Kipa Klaus Kindoki amepangua penalti mbili na kuiwezesha Yanga SC kwenda Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya wenyeji, Alliance FC kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kindoki, mlinda mlango kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alipangua penalti za Dickson Ambundo na Nahodha wa Alliance FC, Siraj Juma, wakati kinda Martin Kiggi aligongesha mwamba wa kushoto.
Waliofanikiwa kumfunga penalti zao upande wa Alliance FC ni Joseph James, Geofrey Luseke na Samir Vincent, wakati za Yanga zilifungwa na beki Paul Godfrey ‘Boxer’, viungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko, Haruna Moshi ‘Boban’ na Deus Kaseke.
Vijana wazaliwa wa Mwanza na walioibukia mkoani hapa kisoka ndiyo waliokosa penalti zote za Yanga, beki Kelvin Patrick Yondan akigongesha mwamba na kiungo Mrisho Khalfan Ngassa mkwaju wake ukipanguliwa na kipa John Mwanda.
Katika dakika 90 za mchezo huo, Yanga SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Heritier Ebenezer Makambo dakika ya 38 kwa shuti la kitaalamu baada ya pasi ya kiungo Pius Charles Buswita.
Alliance FC walisawazisha bao hilo dakika ya 62, kupitia kwa kiungo wake wa ulinzi, Joseph James aliyemalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Mapinduzi Balama kutoka upande wa kulia.
Sasa Yanga itasafiri kuwafuata Lipuli FC Uwanja wa Samora mjini Iringa mwishoni mwa mwezi Aprili katika mchezo wa Nusu wa Fainali.
Nusu Fainali nyingine itafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwakutanisha Azam FC walioitoa Kagera Sugar kwa kuichapa 1-0 jana Bukoba na KMC ya Kinondoni walioitupa nje African Lyon kwa kuipiga 2-0 Jumatano Mbweni.
Kikosi cha Alliance FC leo kilikuwa; John Mwanda, Godlove Mdumule, Siraj Juma, Wema Sadoki, Geoffrey Luseke, Joseph James, Michael Chinedu/Samir Vincent dk58, Paul Maona/ Hussein Javu dk55, Bigirimana Blaise/Martin Kiggi dk90+3, Balama Mapinduzi na Dickson Ambundo.
Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gustapha Simon, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondan, Feisal Salum ‘Fei Toto’/Thabani Kamusoko dk77, Mrisho Ngassa, Papy Kabamba Tshishimbi, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Haruna Moshi ‘Boban’ dk61 na Pius Buswita/Deus Kaseke dk77.
Chanzo- Binzubeiry