Tuesday 3 January 2017

MWENYEKITI WA CHADEMA NA WENZAKE 7 WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Thomas Darabe na wenzake saba wamepandishwa kizimbani kujibu shitaka la kuharibu mali ya thamani ya zaidi ya sh milioni 75.4 na vitunguu.

Pamoja na Darabe, waliopandishwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha/ Arumeru ni Charles Lameck ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji ya ya vijiji saba vilivyoko katika wilaya ya Karatu na George Pius.

Wengine ni Baridi John, Christopher Lameck, Florian Tiofil, Daniel Ninida na Lazaro Emmanuel.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji alishitakiwa na mashitaka manne pekee yake ya thamani ya zaidi ya sh milioni 60 katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha na Mahakama ya Wilaya ya Arumeru.

Akisomewa shitaka la kwanza na Mwendesha mashitaka wa serikali, Charles Gakirwa mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda, alidai kuwa Desemba 28 mwaka huu mtuhumiwa alifanya uharibifu wa mali aina ya pampu ya maji ya thamani ya sh milioni tatu na bomba la maji la sh 448,000.

Shitaka la pili lililosomwa wakili wa serikali Gakirwa mbele ya hakimu mkazi wa wilaya ya Arusha , Devotha Msofe ilidaiwa kuwa Lameck alifanya uharibifu katika wa mfumo wa maji katika kijiji cha Quandet Karatu wa thamani ya zaidi ya sh milioni 1.6.

Mtuhumiwa alikana mashitaka yote na alipewa dhamana ya mtu mmoja na wadhamini wakifanikiwa kukidhi vigezo vyote katika mashitaka hayo. 
Katika mashitaka yaliyowahusu washitakiwa wote, akiwemo Darabe pamoja na Lameck ilidaiwa kuwa wote kwa pamoja walitenda kosa la uharibifu wa mali kwa kuchoma pampu ya maji ya thamani ya zaidi ya sh milioni tatu na injini ya maji ya thamani ya sh milioni 12.

Shitaka la tatu lililokuwa likiwakabili washitakiwa wote ni kuharibu mazao aina ya vitunguu ya thamani ya zaidi ya sh milioni 49 na pampu mbili za sh milioni sita. 
Washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na dhamana zao zilikuwa wazi na upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa bado haujakamilika na kesi hiyo itatajwa tena januari 16 mwaka huu.
Share:

MAJAMBAZI YAPORA MAMILIONI MBELE YA ASKARI POLISI DAR

Watu  wanaodaiwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea  jana saa 4 asubuhi wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo hilo la taa za Tazara.

Watu hao wameporwa katika eneo ambalo huwa askari doria wametanda, lakini wakikamata pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.

Aidha taa za Tazara yaliko makutano ya barabara kutokea Buguruni, Temeke, Kariakoo/Posta na Gongo la Mboto ndilo eneo lenye askari wengi wakiwemo wa usalama barabarani.

Wakati tukio likifanyika kulikuwepo askari wenye magwanda maalumu ya askari doria zaidi ya watano wakivurumushana na waendesha pikipiki upande wa Barabara ya Mandela kutokesa Buguruni. Hata hivyo imeelezwa kuwa watu hao waliokuwa wakipeleka benki hawakuwa na ulinzi kama inavyoshauriwa na Jeshi la Polisi.

Majambazi hao waliokuwa watatu, walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya Toyota Rav4 yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Richard Charles.

Kwenye gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China, aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.

Kwa mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha hizo benki eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao wakiwa na pikipiki aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni wakisubiri taa ziwaruhusu kupita kutoka barabara ya Mandela.

Charles alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi la fedha lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa bastola kabla ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha hizo na kutokomea nazo.

“Kwa kweli hata sielewi mpaka sasa hivi kilichotokea. Walikuja watu wawili mmoja upande wangu mwingine wa bosi wangu wakinitishia kwa bastola nifungue mlango niwape begi la fedha. Ghafla mtu mwingine akavunja kioo cha nyuma kwa kutumia kitako cha bastola na kubeba begi la fedha na kutokomea” alisema Richard.

Askari wenye silaha walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya tukio hilo wakaishia kuhoji. Hata hivyo askari mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake alilaumu tabia ya baadhi ya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuomba ulinzi wa polisi jambo linalohatarisha usalama wao na mali zao.

“Kama walijua wanasafirisha kiasi kikubwa hicho cha fedha kwa nini wasingeomba hata ‘escort’ (kusindikizwa kwa ulinzi) ya polisi? Hili ni tatizo, hasa katika kipindi hiki kigumu cha upatikanaji wa fedha, watu wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema.” alisema askari huyo.

Credit: Habari Leo
Share:

MOTO WATEKETEZA MADUKA 14 ARUSHA

Maduka 14 katika eneo la Mianzini jijini Arusha yameteketea kwa moto jana asubuhi na kusababisha hasara mbalimbali huku jeshi la polisi likiimarisha ulinzi na kusimamia shughuli za uokoaji wa mali zilizosalimika. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye baadhi ya majokofu yaliyokuwa katika baadhi ya maduka hayo. 
Kamanda Mkumbo alisema mara baada ya hitilafu hiyo, moto huo ulishika mitungi ya gesi iliyolipuka na kuanza kusambaa kwa kasi na kuunguza maduka hayo. 
Alisema wamefanikiwa kuokoa baadhi ya mali katika maduka tisa kati ya 14 kwa msaada wa wananchi na wasamaria wema waliokuwa katika eneo la tukio lakini ukubwa wa hasara bado haujajulikana.
 Mmiliki wa moja ya maduka yaliyoteketea, Zena Athuman alisema kabla ya kufungua biashara yake, alifika katika eneo la tukio na kukuta moto huo umeshaanza na hakufanikiwa kuokoa mali yoyote kwa kuwa moto huo ulikuwa ukisambaa kwa kasi ya ajabu. 
Shuhuda wa tukio hilo, Julius Sangeti alisema alifika katika eneo hilo saa 11:30 asubuhi na kushuhudia moto ukiwaka katika duka kubwa la Mianzini na kadri muda ulivyokuwa ukisonga, ndivyo ulivyokuwa ukihamia kwenye maduka mengine na kuteketeza mali.
Share:

RAIS JPM AZUIA CHAKULA CHA MSAADA MISENYI,ASEMA WANANCHI WACHAPE KAZI

Share:

Monday 2 January 2017

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA UDOM

  
KUISOMA
Share:

RAIS ATENGUA UTEZU WA MKURUGENZI MTENDAJI WA TANESCO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 01 Januari, 2017 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Felchesmi Mramba.

Kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Dkt. Tito Esau Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Tito Esau Mwinuka alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Uteuzi wa Dkt. Tito Essau Mwinuka unaanza mara moja.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Januari, 2017
Share:

MAGAZETI YA LEO JUMATATU JANUARY TAREHE 2.1.2017

Share:

LOWASA APONGEZA USHINDI WA TRUMP

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewapongeza raia wa Marekani kwa kumchagua Donald Trump kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Lowassa, Trump atakuwa rais mwenye kufanya uamuzi mgumu kwa kuwa ni shupavu na ana uwezo.

Trump ambaye ni Rais Mteule wa Marekani, alichaguliwa kuwa Rais mpya wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake, Hillary Clinton, mwishoni mwa mwaka jana.

Lowassa aliyasema hayo jana katika misa maalumu ya shukrani ya mwaka mpya 2017 iliyoshirikisha madhehebu mawili ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli na Kanisa Katoliki, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.

Ibada hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa Serikali na wa vyama vya siasa, wakiwamo Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye pia ni Katibu wa Chadema, Mkoa wa Arusha.

“Wamarekani hawakufanya makosa kumchagua Trump kwani anaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza Taifa hilo tajiri duniani ambalo linategemewa na mataifa mengine.

“Dunia imebadilika, amechaguliwa rais mmoja huko Marekani ambaye ni mwamba kweli kweli.

“Hatuwezi kumtabiri mambo yake yatakavyokuwa, lakini inabidi kila mtu afanye kazi kwa bidii na kwa maarifa kwa sababu huyo hakubali upuuzi wowote,”alisema Lowassa.

Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Monduli kwa miaka 20, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuacha kulalamika kwani hiyo ndiyo njia iliyo sahihi ya kuweza kuondokana na umasikini.

“Mwaka jana, tarehe kama hii, tulimuaga Mbunge Julius Kalanga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isack Joseph, nikawaambia nawatakia heri wachape kazi vizuri, naona wamefanya vizuri au siyo?alihoji Lowassa.

Akizungumzia upande wake, Lowassa alisema hivi sasa anafanya siasa za kimataifa tofauti na siasa alizokuwa akifanya kipindi kilichopita.

“Mimi sitaki kusema sana maana watasema napiga siasa. Siku hizi napiga siasa za kimataifa, naomba niwatakie heri ya mwaka mpya na kila mtakachoshika, Mungu akibariki kiwe dhahabu,”alisema
Share:

Tulia: Tanzania mpya inawezekana

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amesema kuwa Tanzania mpya yenye matokeo chanya kwa mwaka 2017 iwapo inawezekana  iwapo kila mmoja wetu atafanya kazi kwa bidii ili kuliletea taifa maendeleo.

Ameyasema hayo wakati wa ibaada maalum  ya mkesha wa kitaifa wa mwaka mpya uliofanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam, Dk. Tulia amewataka watanzania kuwa na ushirikiano wa pamoja ili kufikia maendeleo.

“Tanzania mpya na nchi mpya yenye matokeo chanya kwa mwaka 2017 inawezekana hivyo tushirikiane kwa pamoja na kila mmoja akifanya kazi kwa bidii, lazima maendeleo yatapatikana tu”amesema Dk. Tulia.

Aidha, amewataka watanzania kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali ili waweze kupata maendeleo kwa haraka zaidi.
Share:

Sunday 1 January 2017

MAGAZETI YA LEO JUMAPILI JANUARY TAREHE 1.1.2017

Share:

MWANAFUNZI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA MFANYABIASHARA TARIME



MFANYABIASHARA Robert Mwikwabe, maarufu kama Ndugu, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga risasi ya kichwani na kusababishia kifo papo hapo mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Sirari, Masaite Mrimi(17).
Kutokana na tukio hilo, Mwikwabe ambaye pia ni mmliki Hoteli katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, alinusurika kuteketezwa yeye na familia yake Hali hiyo ilitokea baada ya wananchi kuamua kuchoma moto lori la mfanyabiashara huyo na kwenda nyumbani kutaka kuchoma hoteli.
Mashuhuda walisema tukio hilo ni la juzi mchana, jirani na nyumba anayoishi mwanafunzi huyo, eneo la stendi mpya ya mabasi na malori ya Ngerengere.
Walisema mfanyabiashara huyo alifika akiwa na lori lake likiwa na mawe na alisimama na kutaka kuchukua pumba za mchele, zilizomwagwa na malori yanayosafirisha ng’ombe kwenda nchini Kenya.
Eneo hilo ni jirani na nyumbani kwao marehemu, ambako kulitokea mzozo kati ya Robert na wazazi wa mwanafunzi huyo. Kufuatia mzozo huo, mwanafunzi huyo aliyekuwa na panga mkononi, alimtishia kumkata Robert, ambaye alichomoa silaha yake aina ya bastola na kumpiga risasi kichwani na kumsababisha kifo.
Baada ya tukio hilo, familia ya marehemu na wananchi walianza kumfukuza Robert aliyeacha lori lake likiwa na mawe na kukimbilia lori lake lingine la jirani. Kisha alikimbilia Kituo cha Polisi Sirari, kuokoa maisha yake.
Umati mkubwa wa watu kutoka vijiji vya Ngerengere na Sirari, walikwenda nyumbani kwa mfanyabiashara huyo kwa lengo la kutaka kuchoma moto hoteli na nyumba.
Lakini, polisi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga walifanya juhudi kubwa kuwazuia wananchi hasa vijana, kuacha kuteketeza mali za mfanyabiashara huyo yakiwemo magari, ambayo sasa yamehifadhiwa kituo cha polisi kwa ajili ya usalama.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime-Rorya, Andrew Satta alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kwamba maiti imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Tarime.
Share:

ATUMBUKIA GHAFLA KWENYE CHEMBA YA MAJI TAKA YENYE UREFU WA FUTI 12 DAR


Mkazi wa Temeke Mikoroshoni, Miradji Sanyero, jana alipatwa na mkasa wa kutumbukia katika ‘chemba’ ya kupitishia maji taka yenye urefu zaidi ya futi 12, iliyopo eneo la Bakhresa, Tazara, Barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.
Alipatwa na mkasa huo akiwa katika harakati ya kujitafutia maisha, ambapo ghafla alitumbukia katika chemba hiyo iliyokaa vibaya katika mlango mkuu unaotumiwa na magari makubwa wa ofisi za Bakhresa.
Akijojiwa, akiwa mahututi, alisema “Nilikuwa napita jirani huku nikichukua tahadhari nisigongwe na magari yanayoingia na kutoka katika ofisi hizo, ndipo nikajikuta ghafla nimetumbukia ndani ya chemba hii na kuumia kidole cha mkono wa kulia, miguuni na mbavu ambazo sasa zinauma sasa”.
Wafanyabiashara wadogo (machinga) wa eneo hilo, walisema chemba hiyo ni hatari na watu kadhaa wametumbukia katika kipindi cha hivi karibuni. Walidai huyo alikuwa mtu wa tatu.
“Tunaomba Tanroads wafike eneo hili, waone kisha wazibe chemba hii. Kama hawatafanya hivyo, kuna hatari ya kupoteza maisha hasa watoto wadogo ambao uwezo wao wa kuhimili vishindo ni mdogo sana” alisema machinga mmoja, Ali Tematema.
Gazeti hili lilishuhudia baadaye trafiki wakishirikiana na wananchi, wakimsaidia Sanyero kwenda kupanda bajaji kwenda Polisi kuchukua Fomu Namba 3 ili aende hospitali kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Chanzo-Habarileo
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger