Saturday, 31 August 2024
WAANDISHI WA HABARI WATEMBELEA CHEMCHEMI YA AJABU YA KONDOA MJINI.. "KUNA ULINZI MKALI WA NYOKA WATATU"
Mmoja wa walinzi wanaolinda eneo hilo anasema chemchemi hiyo ina ulinzi mkali wa nyoka watatu wakubwa ambao huonekana nyakati za usiku wakizunguka kwenye chemchemi lakini pia endapo katika eneo hilo akaingia mtu mwenye nia ovu/mbaya nyoka hao huonekana hata kama ni mchana ili kuzuia janga.
NDOTO YA RAIS SAMIA NI KUWA NA MASHIRIKA YENYE UFANISI - BALOZI Dkt. KUSILUKA
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka amesema kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inakuwa na mashirika yenye ufanisi mkubwa na wa viwango vya kimataifa.
Hivyo, amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa taasisi na Mashirika ya Umma kuhakikisha wanatekeleza kwa ukamilifu maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais Samia.
Ametoa kauli hiyo leo Agosti 30, 2024 jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika jijini humo tangu Agosti 27 hadi 30, 2024.
"Serikali itayachukua maazimio yote yaliyokubaliwa na nawaahidi yatafanyiwa kazi, tutawasaidia kuhakikisha yanatekelezeka ili kutimiza ndoto ya Mhe. Rais Samia juu ya taasisi na mashirika ya umma", amesema Balozi, Dkt. Kusiluka.
Amewataka viongozi wa taasisi na mashirika ya umma kujenga utamaduni wa kujifunza mbinu na mikakati mipya kutoka kwa mashirika yaliofanikiwa na kuitazama serikali kwa upana wake.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Mbaga Kida amesema kuwa wamewasilisha malengo na wanaamini watayasimamia malengo hayo ili kuweza kuhakikisha yale waliyojiwekea katika kusimamia na kuboresha utendaji kazi wa taasisi na mashirika ya umma yanaweza kufikiwa.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesoma jumla ya maazimio sita yaliyoazimiwa na viongozi hao ikiwemo, Ushiriki katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2050 na uandaaji wa mipango mkakati wa taasisi za umma; Utawala bora na mawasiliano ya umma pamoja na Usimamizi wa rasilimali watu, mafunzo na uendelezaji wa uongozi bora.
Maazimio mengini ni, Mikakati ya taasisi na mashirika ya umma kuwekeza nje ya Tanzania; Kuongeza uchangiaji na kupunguza utegemezi katika Mfuko Mkuu wa Taifa na kutekeleza kikamilifu maazimio yaliyotolewa kwenye kikao kilichopita ambayo hayajatekelezwa.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba, Kamishna wa Bima Tanzania kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amesema kuwa Wakuu wa Taasisi wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi na wanaahidi kuyatekeleza kwani wana hamu na mageuzi yanayotarajiwa.