi iliyopo Chato mkoani Geita, wamepoteza maisha kwa kuzama katika Ziwa Victoria baada ya mtumbwi waliokuwa wamepanda kupinduka.

Walikuwa ziwani wakifanya mradi (project) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhitimu kidato cha nne.

Mradi wao ulikuwa unahusu ongezeko la watu na athari za mazingira katika eneo la mwalo wa Matofali Kibunda, Kata ya Makurugusi, ambao waliuanza Mei mosi na walikuwa wawasilishe ripoti yao kesho.

Akitoa ufafanuzi juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo, aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Atha Gabriel (19), Manyencha Faustin (18) na Masalu Hamis (22).

Kamanda Mwabulambo alisema wanafunzi watano wakiwa kwenye mafunzo yao ya mradi, walitamani kutembelea mandhari ya ziwa hilo, wakaamua kukodi mtumbwi ili kufanya utalii wa ndani.

Alisema walipanda mtumbwi ambao dereva alikuwa Daud Thomas na wakati wakiwa umbali wa mita 120 kutoka ufukweni, mmoja wao, aliyejulikana kama  Samson Kano  alivua nguo na kutumbukia majini kwa nia ya kuogelea.

Kamanda Mwabulambo alisema kuwa mwanafunzi huyo alipotaka kurudi katika mtumbwi, alivuta ukingo wa mtumbwi huo na ndipo ulipoegemea upande huo na kupinduka.

 “Mtumbwi ulipopinduka wanafunzi wote walizama na kati yao watatu walizama  kabisa, huku wengine wawili wakifanikiwa kuogelea na kutoka,” alisema.

Kamanda Mponjoli aliwataja waliookolewa kuwa ni Abiana Fitina (19) ambaye pia alikunywa maji mengi na hali yake sio nzuri na mwingine ni Yohana Yamonda (19).

Alisema harakati za kuwaokoa zilifanyika chini ya uongozi wa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri, Mkuu wa Polisi wa Wilaya na wananchi ambazo zilichukua siku nzima ya juzi hadi miili kupatikana saa 11 jioni.

Kamanda Mwabulambo aliwaonya wananchi watumiao vyombo vya majini kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni za usafiri huo.


Share:

Kundi la IS ladai kuhusiaka na mashambulizi ya Msumbiji

Kundi linalojiita dola la Kiislam kwa mara ya kwanza limedai kuhusika na uasi nchini Msumbiji lakini wataalam wametilia shaka madai hayo na polisi ya Msumbiji imepuuza taarifa hiyo. 

Uasi wa makundi ya itikadi kali umekuwa ukiongezeka katika jimbo la kaskazini ya Msumbiji la Cabo Delgabo tangu mwaka 2017 ambapo zaidi ya watu 200 wameuwawa na vijiji kuchomwa moto. 

Kulingana na kampuni moja inayofuatilia shughuli za makundi ya itikadi kali, kundi la IS limelitoa taarifa yake hapo jana likidai kuhusika katika makabiliano ya bunduki na jeshi la Msumbuji yaliyotokea hivi karibuni katika jimbo la Cabo Delgado. 

Wapiganaji wa itikadi kali wamekuwa wakivishambulia vijiji na kuua watu mara kwa mara licha ya uwepo wa askari wengi wa polisi na jeshi katika jimbo hilo linalopakana na Tanzania. 

Polisi ya Msumbuji imepuuza madai hayo ya kundi la IS yaliyotolewa wakati Waislam duniani wanasherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.


Share:

Lazaro Nyalandu: CHADEMA itashinda majimbo yote Singida Uchaguzi Mkuu wa Mwakani

Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lazaro Nyalandu, amedai kuwa mwaka 2020, chama hicho kitarejesha majimbo yote ya Mkoa wa Singida ikiwamo jimbo alilokuwa akiliongoza la Singida Kaskazini.
 
Akizungumza katika Kijiji cha Ikungi mkoani Singida  wiki iliyopita, kada huyo alisema kutokana na kazi ya kujenga chama katika mkakati maalum unaofahamika katika chama hicho kama ‘Chadema ni msingi, chama hicho kitaibuka na ushindi katika majimbo yote ya mkoa wa Singida.

“Kama vile huu mkoa wa Singida ulivyokuwa na watu wawili maarufu yupo Tundu Lissu na yupo Nyalandu, sasa timu hii inacheza pamoja ,tutaichukua Singida Mashariki tena, tutaichukua Singida Kaskazini kwa mara ya kwanza ,tutashinda Singida Magharibi, majimbo yote mawili ya Iramba na Itigi”, Nyalandu alisema.

Kada huyo wa Chadema ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Singida Kaskazini na Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu ya nne, hivi karibuni alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wenzake wawili akituhumiwa kwa rushwa na mikutano iliyokatazwa na Serikali.


Share:

Uteuzi Wa Wagombea Udiwani Katika Kata 32 Za Tanzania Bara

Tarehe 31 Mei, 2019, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea katika Uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata Thelathini  na mbili (32) za Tanzania Bara. Uteuzi huo ulifanyika kama ilivyopangwa.

Katika Kata hizo Thelathini na mbili (32), jumla ya wagombea 98 kutoka katika Vyama kumi na nne (14) vya Siasa walichukua Fomu za Uteuzi.  Vyama hivyo ni pamoja na AAFP, UMD, ADA – TADEA, CCK, CCM, CHADEMA, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, NCCR - Mageuzi, NRA, SAU, TLP, UDP na UPDP.

Hadi muda wa mwisho wa uteuzi tarehe 31 Mei, 2019 saa 10: 00 jioni kati ya wanachama 98 waliochukua fomu za uteuzi, 41 walirejesha fomu hizo, kati ya hao 27 walikidhi vigezo na kuteuliwa kuwa wagombea. Wanachama wengine watano (5) hawakuteuliwa kuwa wagombea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kurejesha fomu za uteuzi nje ya muda, kukosa uthibitisho wa malipo ya dhamana na wagombea kuwa na idadi pungufu ya wadhamini. 

Jumla ya wagombea Watano (5) wa nafasi ya Udiwani waliwekewa pingamizi kwa Msimamizi wa Uchaguzi na hivyo kupelekea wagombea wawili (2) kuenguliwa kutoka katika orodha ya wagombea wa nafasi ya Udiwani.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea Rufaa moja (1) kutoka kwa Mgombea Udiwani wa Kata ya Ipole iliyopo Halmashauri ya Wilaya Sikonge kupitia Chama cha Wananchi CUF, na malalamiko kutoka kwa wagombea wa CHADEMA na CUF katika Kata ya Murangi  iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Malalamiko yao ni dhidi ya maamuzi ya Wasimamizi wa Uchaguzi ya kuwaondoa kwenye orodha ya wagombea udiwani.

Tume katika kikao chake kilichofanyika leo tarehe 4 Juni, 2019 kimetoa maamuzi kama ifuatavyo:-

Kwanza, Tume imekubali rufaa moja ya mgombea Udiwani wa CUF katika Kata ya Ipole Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na hivyo kumrejesha kuendelea kuwa kugombea katika nafasi hiyo.

Pili, Tume imekubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi katika Kata ya Murangi  iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ya kuwaondoa Wagombea wa CUF na CHADEMA katika orodha ya wagombea na hivyo Wagombea kuendelea kuenguliwa kugombea Udiwani.

Katika Uteuzi huu wa Udiwani katika Kata thelathini na mbili (32, jumla ya Wagombea udiwani katika Kata 29 wamepita bila kupingwa, na mgombea wa CUF kutoka Kata ya Kyaitoke Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na mgombea wa ACT –Wazalendo kutoka Kata ya Boma iliyopo katika Halmashauri ya Mji  Mafinga wamejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, hivyo Kata moja (1) ndio itakayofanya uchaguzi hapo tarehe 15 Juni, 2019, kata hiyo ni Ipole Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.

Kampeni za uchaguzi zimeshaanza kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi na zitaendelea hadi tarehe 14 Juni, 2019 ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi.

Taarifa zaidi kuhusu walioteuliwa inapatikana kwenye tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya www.nec.go.tz na Ofisi za Tume Makao Makuu.

Imetolewa  tarehe 4 Juni, 2019.
Dr. Athumani Kihamia
MKURUGENZI WA UCHAGUZI


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya June 6




Share:

Wednesday, 5 June 2019

KUTANA NA MWANAMKE BINGWA WA KUUNDA MAJENEZA...MSHAHARA WAKE ZAIDI YA MSOMI WA CHUO KIKUU


 Mama mmoja mjini Nakuru  nchini Kenya amepata umaarufu kutokana na ustadi wake katika kutengeneza majeneza. 

Loyce Atieno aliwacha kazi ya kuuza mboga mwaka wa 2012 na kuingilia kazi hiyo ambayo kwa sasa anaienzi sana. 

Atieno anasema kuwa hajutii hatua yake kwani kwa sasa hutengeneza KSh 45000 kila mwezi pesa ambazo hangepata iwapo angeendelea kuwakatia wakazi wa Nakuru mboga. 
Loyce Atieno akiwa mahali pake pa kazi. 
Si kawaida kwa wanawake kuingilia kazi ya kuunda jeneza nchini Kenya. 
Kisa cha Atieno ni cha kipekee kwani biashara ya jeneza huonekana ya kuogofya ikizingatiwa ni mwiko kwa jamii nyingi nchini Kenya kufikiria biashara inayohusiana na mauti.

 Biashara hiyo huachiwa wachache tu katika jamii na watu hao huwa wanatengwa kwa njia moja ama nyingine. 

"Kuuza mboga hakukuwa kunanipa hela za kutosha kukithi mahitaji ya familia. Niliamua kuiacha na kuingilia utengenezaji wa jeneza ingawa sikumwarifu yeyote. Nilimwambia tu bwanangu nikiwa tayari nimeanza," alisema Atieno. 

Loyce Atieno hutengeneza shilingi 1500 kwa siku katika biashara yake ya kutengeneza majeneza.

Kulingana na Atieno, gharama ya na faida hutegemea muundo wa jeneza huku la wastani akiliuza kwa KSh 30, 000. Ustadi wake katika kupaka na kurembesha jeneza humtenganisha fundi huyu ambaye aliachia masomo yake kidato cha nane lakini kwa sasa anapata takriban KSh 45000 kila mwezi. 

Hicho ni kipato ambacho hata baadhi ya waliosoma hata hadi mpaka chuo kikuu hawakikaribii. 
Chanzo - Tuko
Share:

BENKI YA AKIBA YAKABIDHI VIFAA VYA USAFI KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA 2019

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Mazingira Duniani Juni 05, 2019, benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) imekabidhi vifaa vya usafi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza ili kuimarisha huduma ya usafi sokoni hapo.


Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imeambatana na zoezi la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko Kuu jijini Mwanza ambapo wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika pamoja na wafanyabiashara sokoni hapo kufanya usafi huo.

Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na zoezi endelevu la kufanya usafi katika soko hilo na kuweka mazingira katika hali ya usafi ili kuzuia magonjwa ya milipuko huku akitoa pongezi kwa Serikali kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba aliyepokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella na kuvikabidhi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza, amesema vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa wa kuimarisha usafi na hivyo wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira safi na salama kiafya.

Naye Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola ameishukru benki ya Akiba kwa kutoa vifaa hivyo na kuomba liwe zoezi endelevu huku akitoa rai kwa wafanyabiashara sokoni hapo kuvitumia vyema kuimarisha usafi kama ilivyo desturi yao ya kufanya usafi kila jumamosi.
Meneja wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) tawi la Mwanza, Herieth Bujiku (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (wa pili kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki hiyo ili kuimarisha hali ya usafi eneo la Soko Kuu jijini Mwanza. Zoezi hilo limeambatana na shughuli ya usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Meneja wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) tawi la Mwanza, Herieth Bujiku (kulia) akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa vya usafi ili kusaidia huduma ya usafi katika Soko Kuu jijini Mwanza. Hafla hiyo imeambatana na zoezi la usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Vifaa vilivyokabidhiwa na benki ya Akiba ni pamoja na mifagio, mapipa ya kutunzia taka, koleo, reki, buti za usafi, glovusi, toroli na maski.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola (kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba. Kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (wa tatu kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola (wa pili kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku akisoma taarifa fupi kuhusu vifaa vilivyotolewa na benki hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akizungumza kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amehimiza vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba kutumika vyema kuimarisha usafi katika Soko Kuu jijini Mwanza ambalo amesema miezi michache ijayo litaanza kujengwa upya kuwa la kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamas Nchola akitoa salamu za shukrani kwa benki ya Akiba baada ya kupokea vifaa vya usafi.
Afisa Mazingira (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza), Mangabe Mnilago akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba jijini Mwanza wakijumuika na wafanyabiashara Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi katika maeneo ya soko hilo. 
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wakifanya usafi katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani 2019.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba wakiwa kwenye usasi katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba jijini Mwanza wakijumuika na wafanyabiashara Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi katika maeneo ya soko hilo. 
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika na wafanyabiashara katika Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani, Juni 05, 2019.
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wakiendelea na usafi eneo la Soko Kuu jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) wakiondoa uchafu katika eneo la kukusanyia uchafu lililopo Soko Kuu jijini Mwanza.
HOTUBA YA FUPI YA MENEJA WA TAWI LA MWANZA BI: HERIETH BUJIKU ILIYOSOMWA KATIKA HAFLA YA KUKABIDHI VIFAA VYA USAFI KWA UONGOZI WA SOKO KUU LA MWANZA KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI.



Mheshimiwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza

Uongozi wa Soko la Kuu Mwanza

Ndugu Wanahabari

Wafanya biashara kutoka soko kuu Mwanza

Mabibi na Mabwana

Itifaki ikizingatiwa



Ndugu Mgeni Rasmi

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa ajili ya siku njema ya leo. Nasema ni siku njema kwani sisi kama Benki ya Akiba tumefarijika sana kupata fursa hii ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya usafi katika soko kuu la Jiji la Mwanza.


Soko hili ni kati ya masoko makubwa sana hapa Mwanza na linapokea bidhaa nyingi kutoka sehemu mbali mbali za kanda ya ziwa. Kwa hiyo ni soko ambalo linasaidia kuinua maisha ya wakulima pamoja na kutoa ajira kwa watu mbali mbali. Sisi kama Benki ya Akiba tunao wateja wengi tu tunaowahudumia kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo mikopo ambayo inasaidia kukuza mitaji na kuendeleza biashara za wafanyabiashara mbali mbali katika soko hili.



Ndugu Mgeni Rasmi

Benki ya Akiba inatambua na inathamini mazingira na ni mdau mkubwa katika harakati za kutunza mazingira. Najivunia kusema hilo kwani sera ya Akiba ya huduma za kijamii yaani Corporate Social Responsibility imeweka kipengele cha mazingira kama sehemu mojawapo ambayo Benki itakuwa inashughulikia katika kurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii inayoihudumia.



Kwa kudhihirisha hili napenda kusema kuwa Benki inafanya jitihada nyingi katika eneo hili mathalan Benki imechukua jukumu la kuendeleza na kutunza Viunga vya bustani ya Indepence Square vilivyopo jijini Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi yetu. Viunga vipo katika mandhari nzuri kabisa ya kuvutia na vinapendezesha sana muonekano wa jiji la Dodoma. Jitihada hizi zilianza kuanzia mwaka 2013 na napenda kusema kuwa zoezi hili kwetu litakuwa la kudumu na endelevu.



Pia napenda kusema kuwa jitihada zetu za kufanya usafi pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa zoezi endelevu la usafi limedhihirika sehemu mbali mbali kama Soko la Tandale,Buguruni Jiji la Mbeya n.k. Maeneo haya yameweza kufaidika na huduma hii pamoja na kukabidhiwa vifaa vya usafi kwa ajili ya kuhakikisha kuwepo kwa usafi endelevu. Vivyo vivyo kwa leo hapa Soko Kuu Mwanza zoezi hili linahitimishwa kwa kukabidhi vifaa vya usafi kwa uongozi wa soko kwa ajili ya matumizi ya baadaye.



Ndugu Mgeni Rasmi

Benki ya Akiba ni Benki ya Kibiashara ambayo imejikita kuhudumia wananchi wa hali ya chini na wa kati kwa lengo la kuboresha maisha yao na kuinua jamii kiujumla. Benki hii inatoa huduma zote za kibenki kama nilivyoainisha hapo mwanzo yaani mikopo, amana mbali mbali, kutuma na kupokea fedha nje na ndani ya nchi. Huduma nyinginezo kama za mawakala wa kuuza na kupokea float zinapatikana na Mawakala wa kuuza float yaani M-pesa, Tigo Pesa, Airtel Money, Halo Pesa n.k wanahudumiwa kwa haraka bila kusimama foleni na wengi wao wameweza kukuza mitaji yao kupitia mikopo tuliyowapa.


Huduma nyingine za kurahisisha upatikanaji wa huduma za Kibenki kupitia simu za mikononi yaani Akiba Mobile inaptika masaa 24 na imeleta faraja na unafuu kwa wateja wetu kwani inarahisisha na kuokoa muda. Wateja wengi wanatumia huduma hii kuweka fedha kwenye akaunti zao, kufanya marejesho ya mikopo pamoja na mahitaji mengi kama kulipia ving’amuzi, LUKU, bili za maji n.k.



Aidha, huduma za kuuza na kununua fedha za Kigeni zinapatikana katika matawi yetu na tunawakaribisha mtutembelee kwa ajili ya mahitaji yenu yote ya kuuza na kununua fedha kigeni. Pia huduma ya E-statement inapatikana; huduma hii inaleta wepesi wa mteja kupata taariza za akaunti yake kwa urahisi pasipo kwenda Benki kupitia simu ya mkononi, kompyuta n.k. Mteja anatakiwa tu aende kwenye tawi lake kuhakiki taarifa zake pamoja na kutoa anuani ya barua pepe au E-mail address.



Manufaa ya huduma ya E-statement hayaishii kwa mteja kwani yanasaidia pia katika utunzaji wa mzingira kwa sababu inapunguza na kuondoa matumizi ya karatasi. Hii pia ni jitihada za Benki za kutunza mazingira inaonyesha jinsi ambavyo Benki ya Akiba ni Rafiki Bora wa mazingira.



Ndugu Wanahabari

Kwa kuhitimsha naomba niwashukuru wote kwa kutuunga mkono katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani amabayo kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kupinga Uchafuzi wa Hewa- yaani Air Pollution", sisi kama benki tunauunga na dunia katika hilo kwani tunatambua umuhimu wa kuwa na hewa safi. Takwimu zinasema kwamba 92% ya watu duniani hawavuti hewa safi hili ni tatizo kubwa sana na zinahitajika juhudi za makusudi kwa ajili ya kupambana na tatizo hili kwani linahatarisha afya za watu pamoja na viumbe hai wengine na mazingira kwa ujumla.



Ndugu Mgeni Rasmi

Kwa niaba ya Benki ya Akiba naomba pia nitoe pongezi kubwa kwa Serikali ya awamu ya tano kufuatia juhudi za makusudi za kupiga marufuku matumzi ya mifuko ya Plastiki ambayo kwa kwa kweli inaleta uharibifu mkubwa kwa mazingira. Sisi kama taasisi pia tupo mstari wa mbele katika kutekeleza agizo hili na tunatoa rai kwa wananchi wote hususan wakazi wa Mwanza kuachana na matumizi ya vitu hivi kwa ajili ya kutunza mazingira yetu ili kuhakikisha urithi bora wa vizazi vijavyo.


Mwisho kabisa, naomba nichukue fursa kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi vikiwemo fagio, mapipa ya kutunzia taka, koleo, rake, buti za usafi, gloves, toroli, masks na vingine kwa uongozi wa soko kwa matumizi ya badae. Lengo ni kuhakikisha kuweko kwa zoezi endelevu la usafi katika soko hili kwa ajili ya kutunza mazingira na kuzuia magonjwa ya milipuko. Hili eneo ni muhimu sana kwa jamii kwani mahitaji ya chakula yanapatikana sana katika soko hilo. Kwa umuhimu huo basi naomba uongozi wa soko undelee kutilia mkazo wa usafi katika eneo hili kwani eneo lenye mahitaji muhimu kama haya linahitaji kutunzwa kwa umakini mkubwa.



Asanteni sana kunisikiliza

Herieth Bujiku – Meneja wa Tawi la Mwanza

Akiba Commercial Bank.

Tazama video hapa chini

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger