Sunday, 21 July 2024

MITA ZA LUKU ZA MAJI ZITUMIKE KUMALIZA MALALAMIKO YA WANANCHI - WAZIRI AWESO

...

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema mfumo wa matumizi ya luku kwenye ulipaji wa bili za maji utakuwa mwarobaini wa kumaliza malalamiko ya wananchi waliokuwa wakidai kubambikiwa bili.

Waziri Aweso ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa huduma za maji kwa fedha za hatifungani jijini Tanga na kwamba tekinolojia hiyo umekuwa ikifanya vizuri kwa Taasisi ambazo wameshaanza kuitumia.

"Lazima tukubali sasa kama Wizara ya Maji, tekinolojia zitumike kwenye kufanya mageuzi kwenye sekta ya maji, hatuwezi kukubali kila kukicha mwananchi analalamika amebambikiwa bili ya maji,

"Luku za maji zitumike kwani ndiyo uelekeo sahihi, hatutamvulia Mkurugenzi au Mtendaji ambao hatachukulia uzito wa huduma hii kwa kuona siyo muelekeo sahihi" amesema Aweso.

Mbali na hilo Waziri huyo ameutaka uongozi wa Tanga UWASA kushirikisha jamii pamoja na viongozi wa maeneo ambayo wanakwenda kuweka miradi kwani itasaidia wao kufanya kazi zao kwa uhakika na kufanikiwa katika kukamilisha miradi hiyo.

"Jamii ipo na viongozi wapo ukiwashirikisha utafanikiwa na usiwashirikisha utakwama, wakati mwengine Taasisi zinakwama kutowashirikisha viongozi, utakuta mnaenda kwenye ukaguzi wa mradi lakini hata Mtendaji wa eneo husika hayupo, hii siyo sawa,

"Hawana tatizo ni kiasi cha kuwaambia na kuwaweka wazi hata kama kuna tatizo ni vema kuwapa taarifa na utakapowapa ahadi ukifika siku mliyoahidiana basi liwe limepata ufumbuzi, mnapofanya bila taarifa mnatengeneza malalamiko yasiyo ya lazima" amesema.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Tanga (Tanga UWASA), Geoffrey Hill amesema mradi huo una lenga kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na Tanga UWASA ya maji safi, maji taka pamoja na utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji.

"Mradi huu pia upo kwenye kutekeleza agizo la Rais kwani umelenga kupunguza malalamiko ya wateja wetu kwa kufunga dira janja za malipo ya kabla ambapo mteja atapata maji kulingana na malipo yake, hakuna kudaiana wala kubambikiana bili" amesema.

Hata hivyo amebainisha kwamba awali walilenga kufunga mita za maji za luku zipatazo elfu kumi lakini tkupitia mradi huo wamepata mita nyingine elfu nne na kufanya kuwa na jumla ya mita elfu 14 ambazo zitaanza kufungwa kwa wateja mwezi huu

Sambamba na hayo, Hill amebainisha kwamba mradi pia umelenga kuongeza uzalishaji wa maji ambao utawanufaisha wakazi ndani ya Wilaya nne za Mkoa ambazo ni Tanga, Muheza, Pangani na Korogwe.

"Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kugarimu kiasi cha shilingi bilioni 53.12  na unatazamiwa kumalizika ndani ya kipindi cha miezi 15 mpaka kufikia Octoba 2025 na pia utakuwa unatekelezwa kwa awamu kwa miezi mitatu kila awamu" amesema.

Vilevile amesema mkataba huo uliosainiwa umegawanyika katika makundi matatu, ambapo kundi la kwanza utatekeleza eneo la Mabayani kwa kuboresha zile pampu za kudukumia maji za zamani ambazo ni ndogo na kuweka kubwa, lkini pia utafanya ukarabati mkubwa wa kituo cha kusukumia maji na kujenga bomba kubwa ili kufika kwenye mtambo wa Moe.

Amesema kundi la pili, "utafanya kazi kwenye mtambo wa Moe, kukarabati na kutatua mtambo pamoja na kujenga tanki kubwa la kuhifadhia maji linalotarajiwa kuwa na lita milioni 35 ambapo hata tukiwa na shida ya maji tunaweza kukaa na maji masaa takribani 20,

"Na kundi la tatu, utafanya kazi ya kusambaza mabomba mitaani hasa kwa maeneo yaliyopo pembezoni, lakini pia kazi kubwa ya kufanya ukarabati mkubwa wa eneo la Ngamiani ambalo lina mabomba ya tangu enzi za mkoloni" ameongeza.




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger