Friday 30 December 2016
Thursday 29 December 2016
Bodi ya Mikopo yaja na mbinu nyingine ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu
BODI
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia mwanzoni
mwa Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa sugu
kwenye vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu
ya juu kuanzia wale wa miaka 10 iliyopita.
Bodi
hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30, mwaka
huu, kwa wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo,
vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika
kulipia gharama za kuwasaka na kuendesha kesi.
Pamoja
na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo iliyofanyiwa
marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa kuwabana waajiri
wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi cha kuhakiki
waajiriwa wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB,
na adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi
hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa muda huo wa siku 30
walioutoa, wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa hawajajisalimisha
wenyewe kwa hiari, kulipa madeni yao wataanikwa hadharani na picha zao.
“Tumeamua
kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua wadaiwa
hawa wa bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka ili
waturejeshee fedha zetu,” alisema Badru.
Aidha,
alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni kuutangazia
na kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi wengine kukosa
fursa ya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha iliyopo bado
haitoshelezi.
Alisema
bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na baadaye
kuwaongezea tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka huu,
hivyo kinachofuata ni utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia fursa
hiyo ya kujisalimisha.
Mkurugenzi
huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza kuchapisha
majina na picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa kushindwa
kulipa madeni yao, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kulipia gharama za usumbufu wa kuwatafuta.
Alisema
utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi zaidi,
kupata fursa ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni vyema
wanafunzi wote wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa muda
muafaka uliowekwa kisheria.
Badru
alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo,
imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na mikopo
kutoka miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga na
kutafuta ajira.
Aidha,
alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa
waajiriwa walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya
mishahara yao hadi asilimia 15.
“Tunawashukuru
sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija kwenye sheria hii
katika eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato kifikie hadi
asilimia 30 na zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo
wa wabunge walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,” alisema.
Alisema
ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo hiyo
aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi hiyo
imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria
kupitia marekebisho hayo ya sheria.
“Tumeunda
kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali
nyeti, kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka huu, ya
kuhakiki kila ofisi ya waajiri sugu ili kubaini kama ama wamewasilisha
majina ya wanufaika wa mikopo hii au wanawakata bila kuwasilisha
michango hiyo kwa bodi,” alisema.
Alisema
waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa kutoisaidia
bodi kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato yao,
wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua makato
hayo waliyoshindwa kuyawasilisha na endapo watashindwa watakabiliwa na
adhabu ya kifungo cha muda wa miezi 36 jela.
“Lakini
pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha wanapeleka
wenyewe taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa makato,
yeyote atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye atawajibishwa,” alisisitiza.
Halikadhalika,
Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa wanufaika wa
mikopo hiyo ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira,
ambao nao wanatakiwa kurejesha kiasi kisichopungua Sh 100,000 kila
mwezi.
Akizungumzia
mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa sugu kulipa
wenyewe madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya fedha,
yameongezeka kutoka Sh bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh bilioni
nane.
Alisema
tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza wenyewe
kwa hiari na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote na
wengine wakiyapunguza.
Hadi
sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva,
inazozidai kwa wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140
pekee ndio zimelipwa.
Kwa
mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179
wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu
ianzishwe Juni, mwaka 1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa
wanafunzi hao.
Jumla
ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na mikopo ya
HESLB, wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi cha Sh
trilioni 1.4, baada ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria
kuisha.
Hapi Aishika Pabaya Kampuni Ya ZanteL,Yalipa Mapato Zaidi Ya Milioni 687 Ndani Ya Siku 7 Ilizopewa
KAMPUNI
ya simu za mkononi ya Zantel Tanzania imelipa zaidi ya Sh milioni 687
baada ya kupewa siku saba na halmashauri hiyo iwe imelipa fedha hizo
ambazo zilikuwa za kodi ya pango inazodaiwa na manispaa hiyo.
Fedha
hizo zililipwa Desemba 21 na mkataba huo wa zamani unaisha Januari
mwakani ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema wanaandaa
mpya wenye viwango vya malipo vya sasa.
Aidha
halmashauri hiyo imeamua kuelekeza fedha hizo ambayo ni sh 687,931,040
katika ujenzi wa vyumba vya madarasa 40 katika halmashauri hiyo kwamba
kama itaonekana inawezekana kujenga shule nyingine mpya ya sekondari.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Hapi alisema fedha
hizo zimelipwa baada ofisi yake kubaini mchezo mchafu uliokuwa umefanywa
na watendaji wa halmashauri yake waliokuwepo huko nyuma ambao walificha
mkataba kati yake na Zantel.
Aidha
aliipongeza Zantel kwa kutii maagizo waliyopewa na kulipa fedha hizo na
tayari wamepewa risiti kuonesha kupokea fedha hizo na kwamba watu wote
waliohusika katika jambo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema baada ya malipo hayo, ameelekeza Manispaa kutumia fedha zote hizo kujenga vyumba vya madarasa katika halmashauri hiyo.
“Takwimu
zinaonesha mwaka huu watoto 19,000 walifaulu katika Halmashauri ya
Kinondoni waliochaguli kujiunga na Sekondari ni 12,889 na hadi sasa
wanafunzi 3,169 hawajapata nafasi katika shule zetu kwasababu ya ufinyu
wa madarasa,” alisema Hapi.
Waziri Mkuu Achangia Mabati Ujenzi Wa Zahanati
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani Ruangwa
waharakishe kufyatua matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye
atawachangia mabati.
Ametoa ahadi hizo jana
(Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji
vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na
Chibula na viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita
kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo.
Waziri
Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.Alisema
sera ya Serikali ni kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya
kwa kila kata na kwamba umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya
jimbo hilo inayosema “Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”
Katika
kuhimiza ujenzi wa zahanati hizo, alichangia mabati kati ya 50 na 150
kwa kila kijiji na akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi
wa maboma ili aweze kutimiza ahadi yake ya mabati.
Alisema
katika awamu iliyopita, alikazania sana suala la elimu kwa kusimamia
ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa na
madarasa ya kutosha. Pia alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika
baadhi ya shule.
“Kuanzia
awamu hii na miaka minne iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia
upatikanaji wa maji safi na suala la kuboresha sekta ya afya katika
jimbo zima nikishirikiana na uongozi wa Halmashauri yetu,” alisema.
Pia
alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe
anawasiliana na viongozi wa vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani
zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Wakati
huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar Specialist,
Bw. Ansi Mmasi alisema atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts 300
pamoja na nyaya zake kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji
cha Namilema.
Alisema
anaishukuru kwa kuwapa kazi makandarasi wazawa na akawataka wakandarasi
wenzake watumie vifaa bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa
huduma na taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.
“Tujitahidi
kufanya kazi hizi kwa weledi na tutumie vifaa bora na imara ili watu
wanaotarajia huduma zetu waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani na
wakandarasi wazawa kwamba tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora
unaotakiwa,” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi
J. Bakili alisema atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa
zahanati hiyo ya kijiji cha Namilema. Pia alichangia mifuko 100 kwenye
zahanati ya kijiji cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi
wa zahanati ya kijiji cha Chikundi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Watu 7 Wafikishwa Mahakamani kwa kumchoma mkuki mdomoni mkulima
POLISI
mkoani Morogoro imewafikisha mahakamani watu saba kati ya 12, kujibu
tuhuma za kumjeruhi kwa kumchoma mkuki mdomoni hadi kutokea shingoni,
Augustino Mtitu (35).
Walipandishwa
kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa huku wengine watano,
wote wakazi wa kitongoji cha Upangwa wilayani Kilosa wakisubiri
kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana alipokuwa
anazungumzia msako uliofanywa na polisi na kufanikisha kukamatwa kwa
watuhumiwa hao baada ya kutokea kwa tukio hilo Desemba 25, mwaka huu,
majira ya saa tano asubuhi eneo la kitongoji cha Upangwa, Kijiji cha
Dodoma Isanga, Kata na Tarafa ya Masanze wilayani Kilosa.
Kamanda
Matei alisema katika msako huo, watu 12 walikamatwa na saba kati yao
tayari wamefikishwa mahakamani. Wengine watano watafikisha mahakamani
baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Hata
hivyo, Kamanda huyo aliwataja majeruhi wa tukio hilo mbali na Mtitu
ambaye bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro, kuwa ni George Andrew (68) aliyejeruhiwa kichwani.
Wengine
ni Yohana Wisa (26) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Mathayo Elia (34)
aliyejeruhiwa kichwani na bega la kushoto, Josephat Mtitu (55)
aliyejeruhiwa begani na shavuni na mwingine ni Paulo Thomas (56)
aliyejeruhiwa mbavu na mkono wa kushoto.
Wote
ni wakazi wa kijiji cha Dodoma Isanga na wanaendelea vizuri. Hivi
karibuni, baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai waliwashambulia kwa
silaha za jadi na kuwajeruhi watu sita akiwemo Mtitu mara baada ya
kukamata mifugo ya mtu mmoja aitwaye Ngoyoni Kimang’ati, iliyokuwa
ikiharibu mahindi shambani.
Mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya yaongoza kwa maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI
Kutokana
na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kupungua kwa asilimia 50
duniani kote na kupelekea watu milioni 2.1 tu kuambukizwa Virusi vya
Ukimwi katika mwaka 2015,kumeibua matumaini mapya ya kuwa na watu wasio
na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini Tanzania (TACAIDS) Dkt.
Leonard Maboko aliwaambia waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam
kuwa, nchini Tanzania maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi nayo
yameshuka kwa asilimia 20 ambapo watu 54,000 wameambukizwa virusi hivyo
kwa mwaka 2015 pekee.
Dkt.
Maboko alisema, Ukimwi bado ni janga kubwa duniani na taifa kwa ujumla
huku akitaja kundi la wanawake kuwa ndilo lina kiwango cha juu cha
maambukizi ya VVU huku mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya ukiwa na kiwango
cha juu cha maambukizi hayo kitaifa.
Aidha,
alisema serikali imejiwekea mikakati kuhakikisha kuwa waliogundulika
kuwa wameathirika wanaanzishiwa dawa, kuhimiza matumizi ya mpira wa
kiume, kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 29 na kutoa elimu kwa
wanawake wanaojihusisha na ngono, kupunguza maambukizi ya virusi vya
Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Wassira akimbilia Mahakama ya Rufaa kumpinga Bulaya
WAZIRI
mwandamizi wa serikali ya Tanzania kwa awamu nne za uongozi, Stephen
Masato Wassira, kupitia kwa wafuasi wake watatu, amekata rufaa Mahakama
ya Rufaa, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kuhalalisha ushindi wa
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema).
Wassira
(71 ) alikuwa waziri kwa mara ya kwanza tangu Desemba 07, 1973 akiwa
naibu waziri wa Kilimo na ameendelea kuwa kiongozi mwandamizi wakati wa
serikali ya Mwalimu Julius Nyerere, akarithiwa wakati wa Rais Ali Hassan
Mwinyi, baadaye Rais Benjamin Mkapa na hatimaye uongozi wa awamu ya nne
wa Rais Jakaya Kikwete.
Tayari
wafuasi hao wa Wassira; Magambo Masato, Matwiga Matwiga na Ascetic
Malagaila, wamefungua kesi hiyo na imesajiliwa katika ofisi za mahakama
ya rufaa jijini Mwanza tarehe 16 Desemba, 2016 na itakuwa ni kesi ya
rufaa namba 199 ya mwaka 2016.
Katika rufaa hiyo iliyoandikwa na wakili wao, Constatine Mutalemwa, wametoa sababu kadhaa kama hoja zao za kukata rufaa.
Kwanza, wanadai kwamba jaji hakuzingatia makosa yaliyofanyika baada ya zoezi la kupiga kura.
Pili, Wassira au wakala wake wanadai hakuitwa kwenye majumuisho kujulishwa siku, mahali wanafanyia majumuisho.
Tatu, wanadai kuwa jaji hakutilia maanani kesi zinazofanana na hii zilizotolewa kama mfano mahakamani.
Nne, Jaji alikosea kutoa uamuzi kwa misingi ya maoni binafsi badala ya kuzingatia mambo ya maana.
Wanadai kuwa jaji alisema wananchi wa Bunda ni maskini waachwe wafanye shughuli za maendeleo kwa sasa.
Tano, wanadai jaji alikosea kuamua kuhusu sheria ya viapo na matamko iliyotajwa katika kanuni za kuendesha kesi za uchaguzi.
Novemba
18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitoa uamuzi wa kesi ya
kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliompa ushindi Mbunge wa Bunda
Mjini, Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wassira (CCM).
Kesi
hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu
Kanda ya Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, mkoani Mara.
Mahakama
hiyo ilieleza kutoridhishwa na ushahidi wa kupinga matokeo hayo
uliowasilishwa na upande wa walalamikaji, hivyo ikamthibitisha Bulaya
kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.
Kesi
ya kupinga matokeo hayo ilifunguliwa na wafuasi wa Wassira ambaye
alikuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuondolewa kupitia uchaguzi mkuu
uliofanyika mwaka jana.
Katika
kesi ya msingi, walalamikaji ambao ni wakazi wa Bunda walidai kuwa
uchaguzi haukuwa huru na haki kwakuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa,
mgombea wanaemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo pamoja na
kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.
Katika kesi hiyo, Bulaya alitetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
Credit: FikraPevu
Bodi ya Mikopo yawatosa Watanzania wanaosoma China
Watanzania
waliopata ufadhili wa kusoma nchini China, hawatapata mikopo baada ya
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwaondoa kwenye
orodha ya wanufaika.
Taarifa
iliyotolewa na HESLB, ikijibu Ubalozi wa Tanzania nchini China, kuhusu
madai ya kuchelewa kwa fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaosoma nchini
humo imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia kwamba wanafunzi wote wanaopata ufadhili kutoka
nchi rafiki watajitegemea ikiwamo gharama za tiketi za ndege.
Barua
hiyo ya Desemba 20, 2016 iliyomnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo,
Abdul Razaq Badru inaeleza kuwa mwaka huu wanafunzi hao hawatanufaika na
mikopo kama ilivyokuwa ikitolewa miaka ya nyuma.
Jana,
akizungumza na waandishi wa habari, Badru aliitambua barua hiyo huku
akisita kutolea ufafanuzi wake kwa madai ilikuwa ni majibu kwa wanafunzi
hao wa China.
Hata hivyo, alisema endapo kutakuwa na madai kutoka kwa wanafunzi hao watalazimika kutolea ufafanuzi.
Akizungumzia
suala hilo Naibu Waziri Elimu, Stella Manyanya alisema ni hekima zaidi
kuangalia au kusaidia wanafunzi wa ndani wasiokuwa nacho kuliko
wanaopata ufadhili wa nje ya nchi.
Wednesday 28 December 2016
SEKRETARIETI YA AJIRA DAR IMEFAFANUA TAARIFA KUHUSU KUFUTWA KWA AJIRA SERIKALINI WALIOFAULU USAILI
TAARIFA KWA UMMA
Mnamo tarehe
26 na 27 Desemba, 2016 baadhi ya mitandao ya kijamii imeandika taarifa
zenye nia ya kupotosha Umma ambazo Sekretarieti ya Ajira inapenda
kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo;-
1. Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa ufafanuzi
kufuatia hoja iliyoandikwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii ya
tarehe 27 Desemba, 2016 zenye vichwa vya habari vinavyosomeka “Waliofaulu usaili ajira serikalini kufutwa” na “Taarifa kwa waliokuwa wakisubiri kupangiwa vituo vya kazi kabla ya ajira kusitishwa serikalini”
zikidaiwa kutolewa na Taasisi hii katika majibu ya hoja za mwezi
Novemba, 2016 katika utaratibu wake wa kujibu hoja za kila mwezi kama
ifuatavyo;-
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Sekretarieti ya Ajira
tangu mwezi Juni, 2016 Serikali ilipositisha Ajira hapakuwa na orodha
ya waombaji kazi waliokuwa wakisubiri matokeo ya usaili, kwa kuwa
usaili wa mwisho ulioendeshwa na Sekretarieti ya Ajira ulifanyika mwezi
Mei, 2016 na waombaji waliofaulu walipangiwa vituo vya kazi kwa idaidi
ya nafasi zilizokuwepo.
Aidha, kwa wale ambao walifaulu na hawakuweza
kupangiwa vituo vya kazi kutokana na kukosekana kwa nafasi zilizokuwepo
walihifadhiwa katika kanzidata (Database) ambayo hudumu kwa muda cha
miezi sita (6) baada ya matokeo ya usaili husika kutolewa.
Baada ya ufafanuzi huo hususani aya ya tatu
Sekretarieti ya Ajira ingependa kufafanua zaidi namna kanzidata ya
waliofaulu usaili inavyotumika ili kuweza kuwa na uelewa wa pamoja kwa
wadau na jamii kwa ujumla ili kuepusha kupokea ama kusikia taarifa
zisizo rasmi zenye nia ya kupotosha Umma zinazojitokeza mara kwa mara
hususani katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Kanzidata ya waliofaulu usaili:
Kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa shughuli za
Sekretarieti ya Ajira za mwaka 2016, Kanuni ya 21. (1) - (5) imefafanua
juu ya kanzidata kama ifuatavyo;-
(1) Baada ya waombaji waliofaulu usaili kuwapangia
vituo vya kazi, orodha itakayobaki itatunzwa na Katibu katika kanzidata
ili pale itakapotokea fursa ya ajira orodha hiyo iweze kutumika.
(2) Orodha ya waombaji walioko kwenye kanzidata
itatumika kujaza nafasi wazi kulingana na mahitaji ya Waajiri. Hata
hivyo, wakati wa upangaji, Katibu atazingatia mpangilio wa matokeo ya
alama za ufaulu wa mwombaji kwa aliyepata alama za juu zaidi ya wengine
kufikiriwa kwanza.
(3) Sekretarieti itatangaza nafasi wazi za ajira na
kufanya usaili endapo orodha iliyotunzwa katika kanzidata itakuwa
imekwisha au haina mtumishi mwenye utaalam au sifa zinazohitajika na
Mwajiri.
(4) Endapo katika orodha iliyotajwa kwenye Ibara ya
21(2) kutakuwa na waombaji waliopata alama zinazolingana, utaratibu
ulioainishwa katika Ibara ya 14(1) utazingatiwa.
(5) Orodha ya kanzidata itadumu kwa kipindi cha miezi sita (6) tangu kuidhinishwa kwa matokeo na Wajumbe wa Sekretarieti.
2. Sekretarieti ya Ajira pia
inapenda kutoa ufafanuzi kwa taarifa nyingine iliyoandikwa katika
mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari kinachosema “Mhe
Rais Magufuli nakuomba Sekretarieti ya Ajira uifute maana haina majukumu
sasa hivi lengo la Sekretarieti ya Ajira ni kutangaza kazi na ........”. kama ifuatavyo;-
Ni vyema wadau wa Sekretarieti ya Ajira na Jamii
kwa ujumla ikafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
ilianzishwa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma
Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (1). Kwa mujibu wa Sheria ya
Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.
18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (6) (a-f) na Sera ya Menejimenti ya
Ajira toleo Na. 2 la mwaka 2008 Sekretarieti ya Ajira ina majukumu
yafuatayo;-
i. Kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na
kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam hao ili
kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika,
ii. Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo Vikuu
na Wataalam Weledi (Professionals) kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na
ujazaji wa nafasi wazi za ajira katika Utumishi wa Umma,
iii. Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazotokea katika Utumishi wa Umma.
iv. Kuhusisha wataalam maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji,
v. Kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na ajira,
vi. Kufanya kazi nyingine yoyote inayoendana
na majukumu yake kadri itakavyoelekezwa na Waziri mwenye dhamana ya
Utumishi wa Umma.
Kutokana na ufafanuzi huo Sekretarieti ya Ajira
ingependa jamii ifahamu mbali na jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira
ina majukumu mengine inayoyatekeza kama yalivyoainishwa hapo juu kwa
mujibu wa Sheria.
Riziki V. Abraham
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Sekretarieti ya Ajira.
27 Desemba, 2016.
MWALIMU ASHUSHIWA KIPIGO KWA KUMCHARANGA MAPANGA MWANAFUNZI WAKE SIKU YA KRISMASI
Mwalimu Pendo akipata matibabu
*****
MWANAFUNZI Marco Limbe(14) aliyemaliza
darasa la saba mwaka huu katika shule ya msingi Yitwimila iliyoko kata
ya Kiloleli wilaya ya Busega mkoani Simiyu amelazwa katika kituo cha
afya Busega mara baada ya kuchalangwa mapanga kichwani na mdomoni na
mwalimu wake.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa
11.30 jioni wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akirejea nyumbani kwao
akitokea katika malisho ya mifugo,alipokaribia katika shamba la mwalimu
Pendo Gabriel ndipo mwalimu huyo alimkamata kijana huyo na kuanza
kumcharanga kwa panga na kusababisha kijana Limbe kupoteza fahamu kwa
muda wa masaa 6.
“Shuhuda wa tulio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Manoga anasema
ilikuwa kama mchezo lakini kumbe ni kweli kwani niliona mifugo ya Limbe
iliyokuwa ikielekea nyumbani na huku Limbe akiwa nyuma ya mifugo hiyo
katika barabara ambayo iko karibu na maeneo ya shule, ghafla nilimuona
mwalimu Pendo wakishikana na kijana huyo na ndipo nikamuona akiwa na
panga na kuanza kumcharanga”,alieleza.
"Nilikimbia katika tukio na kutoa msaada kwa wote lakini, watu walijaa
na kuanza kumshambulia mwalimu Pendo kwa kumpiga ingawa jaribio hilo
lilikwama baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho Mshemas Bahai.
Mwandishi wa habari hizi alikwenda katika kituo cha afya cha Nyashimo na
kujionea hali mbaya kwa kijana Limbe ambaye alikuwa amepoteza fahamu
kwa muda wa masaa 6 bila kujitambua na huku akiwa anaongezewa drip na
kwa pembeni mwalimu Pendo Gabriel naye akipata matibabu ya jeraha lake
kichwani ambAlo alishambuliwa na wananchi na huku akiwa chini ya ulinzi
wa jeshi la polisi.
Mwenyekiti wa Sogesca Bahai Mshemas alisema sikukuu Krismasi imekuwa ni
mbaya katika kijiji chake baada ya wananchi wenye hasira kali kufanya
shambulio la kumshambulia mwalimu Pendo kwa kosa la kumcharanga na panga
mwanafunzi wake aliyekuwa akitokea kwenye malisho na kupita karibu na
shamba lake la mahindi akitokea katika malisho.
Hata hivyo alisema alifanikiwa kuwatuliza wananchi wa kijiji chake na
kuanza kufanya mikakati ya kuwapeleka kituo cha afya ili wapate huduma
za matibabu.
Aliongeza kuwa walifika polisi na kuandikiwa barua ya kwenda kutibiwa wote wawili mwalimu pamoja na mwanafunzi.
Kwa upande wake kaimu mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya Dk. Ayubu
Ismail alithibitisha kuwapokea kwa majeruhi hao na kudai kuwa kijana
Limbe ndiye aliyekuwa na hali mbaya zaidi kuliko mwalimu Pendo.
Aliongeza kuwa kijana ameshonwa nyuzi 9 katika sehemu zake zote alizopatwa na majeraha na huku mwalimu akishonwa nyuzi 6.
“Ni kweli Limbe alikuwa ametokwa na damu nyingi sana na hivyo kumpelekea
kupoteza fahamu kwa muda wa masaa 6 lakini hali yake inaendelea vizuri
alisema Dk. Ismail”.
Na Shushu Joel- Busega