Sunday, 31 March 2019

Picha : TIMU YA WAKONGWE 'SHYTOWN VETERAN' YAZINDULIWA RASMI UWANJA WA CCM KAMBARAGE




Timu ya wakongwe (Shytown Veteran Sports Club) imezinduliwa rasmi kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga Mjini, kwa kufanya Bonanza la michezo ambalo limeshirikisha timu za wakongwe kutoka mikoa mitatu Tabora, Simiyu pamoja na wenyeji Shinyanga Veteran.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Machi 31,2019 kwenye uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao.

Akizungumza, Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa timu hiyo ya Shytown Veteran, Afisa Tawala wa wilaya ya Shinyanga Kamara Beda akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Jasinta Mboneko, alisema Serikali itashirikiana bega kwa bega na timu hiyo ikiwemo kutatua changamoto ambazo zinawakabili.

“Mkuu wa wilaya ya Shinyanga amenituma kuwaletea salamu zake kuwa michezo ni mazoezi na inainua vipaji, hivyo ameahidi Serikali itashirikiana nanyi kikamilifu katika kuhakikisha mnayafikia malengo yenu,”alisema Beda.

“Hivyo kwa kuunga mkono nami natoa mipira miwili kwenye Timu hii ya Shtown Veteran Sports Club ambayo mtakuwa mkiitumia kwenye michezo yenu, ambapo nawaomba pia mpange siku ili mje kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya tupate kuzungumza kwa pamoja ili kupanga mikakati dhidi ya timu yenu,”aliongeza.

Naye Katibu mkuu wa timu hiyo Mohamed Katoto akisoma Risala kwa mgeni huyo rasmi, alisema Timu hiyo waliiunda Machi 23,2018 na kupata usajili kutoka kwenye Baraza la Michezo Novemba 20,2018, ambapo leo ndiyo wameamua kuizindua rasmi ikiwa na wanachama 55.

Alisema changamoto ambayo inawakabili kwa sasa ni ukosefu wa fedha za kuendeshea Timu hiyo kutokana na kutopata wadhamini, ambapo wameomba wajitokeze kuwafadhili ili kutoa hamasa kwenye timu za wakongwe.

Aidha kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao ambaye naye amehudhuria uzinduzi huo wa Timu ya Shytown Veteran, amewapongeza wakongwe hao kwa kuunda Timu hiyo na kuahidi kuwapatia mipira miwili.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI

Mgeni Rasmi Afisa tawala wilaya ya Shinyanga Kamara Beda akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo Jasinta Mboneko kwenye uzinduzi wa Timu ya wakongwe Shytown Veteran Sports Club, kwa kupiga mkwaju wa Penati ambao ulimshinda Golikipa wa timu hiyo ya Shytown Veteran. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga Kamara Beda, akizungumza kwenye uzinduzi wa timu ya Shytown Veteran Sports Club na kuahidi Serikali itashirikiana nao kikamilifu kwa kutatua baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili.

Katibu mkuu wa timu ya Shytown Veteran Sports Club Mohamed Katoto akisoma risala ya timu hiyo na kueleza changamoto ambazo zinawakabili ambazo ni ukosefu wa fedha za kuendeshea timu, ukosefu wa kiwanja pamoja na vifaa vya michezo, na kuomba wafadhili wajitokeza kuwekeza kwenye timu hiyo.

Mwenyekiti wa timu ya Shytown Veteran Sports Club Christopher Msigwa akitoa shukrani kwa viongozi kujitokeza kuahidi kuisaidia timu hiyo pamoja na kutoa ahadi ya kuipatia mipira.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao, akitoa pongezi ya kuanzishwa kwa timu hiyo ya wakongwe Shytown Veteran Sports Club na kuahidi kutoa zawadi ya mipira miwili.

Diwani wa Kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga Hassan Mwendapole mahali ambapo uwanja huo wa michezo upo kwenye Kata yake akitoa ahadi ya kutoa mpira mmoja kwa timu hiyo ya Shytown Veteran Sports Club.

Katibu mkuu wa timu ya Shytown Veteran Mohamed Katoto akishikana mikopo na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao mara baada ya kumaliza kusoma risala ya timu hiyo.

Mgeni Rasmi Afisa Tawala wa wilaya ya Shinyanga Kamara Beda akishikana mikono na wachezaji wa timu ya Shytown Veteran Sports Club tayari kwa ufunguzi wa bonanza hilo la michezo.

Utoaji wa salamu ukiendelea kwa mgeni rasmi.

Mgeni rasmi akitoa salamu kwa timu ya Busulwa Veteran ambayo kwa ajili ya mchezo dhidi ya Shytown Veteran kwa ufunguzi wa bonanza hilo la michezo la kuzindua rasmi timu hiyo ya Shytown Veteran Sports Club.

Mchezo ukichezwa kati ya Busulwa Veteran wenye Jezi ya Njano, pamoja na Shytown Veteran Sports Club ambao waliiubuka na ushindi wa magoli mawili yaliyofungwa na Mdee Aboo pamoja na Mohamed Katoto.

Mchezo ukiendelea kati ya Simiyu Veteran wenye Jezi ya blue pamoja na Unyanyembe Veteran ya Tabora ambapo walitoka suluhu ya kufungana goli moja kwa moja.

Mchezaji wa Simiyu Veteran akiwa chini akigangwa mara baada ya kukanywaga kwenye mchezo wao dhidi ya Unyanyembe Veteran ya Tabora.

Kabumbu likiendela kusakatwa kwenye uzinduzi wa timu ya Shytown Veteran Sports Club.

Shytown Veteran Sports Club wenye Jezi ya rangi ya machungwa, wakiwa na Unyanyembe Veteran ya Tabora, ambao waliibuka na ushindi wa goli Moja.

Kabumbu likiendelea kusakatwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.

Wadau wa michezo pamoja na baadhi ya wachezaji wa timu ya Shytown Veteran Sports Club wakishuhudia Kandanda safi likiendelea kuchezwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage.

Wadau wa michezo pamoja na baadhi ya wachezaji wa timu ya Shytown Veteran Sports Club wakishuhudia Kandanda safi likiendelea kuchezwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage.

Awali Mgeni rasmi Afisa tawala wa wilaya ya Shinyanga Kamara Beda akisalimiana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao kabla ya kuzindua bonanza la michezo la uzinduzi rasmi wa timu ya Shytown Veteran Sports Club.

Wachezaji wa timu ya Shytown Veteran wakipiga picha ya pamoja na mgeni rasmi Afisa Tawala wa wilaya ya Shinyanga Kamara Beda, Diwani wa Kata ya Kambarage Hassan Mwendapole pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 blog
Share:

SIMBA SC WAITWANGA MBAO 3 - 0

Dakika 90 za mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na Mbao zimekamilika uwanja wa Jamhuri, Morogoro, kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.


John Bocco alianza kufunga bao la kuongoza kwa Simba dakika ya 24 akimalizia faulo iliyopigwa na Mohamed Hussein.

Bocco alipachika bao la pili kwa Simba kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa Mbao FC, Peter Mwangosi kunawa mpira uliopigwa na Mzamiru Yassin dakika ya 58.

Meddie Kagere alipachika bao la tatu kwa Simba baada ya beki wa Mbao kumchezea rafu Kagere eneo la hatari na mwamuzi kutoa penalti iliyopigwa na Kagere dakika ya 79.

Simba leo wameanzisha jeshi lao kamili huku mlinda mlango namba moja Aishi Manula akiwa ameanzia benchi akimtazama Deogratius Munish.

Mashabiki waliojitokeza ni wengi kuona namna timu zao zitakavyoonyesha umwamba leo huku Mbao wakiwa na kumbukumbu ya ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Share:

Picha : AGAPE YATOA MAFUNZO YA SHERIA KWA WASAIDIZI WA KISHERIA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WASICHANA KWENYE MASOKO

Jumla ya Wasaidizi wa Kisheria 36 katika Masoko ya Manispaa ya Shinyanga wamepatiwa mafunzo ya sheria na Shirika la Agape AIDS Control Programme ili wakasaidie kutoa elimu hiyo kwa wafanyabiashara kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake wafanyabiashara sokoni. 

Mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa siku tatu katika Ukumbi wa Katemi Hoteli Mjini Shinyanga yamefungwa leo Jumapili Machi 31,2019 na Mkurugenzi wa shirika la Agape,John Myola. 

Myola amesema katika mafunzo hayo,Wasaidizi wa Kisheria wamepewa elimu kuhusu sheria mbalimbali na kutambua haki za binadamu,haki za kiuchumi,jinsi ya kufanya biashara,ukatili wa kijinsia na mahali sahihi pa kutoa taarifa za vitendo vya kikatili. 

Amesema mafunzo hayo ni Mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa “Mpe Riziki Si Matusi” kwa lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wafanyabishara katika masoko unaofadhiliwa na shirika la UN WOMEN kupitia Shirika la kitaifa la Equality for Growth (EfG). 

“Naomba mafunzo haya mliyopata yatakuwa msaada kwenu binafsi lakini pia nendeni mkawasaidie wananchi,katoeni huduma bila upendeleo na bila kuonea mtu ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata haki sokoni”,alisema Myola. 

“Nawashauri pia kutunza siri za watu,msiwe waoga kutatua migogoro inayotokea sokoni,naamini mtakuwa mstari wa mbele kupiga vita dhuluma mbalimbali ikiwemo rushwa ya ngono na kuwapigania akina mama na wasichana ambao wana maumivu ya kutendewa vitendo vya kikatili”,aliongeza Myola. 

Aliyataja masoko ambako mradi huo unatekelezwa katika manispaa ya Shinyanga kuwa ni soko Kuu Mjini Shinyanga,Kambarage,Nguzo Nane,Ibinzamata,Ngokolo Mitumbani na Majengo Mapya.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Sheria ya siku tatu kwa Wasaidizi wa Kisheria ili wakataokwenda kutoa elimu kwa wafanyabiashara kwenye masoko yaliyopo katika Manispaa ya Shinyanga ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake na wasichana wafanyabiashara sokoni - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akiwasisitiza Wasaidizi wa kisheria kutumia mafunzo waliyopata kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye masoko.
Wasaidizi wa Kisheria kwenye masoko wakimsikiliza Myola.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape,John Myola akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Awali Afisa Masoko Manispaa ya Shinyanga,Alex Hinda akitoa mada kuhusu namna bora ya kufanya biashara na kuwataka wafanyabiashara kujitahidi kutunza taarifa zao za fedha.
Afisa Masoko Manispaa ya Shinyanga,Alex Hinda akitoa mada wakati wa mafunzo hayo.
Wasaidizi wa Kisheria wakiwa ukumbini.
Wasaidizi wa kisheria wakiwa ukumbini.
Wasaidizi wa Kisheria wakifanya Mtihani wa kipimo cha uelewa wa mafunzo waliyopatiwa kwa kipindi cha siku tatu kuhusu masuala mbalimbali ya sheria ili kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wafanyabiashara sokoni.
Wasaidizi wa Kisheria wakifanya mtihani.
Wasaidizi wa Kisheria wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo kufungwa.
Wasaidizi wa Kisheria wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo kufungwa.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

CAG AKABIDHI RIPOTI 17 ZA UKAGUZI KWA RAIS MAGUFULI

Ripoti 17 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2018 zimekabidhiwa rasmi kwa Rais Dk. John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), ripoti hiyo imewasilishwa na CAG katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam juzi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ofisi hiyo. 

CAG alimkabidhi Magufuli ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu, Ripoti ya Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma na Ripoti ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo. 

Pia alikabidhi Ripoti ya Ukaguzi wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi na ripoti 11 za ukaguzi wa ufanisi katika sekta mbalimbali. 

Sekta hizo ni pamoja na usimamizi wa shughuli za ujenzi wa miradi ya umwagiliaji, usimamizi wa miradi ya maji vijijini, usimamizi wa miradi ya maji itokanayo na visima virefu. 

Nyingine ni matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme, usimamizi wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, usimamizi wa mfumo wa ununuzi wa magari ya Serikali kwa pamoja pia sekta ya ufuatiliaji wa shughuli za ujenzi na majengo ya mijini, usimamizi wa utoaji wa huduma za afya za rufaa na dharura kwa hospitali za rufaa ngazi ya juu, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo, usimamizi wa utoaji wa huduma ya bima ya afya na ufuatiliaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa ufanisi.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Magufuli aliipongeza ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na pia kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kwa karibu na katika kukabiliana na kudhibiti matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 143 kifungu kidogo 2 na 4, kinamtaka CAG kukabidhi ripoti hizo kwa Rais kabla ya Machi 31, kila mwaka na baada ya hapo zinawasilishwa bungeni siku saba za mwanzo za kikao cha Bunge kinachofuata. 

Share:

ASKARI ANUSURIKA KUFA POLISI WAKIUA MAJAMBAZI WATATU KIGOMA


Na Rhoda Ezekiel Kigoma.
Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma limewaua watu watatu wanaosadikikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa wamejipanga kufanya uporaji katika baadhi ya nyumba za wananchi wilayani Kibondo.

Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa Wilaya ya Kimbondo,Louis Bura ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo amesema katika jana usiku majira ya saa tatu Askari polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi, kuwa kuna majambazi wanataka kuvamia baadhi ya nyumba ndipo walipofika eneo la tukio na kuanza kurushiana risasi.

Katika tukio hilo askari mmoja aliyefahamika kwa jina la James Mwita (37) na mama mmoja Sophia Dicksoni (60) walijeruhiwa na sasa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Kibondo.

Alisema askari huyo alipatiwa matibabu ya awali na sasa hali yake sio mbaya na amepatiwa rufaa kwa ajili ya kwenda kwenye matibabu katika hospitali ya taifa Muhimbili kwa kuwa amejeruhika sana mguuni.

Amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano  kwa vyombo vya ulinzi na usalama pia na polisi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwa ni kazi ngumu na sasa wananchi wataendelea kutoa ushirikiano kwa kuwa polisi wako kazini.

Ametoa rai kwa wote wanaojihusisha na matukio ya ujambazi kuacha mara moja kwa kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na matukio hayo.

Aidha amewataka wananchi kuacha kuwaingilia katika utendaji kazi wao kwa kuwa wapo baadhi wanawakamata wakiwatuhumu kwa ujambazi lakini ndugu zao wanawatetea na kudai sio majambazi.

"Niwaambie tu wananchi hatutavumilia kuona majambazi wanaendelea kututesa Kibondo tumechoka, na kuanzia sasa niwaombe wananchi wale wanaoshirikiana na raia wa Burundi kuvamia watu muache maana jambazi hawezi kuja bila kupewa taarifa na watu ambao wanafahamu ni nani ana pesa, niseme tu kwa sasa tumejipanga tumechoka haya mambo hatuta wavumilia", alisema Bura.

Aidha amewataka wananchi kuacha kutoka nje pindi wanaposikia milio ya risasi kwa ajili ya usalama wao kwa kuwa ni hatari sana kufuata milio hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa sana.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Kibondo Sebasitiani Pima alisema walipokea watu watatu wakiwa wamefariki naa majeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Kibondo na mmoja wamekwisha msafirisha kuelekea Kigoma kwa ajili ya matibabu.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kibondo Khamisi Tahilo aliipongeza serikali na polisi kwa kazi wanayoifanya na kwamba wananchi wamefurahi sana kwa kuwa wameshuhudia wenyewe kwa macho yao Jambazi mmoja ambae wamekuta amefia katika mfereji wa maji wa Soko la mjini na wametoa kiasi cha shilingi laki moja kuwapa pole askari hao.

Amesema matendo yaliyokuwa yakifanya na majambazi hao Wilayani humo yamewachosha ba sasa Wanafuraha sana kwa kuwa Serikali imeimalisha usalama na ikitokea tatizo lolote wanawakamata.

Kwa upande wake mmiliki wa nyumba ambayo walikuwa wamepanga kuvamia Hamis Salumu amesema yeye alipigiwa simu na kuambiwa kwamba nyumbani kwake kuna watu wanapiga risasi ndipo alipokimbia polisi na kukuta tayari polisi walishakwenda nyumbani kwake.

Alisema hakuna aliyejeruhiwa wala kilichoibiwa nyumbani kwake na ametoa pongezi nyingi kwa jeshi la polisi kwa ushirikiano wanaouonyesha na kuwataka wengine wanao jihusisha na shughuli hizo kuacha mara moja kwani mwisho wao ni mbaya.
Share:

NEC YAPULIZA KIPENGA UCHAGUZI JIMBO LA JOSHUA NASSARI...UCHAGUZI MEI 19


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki ni Mei 19, 2019.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Machi 31, 2919 mkoani Morogoro amesema tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha sheria ya taifa ya uchaguzi aliitaarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi ya ubunge katika jimbo hilo.

"Nafasi ya jimbo la Arumeru ipo wazi na imetokana na aliyekuwa mbunge Joshua Samwel Nassari kupoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika," amesema Jaji Kaijage.

Amesema amevitaka vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya uchaguzi wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo.

Machi 14, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage kumtaarifu jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi kutokana na kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo.

Mikutano hiyo ni ule wa 12 wa Septemba 4 hadi 14 mwaka 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16 mwaka 2018 na mkutano wa 14 wa 29 Januari hadi Februari 9 mwaka 2019.

Na Lilian Lucas, Mwananchi
Share:

Uteuzi Mpya Uliofanywa na Rais Magufuli Lro Jumapili March 31

Rais wa Tanzania, John Magufuli amemteua Adolf Ndunguru kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia sera.

Taarifa  iliyotolewa leo Jumapili Machi 31, 2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Ndunguru ameteuliwa kushika nafasi hiyo kujaza nafasi iliyokuwa wazi.

Imesema kabla ya uteuzi huo, Ndunguru alikuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kufuatia Uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Msafiri Lameck Mbibo kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA.

Kabla ya uteuzi huo, Mbibo alikuwa Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo Jumapili Machi 31, 2019.



Share:

Lugola Atangaza Vita Dhidi Ya Matrafiki Wala Rushwa Akifungua Kongamano La Taifa La Usalama Barabarani

Na Felix Mwagara, MOHA.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka Askari Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, kusimamia sheria kikamilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia ambao hufariki, kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.

Akizungumza kabla ya kulizindua kongamano la kitaifa la wadau wa usalama barabarani nchini, Lugola ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, alisema wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa.

“Usalama Barabarani unaanza na kila mmoja wetu, nawaomba sana tutumie fursa hii kikamilifu kwa kutoa mawazo na maoni yetu katika kongamano hili kwa manufaa na mustakabali wa Usalama wetu hivi sasa na vizazi vijavyo,” alisema Lugola.

Pia aliwataka wadau hao, watumie fursa ya kongamano hilo kuzungumza kwa uwazi, kutoa mawazo yao ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa Baraza Usalama Barabarani na vyombo vingine ambavyo vinasimamia Sheria ya Usalama Barabarani.

Lugola alisema Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kutokomeza ajali za barabarani nchini, hivyo aliwataka wadau wa usalama barabarani wajipange kikamilifu kwa kiuweka mikakati thabiti kwa lengo la kutokomeza ajalin nchini.

“Ni wazi kwamba wasimamizi wa Sheria wakisimamia sheria kikamilifu na elimu ikaendelea kutolewa kwa watumiaji wengine wa barabarani na wakabadili tabia zao, uwezekano wa kupunguza ajali zaidi ni mkubwa,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alilitaka Baraza la Usalama barabarani kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Baraza Awamu ya Nne, ambao umezinduliwa Waziri huyo ameuzindua na Muongozo wa Utendaji na Utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya ili kudhibiti ajali za Barabarani na Kuimarisha Utendaji wa Kamati.

Lugola pia aliwataka kusimamia ukaguzi wa magari ili Kuhakikisha Magari mabovu yanaondoka barabarani, na Baraza likamilishe Uundwaji wa Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya haraka ili Kamati hizo zianze kazi ili kwenda na Mabadiliko yanayofanyika ndani ya Baraza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masuani alisema takwimu za usalama barabarani zimepungua nchini kutokana na Baraza lake kuweka mikakati za kupambana na ajali nchini.

Kongamano hilo ni mbadala wa Wiki ya Nenda kwa usalama barabarani ambayo kila mwaka ufanyika katika mkoa ambao uchaguliwa na wajumbe wa Baraza hilo.


Share:

Rais Magufuli Kuanza Ziara Ya Kikazi Mkoani Mtwara.

Na Bakari Chijumba, Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Dkt.John Pombe Magufuli, anatarajia kufanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kuanzia 02 April hadi April 04, Mwaka huu wa 2019 .

Akizungumza na wanahabari leo Jumamosi 30 Machi 2019, mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema katika ziara hiyo Rais Magufuli atazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara na lingine la ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata (Km 50),pia ataweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin kilichopo Msijute na ataweka pia jiwe la msingi katika chuo cha ualimu cha Kitangali.

Mh.Byakanwa amesema licha ya kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali, Rais Magufuli atazindua kituo cha afya cha Mbonde wilayani Masasi na barabara ya Mangaka-Mtambaswala na pia Mangaka -Nakapanya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

"Miradi inayozinduliwa ni mikubwa ambayo itasaidia kuchochea kukua kwa uchumi wa Mtwara na kwa uchumi wa Mtwara na nchi kwa ujumla na pia ni miradi ambayo kwa Mtwara ina tija kubwa sana, hivyo amewaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika maeneo yote yenye miradi ya maendeleo itakayozinduliwa ili kumsikiliza Mh.Rais" amesema   Mkuu wa mkoa huyo wa Mtwara.

Hii ni ziara ya pili kwa Rais Magufuli kutembelea Mkoa wa Mtwara tangu alipoapishwa kuwa Rais mwaka 2015, ambapo safari hii anatarajia kuzunguka katika wilaya zote za Mkoa huu.


Share:

Mkurugenzi TAMWA Awasihi Wazazi Kuacha Kuwahamasisha Watoto Kujifelisha Mitihani Kwa Makusudi.

Na Bakari Chijumba,Lindi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari  Wanawake Tanzania (TAMWA) Bi Rose Reuben, amewataka wanawake wa Ruangwa kubadilika na waweke juhudi katika kupinga kuishi kwenye maisha ya ukatili wa kijinsia.

Aidha amewataka wazazi kuacha kuwanyima watoto haki ya kupata elimu, kwani ni jukumu la mzazi kumpatia mtoto elimu na si kumshawishi afanye vibaya katika mitihani yake ya mwisho.

Mkurugenzi huyo, ameyasema hayo  Machi 29 March 2019, wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili mbinu mkakati ya  kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika ukumbi wa Rutesco uliopo  Ruangwa mjini,katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Bi Rose alisema lengo la TAMWA ni kusaidia jamii kuondokana na changamoto za ukatili wa kijinsia hivyo wataendelea kuhakikisha changamoto hizo zinaisha katika jamii ya Ruangwa

"Suala la kupinga ukatili wa kijinsia si la TAMWA pekee yake ni jukumu la kila mwananchi hivyo tusaidiane kubainisha changamoto hizo na sisi tutasimamia kutoa elimu katika kuhakikisha tunatokomeza hizo changamoto"alisema Bi Rose.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa, ametoa rai kwa wananchi wa Ruangwa kuacha kuwahamasisha watoto kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ya darasa saba na kidato nne kwa makusudi.

Mheshimiwa Mgandilwa  alisema mzazi atakayebainika anafanya jambo la kushawishi mtoto kufeli kwa kisingizo cha kukosa uwezo wa kusomesha atamchukulia hatua za kisheria.

Pia aliwataka wazazi wa Ruangwa kubeba majukumu yao kama wazazi kwa kuwasimamia watoto wao katika mienendo iliyobora na kuwahamasisha watoto hao kufanya vizur katika masomo yao.

Mgandilwa ametoa rai kwa uongozi wa TAMWA kusaidia kutatua changamoto zilizobainishwa na wadau ili kumaliza matatizo yanayowakabili watoto na wanawake.

"Nitoe shukurani za dhati kwa jitihada mnazozifanya TAMWA na nitapenda sana siku mkiniambia nije nizindue bweni mlilojenga kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotembea umbali mrefu hasa wa kike" alisema Mgandilwa.

Mjumbe wa mkutuno huo Esha Issa, amesema wanaochangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto ni wamama wenyewe kwani wamekuwa ndiyo watu wenye sauti kubwa katika familia na wanaitumia sauti hiyo vibaya.

"Wamama hatutaki watoto wetu wasemwe wakikosea hata ukiletewa mashitaka ya mtoto anafanya uhuni unakuwa mkali utaki kuamini na hata akipata mimba unaishia kusema acha aongeze dunia"alisema na kuongeza;

"Hili ni tatizo sana kwani watoto wetu wanakuwa hawana adabu na wanapata nguvu ya kufanya mambo ya ajabu kwasababu anaona mzazi mwenyewe unafurahia ujinga anaoufanya".

Mjumbe huyo amewashukuru uongozi wa TAMWA na  aliuomba uongozi huo kutoa elimu ya madhara ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watu wa ngazi ya kata na vijiji mara kwa mara ili kumaliza matatizo hayo katika jamii ya Ruangwa.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumapili ya March 31

















Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger