Wednesday, 11 January 2017
MOKIWA AKATAA KUJIUZULU NGOMA BADO NZITO
Hali
ya amani ndani ya Kanisa la Anglikana nchini, bado si nzuri baada ya
Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa aliyevuliwa
uaskofu kutoa msimamo wake na kudai kuwa yeye ni msafi, na ndio Askofu
wa Dar es Salaam, hang’oki hata kwa dawa, na amewasamehe wanaompinga.
Askofu Mokiwa aliyasema hayo kwenye Kanisa la Anglikana Ilala jana, alipozungumza na waandishi wa habari. Alisema licha ya kusemwa mambo magumu, lakini yeye kama Askofu, kazi yake ni kuwaombea waliomkosea na hana matatizo nao, kwani amekwisha wasamehe.
Askofu
Mokiwa pia alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa Dayosisi ya Anglikana Dar
es Salaam haina mgogoro, bali viongozi watano wa dayosisi hiyo ndio
wanatengeneza mgogoro huo kwa maslahi binafsi, wakitumia Kanisa la
Anglikana la Mtakatifu Andrea la Magomeni kama njia ya kupitishia
migogoro yao.
“Siogopi
kusema baba askofu kapotoka katika hili, ameshauriwa vibaya na washauri
wake wa kisheria,”alisema Askofu Dk Mokiwa ambaye alimtaja Profesa
Palamagamba Kabudi kuwa mshauri wa kisheria wa askofu mkuu.
Kauli
hiyo ya Mokiwa imekuja siku chache baada ya kuvuliwa uaskofu, kwa kile
kilichoelezwa mashtaka 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa hilo
Dayosisi ya Dar es Salaam, yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, ndio
sababu ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Jacob Chimeledya kumvua
uaskofu.
Hata
hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo, kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni
Sinodi ya Dar es Saalam, ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na si
askofu mkuu; au askofu mwingine yeyote wa kanisa hilo Tanzania.
Uamuzi
wa kumvua uaskofu, ulichukuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Askofu
Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu, kama ilivyoshauriwa
na Nyumba ya Maaskofu, ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa
hilo na kukiuka maadili ya kichungaji, ambayo yalibainishwa kwenye
ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.
Akizungumzia suala hilo, Mokiwa alisema, “Alikuja
na maaskari zaidi ya 12 ambao wamevaa sare, na wengine ambao hawakuvaa
sare sijawajui idadi yake, askofu mkuu alidai amekuja kuleta mrejesho wa
halmashauri kuu, na matokeo yake akaishia kusema ameniondoa kwenye
huduma ya uaskofu.
"Nimesema
siondoki, na nimeona wanasema wataweka kila kitu hadharani, nawambia
hivi, mimi ni msafi na sina uchafu sehemu yoyote ile, wawe huru na amani
kuanika madudu yangu kama yapo, waweke tu hadharani wala siogopi.
“Ninavyo
vyombo halali kwenye Dayosisi hii ambayo hakutaka kukutana navyo
ambavyo ni Halmashauri ya Kudumu, hakuwahi kutaka kuwasiliana na sisi,
sisi tulitaka kuwasiliana na yeye, angejibu mawasiliano yetu ya kujenga
mahusiano na kutekeleza yaliyoamuliwa, hukutaka kutekeleza leo unakuja
na hoja ya kuniaondoa.
“Halmashauri
ya Kudumu inamwambia hatujawahi kumpelekea mgogoro sisi kama Dayosisi
ya Dar es Salaam, waswahili wanasema ‘jipu linamsumbua mwenye mwili
wake’, hujawahi kupelekewa neno lolote la machafuko, ni nani
aliyekwambia Dayosisi ya Dar es Salaam ina migogoro?
“Askofu
anafanya kazi na sisi, askofu ana vyombo vya kutawala, hana mamlaka ya
kujiamulia mambo yake mwenyewe, ukisema Dar es Salaam kuna machafuko
wewe Askofu Mkuu tunajua unasimama na watu na makundi katika Dayosisi
hii.
“
Yeye ni askofu kama mimi, yeye yupo Mpwapwa, tuna taratibu zetu kama za
bendera ukiingia mahali unashusha bendera kidogo, kwa nini Askofu Mkuu
afanye kazi na watu ambao sio sehemu ya mamlaka ya Dayosisi ya Dar es
Salaam.
“Halmashauri
Kuu inamwambia kwa kuwa amekuja na tamko lake bila ya kuwashirikisha,
wamemwambia Dar es Salama kuna askofu mmoja tu ni Mokiwa.
“Yeye
kama Askofu Mkuu hakupaswa kucheza nje ya Nyumba ya Maaskofu, mimi pia
naingia kwenye Nyumba ya Maaskofu, kuchomoka na kufanya kazi nje ya
taratibu, hii sio sawa.
"Askofu
Mkuu ana timu yake ya maofisa ambao wamemshauri vibaya, na yote
yaliyonukuliwa yote yamekosewa katika kusimamia taasisi, kila taasisi
ina uhuru wa kurekebisha pale palipoharibika pasipo kuingiliwa.
“Dayosisi
ya Dar es Salaam haina mgogoro na mimi ndio Askofu wake, mgogoro uliopo
ni wa kutengeneza, katika timu yake kuna watu wenye ‘interest maalum’
ambao ni Profesa Palamagamba Kabudi, yeye ndio mshauri mkuu wa askofu
lakini amekuwa akimpotosha, askofu akikosea na yule ni mwanasheria
aliyebobea na ndiye anayeingiza kanisa kwenye migogoro iliyobobea.
“Tumewahi
kuandikiwa barua na serikali Kanisa letu ndio vinara wa migogoro,
wamekuwa wakitengeneza mgogoro kati ya waumini na maaskofu wasielewane,
wakubwa waingie kushika hatamu za uongozi hapa.
“Nina
kibali cha kuzungumzia Dayosisi ya Victoria Nyanza Mwanza, uongozi wa
kanisa umeingia pia na kufanya kazi na makundi, kando ya taratibu,
kugombanisha askofu na watu wanaowangoza na kusababisha maumivu makubwa,
lakini nasema bila kufuata taratibu yeye akiwa kiongozi mkuu, ni hatari
sana kiongozi anayeacha kuongoza kwa taratibu na kufuata matakwa yake
mwenyewe. "
Ataja majipu 5 ndani ya Kanisa
Askofu
Mokiwa alisema kuwa ndani ya Kanisa hilo, kuna majipu ambayo yamekuwa
kiini cha migogoro kila kukicha na kuchafua taswira nzima ya kanisa
hilo.
“Askofu
Mkuu anashauriwa na Mwanasheria (Profesa Kabudi) anayeheshimiwa na watu
wengi, aliyezalisha wanasheria wengi zaidi katika nchi hii lakini
halitendei haki kanisa, halisaiidi kusimama sawa sawa, kuliokoa kanisa
na mvurugiko, haonekani mara zote kwa kuwa amejificha nyuma ya taratibu
hizo.
“Mwingine
ni askofu Oscar Mnung’a, Makamu Askofu Mkuu, huyu anakuja kufanya kazi
na makundi Dar ili aje kuwa askofu mkuu, alikuwa padri wangu na ni
askofu wa Newala, naamini watu wa Mpwapwa na Newala wanawafahamu, kuwa
ndio viongozi wao ndio chanzo cha maumivu kwenye kanisa hili.
“Mwingine
ni Johnson Chinyong’ole ni Katibu Mkuu, Padri wa Dayosisi ya Morogoro,
moyoni mwake anaamini mimi ndiye niliyebana asiwe askofu mkuu, nataka
kusema Kanisa Anglikana ni Kanisa kubwa nchi hii, alipaswi kuonekana na
dalili yoyote ya migogoro, lina uwezo wa kufanya mambo yake ndani bila
ya kuvuana nguo kama ilivyo sasa tena bila ya sababu za msingi.
“Askofu
mkuu anafanya kazi na Kanisa la Andrea Mtakatifu Magomeni, kule kuna
mtu anaitwa John Mhina, yule alikuwa Padri katika dayosisi yangu na
tulimuondolea haki za sakramenti na huduma za kichungaji mikononi mwake,
tulifanya hivyo kwa sababu ya kukiuka jambo moja tu la utii.
“Tulifanya
uhamisho katika Dayosisi ya Dar akagoma, akatengeneza tuhuma kwa
taasisi moja kubwa ambayo naiheshimu, na sitaki kukosea ikavurugikiwa
kwa sababu ya maneno ya kinywa changu, taasisi hiyo sina uchafu nao, na
sina uchafu popote.
“Sababu
ya Mhina kumuondoa ni kwamba haifai, mtu ni kuhani wa Mungu halafu
anaenda kukopa benki na kukimbia vielelezo ninavyo, benki alizokopa ni
BOA, Akiba Commercial Bank na Tanzania Investment ambayo iliwahi kumtoa
mpaka picha zake.
“Mwingine
ni Paul Mtweve alikuwa mkuu wa idara ya Uinjilisti, naye nilimuondoa
kwa sababu za kiuaminifu, kulikuwa na Saccos ambayo alijikopesha na sasa
imefungwa, wamechafua taswira nzima ya Dar es Salaam na ndio wamekuwa
wakitumika na askofu mkuu, ndio wamekuwa vinara wa kutengeneza mashaka.
Kuthibitisha kuwa wanafanya kazi na Askofu mkuu, uhamisho wa Mhina,
alipopinga kuhama, askofu Mkuu ‘alisapoti’, kwangu mimi kwa Dar es
Salama sio tena Askofu, mwaka jana sikukuu ya Matende alisema amehamina
Mpwapwa sasa sijui amebaki huko au vipi maana hapa sijamuona.
“Nilisali
Ubungo siku ya Krismasi, e-mail zilinaswa ambazo zilikuwa zikisambazwa
kwa wanangu wa Magomeni ambao hawakusali Krismasi kwa sababu walipewa
taarifa kupinduliwa kwangu, hivyo walijua kutakuwa na mapinduzi.
“Taasisi za dini hazipaswi kufanya kama hivi ni aibu, waumini wakimbilie wapi wakati wanaamini Kanisa ndio mahali salama.
“Waumini
watulie, kwa jimbo la Dar es Salaam hawatatusikia katika migogoro
yoyote, bado nina imani na waumini wa Dayosisi hii, tushikane pamoja,
kuifanya kazi ya Mungu.
“Tuna
shule, vituo vya watoto yatima, nataka ninaofanya nao kazi bila njaa,
na wale wanaocheza nje ya zizi, warudi kundini nitawakaribisha,” alisema.
Mokiwa
alifunguliwa mashtaka 10 Machi 2015 ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar
es Salaam, kupeleka michango pasipo maelekezo ya Sinodi ya Dayosisi ya
Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa Kanisa la
Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na Jimbo,
kinyume na katiba ya dayosisi.
Mashitaka
mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye
viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la Mtoni Buza na miradi
mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina
ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB,
kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu
huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na
waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke
na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa
yadi ya kuuza magari.
Pia
alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na
watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa
maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.
Askofu
Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation
iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo
ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi
kukaguliwa.
Tuhuma
zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga
mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia
fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga
Kalemi .
Hata hivyo akijibu tuhuma hizo Mokiwa alisema; Nyumba ya Maskofu Oysterbay
“Ile
nyumba haijatekelezwa bali vigae vilikuwa vinaanguka, nina kijana wangu
ambae ana matatizo mpaka sasa ni mkubwa lakini hasemi vizuri kuna siku
nilimkuta anacheza na nyoka, paa linavuja mvua zikinyesha, ndio niliamua
kuhama na sasa naishi nyumbani kwangu Mbezi Luisi.
“Kuna fedha Sh milioni 60 ambazo zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hiyo ikikamilika nitarudi kukaa.
“Silverhok
iliyopo Upanga, nyumba haikuwa kwenye hali nzuri jengo halikua salama,
ndio maana tuliwahamisha na jengo halijatekelezwa kwani tunataka
kulifanya la kisasa kama majengo mengine yanayozunguka eneo lile la
Mindu.
"Fedha
za DCB Kuna watu wanaeneza nimekuwa nikilipwa Shilingi bilioni 6 na
DCB, huku ndani mimi nimewahi kuunda chombo ambacho kinahusisha DCB
Magomeni, wa wawakilishi wa dayosisi, lakini Magomeni wenyewe ndio
wanakimbia vikao, DCB ndio waliojenga na ndio wanaolipa Kanisa Dayosisi
ya Anglikana.
“Kama
ni vita yenye maslahi, fanyeni uchunguzi mjue anayepokea fedha kutoka
DCB ni nani, mtapa ukweli kuwa ni Magomeni wenyewe, inashangaza wao ndio
wanakula na kushiba lakini ndio wamekuwa wakipiga kelele na kupotosha
watu.
“Kwa
mikono yangu niliwaidhinishia Sh milioni 200 za ujenzi wa Kanisa lakini
mpaka leo halijajengwa, mabati yapo pale yamesimama kama kaburi, hakuna
kilichofanyika na hela zimeliwa, waseme yote kwa ukweli na sio kuweka
siasa. "
Tuesday, 10 January 2017
MAPENZI YAZIDI KUCHUKUA ROHO ZA WATU JIJINI MBEYA
Katika
kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni ubaya wa mapenzi, kijana mmoja mkazi
wa Mbalizi Mbeya amefariki dunia kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni
wivu wa mapenzi baada ya baba wa mpenzi wake kumvamia kijana huyo na
kumshambulia.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya DCP Dhahiri Kidavashari amesema kuwa mnamo
tarehe 07.01.2017 majira ya saa 03:00 asubuhi katika Kijiji cha Dimbwe
kilichopo Kata ya Ulembo, Wilaya ya Kipolilsi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya,
mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la VARENCY POSTA mkazi wa kijiji cha
Dimbwe alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika kituo cha afya
Ilembo baada ya kuchomwa kitu chenye ncha kali kichwani na mtu
aliyefahamika kwa jina la MISIS EDWARD mkazi wa Dimbwe.
Inadaiwa
kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kutokana na binti wa
mtuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu.
Inadaiwa
kuwa mtuhumiwa kabla ya kutenda kosa hilo alimvizia njiani marehemu
akiwa anatoka kuangalia mpira na kisha kumchoma kitu chenye ncha kali
hali iliyosababisha kutokwa damu nyingi na kupelekea kifo chake akiwa
anapatiwa matibabu.
Kidavashari amesema mtuhumiwa amekamatwa na mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Katika
matukio mengine, Kamanda Kidavashari ametoa taarifa nyingine za mauaji
ambapo watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi waliuawa na wananchi
walioamua kujichukulia sheria mkononi baada ya kuvamia eneo la
wachimbaji wadogo wa dhahabu wakiwa na silaha aina ya Short gun
iliyotengenezwa kienyeji kwa lengo la kufanya unyang’anyi na ndipo
walizidiwa nguvu na wananchi hao.
Pia
amesema mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NURU ROMAN MWANG’OLELA
Mkazi wa Ubaruku Wilaya ya Mbarali na mwenyeji wa Bujela Kisale Wilaya
ya Kyela aliuawa kwa kupigwa mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na
kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa tuhuma za wizi.
Dr. Shein Akerwa na Kauli za Maalim Seif.......Asisitiza Yeye Ndo Rais Halali wa Zanzibar
Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi visiwani humo
kuacha kusikiliza maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani kwa kuwa
katu hakuna Rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo
madarakani.
Amesema
kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakipita mitaani na kujinadi kwa
wananchi kuwa huenda wakawa marais wakati wowote, huku wakimkataa yeye
kuwa si Rais halali wa Zanzibar.
Shein
alisema hayo jana baada ya kuzindua soko na ofisi ya Baraza la Mji la
Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 53 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Ingawa
Dk Shein hakutaja jina, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
ndiye ambaye amekuwa akitoa kauli za namna hiyo na juzi akihutubia
mkutano wa kampeni alisema, “Hata wafanye kitu gani mwaka huu msumari umewaganda na hivi karibuni Wazanzibari watafurahia mambo yao mazuri.”
Alisema mipango imara ya kuhakikisha kuwa mambo hayo yanakaa sawa inakwenda vizuri na wakati wowote matunda hayo yataonekana.
Maalim
Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015,
aliwataka wananchi na wanachama wa CUF wakae mkao wa kula.
“Sidhani
kama nitashindwa ila ikiwa nitaona dalili za kushindwa nawaahidi kuwa
nitawaambieni hadharani ili mchukue uamuzi ninyi wenyewe ya kudai haki
yenu katika uchaguzi uliopita,” alisema Maalim.
Maalim
Seif alifafanua kuwa ni jambo la kushangaza kuona kuwa Dk Shein
analazimisha wananchi kumtaja ndani ya misikiti, huku akihoji kama yeye
(Dk Shein) ni Rais kwa nini alazimishe kutajwa?
Lakini,
jana Dk Shein aliwataka wananchi kuacha kusikiliza na kufuata kasumba
hizo za wanasiasa kwa kuwa Serikali tayari imeshaundwa na yeye ni Rais
halali wa Zanzibar.
Alisema
anashangazwa kuona kuna watu wa aina hiyo wa kuwadanganya wananchi huku
wakifikiri kuna watu wa nje wenye uwezo wa kuingilia mambo ya Zanzibar.