Wednesday, 24 July 2024

WATUMISHI WANNE SHINYANGA DC WAKAMATWA TUHUMA ZA KUIIBIA MAPATO SERIKALI

...


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu 7 kwa tuhuma mbalimbali na uhalifu,wakiwamo watatu ambao wamekamatwa na vipande 20 vya madini ya dhahabu,pamoja na watumishi wanne wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa tuhuma za kuiibia mapato serikali,kwa kutumia POS mashine ambayo haiingizi mapato serikalini.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, amebainisha hayo leo julai 24,2024 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kufuatia misako,doria na operesheni ambayo wameifanya kwa kipindi cha kuanzia juni 26 hadi julai 26 mwaka huu.
Amesema kwa kipindi hicho wamewakamata watu watatu wakiwa na vifaa vya kutendea uhalifu,ambavyo ni gari moja Toyota Crown, vipande 20 vya dhahabu, brashi 26 za kusungulia madini hayo na mezani 3.

Amesema pia wanawashikilia watumishi 4 wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, kutokana na kutumia POS Mashine ya ukusanyaji mapato,ambayo haiingizi mapato Serikalini na kuiibia Serikali.
“Polisi tunaendelea na upelelezi juu ya watuhumiwa hawa wote, ukikamilika watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria,”amesema Magomi.

Aidha,amesema katika msako huo pia wamefanikiwa kukamata vitu mbalimbali vya wizi pamoja na madawa ya kulevya,zikiwamo pikipiki 14,bomba tatu za chuma, spana 22, redio tatu,simu tano, laptop moja, kinu kimoja cha mashine ya kusaga unga, Tv moja, Solar, betri, kaboni,na deki moja.

Vitu vingine walivyokamata ni mafuta ya dizeli lita 20, bati 10, Shock up nne za pikipiki, pombe ya moshi lita 176 na bangi kilogramu 65.

Amesema kwa makosa ya usalama barabarani, madereva wawili wamefungiwa leseni zao kwa kipindi cha miezi mitatu, kwa kosa la kuendesha gari kwa mwendokasi zaidi ya kilomita 100 kwa saa, huku wakikamata makosa ya barabarani 3,943 magari makosa 2,752 pikipiki na bajaji makosa 1,191 ambapo wahusika walilipa faini.
Katika hatua nyingine ametaja jumla ya kesi 15 zimepata mafanikio, ambapo watuhumiwa mbalimbali wamefungwa jela, huku akibainisha kuwa jeshi hilo limetoa elimu na kufanya jumla ya mikutano 71 ya uelimishaji wananchi katika maeneo ya shule, nyumba za ibada na vyombo vya habari ili kusaidia kupunguza makosa ya uhalifu na ukatili.

Amewashukuru wananchi wa Shinyanga kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha usalama wa Mkoa unaendelea kuwa shwari, huku akitoa wito kwa madereva pamoja na wananchi kuendelea kutii sheria za nchi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger